Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Salome A, MD & Dkt. Benjamin L, MD
5 Juni 2025, 06:31:58

Kukosa hedhi na kipimo cha mimba kuwa hasi
Swali la msingi
Habari! Kitu gani kinampelekea mtu kukosa hedhi na akipima ujauzito ni negative, na nini afanye ili akae sawa?
Majibu ya awali
Kukosa hedhi huku vipimo vya mimba vikiwa hasi (negative) kunaweza kutokana na sababu nyingi ambazo si ujauzito. Hali hii hujulikana kitaalamu kama amenorea ya upili, yaani kukosa hedhi baada ya kuwa na mzunguko wa kawaida hapo awali.
Baadhi ya sababu za kawaida ni msongo wa mawazo, mabadiliko ya uzito, mazoezi ya kupita kiasi, matatizo ya homoni kama sindromu ya ovari yenye vifukomaji vingi au matatizo ya tezi ya shingo (thairoid). Mara nyingine, inaweza kuwa matokeo ya matumizi ya dawa fulani au mabadiliko ya kimaisha (mfano kulala ovyo, kula vibaya, kukosa usingizi, au safari nyingi).
Visababishiinazowezekana Kisayansi
Mbali na ujauzito, miongoni mwa visababishi vikuu vya kukosa hedhi kunaweza kusababishwa na sababu zingine zifuatazo:
Kisababishi | Maelezo |
1. Msongo wa mawazo (stress) | Hupunguza homoni zinazochochea uovuleshaji |
2. Sindromu ya ovari yenye vifukomaji vingi | Ovari zina mifuko mingi midogo yenye maji, hedhi huchelewa au kutoweka |
3. Uzito kupungua au kuongezeka kupita kiasi | Mafuta mwilini huathiri estrojeni na projesteroni |
4. Upungufu wa homoni za thairoidi | Upungufu wa homoni ya tezi huchanganya mzunguko |
5. Dawa | Mfano: antidepressants, antipsychotics, au dawa za kifafa |
6. Mazoezi makali sana | Wanariadha huathirika kwa sababu ya kupoteza mafuta mwilini |
7. Kufikia komahedhi mapema (chini ya miaka 40) | Ovari hushindwa kutoa yai na hedhi hukoma mapema |
Nini cha kufanya ili Mwili Urejee Kawaida?
Hatua za Nyumbani
Rekebisha lishe – Kula mlo kamili na wa kutosha (mboga, protini, matunda, mafuta bora).
Punguza msongo – Fanya mazoezi ya kupumzika kama yoga, kutembea, au kusali.
Lala vya kutosha – Angalau saa 7 hadi 8 kila siku.
Punguza mazoezi makali – Badilisha na mazoezi ya kawaida yasiyo chosha.
Epuka kahawa nyingi, sigara na pombe – Huvuruga homoni.
Mimea inayosaidia kurekebisha mzunguko
Tangawizi
Mdalsini
Fennel (haradali ya kiasia)
Tumia kama chai mara 2 kwa wiki, lakini usiitumie kupita kiasi.
Lini Umwone daktari?
Hedhi haijarudi ndani ya miezi 3
Una nywele nyingi usoni/kifuani au chunusi nyingi (dalili za sindromu ya ovari yenye vifuko maji vingi)
Kipimo cha ujauzito kinaonyesha negative lakini bado unapata dalili kama mimba
Unapata maumivu ya nyonga au kutokwa na damu isiyo ya kawaida
Unajaribu kupata mimba bila mafanikio kwa miezi 6 au zaidi
Vipimo vya Kitabibu vinaweza kujumuisha
Kipimo cha damu cha mimba (β-hCG)
Kipimo cha homoni: FSH, LH, Prolactin, TSH
Ultrasound ya fupanyonga (kuangalia ovari na uterus)
Kipimo cha tezi (thyroid profile)
Kipimo cha PCOS na kazi ya ovari
Matibabu
Matibabu hutegemea kisababishi, baadhi yake ni kama ilivyoorodheshwa hapa chini:
Kisababishi | Matibabu |
Sindromu ya oavari yenye vifukomaji vingi | Dawa za kurekebisha uovuleshaji (clomiphene, metformin) |
Upungufu wa homoni ya tezi thairoidi | Levothyroxine (dawa ya kuongeza homoni ya tezi) |
Mzongo wa mwili au mawazo | Ushauri tiba, kupumzisha mwili |
Upungufu wa homoni | Dawa za kuongeza homoni ya uzazi |
Hitimisho
Kukosa hedhi bila ujauzito si hali ya kawaida, na ni vyema kufuatilia kwa umakini. Hatua za mapema, lishe bora, kupunguza msongo, na kupata ushauri wa daktari husaidia kurejesha mzunguko wa kawaida. Usikae kimya. Fuatilia mwili wako na chukua hatua kwa afya yako.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeboreshwa,
5 Juni 2025, 07:28:36
Rejea za mada hii
American College of Obstetricians and Gynecologists. Practice Bulletin No. 128: Amenorrhea. Obstet Gynecol. 2012;120(4):1043–57.
Balen AH, et al. Polycystic ovary syndrome: pathophysiology and management. BMJ. 2016;355:i6884.
World Health Organization. Family planning: a global handbook for providers. 2018 update.
Trussell J. Emergency contraception: A last chance to prevent unintended pregnancy. Princeton University; 2019.
Mayo Clinic. Amenorrhea: Symptoms and Causes. [Internet] 2024. Available from: https://www.mayoclinic.org