Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
19 Juni 2021, 11:30:24

Kucheua nyongo
Kucheua nyongo hutokea endapo nyongo iliyohifadhiwa ndani ya kibofu cha nyongo itaingia tumboni na kubaki humo au kupita kwenye umio kisha kutoka kinywani mithiri ya majimaji au matapishi.
Kucheua nyongo huweza kusababisha tatizo la kucheua tindikali ambalo linasababisha michomo kwenye umio na kinywa.
Matibabu ya kucheua nyongo huhusisha kubadili mtindo wa maisha na chakula au upasuaji endapo tatizo ni kubwa.
Dalili ambatwa
Dalili za kucheua nyongo mara nyingi hufanana na dalili za kucheua tindikali, hii inafanya vigumu sana kutofautisha dalili hizi mbili na wakati mwingine hutokea kwa pamoja. Endapo una tatizo la kucheua nyongo, dalili zifuatazo zinawea ambatana;
Maumivu ya chembe ya moyo yanayoweza kuwa ya kawaida au makali zaidi
Kiugulia cha mara kwa mara kinachoweza kusambaa kwenye koo
Ladha ya uchachu kwenye midomo
Kichefuchefu
Kutapika matapishi ya rangi ya kijani yanayoelekea njano
Kwa baadhi ya watu kupotea kwa sauti kutokana na kuungua kwenye boksi la sauti
Kukohoa baadhi ya nyakati
Kupungua uzito bila sababu
Wakati gani wa kutafuta msaada wa daktari?
Ni muhimu ukatafuta msaada wa daktari endapo una cheua nyongo pamoja na dalili zifuatazo;
Dalili za kucheua tindikali kutoisha- hii inaweza kuashiria unacheua nyongo pia
Dalili kuwa kali zaidi
Fiziolojia ya kuachiliwa kwa nyongo kutoka kwenye kibofu cha nyongo
Kwa kawaida nyongo inapozalishwa na ini, huingia kwenye kibofu cha nyongo kinachokaa mkabala na ini kupitia mirija maalumu. Nyongo hii hukaaka humo mpaka pale chakula kutoka tumboni kitakaporuhusiwa kuingia sehemu ya utumbo mwembamba iitwayo duodenamu kwa kuruhusiwa na koki ya pailoriki. Koki ya pailoriki huruhusi chakula kiasi kidogo tu kuingia kwenye duodenum ili kikutane na kuchanganyika na nyongo tayari kwa kumeng’enywa. Endapo kozi hii ya pailoriki inafunguka kwa muda mrefu, huruhusu nyongo kutoka kwenye duodenamu na kuingia tumboni.
Nyongo inatokaje tumboni kwenda kwenye umio au kuonekana mdomoni?
Endapo fiziolojia iliyoelezewa hapo juu imeenda vibaya na nyongo imeingia tumboni, nyongo hii huweza kufika kwenye umio au kinywa kupitia koki ya chini ya esofajio iliyo kati ya umio na tumbo. Koki ya chini ya esofajio endapo haifanyi kazi yake vema, huruhusu vilivomo tumboni kuingia kwenye umio na hivyo kusabisha kucheua. Fiziolojia ya kawaida ya ufanyaji kaziwa koki ya esofajio ni kwamba, inafunguka tu endapo kuna chakula kwenye umio ili kukiruhusu kuingia tumboni na hufunga endapo hakuna chakula kwenye umio kufanya kazi kinyume na hapo huleta tatizo la kucheua tindikali au kucheua nyongo
Visababishi
Upasuaji wa tumbo
Upasuaji wa tumbo unaweza kuleta madhaifu ya koki ya esofajio na pairoliki mfano upasuaji wa kutoa sehemu ya tumbo au tumbo lote au upasuaji wa kuchepuka tumbo
Vidonda vya tumbo
Vidonda vya tumbo huunguza koki ya pailoriki na kufanya isiweze kufunguka au kufnaya kazi yake kama inavyotakiwa.
Upasuaji wa kibofu cha nyongo
Tafiti zinaonyesha, wagonjwa ambao wamefanyiwa upasuaji wa kutoa kibofu cha nyongo wanapata dalili za kucheua tindikali sana kuliko wale wenye kibofu cha nyongo.
Utambuzi
Baada ya kuulizwa maswali kuhusu dalili zako na kufanyiwa uchunguzi wa awali na daktari, vipimo vifuatavyo vinaweza agizwa kufanyika;
Kipimo cha endoskopi
Ni kipimo cha kuangalia ndani ya umio tumbo na utumbo lengo ni kuangalia endapo kuna ishara ya michomo na ukubwa wa tatizo, kuchukua nyama ya kipimo na kupanga matibabu.
Kipimo cha tindikali
Hutumika kupima muda gani na kiasi gani cha tindikali kinaingia kwenye umio, kipimo hiki kinaweza kutofautisha kati ya kucheua tindikali na kucheua nyongo. Kipimo hiki hufanyika pia kwa msaada wa endoskopi.
Matibabu
Matibabu ya kucheua nyongo ni magumu kufanikiwa kirahisi hivyo nzuri na inayofanya kazi vema ni kubadili mtindo wa maisha na chakula.
Matibabu ya dawa
Matibabu ya upasuaji
Matibabu ya kubadili mtindo wa maisha
Dawa
Dawa zinazotumika kutibu kucheua nyongo ni;
Ursodeoxycholic acid.
Sucralfate
Bile acid sequestrants
Upasuaji
Upasuaji wa kuchepusha nyongo- huleta kufanya nyongo imwakike mbali na utumbo wa duodenum ili isiweze kucheuliwa kirahisi
Upasuaji wa kuimarisha koki ya chini ya esofajio
Madhara ya kucheua nyongo
Madhara ya kucheua nyongo ni;
Michomo mcheuo tumboni
Michomo mcheuo tumboni inahusishwa kuambatana na saratani ya tumbo katika tafiti mbalimbali. Hata hivyo si watu wote wanaocheua nyongo hupata saratani. Endapo unapata dalili hii pata matibabu ili kuzuia madhara.
Kucheua tindikali
Kucheua tindikali huongeza hatari ya kuchoma umio na hivyo kuleta dalili za maumivu ya chembe ya moyo na kiungulia.
Umio la barett
Umio la barett ni madhara ya kuchomwa na tindikali kwa muda mrefu sana katika sehemu ya chini ya umio na hiyo kusababisha vidonda na uvimbe suguwenye hatari ya kubadilika kuwa saratani.
Saratani ya umio
Kuna mahusiano kati ya saratani ya umio na kucheua tindikali yaliyoonekana kwenye tafiti. Saratani ya umio inaweza isigunduliwe mapema mpaka pale itakapokuwa kwneye hatua za mwisho.
Matibabu ya nyumbani na kubadili mtindo wa maisha
Mambo yafuatayo yanaweza kupunguza au kuondoa kupata dalili za kucheua tindikali na nyongo;
Acha kuvuta sigara
kuacha kuvuta sigara kutapunguza kiwango cha tindikali zinazozalishwa tumboni.
Kula mlo kidogo na mara nyingi badala ya kula mlo mkubwa mara moja
Hii itapunguza shinikizo kwenye koki ya chini ya esofajio kisha kufanya isifunguke kabla ya wakati hivyo kuzuia kucheua vilivyomo tumboni
Kaa wima wakati unakula na subiri kwa masaa mawili hadi matatu kabla ya kulala
Hii itaipa muda tumbo kumeng’enya chakula na kuzuia usicheua
Punguza vyakula vya mafuta
Hii itasaidia kufanya koki ya chini ya esofajio kutofunguka muda mwingi na kupunguza kiwango cha chakula kinachotoka tumboni
Zuia kula vyakula vinavyoongeza uzalishaji wa tindikali
Kama vyakula vyenye minti, vyakula vyenye kaboni, vyakula vichachu na juisi, viungo kwa wingi, vitunguu kwa wingi au nyanya kwa wingi.
Punguza au acha kunywa pombe
Hii itasaidia koko ya chini ya esofajio isilegee muda mwingi.
Punguza uzito
Inua kitanda chako au tumio mto wakati wa kulala ili kuzuia kucheua wakati umelala
Acha msongo
Tumia njia mbalimbali za kuondoa msongo kama tafakuri- hii itasaidia kupunguza au kuondoa dalili za kucheua tindikali au nyongo.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021, 04:52:44
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases. Acid reflux (GER & GERD) in adults. https://www.niddk.nih.gov/health-information/digestive-diseases/acid-reflux-ger-gerd-adults/all-content. Imechukuliwa 18.06.2021
2. Merck Manual Professional Version. Ambulatory pH monitoring. https://www.merckmanuals.com/professional/gastrointestinal-disorders/diagnostic-and-therapeutic-gastrointestinal-procedures/ambulatory-ph-monitoring. Imechukuliwa 18.06.2021
3. Brunicardi FC, et al., eds. Stomach. In: Schwartz's Principles of Surgery. 11th ed. McGraw-Hill; 2019. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 18.06.2021
4. Caspa Gokulan R, et al. From genetics to signaling pathways: Molecular pathogenesis of esophageal adenocarcinoma. Biochimica et Biophysica Acta. Reviews on Cancer. 2019; doi:10.1016/j.bbcan.2019.05.003.
5. Uptodate. Fass R. Approach to refractory gastroesophageal reflux disease in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 18.06.2021
6. Guirat A, et al. One anastomosis gastric bypass and risk of cancer. Obesity Surgery. 2018; doi:10.1007/s11695-018-3156-5.
7. Hall JE. Propulsion and mixing of food in the alimentary tract. In: Guyton and Hall Textbook of Medical Physiology. 13th edition. Elsevier; 2016. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 18.06.2021
8. Hammer GD, et al., eds. Gastrointestinal disease. In: Pathophysiology of Disease: An Introduction to Clinical Medicine. 8th ed. McGraw-Hill; 2019. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 18.06.2021
9. McCabe ME, et al. New causes for the old problem of bile reflux gastritis. Clinical Gastroenterology and Hepatology. 2020 doi:10.1016/j.cgh.2018.02.034.
10. Rakel D, ed. Gastroesophageal reflux disease. In: Integrative Medicine. 4th ed. Elsevier; 2018. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 18.06.2021
11. Townsend CM Jr, et al. Stomach. In: Sabiston Textbook of Surgery: The Biological Basis of Modern Surgical Practice. 20th ed. Elsevier; 2017. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 18.06.2021