Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
10 Julai 2021 19:52:21
Ujauzito na VVU
Je naweza pata mtoto asiye na maambukizi ya VVU endapo nitabeba mimba?
Ndio kuna uwezekano mkubwa wa kupata mtoto asiye na maambukizi ya VVU endapo matumizi ya dawa za ARV wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha yatazingatiwa wakati wote na mama ahathudhuria madarasa maalumu.
Kwa kawaida mama mjamzito mwenye maambukizi ya VVU anaweza kumwambukiza kijusi VVU wakati akiwa anakua tumboni, wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha.
Kwa vile si kila mtu mwenye VVU huwa anafahamu hali yake ya maambukizi, ni vema kila mwanamke kupima na kufahamu hali yake kabla ya kuwa mjamzito.
Ni nini cha kufanya kabla ya kupata ujauzito?
Kama wewe au mpenzi wako ana maambukizi ya VVU na mmepanga kupata mtoto, mnapaswa kuwasiliana na kwa ushauri. Baadhi ya mambo ambayo mtashauriwa na daktari ni;
Kutumia dawa za ARV kila siku
Mama kutumia madini ya folic acid angalau miezi mitatu kabla ya kupata mimba
Mwanaume kutumia madini ya zink ili kuongeza uzalishaji wa manii na PEP kujikinga na VVU kama hana maambukizi
Kutumia kondomu endapo mpenzi wako au wote mna maambukizi ya VVU kabla ya kupata mimba
Kupima magonjwa ya zinaa na kupata matibabu wote kama mmojawapo anayo
Kutumia dawa za ARV kila siku husaidia nini?
Matumizi ya dawa za ARV husaidia kupunguza nakala ya virusi kwenye damu na kuongeza uzalishaji wa CD4, matokeo yake ni kupunguza uwezekano wa mtoto kupata maambukizi akiwa tumboni, wakati wa kujifungua au wakati ananyonya. Endapo bado hujaanza kutumia ARV unapaswa kuanza kutumia mara moja.
Namna ya kupunguza hatari ya mtungisho wa yai lenye VVU
Kama mpenzi wako hana VVU, na wewe unatumia ARV ipasavyo na kiasi cha nakala ya virusi kwenye damu kipo chini ya kopi 50 kwa mililita moja ya damu, unaweza shiriki ngono na kupata mimba bila kuambukiza yai wakati wa utungishaji Kama mpenzi wako mwenye VVU anatumia pia dawa za ARV na wote mna nakala ndogo za virusi kwenye damu yaani chini ya kopi 50 kwa mililita mnaweza kushiriki ngono na ukapata mimba bila kumwambukiza mtoto wakati wa utungishaji. Jambo muhimu la kuzingatia ni kufanya maandalizi kabla ya kujamiana ili kuondoa uwezekano wa kupata michubuko isiyo ya lazima.
Namna ya kujamiana pasipo kupata michubuko
Wakati wa kujamiana, mnatakiwa kufanya maandalizi mazuri ya kusisimuana ili kuzalisha ute ute wa kutosha au kutumia mafuta ya KY kwa ajili ya kulainisha uke. Hii itasaidia kufanya tendo lisiwe na michubuko. Shiriki tendo la ndoa kipindi cha hatari tu bila kondom endapo ni wewe tu una maambukizi ya VVU.
Kipindi gani cha hatari kupata mimba?
Kama wewe na mpenzi wako hamna matatizo ya uzazi, kipindi hatari cha kupata mimba ni pale yai linapotolewa kutoka kwenye ovari. Kwa mwanamke mwenye mzunguko wa siku 28, siku za hatari ni kuanzia siku ya 12 hadi 16. Wakati unafanya ngono unashauriwa kuruka siku moja, yaani shiriki siku ya 12, kisha shiriki siku ya 14 na siku ya 16 kuongeza uwezekano mkubwa wa kupata mimba. Jifunze zaidi namna ya kupata ujauzito katika Makala zingine ndani ya tovuti hii ya ulyclinic.
Je ujauzito unaongeza ukali wa dalili za UKIMWI?
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa, ujauzito hauongezi hatari ya kupata dalili kali za VVU au kuongeza hatari ya kufa kutokana na VVU.
Madhara ya HIV kwenye ujauzito ni yapi?
Haifahamiki vema kama VVU au dawa za ARV huongeza hatari ya madhara ambayo hutokea kwa wamama wenye maambukiziya VVU kwenye ujauzito ambayo ni;
Kujifungua kabla ya wakati
Kujifungua mtoto njiti
Madhaara mengine yanayoweza kutoke ni;
Mtoto kupata maambukizi
Ni nini utafanyiwa ukishabeba mimba?
Unapaswa kushirikiana na daktari na kuhudhuria kliniki ili upate huduma itayosaidia kufanya ujauzito wako uwe na matokeo mazuri. Wakati unahudhuria kliniki utafanyiwa;
Kipimo cha kiwango cha kinga za mwili (CD4)
Kipimo cha idadi ya nakala za virusi kwenye damu
Kipimo cha kuangalia mabadiliko ya kirusi au kwa kuangalia kama kuna ishara za usugu wa kimelea kwenye dawa kwa kutumia dalili tu
Vipimo vingine ambavyo hufanyika kama kawaida, mfano vipimo vya magonjwa ya zinaa, mkojo, wingi wa damu n.k
Kipimo cha kuangalia ugonjwa wa kisukari kati ya wiki ya 24 hadi 28 kama unatumia ARV
Dawa za ARV wakati wa ujauzito
Wakati wa ujauzito, unapaswa kutumia dawa za ARV zenye muunganiko wa dawa zaidi ya moja, endapo bado hujaanza dawa, unapaswa kuanza mara moja. Tafiti zinaonyesha kuanza ARV mapema au kabla ya ujauzito hupunguza kwa kiasi kikubwa nakala ya virusi kwenye damu kipindi cha kujifungua. Nchi mbalimbali zina utaratibu wake wa kutoa aina Fulani ya dawa kwenye ujauzito.
Dawa za ARV wakati wa ujauzito
Baada ya kuwa mjamzito, utatakiwa endelea kufanyiwa uchunguzi wa mwili wako kwa vipimo mbalimbali kila utakapohudhuria kliniki yako ya ujauzito. Vipimo vya CD4, na nakala za VVU kwenye damu hufanyika baada ya muda Fulani kupita, pia utafanyiwa kipimo cha picha mionzi sauti ya ndani ya mfuko w akizazi ili kuangalia hali ya mtoto haswa kwenye wiki 18 hadi 20 za ujauzito ili kuangalia ukuaji wa mtoto. Kipimo kingine kinaweza fanyika kipindi cha tatu cha ujauzito.
Endapo hutaki kuanza dawa mapema ufanyaje?
Baadhi ya watu wanawake wenye kichefuchefu kikali na kutapika wakati wa ujauzito na bado hawajaanza kutumia ARV, wanaweza wasianze kutumia dawa kwa hofu ya kutapika dawa hizo kipindi cha kwanza cha ujauzito. Wajawazito wa namna hii wanaweza kuanza dawa baada ya kipindi hiki kupita yaani kuanzia wiki ya 13 na kuendelea. Ongea na daktari wako kwa ushauri zaidi wa nini cha kufanya kama una dalili kali za kutapika kutokana na ujauzito.
Unaweza acha dawa za ARV kwa sababu ya kutapika?
Hapana, kama umeshaanza kutumia ARV kabla ya kuwa mjamzito, unapaswa kuendelea kutumia dawa hizo kila siku kwa maisha yako yote ili kuepuka kumwambukiza mtoto na usugu wa VVU kwenye dawa. Mtu ambaye anaweza subiria kipindi hiki cha kwanza kiishe ndipo anywe dawa ni yule ambaye bado hajaanza kutumia ARV. Endapo hata hivyo unatapika sana kipindi hiki, ongea na daktari wako upate msaada wa nini cha kufanya ili kutibu hali hiyo au kubadilishiwa dawa endapo kuna uchaguzi wa dawa kituoni.
Dawa za ARV za kuepuka wakati wa ujauzito
Kuna baadhi ya dawa za ARV unapaswa kuepuka kutumia wakati wa ujauzito isipokuwa endapo zina faida kuliko hasara. Utashauriwa na daktari endapo dawa ulizokuwa unatumia ni salama au si salama. Usalama wa dawa hutambuliwa kwa, kuangalia mwingiliano wa dawa hizo na dawa zingine na madhara ya dawa kwenye ujauzito na endapo dawa inafahamika kuleta madhaifu ya kiuumbaji kwa mtoto
Ongea na daktari wako kuhusu usalama wa dawa za ARV na ujauzito wako, usiache kutumia dawa isipokuwa umeshauriwa na daktari wako. Soma kuhusu dawa mbalimbali na ushauri wake wakati wa ujauzito kwenye Makala ya ‘ushauri wa matumizi ya dawa wakati wa ujauzito’ ndani ya tovuti hii ya ulyclinic.
Dawa zisizo za ARV za kuepukwa wakati wa ujauzito
Kuna dawa ambazo hufahamika kusababisha madhaifu ya kimaumbile kwa kichanga endapo zitatumika na hivyo zinapaswa kuepukwa. Dawa hizo ni;
Aminopterin
Androgens
Benazepril (Lotensin)
Captopril (Capoten)
Carbamazepine (Tegretol)
Carbimazole/Methimazole
DES (Diethylstilbestrol)
Doxycycline (Vibramycin)
Enalapril (Vasotec)
Fosinopril Sodium (Monopril)
Isotretinoin (Accutane, Retin-A)
Kokeni
Lisinopril + Hydrochlorothiazide (Zestoretic, Prinzide),
Lisinopril (Zestril, Prinivil)
Lithium (Eskalith, Lithob)
Methotrexate (Rheumatrex)
Paramethadione (Paradione)
Penicillamine (Ciprimene, Depen)
Phenytoin (Dilatin)
Pombe
Quinapril (Accupril)
Ramipril (Altace)
Streptomycin
Tetracycline (Achromycin)
Thalidomide (Thalomid)
Thiouracil/Propylthiouracil
Trimethadione (Tridione)
Valproic Acid (Depakene, Valprotate)
Warfarin (Coumadin)
Kama chupa ya uzazi itapasuka kabla ya wiki 37 za ujauzito nini kifanyike?
Kama chupa ya uzazi imepasuka kabla ya wiki 37 za ujauzito lakini baada ya wiki 35 za ujauzito, utashauriwa na daktari wako endapo kuna umuhimu wa kuendeleza ujauzito mpaka ufikie wiki 37 au kuanzisha uchungu. Kama chupa itapasuka kabla ya wiki 35 za ujauzito, utashauriwa na daktari wako kuendeleza ujauzito mpaka utakapofikisha wiki 37 au kujifungua kama kuna hatari kubwa ya maambukizi ya bakteria kwa kichanga tumboni. Soma taarifa zaidi kuhusu ‘kupasuka chupa ya uzazi’ na matibabu yake sehemu nyingine ya tovuti hii kwa maelezo zaidi.
Endapo chupa itapasuka baada ya kukamilisha wiki 37 itakuwaje?
Kama chupa ya uzazi imepasuka baada ya wiki 37 na idadi ya nakala ya virusi kwenye damu ipo chini ya 50 na una CD4 zaidi ya 400, utaanzishiwa uchungu ili ujifungue kwa njia ya kawaida. Endapo ulikuwa umepanga kujifungua kwa njia ya upasuaji, utatakiwa kufika hospitali haraka kwa upasuaji.
Uchunguzi wa mwili wakati wa ujauzito
Baada ya kuwa mjamzito, wakati wa kliniki yako utaendelea kufanyiwa uchunguzi wa mwili kwa vipimo mbalimbali. Vipimo vya CD4, na nakala za VVU kwenye damu hufanyika baada ya muda Fulani kupita, pia utafanyiwa kipimo cha picha mionzi sauti ya ndani ya mfuko w akizazi ili kuangalia hali ya mtoto haswa kwenye wiki 18 hadi 20 za ujauzito ili kuangalia ukuaji wa mtoto. Kipimo kingine kinaweza fanyika kipindi cha tatu cha ujauzito.
Dawa za ARV wakati wa uchungu na kujifungua
Wakati wa uchungu endapo nakala ya virusi vya UKIMWI ipo juu ya kiwango cha kopi 400, utapewa zidovudine moja ya dawa ya ARV kupitia mishipa ya damu ili kupunguza hatari.
Njia gani salama ya kujifungua?
Njia salama kuliko zote kujifungua mwanao ni njia itakayozuia mwanao kupata maambukizi, ambayo itaamuliwa kutegemea kiwango cha nakala za virusi kwenye damu. unaweza jifungua kwa njia ya uke endapo kiwango cha nakala ya virusi kwenye damu ni kidogo na hakuna kipingamizi kingine cha kujifungua kwa njia hii au kwa njia ya upasuaji endapo imeonekana kuwa salama.
Kuwa na nakala ndogo za virusi humaanisha nini?
Nakala ya virusi ni idadi ya virusi ambavyo vinapatikana kwenye damu, ara nyingi endapo nakala hizo zipo chini ya 50 kwa mililita moja ya damu, husemekena una nakala ndogo za virusi hivyo unaweza kujifungua kwa njia ya kawaida na kuwa na uhakika mkubwa wa usalama kwa mtoto. Nakala za virusi zikizidi 50 kwenye mililit amoja ya damu, hii hufahamika una nakala nyingi za virusi na utapaswa kujifungua kwa upasuaji kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kumwambukiza mwanao.
Wakati gani sahihi wa kujifungu?
Kama una nakala nyingi za virusi kwenye damu licha ya kutumia dawa za ARV, utashauriwa kujifungua baada ya wiki 38 za ujauzito hata kama uchungu haujaanza.
Matunzo kwa mama baada ya kujifungua
Baada ya kujifungua, unapaswa kuendelea kutumia ARV kila siku. Utaendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya yako ikiwa pamoja na sonona baada ya kujifungua. Utapewa pia ushauri kuhusu njia za uzazi wa mpango, chakula, usafi na maziwa.
Matunzo kwa kichanga baada ya kuzaliwa
Vichanga waliozaliwa na mama mwenye VVU hupewa dawa za ARV wiki nne hadi 6 baada ya kuja duniani. Dawa hizi husaidia kuzuia maambukizi ya VVU kwa mtoto ambayo yanaweza kutokea wakati wa kujifungua. Dawa zinazoshauriwa kutumika ni;
ZDV
Lamivudine
Nevirapine
Njia salama ya kumpa chakula kichanga ni ipi?
Kwa nchi zilizondelea, mara nyingi hawaruhusiwi kunyonyesha watoto ziwa au maziwa ya mama, hata hivyo kwa nchi zinazoendelea kwa sababu za gharama ya maziwa ya kopo ambayo yametengenezwa kufanana na maziwa ya binadamu, wamama wengi huchagua kumnyonyesha mtoto ziwa la mama. Utapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kumwambukizi mtoto baada ya kuzaliwa kwa kutumia maziwa ya kopo badala ya kumnyonyesha ziwa lako. Kumbuka hata kama unatumia ARV, bado kuna uwezekano wa kumwambukiza kichanga wakati wa kunyonyesha.
Vipimo vya UKIMWI kwa kichanga baada ya kuzaliwa
Kwa kawaida kipimo cha antibodi ya HIV hutumika kutambua uwepo wa maambukizi kwa watu wazima, kwa watoto vipimo tambuzi huwa tofauti. Kipimo cha antibodi hakifanyiki kwa sababu kichanga anapozaliwa huwa na antibodi kutoka kwa mama na hivyo endapo atapimwa kwa kipimo hiki ataonekana kuwa na maambukizi ya VVU, majibu yanayoweza kuwa ni kweli au si la. Kipimo hiki kitasema majibu ya kweli endapo kichanga amefikisha umri wa wiki sita bila kunyonya maziwa ya mama. Kipindi hiki, antibodi za mama huwa zimeisha kwenye damu ya mtoto, isipokuwa endapo aliendelea kunyonya.
Kipimo kipi kizuri kutambua maambukizi ya VVU kwa kichanga mwenye umri chini ya miezi sita?
Kipimo kinachotakiwa fanyika ili kutambua kama kichanga wa chini ya miezi sita ana maambukizi ya VVU ni kipimo cha HIV PCR. Kipimo hiki hufanyika siku mbili baada ya mtoto kuzaliwa na hupima protini za kirusi kwenye damu, kipimo kinatakiwa rudiwa fanyika baada ya umri zaidi ya wiki 2 na kingine akiwa na zaidi ya wiki 4 na vyote vinatakiwa kufanana majibu. Licha ya kupima mara mbili au zaidi ya mara tatu, majibu ya kipimo hiki huwa si ya mwisho kusema mtoto ana mambukizi au hana. Mtoto anapofikisha miezi sita bila kunyonya maziwa ya mama, anaweza kufanyiwa kipimo cha antibodi na kitatoa majibu yaliyo sahihi.
Matarajio ya majibu ya kipimo cha HIV PCR
Mara nyingi, endapo umetumia dawa zako vema, majibu huwa negative kwa HIV, hata hivyo si kwa asilimia 100. Ikitokea majibu sio mazuri yaani ni chanya kwa maambukizi ya VVU, huna haja ya kusikitika au kulia kwa sababu kuna dawa za ARV ambazo mtoto atatumia katika maisha yake yote ambazo zitamfanya aweze ishi sawa na watu wengine wasio na maambukizi na kufikia malengo yake.
Ni wakati gani majibu ya kipimo cha VVU kwa mtoto huwa ya uhakika?
Vipimo vinaweza kusema mtoto hana maambukizi au anayo bila kuwa na uhakika wa majibu hayo kama ni ya kweli au la. Majibu ya kipimo cha VVU yatakuwa sahihi endapo mtoto asiyeyonyeshwa maziwa ya mama atapimwa vipimo viwili na kuwa na majibu yake yale.
Kipimo cha kwanza cha HIV PCR kinatakiwa fanyika mtoto akiwa na umri chini ya mwezi mmoja na kingine akiwa na umri zaidi ya miezi minne
Au
Kufanyiwa kipimo cha Antibodi kutoka kwenye sampuli mbili tofauti mtoto akiwa na umri wa zaidi ya miezi sita
Je kuna lishe maalumu wunapaswa kupata mjamzito?
Wakati wa ujauzito kama ilivyooelezewa hapo juu unahitaji kupata folic acid na madini chuma ya kutosha, hata hivyo baada ya kujifungua, unapaswa pia kupata mlo kamili kutoka kwenye makundi matano ya chakula. Kula vyakula vinavyoweza kukupa nguvu na kuongeza uzazalishaji wa maziwa endapo umechagua kunyonyesha mtoto maziwa yako.
Wapi unatapa taarifa zingine zaidi?
Pata taarifa zaidi zilizo sahihi kuhusu VVU na ujauzito kutoka kwa daktari wako au kupitia Makala zingine za ULY CLINIC kwa kubofya linki zinazofuata au rejea chini ya tovuti hii. 1. https://www.ulyclinic.com/post/dawa-kinga-ya-ukimwi-ulyclinic 2. https://www.ulyclinic.com/ukimwi 3. https://www.ulyclinic.com/dalili-za-ukimwi
Majina mengine ya Makala hii
Ujauzito wa mwathirika wa VVU
Nina VVU, naweza pata mtoto asiye na maambukizi
Namna ya kupata mtoto huku nikiwa na maambukizi ya VVU
Naweza kupamba mimba wakati naishi na VVU?
Madhara ya HIV kwa kichanga tumboni
Mimba ya mgonjwa wa VVU/UKIMWI
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
30 Oktoba 2021 14:54:42
Rejea za dawa
Imechukuliwa 10.07.2021
Centers for Disease Control and Prevention (CDC). http://www.cdc.gov/hiv/group/gender/pregnantwomen/index.html. Imechukuliwa 10.07.2021
HIV/AIDS Treatment Information Service. http://clinicalinfo.hiv.gov/. Imechukuliwa 10.07.2021
British HIV Association (BHIVA): www.bhiva.org. Imechukuliwa 10.07.2021 5. NAM, a UK-based organisation: www.aidsmap.com. Imechukuliwa 10.07.2021
HIV and pregnancy. https://www.rcog.org.uk/en/patients/patient-leaflets/hiv-and-pregnancy/. Imechukuliwa 10.07.2021