Imeandikwa na ULY CLINIC
25 Machi 2021 09:28:58
Mkojo kutoka wenyewe
Kushindwa kuzuia mkojo, kwa jina jingine pia la 'mkojo kutoka wenywe' ni dalili inayotokea endapo mkojo unatoka wenyewe bila taarifa.
Kwa kawaida bindamu ana uwezo wa kuzuia mkojo usitoke bila ridhaa, endapo hali hii imetokea, inaweza kuwa ishara ya hali au ugonjwa fulani ndani ya mwili.
Dalili kuu ya mkojo kutoka wenyewe ni kutokwa na mkojo wakati unacheka, kukohoa, kunyanyua vitu vizito, kupiga chafya, kufanya mazoezi ya viungo vya mwili au kushindwa kuzuia mkojo kutoka mara unapohisi hamu ya kwenda haja ndogo au kutokwa na matonetone ya mkojo mara kwa mara,
Mkojo kutoka wenyewe kwa jina jingine inaweza kufahamika kama kuponyoka kwa mkojo. baadhi ya visababishi vimeelezewa hapa chini.
Visababishi
Visababishi vya kitaalamu wa kushindwa kuzuia mkojo ni;
Kuvimba kwa tezi dume
Tezi dume in sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Inaundwa na sehemu mbili ambazo zimeungwanishwa na kufunikwa kwa njee kwa utando wa tishu. Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na chini kidogo ya shingo ya kibofu cha mkojo.
Kikohozi cha muda mrefu
Kikohozi cha mara kwa mara kwa muda mrefu ni kiashiria kuwa kuna ugonjwa wa, virusi au bakteria kwenye mfumo wa hewa wanaosababisha kikohozi. Pata uchunguzi wa kutoka kwa daktari wako endapo mkojo unaponyoka wenyewe wakati unakohoa
Kupiga Chafya mara kwa mara
Wakati unapiga chafya, nguvu nyingi hutumika na hupelekea ongezeko la shinikizo tumboni na misuli ya kibofu inayopelekea mkojo kutoka wenyewe.
Ujauzito
Mabadiliko ya homoni yanayoongeza uzito kwa mtoto huongeza mgandamizo wa kibofu cha mkojo hivyo kusababisha hali ya kushindwa kuzuia mkojo.
Kujifungua
Kujifungua kwa njia ya uke hudhoofisha misuli ambayo inakazi ya kuzuia mkojo kutoka kwa muda fulani. Hali hii huisha kwa mazoezi ya misuli ya sakafu ya nyonga.
Kuchomoza kwa maungo ya ndani ya mwili kupitia uke
Kuchomoza kwa kibofu cha mkojo, mfuko wa kizazi au utumbo au kifuko cha kutunza kinyesi huweza kuambatana na mkojo kutoka wenyewe kwa sababu kuchomoza huku husababishwa na madhaifu ya misuli ya sakafu ya nyonga.
Umri mkubwa
Jinsi mtu anavyozeeka, kuongezeka kwa umri huenda sambamba na kudhoofika kwa misuli mbalimbali ya mwili pamoja na misuli inayodhibiti mkojo kutoka wenyewe.
Koma hedhi
Wanawake wanaofuka komahedhi au walio kwenye koma hedhi wanazalisha kwa kiasi kidogo cha homon estrogen, homon inayofanya kuta za ndani ya kibofu na mrija wa urethra uwe na afya njema. Endapo kuta hizi zikiisha au kuwa dhaifu hupelekea kupata tatizo la mkojo kutoka wenyewe
Saratani ya tezi dume
Saratani ya tezi dume ambayo haijatibiwa huweza pelekea tatizo la mkojo kutoka wenyewe au kutoka mara kwa mara.
Kizuizi
Endapo kuna kizuizi katika njia ya mkojo sehemu yoyote ile, kizuizi hiko huzuia mkojo kutoka kirahisi na hivyo kusababisha mkojo kutoka wenyewe na mara kwa mara
Madhaifu ya mfumo wa fahamu(neva)
Madhaifu ya mfumo wa neva kama vile ugonjwa wa Multiple sclerosis, Parkinson's , kiharusi, saratani ya ubongo au uti wa mgongo huweza kuharibu mishipa ya fahamu inayosababisha kudhibiti mkojo kutoka na hivyo kupelekea mkojo kutoka wenyewe.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba' chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
7 Februari 2022 19:28:51
Rejea za mada hii
1 .Wolfgang Fischer,Acta obstetricia et gynecological scandinavica 62 (6), 579-583,1983
2. USA Gilpin, JA Gosling, ARB Smith, DW , WarrellBJOG:An international journal of obstetrics &Gynecology 96(1), 15-23, 1989.
3. Barbara Pieper, Virginia Cleland, David E Johnon, Jodie Lee O’ ReilyImage: the journal of Nursing Scholarshp 21 (4), 205209, 1989