top of page

Mwandishi:

Dkt. Mangwella S, MD

Mhariri:

Dkt. Peter A, MD

Jumatano, 1 Desemba 2021

Mazoezi ya kibofu cha mkojo

Mazoezi ya kibofu cha mkojo

Mazoezi ya kibofu cha mkojo huimarisha uwezo wa kibofu kutunza mkojo na hivyo kutibu ugonjwa wa kuponyoka kwa mkojo, hali inayotokea sana kwa wanawake waliojifungua au walio kwenye koma hedhi.Je ni sahihi kwangu kufanya mazoezi ya kuongeza uwezo wa kibofu?

Maamuzi ya kufanya mazoezi ya kuimalisha uwezo wa kibofu cha mkojo mara nyingi hutegemea kisababishi na hutumika kutibu tatizo la kushindwa zuia mkojo kutoka au kuponyokwa na mkojo. Kuponyoka kwa mkojo hutokea sana kwa wanawake waliotoka kujifungua na wale walioingia komahedhi.


Aina za kuponyoka kwa mkojo


Kuna aina mbalimbali za kuponyoka kwa mkojo ambazo ni;


Kuponyoka mkojo kutokana na msongo


Msongo kwenye njia za mkojo hutokana na hali yoyote inayoongeza shinikizo ndani ya via vilivyo kwenye tumbo ikiwa pamoja na kibofu mfano kukohoa, kupiga chafya au kucheka huweza pelekea mkojo kuponyoka.


Kuponyoka mkojo kutokana na hamu ya kukojoa


Aina hii hutokea pale unapopata haja kali ya kukojoa na kutokana na kibofu kufanya kazi pasipo kudhibitiwa, unajikuta umekojoa kabla hata ya kufika chooni.


Kuponyoka mkojo kutokana na sababu mbalimbali


Aina hii hutokana na ainambili zilizotajwa hapo awali, yaanikutokana na msongo pamoja na hamu kali ya kukojoa.


Kuponyoka kwa mkojo kutokana na kibofu kujaa


Hutokea pale endapo kibofu kimejaa mkojo kisha kutoka wenyewe licha ya kutouruhusi kutoka.


Njia za kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo


Kabla ya kuanza mazoezi haya, unapaswa kuandika kumbukumbu kwenye kitabu chako cha kumbukumbu kuhusu hali yako ya kukojoa, taarifa unazotakiwa kuwa nazo ni za kila siku zinazohusu muda unapopata hamu ya kukojoa au mkojo unapoponyoka.


Kwa kutumia kumbukumbu hizio, unapofanya mazoezi haya utaweza kufanya vema mazoezi haya na kugundua kama yanakusaidia au la.


Kujiwekea muda wa kwenda haja ndogo

Kwa kutumia kumbukumbu za muda wako wa kwenda haja ndogo, chelewesha kukojoa kwa muda wa dakika 15 kwenye kila unapopata haja. Utaendelea kuongeza muda kwa jinsi wiki zinavyoenda mpaka uhisi kuwa muda unatosha.


Kuchelewesha kukojoa

 • Unapopata hamu ya kwenda haja ndogo, zuia kukojoa kwa muda wa dakika 5 kwanza na kisha kwenda kukojoa. Baada ya hapo unaweza kuendelea ongeza muda huo kwa dakika 10 mpaka pale utakapoweza kuchelewesha kukojoa kwa muda wa masaa 3 hadi 5.

 • Kama hamu inakuwa kali zaidi, jaribu kusahaulisha akili yako kwa kuhesabu namba kwa kurudi nyuma kutoka 100 hadi 1 au kufanya tafakuri wakati unavuta pumzi kwa kina.

 • Ikiwa unashindwa kuzuia kwa muda mrefu zaidi baada ya hizi mbinu, unapaswa kuruhusu mkojo utoke na kisha kufanya hivyo utakapopata haja ndogo nyingine.


Mazoezi ya kegeli

Mazoezi ya kegel ni mazoezi ya kuimalisha sakafu ya nyonga ambayo huimarisha misuli inayosukuma au kuzuia mkojo kutoka. Tafiti zimeonyesha kuwa, kuchanganya mazoezi haya na mazoezi mengine ya kudhibiti mkojo kutoka huleta matokeo mazuri zaidi ya kutibu tatizo la kuponyoka kwa mkojo kwa wanawake. Kwa kawaida mazoezi haya hufanyika kwa kubana misuli inayoruhusu mkojo kutoka kwa sekunde 5 kisha kuachia. Muda wa mazoezi huongezeka taratibu kutoka dakika 5 hadi 10 na kuachia mkojo kisha kuongeza muda. Soma zaidi kwenye Makala ya mazoezi ya kuimalisha sakafu ya nyonga.


Njia zingine za kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo


Ili kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo unaweza fanya mambo yafuatayo;


 • Dhibiti kiwango cha vinywaji unachokunywa haswa vile vinavyoongeza haja ya kukojoa mfano soda, kahawa na chai.

 • Punguza kiasi cha maji unachokunywa kabla ya kulala kama unakojoa mara kwa mara wakati wa usiku

 • Kojoa kabla ya kwenda kulala na mara unapoamka asubuhi

 • Endelea kutunza kumbukumbu za unapopata haja ya kwenda kukojoa na unapokojoa


Mazoezi haya husaidia nini?


 • Mazoezi ya kibofu husaidia

 • Kupunguza muda wa kukojoa kwa siku

 • Kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo mwingi zaidi

 • Kudhibiti haja ya kwenda kukojoa


Matokeo huonekana ndani ya muda gani?


Inaweza kuchukua muda wa hadi wiki 12 kupata matokeo mazuri ya mazoezi haya. Unapaswa kuwa mvumilivu na kuednelea kufanya mpaka utakapopata matokeo unayoyategemea.


Kama utafanya mazoezi haya kwa wiki kadhaa bila kupata matokeo yoyote, unapaswa kuonana na daktari ili kuweza kupatiwa matibabu mengine ikiwa pamoja na dawa au upasuaji.


Umuhimu wa mazoezi haya kwa watoto?


Mazoezi ya kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo yanaweza kutumika kuzuia watoto kukojoa kitandani.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

1 Desemba 2021 18:32:05

Rejea za mada hii:

1. Demaagd, et al. “Management of urinary incontinence.” P & T : a peer-reviewed journal for formulary management vol. 37,6 (2012): 345-361H.

2. Overflow Incontinence. https://www.uofmhealth.org/health-library/uh1227#:~:text=Overflow%20incontinence%20is%20the%20involuntary,feels%20no%20urge%20to%20urinate. Imechukuliwa 29.11.2021

3. Inh N. Tran, et al. Urinary Incontinence. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK559095/. Imechukuliwa 29.11.2021

bottom of page