Mwandishi:
Dkt. Salome A, MD
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
24 Novemba 2021 07:55:13
UTI kwa mjamzito
Mambukizi ya mfumo mkojo ambayo hujulikana kama UTI ni miongoni mwa magonjwa yanayojitokeza sana wakati wa ujauzito, hata hivyo wanawake wengi hupata UTI hata kabla ya kuwa wajawazito na kuongeza hatari ya UTI wakati wa ujauzito.
Hali ya ujauzito huchangia sana kufanya UTI kuwa ugonjwa unaojitokeza katika kipindi hiki kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kifiziolojia katika mfumo wa mkojo, mabadiliko ya homoni , mgandamizo wa mfuko wa uzazi katika kibofu cha mkojo na hali ya kushuka kwa kinga ya mwili.
Wajawazito wengi huwa hawaoneshi dalili wala viashiria vya UTI au huwa na dalili na viashiria ambavyo si shahidi sana hivyo wengi wao hugundulika katika vipimo vya mkojo wakati wa kliniki. Aina hii ya UTI isipotibiwa husababisha ugonjwa kukomaa na maabukizi kufika hadi katika figo hali ambayo ni hatari, hivyo ni muhimu wajawazito wote wanaongundulika na vimelea katika mkojo kuanzishiwa matibabu bila kujali kama wana dalili na viashiria vya UTI au la ili kuepuka madhara yake kwa mama na mtoto.
Si vema kutumia dawa za UTI wakati wa ujauzito bila kuandikiwa na daktari kwani si dawa zote zinazotibu UTI ni salama kwa mtoto aliye tumboni, endapo mama anahisi dalili za UTI ni vema kupata msaada wa kitabibu kabla ya kunywa dawa yoyote.
Muundo na kazi za mfumo wa mkojo
Mfumo wa mkojo umeundwa kwa ogani ambazo kazi yake ni kukusanya, kusafirisha, kutunza na kutoa taka mwili katika hali maji yaani mkojo na kurekebisha kiwango cha maji na madini katika mwili.
Viungo vinavyotengeza mfumo wa mkojo ni;
Figo ya kulia na kushoto
Mirija ya ureta kulia na kushoto
Kibofu cha mkojo
Mrija wa urethra
Mkojo hutengenezwa katika figo na kusafiri kupitia mirija ya ureta hadi kwenye kibofu cha mkojo, mkojo hutunzwa kwa muda kwenye kibofu hadi utakapotolewa kupitia mrija wa urethra.
Mfumo wa mkojo umegawanyika katika sehemu mbili yaani mfumo wa mkojo wa juu na mfumo wa mkojo wa chini kama ifuatavyo;
Mfumo wa mkojo wa juu - umeundwa na figo pamoja na mirija ya ureta
Mfumo wa mkojo wa chini - umeundwa na kibofu cha mkojo na mrija wa urethra
Vihatarishi
Sababu zinazomuweka mjamzito katika hatari ya kupata UTI ni;
Sababu za kimaumbile
Wanawake wote wapo katika hatari ya kupata maambukizi katika mfumo wa mkojo kuliko wanaume kwa sababu ya kuwa na mrija mfupi wa urethra kama ilivyo kwa wanaume, mrija wa urethra kwa mwanamke una urefu wa sentimeta 4 wakati kwa mwanaume ni kati ya sentimeta 15 hadi 20. Hivyo ni rahisi vimelea kuingia katika mfumo wa mkojo wa mwanamke kuliko wa mwanaume.
Sababu nyingine ni ukaribu uliopo kati ya mrija wa urethra na maeneo mengine ya wazi ambayo yana bakteria (uke na tundu la njia ya haja kubwa). Bakteria eschelichia coli ambaye kwa asilimia kubwa husababisha UTI huishi katika maeneo hayo kwahiyo ni rahisi kuingia katika mfumo wa mkojo hasa wakati wa kujamiiana au kuwekewa mpira wa mkojo.
Mabadiliko wakati wa ujauzito
Mji wa uzazi unavyotanuka kadri mtoto anavyokua mkubwa husababisha mgandamizo katika kibofu na kupelekea kukojoa kidogo na mkojo mwingine kubaki na kusababisha kuzaliana kwa bakteria.
Wakati wa ujauzito homoni progetrerone huzalishwa kwa wingi, homoni hii husababisha kutanuka kwa mirija ya ureta hivyo mkojo kukawia kufika katika kibofu, pia kurudi kwa mkojo ambao tayari umefika katika kibofu katika mirija ya ureta. Sababu hizi hutoa mwanya wa bakteria wanaosababisha UTI kuzaliana.
Ujazito hupunguza kinga ya mwili kwahiyo mjamzito yupo katika hatari ya kupata maambukizi mbalimbali ikiwamo UTI kuliko mwanamke ambaye si mjamzito.
Sababu nyinginezo
Historia ya kuwa na UTI kabla ya ujauzito
Kujamiiina
Kisukari wakati wa ujauzito
Umri mkubwa
Zao nyingi
Ugonjwa wa seli mundu
Hali duni ya maisha
Kasoro za kimaumbile katika mfumo wa mkojo
Vimelea wa UTI kwa wajawazito
Vimelea wanaosababisha maambukizi katika mfumo wa mkojo hawatofautiani na wale wanaosababisha maambukizi kwa watu wengine. Bakteria hawa ni;
Escherichia coli
Klebsiella pneumoniae
Staphylococcus
Streptococcus
Proteus na
Spishi wa Enterococcus
Baketria Escherichia coli husababisha zaidi maambukizi katika mfumo wa mkojo kuliko bakteria wengine tajwa hapo juu, inakadiriwa takribani asilimia 80 ya maambukizi katika mfumo wa mkojo husababishwa na bakteria huyu.
Aina za UTI wakati wa ujauzito
Kuna aina kuu tatu za maambukizi katika mfumo wa mkojo wakatiwa ujauzito kama ifuatavyo
UTI isiyo na dalili
Ni hali ya kugundulika na bakteria wanaosababisha UTI kwa mtu ambaye hana dalili na viashiria vya UTI, katika lugha ya kimaabara humaanisha kuwa na zaidi ya bakteria 1,000,000 katika mililita moja ya mkojo kwa kwa mtu ambaye hana dalili na viashiria vya UTI.
Aina hii ya UTI huwapata wanawake wengi hata kabla ya ujauzito na isipotibiwa husababisha aina nyingine za UTI ambapo dalili na viashiria huonekana.
UTI ya kibofu cha mkojo
Pia huusisha maambukizi katika mrija wa urethra na hujulikana kama maambukizi ya mfumo wa chini wa mkojo. Mgonjwa huwa na dalili na viashiria vya UTI hata kabla ya kugundulika katika kipimo cha mkojo.
UTI ya figo
Hujulikana kama maambuki ya mfumo wa juu wa mkojo. Huusisha figo pamoja na sehemu ya mirija ya ureta iliyopo ndani ya figo. Maambukizi haya huwa ni hatari zaidi kuliko aina zingine tajwa hapo juu na huchukuliwa kama dharura.
Dalili na viashiria
Dalili na viashiria vya UTI wakati wa ujauzito hutegemea aina ya UTI na sehemu ya mfumo wa mkojo iliyoathiriwa kama ifuatavyo
UTI isiyo na dalili
Huwa haina dalili wala viashiria vyovyote vya maambukizi, hugundulika katika vipimo vya mkojo.
UTI ya kibofu cha mkojo
Huwa na dalili zifuatazo;
Kujojoa mara kwa mara
Maumivu wakati wa kukojoa
Maumivu ya tumbo la chini
Hali ya ulazima wa kwenda kukojoa mara kwa mara
Kupanda kwa joto la mwili
Dalili kwa mjamzito
Dalili kuu za aina hii ya UTI katika kipindi ujauzito ni;
Kukojoa mara kwa mara
Kuhisi kubanwa na mkojo mara kwa mara.
UTI ya figo
Huwa na dalili zifuatazo;
Joto la mwili kupanda sana
Hali ya kuhisi baridi na kutetemeka
Kichefuchefu
Kutapika
Kupumua kwa haraka haraka
Shinikizo la damu kushuka
Maumivu ya kichwa
Damu katika mkojo
Maumivu nyuma ya mgongo chini ya usawa wa kifua
Kuukojoa mkojo kidogo
Kuchanganyikiwa
Vipimo vya kubaini UTI
Vipimo vifuatavyo hufanyika ili kubaini uweo wa vimelea wa UTI
Kipimo cha urine dipstick
Ni kipimo cha haraka kinachotumika kupima UTI katika mazingira ambayo hakuna maabara au vifaa tiba vya kisasa kama vile hadubini.
Hufanywa kwa kudumbukiza karatasi maalumu kwenye mkojo kisha kuangalia mabadiliko ya rangi kwa kulinganisha na chati maalumu ya rangi, rangi hubadilika kutokana na uwepo wa vitu mbali mbali katika mkojo.
Uwepowa vitu vifuatavyo humaanisha uwepo wa vimelea katika mkojo;
Uwepo wa vimen’enya vinayozalishwa na seli nyeupe za damu
Uwepo wa kampaundi ya nitrite
Kipimo hiki kinaweza kutumika kutambua uwepo wa magonjwa mengine katika ujauzito kama vile kisukari na shinikizo la juu la damu linalosababishwa na ujauzito.
Urinalysis
Huusisha hatua tatu za uchunguzi wa mkojo kwa kuangalia mabadiliko yanayooneka kwa macho kama vile uzito, rangi nk, kupima vitu mbali mbali vilivyo katika mkojo ( kama ilivyo kwenye urine dipstick) na kuchunguza uwepo wa vimelea kupitia hadubini.
Tofauti na urine dipstick upimaji huu husaidia kuona vimelea katika mkojo pamoja na viambata vingine vinanyoashiria UTI kwa kutumia hadubini.
Kipimo cha kuotesha mkojo na utambuzi wa dawa inayoua vimelea
Mkojo huoteshwa katika maabara ili kujua aina ya bakteria na dawa zinazoweza kuwaua, tofauti na vipimo vingine kipimo hiki ni cha uhakika katika kugundua UTI
Kipimo cha ultrasound
Hufanyika endapo mgonjwa ana dalili na viashiria vya maambukizi katika mfumo wa juu wa mkojo. Ultrasound ya figo husaidia kutofautisha UTI na magonjwa mengine ya figo ambayo yana dalili na viashiria saw ana UTI katika figo, kwa mfano mawe katika figo,
Pia husaidia kugundua kasoro mbali mbali za kimaumbile katika mfumo wa mkojo ambazo ni moja ya vyanzo vya UTI inayojirudia mara kwa mara.
Vipomo vingine
Hivi ni vipimo vinavyofanyika kulingana na hali ya mgonjwa, baadhi ya vipimo hivi ni;
Kipimo cha picha nzima ya damu (FBP)- hufanyika endapo mgonjwa na dalili na viashiria vya maabukizi katika damu
Kipimo cha utendaji kazi wa figo- hufanyika kwa mgonjwa ambaye amepata athari ya UTI katika figo kutokana na kuchelewa kupata matibabu .
Matibabu ya UTI wakati wa ujauzito
Matibabu ya UTI wakati wa ujauzito hutofautiana na watu wengine au wanawake ambao sio wajawazito hasa katika uchaguzi wa dawa, vile vile matibabu hutegemea aina ya UTI kama ifuatavyo;
Dawa zinazotumika kutibu UTI wakati wa ujauzito
Uchaguzi wa dawa katika matibabu ya UTI wakati wa ujazuzito hujali zaidi usalama wa mama na mtoto kwani si dawa zote zinazotumika kutibu UTI zinafaa katika kipindi cha ujauzito.
Zifuatazo ni dawa ambazo ni salama katika matibabu ya UTI wakati wa ujauzito;
Dawa katika kundi la penicillin- dawa zinazotumika sana ni amoxycillin- clavulanic acid, ampicillin na amoxycillin
Dawa katika kundi la cephalosprorin- dawa zinazotumika sana ni cephalexin na ceftriaxone
Dawa katika kundi la nitrofurans- dawa inayotumika sana n nitrofurantoin
Dawa katika kundi la anti-folate- dawa inayotumika sana ni trimethoprim- sulfamethoxazole maarufu kama septrin
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la usugu wa dawa kwa bakteria aina ya e.coli ambaye ndio chanzo kikuu cha UTI kwa dawa katika kundi la penicillin ukilinganisha na makundi mengine hivyo ufanisi kwa dawa za kundi la penicillin huwenda ukawa mdogo kwa baadhi ya watu.
Sio salama kutumia septrin katika kipindi cha kwanza cha ujauzito kwasababu ina madhara kwa mtoto, kwahiyo dawa hii hutumika kwa mjamzito aliye katika kipindi cha kwanza na cha tatu cha mimba tu.
Matibabu kulingana na aina ya UTI
Uchaguzi wa aina ya matibabu hutegemea aina ya UTI pamoja na hali ya mgonjwa kwa ujmla kama ifuatavyo
UTI isiyo na dalili
Endapo mjamzito atagundulika na UTI bila kuonesha dalili zozote anatakiwa kuanzishiwa dawa za kunywa. Dawa zinazotumika sana kwa aina hii ya UTI ni cephalexin, amoxycillin- clavulanic acid, amoxycillin, nitrofurantoin na trimethoprim- sulfamethoxazole. Hata hivyo unahitaji ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa ili kuona usalama wake kwako na mwanao.
UTI ya kibofu cha mkojo
Maambukizi katika mfumo wa chini wa mkojo hutibiwa kwa dawa za vidonge kutoka makundi salama ya dawa salama kama ilivyoainishwa hapo awali. Dawa zinazotumika ni sawa na zile za UTI isiyo na dalili.
UTI ya figo
Huwa ni dharura na mgonjwa hupatiwa matibabu akiwa hospitalini, mgonjwa hutibiwa kwa dawa za sindano kutoka katika makundi salama ya dawa za UTI katika ujauzito. Mgonjwa anapopata nafuu huendelea na dawa za vidonge kwa muda wa siku 5 hadi 7.
Matibabu mengine hutegemea hali ya mgonjwa mfano kutibu homa, kuongezwa maji, dawa za kuzuia kutapika nk.
Madhara ya UTI wakati wa ujauzito
Madhara kwa mama
Kupasuka kwa chupa kabla ya uchungu
Kupata uchungu kabla ya mimba kukomaa
Kupata ugonjwa wa shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito
Upungufu wa damu
Maambukizi ya bakteria katika damu
Madhara kwa mtoto
Mtoto kudumaa akiwa tumboni
Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo
Mtoto kupata maambukizi ya bacteria mara baada ya kuzaliwa
Kinga
Jinsi ya kuzuia UTI wakati wa ujauzito
Njia zifuatazo husaidia kuzuia UTI kwa wajawazito na wanawake ambao si wajawazito;
Usafi wa sehemu za siri; kabla na baada ya kujamiiana, inashauriwa kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma ili kuizia vimelea karibu na njia ya haja kubwa kuingia katika mfumo wa mkojo
Kuepuka kubana mkojo; kukojoa kila unapohisi kubanwa na mkojo na kukojoa baada ya kujamiiiana.
Kupima na kutibu wajawazito ambao wana wanaongundulika na vimelea katika mkojo
Kutumia vitamin C
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
28 Novemba 2021 19:54:27
Rejea za dawa
Patricia j. Habak; robert p. Griggs, jr. Urinary tract infection in pregnancy. Https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/nbk537047/. Imechukuliwa 24.11.2021
Duane r. Hickling, tung-tien sun,and xue-ru wu. Anatomy and physiology of the urinary tract: relation to host defense and microbial infection. Doi: 10.1128/microbiolspec.uti-0016-2012. Https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/pmc4566164/. Imechukuliwa 24.11.2021
Joanna matuszkiewicz-rowińska, jolanta małyszko and monika wieliczko. Urinary tract infections in pregnancy: old and new unresolved diagnostic and therapeutic problems. 2015 mar 14. Doi: 10.5114/aoms.2013.39202. Https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/pmc4379362/. Imechukuliwa 24.11.2021
Abilash j. Bhansali, leeberk r. Inbaraj, carolin e. George, and gift norman. Can urine dipstick test be an alternative to detect urinary tract infection in limited resource setting? – a validity studyfrombangalore,india.2020feb28.doi:10.4103/jfmpc.jfmpc_696_19. Https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/pmc7114041/. Imechukuliwa 24.11.2021
David m. Roxe. Clinical methods: the history, physical, and laboratory examinations. 3rd edition. Chapter 191urinalysis. Https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/nbk302/. Imechukuliwa 24.11.2021
Raisa o platte, md, phd urogynecology associate, department of obstetrics and gynecology, geisinger health system. What is the role of renal ultrasonography in the diagnosis of urinary tract infection (UTI) during pregnancy?. Https://www.medscape.com/answers/452604-54662/what-is-the-role-of-renal-ultrasonography-in-the-diagnosis-of-urinary-tract-infection-uti-during-pregnancy. Imechukuliwa 24.11.2021
Flavia ghouri, amelia hollywood and kath ryan. A systemic review of non-antibiotic measures for the prevention of urinary tract infections in pregnancy. Https://bmcpregnacychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-018-1732-2