Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter Mangwella
12 Juni 2021 14:38:36
Kichomi cha kifua
Kichomi ni maumivu makali, ya ghafla na yanayotokea na kupotea ndani ya muda mfupi sana (hudumu kwa sekunde chache). Kichomi kinapotokea, humfanya mtu aache kufanya kile alichokuwa anafanya na huweza tokea muda wowote ikiwa umepumzika au unafanya shughuli zako.
Kwa kawaida vichomi vinaweza kutokea sehemu yoyote ile ya mwili, na pia maumivu yanaweza kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa haraka sana mithiri ya kupigwa shoti ya umeme.
Makala hii imeandikwa makusudi kuelezea visababishi vya vichomi kifuani. Kumbuka, maumivu ya kichomi hudumu kwa sekunde chache, endapo una maumivu yanayodumu kwa muda mrefu, tafadhali soma visababishi vingine katika makala ya maumivu ya kifua kupata uelewa zaidi.
Nini husababisha vichomi kifuani?
Hali na matatizo yafuatayo vinaweza kuwa visababishi vya kichomi kifuani;
Matatizo ya moyo
Wasiwasi uliopitiliza na mshiko wa hofu
Matatizo ya kifua na upumuaji
Mgandamizo, kuteguka kwa misuli au maumivu ya mifupa ya kifua
Prikodio kachi Sindromu (SKS)
Kucheua tindikali
Kucheua tindikali
Kucheua tindikali ni udhaifu unaotokana na kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa kwa koki inayoruhusi chakula kuingia tumboni. Koki hii huwa na tabia ya kufunguka ili kuruhusi chakula kiingie ndani ya tumbo na haitakiwi kuruhusu chakula kurudi nyuma, yaani kutoka kwenye tumbo kwenye kwenye umio hadi mdomoni. Koki inaporuhusu vilivyomo tumboni kurudi nyuma, tindikali za tumbo huunguza njia ya juu ya chakula yaani umio na koo hivyo kuambatana na dalili ya kiungulia au maumivu ya chembe ya moyo na kichomi. Kwa maelezo zaidi kuhusu dalili zingine zinazoambatana na kucheua tindikali au kiungulia na matibabu soma kwenye makala za ulyclinic kupitia link hizi.
Sindromu ya prikodio kachi (SPK)
Sindromu ya prikodio kachi huonyesha dalili ya maumivu makali ya kuchoma na kisu(mshale) kwenye sehemu ndogo tu ya kifua, mara nyingi hutokea wakati wa kuvuta hewa wakati mtu amepumzika au anapotaka kubadilisha pozi la kukaa au kulala.
Kichomi cha SPK hakitakiwi kuwa cha kuogopesha kwa kuwa hupotea ndani ya sekunde au dakika chache na hakina mahusiano na matatizo ya mapafu au moyo. Sifa zingine za kichomi hiki ni hutokea kwa vijana wadogo na umri wa kati, na mara chache kwa watu wenye umri mkubwa pia huweza kupata, maumivu huongezeka wakati wa kuvuta hewa, hupotea haraka ndani ya sekunde 30 hadi dakika 3, huamshwa sana na wasiwasi au hofu iliyopitiliza na huwa hakiambatani na dalili zingine.
.
Visababishi vya SPK hudhaniwa
Kubanwa kwa mishipa ya fahamu
Degedege la misuli ndani inayofunika kifua
Ukipata SPK hutahitaji matibabu, isipokuwa endapo dalili ni endelevu au zinatokea mara kwa mara, utahitajika kufika hospitali kwa uchunguzi zaidi.
Mgandamizo, kuteguka kwa misuli au maumivu ya mifupa ya kifua
Mgandamizo mkubwa kwenye misuli au mifupa ya kifua (mbavu)hupelekea mgandamizo kwenye mishipa ya fahamu kisha kuleta maumivu makali ya ghafla kwenye kifua. Mgandamizo unaweza kutokana na majeraha pamoja na kuvia damu kwenye mbavu au nyama zinazotengeneza kifua.
Visababishi vya majeraha kifuani vinaweza kuwa tatizo la fibromyalgia, kuvunjika kwa mbavu au kuvilia damu kwenye mbavu, michomo katileji za mbavu au maambukizi kwenye mbavu na katileji zake na vihatarishi vinaweza kuwa kubeba vitu vizito au kuangukia kifua.
Matatizo ya kifua na upumuaji
Matatizo ya mapafu na upumuaji huweza pelekea dalili ya maumivu makali ya y a ghafla, baadhi ya matatizo yaneweza kuhitaji matibabu ya haraka, endapo una dalili ya maumivu ya kifua yanayoongezeka jinsi unavyovuta pumzi kwa kina au yanayoambatana na kukohoa, onana na daktari kwa uchunguzi zaidi.
Visababishi vya kichomi kutokana na matatizo ya kifua au mfumo wa upumuaji ni;
Maambukizi kwenye mapafu
Shambulio la pumu
Nimonia
Michomo ya kuta za ndani ya mapafu
Embolizimu ya pulmonari
Kubomoka kwa mapafu
Kuongezeka kwa shinikizo la damu kwenye mapafu. (shinikizo la juu la palimonari)
Wasiwasi uliopitiliza na mshiko wa hofu
Wasiwasi uliopitiliza na mshiko wa hofu husababisha pia maumivu makali ya kifua. Matatizo haya ya kiakili yanaweza kutokea bila sababu yoyote ile, hata hivyo baadhi ya watu hutokea kutokana na tatizo la msongo wa mawazo au kuumizwa hisia. Dalili zngine mbali na kichomi zinazoweza tokea ni;
Kuishiwa pumzi
Mapigo ya moyo kasi au kupiga kwa nguvu
Kizunguzungu
Kutokwa jasho
Kutetemeka
Ganzi miguuni au mikononi
Kuzimia
Matatizo ya moyo
Kadiomayopathi
Ni ugonjwa wa moyo, unaweza kuwa wa kurithi au kutokea baada ya kuzaliwa na huambatana na dalili za moyo kuferi kama kuvilia damu, kushindwa kupumua, kujaa kwa maji tumboni, kuvimba miguu n.k
Kuchanika kwa mshipa mkuu wa aota
Hii hutokea kutokana na udhaifu wa mshipa wa aota, tatizo linapotokea huwa na maumivu makali sana ya kifua na yanayodumu, dalili zingine ni kushuka kwa shinikizo la damu na hatimaye kifo kama mgonjwa asipofika haraka hospitali.
Mayokadaitiz
Ni ugonjwa wa misuli ya moyo (mayokadia) ambapo mara nyingi husababishwa na maambukizi ya virusi. Tatizo linapokuwa sugu huweza kuambatana na dalili za moyo kuferi
Perikadaitiz
Huzalisha maumivu makali ya ghafla yanayodumu kwa muda mfupi na huwa makali zaidi unapovuta pumzi. Husababishwa na michomo kwenye ukuta wa perikadia.
Matatizo mengine ya moyo
Matatizo mengine yanayoweza kuambatana na maumivu ya kifua yasiyo makali na kudumu kwa sekunde chache ni;
Mshituko wa moyo
Mshituko wa moyo wanapopata huwa hauleti dalili ya kichomi, bali dalili ya maumivu yaliyo butu yanayoambatana na hisia za mgandamizo au kubanwa na kitu kizito kifuani au kuhisi maumivu ya kuungua ndani ya kifua.
Maumivu ya shambulio la moyo pia huwa na sifa zingine za kudumu kwa dakika kadhaa au zaidi, na yaliyosambaa, hivyo ni ngumu kusema maumivu yalikuwa sehemu hii ya kifua. Baadhi ya watu maumivu huhamia kwenye taya au shingoni au bega la kushoto au kwenye kidole kidogo mkono wa kushoto.
Dalili za hatari
Kama una maumivu yanayoambatana na dalili zifuatazo pata uchunguzi wa haraka kwa daktari wako;
Kutokwa jasho
Kichefuchefu
Maumivu yanayosambaa shingoni au kwenye taya
Maumivu yanayosamba akwenye mabega, mikono au mgongoni
Kizunguzungu au kuhisi kichwa chepesi
Kuishiwa pumzi
Kuzimia au mapigo ya moyo kupiga kwa nguvu
Uchochovu mkali
Anjaina
Maumivu yake hufanana na maumivu ya shambulio la moyo, na hutokana na kuziba kwa mishipa ya damu inayolisha moto.
Magonjwa mengine
Madhaifu mengine yanayoweza kusabaisha maumivu ya kifua yanayofanana na kichomi ni;
Mkanda wa jeshi maeneo ya kifua
Degedege la misuli ya kifua
Mawe kwenye kibofu cha nyongo
Michomo kwenye kongosho
Madhaifu ya umezaji chakula
Nini cha kufanya unapotapa kichomi?
Baada ya kupata kichomi, fahamu kisababishi ni nini, endapo kisababishi ni sababu za kawaida basi haina haja ya kuhofu, endapo kisababishi si cha kawaida, pata matibabu na fuata ushauri wa daktari wako. Unashauriwa kusoma zaidi visababushi vya maumivu ya kifua kwa uelewa zaidi sehemu nyingine katika tovuti ya ulyclinic.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021 04:52:39
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Pericarditis. nhs.uk/conditions/pericarditis/. Imechukuliwa 12.06.2021
2. Is your chest pain a sign of a heart attack, or something else?. healthtalk.unchealthcare.org/is-your-chest-pain-a-sign-of-a-heart-attack-or-something-else/. Imechukuliwa 12.06.2021
3. Hsia RY, et al. A national study of the prevalence of life-threatening diagnoses in patients with chest pain.10.1001/jamainternmed.2016.2498. Imechukuliwa 12.06.2021
4. Chest pain that isn’t caused by a heart attack.
healthcare.utah.edu/the-scope/shows.php?shows=0_w2kx6v18. Imechukuliwa 12.06.2021
5. Am I having a panic attack or a heart attack?. adaa.org/living-with-anxiety/ask-and-learn/ask-expert/how-can-i-tell-if-i%E2%80%99m-having-panic-attack-or-heart-atta. Imechukuliwa 12.06.2021
6. Acid reflux.patients.gi.org/topics/acid-reflux/. Imechukuliwa 12.06.2021
7. Myocarditis and Pericarditis Following mRNA COVID-19. https://www.cdc.gov/coronavirus/2019-ncov/vaccines/safety/myocarditis.html#. Imechukuliwa 12.06.2021
8.Mayo Clinic. Myocarditis - Symptoms and causes - https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/myocarditis/symptoms-causes/syc-20352539. Imechukuliwa 12.06.2021