top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

20 Agosti 2026, 05:09:52

shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.
Maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa

Maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa

Hisia za maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa huwapata watu wengi duniani na mara nyingi husababishwa na hali au magonjwa yanayozuilika na kutibika mfano haja ngumu, mpasuko njia ya haja kubwa, bawasiri, kuchomoza kwa puru, kaswende, klamidia, kuhara, n.k. Upatwapo na dalili hii wasiliana na daktari kwa uchunguzi na tiba.


Visababishi vya maumivu wakati wa kutoa hajakubwa

  • Mpasuko kwenye njia ya haja kubwa

  • Bawasiri

  • Haja ngumu

  • Kuchomoza kwa puru

  • Kuhara

  • Ugonjwa wa Michomo kinga kwenye matumbo (IBD)

  • Endometriosis

  • Kaswende au klamidia

  • Saratani ya puru

  • Maambukizi ya kirusi cha HPV


Wakati gani wa kuonana na daktari kama una maumivu wakati wa haja kubwa?

Onana na daktari mara moja kwa uchunguzi wa kisababishi cha tatizo lako endapo unapata dalili zifuatazo;

  • Maumivu wakati wa kutoa haja kubwa yanayodumu zaidi ya wiki moja

  • Kutokwa na damu njia ya haja kubwa kunakodumu zaidi ya wiki moja

  • Kupatwa na homa au uchovu usio wa kawaida

  • Kutokwa na uchafu usio wa kawaida wakati unatoa haja kubwa

  • Maumivu wakati wa kushiriki ngono haswa endapo umepata mpenzi mpya au una wapenzi wengi

  • Maumivu makali ya kubana ya mgongo au tumbo

  • Kuonekana kwa uvimbe mpya kwenye njia ya haja kubwa


1. Mpasuko kwenye njia ya haja kubwa

Mpasuko huu unaweza kutokana na kupitisha kinyesi kigumu na mara nyingi huambatana na damu kidogo kwenye kinyesi.


Dalili

  • Kuonekana kwa mpasuko kwenye tundu la haja kubwa

  • Kuota kwa ngozi eneo lenye mpasuko

  • Maumivu makali kwenye njia ya haja kubwa wakati wa kupitisha kinyesi

  • Kupata damu kwenye kishu utakayotumia kufuta njia ya haja kubwa baada ya kumaliza haja

  • Muwasho njia ya haja kubwa

  • Hisia za kungua kwenye maeneo yanayozunguka njia ya haja kubwa


Mara nyingi mpasuko njia ya haja kubwa huwa hauhitaji matibabu na unaweza isha bila kupata matibabu.


Matibabu

Unaweza kufanya mambo kadhaa ili kupona haraka,

  • Kwanza kutumia dawa za kulainisha haja kubwa au kula chakula chenye nyuzinyuzi kwa wingi pamoja na maji ya kutosha

  • Pili, kalia maji ya uvuguvugu yenye detol kwa muda wa dakika 20 mara mbili kila siku kwa muda wa siku 5

  • Tatu, kama muwasho unaendelea unaweza kupaka dawa jamii ya hydrocortisone ili kuondoa muwasho na muchomo kutokana na maambukizi kwenye njia ya haja kubwa

  • Nne, kama maumivu yanaendelea, tumia dawa za kupaka kwa ajili ya kupunguza maumivu


2. Bawasili

Bawasili kwa jina jingine hutokana na kuvimba kwa mishipa ya damu ndani ya puruna njia ya haja kubwa, mara nyingi hutokana na kuongezeka kwa shinikizo kwenye mishipa ya maeneo haya.


Dalili

Dalili kuu ni ni maumivu wakati wa kutoa haja kubwa pamoja na;

  • Muwasho mkali na maumivu njia ya haja kubwa

  • Uvimbe kwenye njia ya haja kubwa unaouma na kuwasha

  • Kutokwa na majimaji njia ya haja kubwa

  • Kuona damu kwenye tishu unapojisafisha njia ya haja kubwa baada ya kumaliza haja kubwa


Matibabu ya nyumbani

Unaweza kujitibu bawasiri mwenyewe nyumbani kwa njia zifuatazo;

  • Kuoga maji ya uvuguvugu kwa muda wa dakika 10 kila siku ili kupuguza maumivu

  • Paka dawa za kuzuia muwasho na hisia za kuungua njia ya haja kubwa

  • Kula mlo wenye nyuzinyuzi kwa wingi kama mboga za majani, nafaka zisizokobolewa na vyakula vyenye majimaji kwa wingi.

  • Tumia dawa nyongeza za kuongeza nyuzinyuzi kwenye tumbo

  • Kalia maji ya uvuguvugu yaliyotiwa deto kwa muda wa dakika 20 mara mbili kwa siku

  • Safisha vema njia ya haja kubwa mara baada ya kujisaidia na wakati unaoga, tumia sabuni zisizo na marashi na safisha taratibu( soma zaidi njia za kiafya ya kusafisha njia ya haja kubwa)

  • Tumia tishu laini kama unapendelea kutumia tishu kujifuta njia ya haja kubwa baada ya haja

  • Kanda njia ya haja kubwa kwa barafu kama kuna uvimbe kwenye njia hiyo

  • Tumia dawa za kupaka kuzuia maumivu, muwasho kama ibuprofen, naproxen n.k


Kama hali bado inaendelea zaidi ya wiki mbili licha ya kufanya mambo yaliyoainishwa hapo juu, utapaswa kuonana na daktari kwa ushauri na tiba zaidi


3. Haja ngumu

Haja ngumu hufahamika pia kama konstipesheni hutokea endapo unapata shida kupitisha kinyesi kutokana na kinyesi kigumu au kutopata kinyesi chini ya mara tatu kwa wiki.


Dalili

Dalili kuu ni kupata maumivu wakati wa kupitisha kinyesi na zingine ambazo ni;

  • Kupata haja kubwa ngumu, iliyokauka na inayotoka kama golori au vipande vidogodogo vilivyoungana

  • Maumimu ya tumbo wakati wa kujisaidia

  • Hisia za kutaka kujisaidia mara baada ya kumaliza haja kubwa

  • Tumbo kujaa gesi kuuma

  • Maumivu nyumba ya mgongo wa chini

  • Hisia za kitu kimeziba utumbo


Matibabu ya nyumbani

Unaweza kujitibu nyumbani kwa kufanya mambo yafuatayo

  • Kunywa maji ya kutosha angalau glasinane kwa siku

  • Punguza kutumia kahawa na pombe

  • Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi kwa wingi au kunywa vidonge vya nyuzinyuzi ili kulanisha haja kubwa

  • Kunywa maziwa mtindi

  • Punguza kula vyakula vinavyokausha haja kubwa kama vile kula nyama kila siku

  • Kufanya mazoezi angalau dakika 30 kwa siku kama kutembea, kuogelea kukimbia, kucheza mziki n.k

  • Jisaidia mara unapopata hamu ya kutoa haja kubwa

  • Tumia dawa za kulainisha njia utumbo baada ya kuongea na daktari wako


4. Kuchomoza kwa puru

Hutokea pale endapo kuta za ndnai ya njia ya hajakubwa zimechomoza nje kisha kupata michomo ya kingaya mwili. Ni dalili inayotokea sana kwa watu wenye maambukizi ya magonjwa ya zinaa, wanaopata matibabu ya saratani kwa mionzi, magonjwa ya michomo kwenye utumbo mfano vidonda vya kolaitiz n.k


Dalili

  • Dalili kuu ni maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa pamoja na;

  • Kuharisha

  • Kutokwa damu wakati wa kujisaidia

  • Kutokwa na uteute kama kamasi njia ya haja kubwa

  • Hisia za kutaka kujisaidia haja kubwa mara baada ya kumaliza haja kubwa


Matibabu na kinga

  • Tumia kondomu wakati wa kufanya ngono ili kujikinga na magonjwa ya zinaa

  • Usifanye ngono ya njia ya haja kubwa

  • Usishiriki ngono na mtu mwenye vidonda au uvimbe maeneo ya siri

  • Kunywa antbayotiki au dawa za kupambana na virusi kutibu maambukizi ya bakteria na virusi kama unafikiria una magonjwa ya zinaa baada ya kuwasiliana na daktari wako

  • Kunywa dawa za kuzuia madhara ya matibabu ya mionzi kama mesalamine (Canasa) au metronidazole (Flagyl).

  • Tumia dawa za kulainisha utumbo zinazopatikana kwenye maduka ya dawa muhimu

  • Tumia dawa za kuzuia michomo ya kinga za mwili kwenye puru kama vile mesalamine (Canasa), prednisone (Rayos), infliximab (Remicade)

  • Pata matibabu ya upasuaji ili kuondoa sehemu ya haja kubwa iliyo na shida


Kuhara

Kuharisha hutokea pale endapo unapata choo kilani kama maji zaidi ya mara tatu kwa siku.


Dalili

Mara nyingi kuhara hakusabaishi upate hisia za maumivu njia ya haja kubwa hata hivyo unapopitisha haja kubwa na kujifuta mara nyingi zaidi hupelekea kuanza kupata maumivu wakati w akupitisha haja kubwa.


Unaweza kupata dalili za kuvimba kwa njia ya haja kubwa na michubuko


Dalili zingine ni

  • Kichefuchefu

  • Maumivu ya tumbo

  • Kuishiwa maji

  • Hisia za tumbo kujaa

  • Kupata damu kwenye kinyesi

  • Homa

  • Kupata kinyesi kikubwa


Matibabu na kinga

Matibabu kuhara huhusisha kurejesha kiwango cha maji kilichopotea kwa kunywa au kuwekewa kwenye mishipa. Kama kisababishi ni maambukizi, dawa za antibayotiki hutumika. Unaweza kufanya mambo yafuatayo kujikinga;


Nawa mikono kwa kutumia sabuni na maji safi kabla na baada ya kula

Safisha matunda na pika chakula kiive vema na kukila. Epuka kula masalia ya chakula kabla ya kupashwa.

Usitumie maji ya bomba ambayo hayajatiwa dawa ya kuua vimelea kunywa au kuosha matunda badala yake tumia maji ya kununua kwenye chupa


5. Michomo kinga kwenye matumbo (IBD)

Michomo kinga kwneye matumbo ni ugonjwa unaosababishwa na mwitikio wa kinga za mwili dhidi ya chembe hai za kuta za mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Magonjwa yaliyo kwenye kundi hili ni ugonjwa wa Crohn’s, asaletivu colaitiz, na ugonjwa wa sindromu kuchokozwa tumbo (IBD)


Dalili

  • Dalili kuu ya michomo kwenye matumbo ni maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa pamoja na;

  • Kuharisha

  • Hisia za kuishiwa nguvu

  • Maumivu au kutojihisi cema ndani ya tumbo

  • Kupoteza uzito bila sababu

  • Kupata kinyesi chenye damu

  • Kutojihisi njaa hata kama hujala muda mrefu


Matibabu

Mambo unayoweza kufanya ili kupunguza dalili za muchomo kinga kwenye matumbo

  • Tumia dawa za kuzuia michomo kama, mesalamine (Delzicol), olsalazine (Dipentum)

  • Dawa za kushusha kinga ya mwili kama azathioprine au methotrexate (Trexall)

  • Dawa za kudhibiti mwitikio wa mfumo wa kinga mwilini kama adalimumab (Humira) au natalizumab (Tysabri)

  • Dawa za kuzuia maambukizi kama vile metronidazole (Flagyl)

  • Dawa za kuzuia kuharisha kama vile methylcellulose (Citrucel) au loperamide (Imodium A-D)

  • Dawa za maumivu kama vile acetaminophen (Tylenol)

  • Dawa za kurejesha madini chuma mwilini

  • Vidonge vya calcium au vitamin D kuzuia hatari ya kuwa na mifupa dhaifu

  • Kufanyiwa upasuaji w akuondoa sehemu ya utumbo yenye shida

  • Kula vyakula vyenye maziwa kidogo, nyama kidogo, vyenye nyuzinyuzi kwa wastani na kuwa na kahawa au pombe kwa kiasi kidogo sana


6. Ugonjwa wa klamidia au kaswende

Magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na chlamydia au kisonono huambukizwa kwa njia ya kujamiana. Mtu anaweza kupata magonjwa haya kwa kufanya ngono inayohusisha njia ya haja kubwa. Maambukizi ya kisonono na chlamydia husababisha puru kuvimba na kuwa na maumivu wakati wote au wakati wa kujisaidia


Dalili

Mbali na dalili ya kuvimba puru na maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa dalili zingine ni pamoja na;

  • Hisia za kuungua njia ya haja kubwa

  • Maumivu ya kuungua wakati wa kukojoa

  • Kutokwa na uchafu sehemu za siri

  • Maumivu wakati wa kujamiana


Matibabu

  • Matumizi ya dawa za kutibu kaswende na chlamydia wewe na wote unaoshiriki nao ngono

  • Kuacha kushiriki ngono wakati unatumia dawa za kutibu magonjwa ya zinaa

  • Tumia kondomu wakati unashiriki ngono yoyote ile iwe ya mdomo, uume, uke na puru


7. Endometriosisi

Endometriosis hutokea pale tishu zilizo ndani ya kizazi zimeota sehemu nyingine ya nje ya kizazi. Tishu hizo hufahamika kama endometriamu na huweza kujipandikiza kwenye utumbo mpana na hivyi kupelekea uchokozi wa utumbo huo na kutengeneza makovu kutokana na michomo. Uchokozi wa utumbo na michomo hupelekea dalili ya maumivu wakati wa kutoa haja kubwa.


Dalili

  • Mbali na maumivu wakati wa kutoa haja kubwa, dalili zingine zinazoweza kuonekana kwa mtu mwenye endometriosis ya utumbo mpana ni;

  • Maumivu ya tumbo kipindi cha hedhi

  • Maumivu ya kubana ya tumbo la chini na mgongo kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa hedhi

  • Kuwa na hedhi nzito

  • Maumivu wakati wa kushiriki ngono au baada ya ngono

  • Ugumba


Matibabu

  • Matumizi ya dawa za maumivu kama ibuprofen

  • Matumizi ya gonadotropin-releasing hormone (GRNH) kudhibiti ukuaji wa tishu kwa kuzuia uzalishaji wa estrogen

  • Matumizi ya dawa za uzazi wa mpango jamii ya medroxyprogesterone

  • Tiba ya upasuaji wa mionzi kupunguza tishu zilizokua

  • Upasuaji wa kuondoa kizazi na mirija yake pamoja na ovari. Hufanyika kama tiba ya mwisho


8. Saratani ya puru

Ni nadra sana kwa saratani ya puru kuwa miongoni mwa sababu ya maumivu ya njia ya haja kubwa wakati wa kupitisha kinyesi licha ya kuweza kusababisha dalili hii.


Dalili

  • Mbali na dalili ya maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa, dalili zingine ni

  • Kubadilika ghafla kwa umbile la kinyesi na rangi yake

  • Kupitisha kinyesi kidogo na chembemba

  • Damu kwenye kinyesi au tishu unayojifutia baada ya kumaliza haja kubwa

  • Kuota uvimbe mpya au usio wa kawaida unaouma unapoukandamiza

  • Muwasho maeneo ya kuzunguka njia ya haja kubwa

  • Kutokwa uchafu usio wa kawaida kwenye njia ya haja kubwa

  • Kuharisha mara kwa mara au kupata hajangumu

  • Kuishiwa nguvu

  • Tumbo kujaa gesi na kubeua

  • Kupungua uzito

  • Maumivu ya tumbo ya kudumu


Matibabu

Unapaswa kuonana na daktari kwa uchugnuzi na tiba endapo unapata dalili zilizoorodheshwa hapo juu kwa uchunguzi na tiba. Matibabu yanaweza kuhusisha;


9. Dawa za kuua chembe za saratani

Upasuaji wa kuondoa saratani na kuzuia kusambaa kwa saratani sehemu zingine za mwili

Matibabu ya mionzi


10. Maambukizi ya kirusi cha human papilloma (HPV)

Kirusi cha Human papilloma (HPV) huweza kusababisha sunzua kubwa maeneo karibu na njia ya haja kubwa, kwenye maeneo ya siri, mdomoni na kwenye koo. Sunzua kwenye njia ya haja kubwa zinaweza kuchokozwa na kinyesi hivyo kuleta dalili ya maumivu wakati wa kutoa haja kubwa.


Baadhi ya virusi vya HPV huweza kusababisha saratani kama usipopata matibabu. Unaweza kujikinga na maambukizi haya kwa;

  • Kupata chanjo ya kirusi

  • Kutumia kondomu wakati wa kushiriki ngono

  • Kufanya kipimo cha Pap smear kama unashiriki ngono mara kwa mara


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara kuhusu maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa

1. Mtu akiwa na maumivu kwenye njia ya haja kubwa wakati wa kujisaidia na kinyesi ni kilaini, ni maambukizi au hali ya kawaida tu?

Si lazima iwe maambukizi. Maumivu yanaweza kutokea hata kama kinyesi ni kilaini, kwa mfano kutokana na mpasuko mdogo kwenye njia ya haja kubwa, bawasiri, muwasho au michubuko ya ngozi inayozunguka tundu la haja kubwa. Hali hii inaweza kutokea hasa kama mtu amekuwa akijisaidia mara nyingi au anajifuta kwa nguvu.


Maambukizi yanawezekana zaidi ikiwa maumivu yanaambatana na dalili nyingine kama kutokwa na ute au usaha, kuwaka kwenye njia ya haja kubwa, damu, vidonda, homa au historia ya kufanya ngono inayohusisha njia ya haja kubwa. Maambukizi ya baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha kuvimba kwa puru na kufanya kujisaidia kuwa na maumivu.


Kwa hiyo, kinyesi kuwa kilaini hakutoshi kuamua kwamba tatizo ni la kawaida wala kwamba ni maambukizi. Ikiwa maumivu yanaendelea, yanazidi au yanaambatana na damu, uchafu au vidonda, uchunguzi wa daktari unahitajika ili kutambua chanzo.

2. Kwa nini ninaumia wakati wa kujisaidia lakini nikimaliza maumivu yanaisha?

Hali hii inaweza kutokea kwa sababu maumivu yanachochewa wakati kinyesi kinapopita kwenye eneo lenye jeraha au muwasho. Mfano unaojulikana ni mpasuko mdogo wa njia ya haja kubwa, ambapo kupita kwa kinyesi kwenye eneo hilo kunaweza kusababisha maumivu makali wakati wa kujisaidia.


Maumivu yanayoanza wakati wa kujisaidia na kupungua baada ya kumaliza yanaweza pia kuhusiana na bawasiri au msukumo unaowekwa kwenye tishu zinazozunguka njia ya haja kubwa. Kwa hiyo, muda ambao maumivu hutokea ni taarifa muhimu kwa daktari wakati wa kutafuta chanzo.


Hata kama maumivu yanaisha baada ya kujisaidia, si vizuri kuyapuuza ikiwa yanajirudia mara kwa mara. Maumivu yanayodumu au kujirudia yanaweza kuhitaji uchunguzi wa eneo la haja kubwa ili kubaini tatizo linalosababisha.

3. Maumivu ya njia ya haja kubwa yanaweza kusababishwa na kufanya ngono ya njia ya haja kubwa?

Ndiyo. Ngono ya njia ya haja kubwa inaweza kusababisha michubuko, mpasuko mdogo au kuwasha kwa tishu za eneo hilo, hasa ikiwa kulikuwa na msuguano mkubwa. Maumivu yanaweza kuonekana wakati wa kujisaidia kwa sababu kinyesi kinapopita kwenye eneo lililochubuka.


Pia, ngono ya njia ya haja kubwa inaweza kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya maambukizi ya zinaa yanayoweza kuathiri puru. Maambukizi hayo yanaweza kusababisha maumivu, kuwasha, ute au usaha, damu na wakati mwingine hisia ya kutaka kujisaidia mara kwa mara.


Ikiwa maumivu yalianza baada ya ngono ya njia ya haja kubwa na yanaendelea, hasa kama kulikuwa na mwenza mpya au ngono bila kondomu, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi badala ya kudhani kuwa ni jeraha pekee. Vipimo vya maambukizi ya zinaa vinaweza kuhitajika kulingana na historia na dalili.

4. Kwa nini nahisi kama nataka kujisaidia tena mara tu baada ya kumaliza?

Hisia ya kutaka kujisaidia tena baada ya kumaliza inaweza kutokea wakati puru au sehemu ya mwisho ya utumbo imevimba au imechokozwa. Mtu anaweza kuhisi bado kuna kinyesi ndani hata kama tayari amejisaidia.


Hali hii inaweza kuonekana pamoja na maambukizi yanayoathiri puru, magonjwa ya uchochezi wa utumbo au matatizo mengine yanayosababisha uchokozi wa eneo hilo. Ikiwa hisia hiyo inaendelea mara kwa mara, hasa ikiwa inaambatana na maumivu, ute au damu, inahitaji uchunguzi.


Si lazima hisia hii iwe maana kwamba kuna kinyesi kingi kimebaki tumboni. Wakati mwingine ni mwitikio wa puru iliyochokozwa au iliyovimba.

5. Je, maumivu wakati wa haja kubwa yanaweza kuhusiana na maumivu wakati wa tendo la ndoa?

Ndiyo. Baadhi ya matatizo yanayoathiri eneo la puru na nyonga yanaweza kusababisha maumivu wakati wa kujisaidia pamoja na wakati wa tendo la ndoa. Hii inaweza kutokea kwa sababu viungo hivi viko karibu na vinaweza kuathiriwa na mchakato huo wa ugonjwa.


Kwa wanawake, endometriosis ni mojawapo ya hali zinazoweza kuhusishwa na maumivu wakati wa kujisaidia na maumivu wakati wa tendo la ndoa, hasa ikiwa dalili huwa mbaya zaidi karibu na kipindi cha hedhi. Hata hivyo, si kila mtu mwenye dalili hizi ana endometriosisi.


Maumivu ya aina hii yanayojirudia yanahitaji uchunguzi wa kina kwa sababu yanaweza pia kusababishwa na matatizo mengine ya mfumo wa uzazi, utumbo au njia ya haja kubwa. Kutoa taarifa kuhusu uhusiano wa maumivu na hedhi, tendo la ndoa na kujisaidia kunaweza kumsaidia daktari kuelewa chanzo.

6. Je, damu kidogo kwenye karatasi baada ya kujisaidia ni kawaida?

Damu kidogo inayotokea baada ya kujisaidia inaweza kutokana na matatizo kama bawasiri au mpasuko wa njia ya haja kubwa. Hasa ikiwa damu ni nyekundu na inaonekana kwenye karatasi ya kujifutia au juu ya kinyesi, chanzo kinaweza kuwa karibu na tundu la haja kubwa.


Hata hivyo, damu kutoka njia ya haja kubwa haipaswi kuchukuliwa kuwa ya kawaida kila wakati. Kuna sababu nyingine zinazoweza kusababisha damu, na aina, kiasi, muda na namna damu inavyotokea husaidia kutofautisha visababishi.


Ikiwa damu inajirudia, inaongezeka, inaambatana na maumivu makali, mabadiliko ya tabia ya haja kubwa, kupungua uzito au uchovu usioelezeka, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu badala ya kujitibu kwa muda mrefu bila kujua chanzo.

7. Kwa nini njia ya haja kubwa inawasha na kuuma baada ya kujisaidia?

Muwasho unaweza kusababishwa na ngozi inayozunguka njia ya haja kubwa kuchokozwa na kinyesi, kuhara, unyevu au kujisafisha kwa nguvu. Matumizi ya sabuni zenye manukato au bidhaa zinazokera ngozi yanaweza pia kuongeza muwasho.


Bawasiri na mpasuko wa njia ya haja kubwa ni sababu nyingine zinazoweza kuambatana na maumivu na muwasho. Maambukizi au magonjwa ya zinaa yanaweza pia kuhusika, hasa ikiwa kuna vidonda, uchafu, uvimbe au historia ya ngono inayohusisha eneo hilo.


Ikiwa muwasho unaendelea licha ya kutunza usafi wa eneo hilo au unaambatana na dalili nyingine, ni bora kutafuta chanzo badala ya kutumia dawa za kupaka kwa muda mrefu bila uchunguzi.

8. Je, maumivu wakati wa haja kubwa yanaweza kuwa dalili ya saratani?

Inawezekana, lakini saratani si sababu ya kawaida ya maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa. Kuna sababu nyingi zilizo za kawaida zaidi, kama bawasiri, mpasuko wa njia ya haja kubwa, haja ngumu na muwasho au uchochezi wa eneo hilo.


Wasiwasi wa saratani huongezeka zaidi ikiwa maumivu yanaambatana na dalili kama damu inayojirudia, mabadiliko mapya ya tabia ya haja kubwa, kupungua uzito bila sababu, uchovu usioelezeka, mabadiliko yasiyo ya kawaida ya umbo la kinyesi au uvimbe mpya kwenye eneo la haja kubwa.


Kwa hiyo, mtu hapaswi kuhitimisha kwamba ana saratani kwa sababu tu ana maumivu wakati wa kujisaidia. Lakini dalili zinazoendelea au zinazoambatana na ishara za tahadhari zinapaswa kuchunguzwa mapema.

9. Nimekuwa na maumivu wakati wa kujisaidia kwa muda mrefu lakini sina damu, je, bado ninahitaji kumuona daktari?

Ndiyo, hasa ikiwa maumivu yamekuwa yakijirudia au yamedumu kwa muda mrefu. Kutokuwepo kwa damu hakumaanishi kwamba hakuna tatizo linalohitaji matibabu. Baadhi ya matatizo ya njia ya haja kubwa yanaweza kusababisha maumivu bila damu kuonekana.


Historia ya maumivu inaweza kusaidia sana katika kutafuta chanzo. Daktari anaweza kuuliza kama maumivu huanza kabla, wakati au baada ya kujisaidia, kama yana uhusiano na kinyesi kigumu au kuhara, kama kuna muwasho, uvimbe, ute, homa au kama kuna uhusiano na tendo la ndoa.


Uchunguzi wa mapema ni muhimu hasa pale maumivu yanapoendelea licha ya kubadilisha namna ya kujisaidia au kutunza eneo hilo. Matibabu sahihi hutegemea chanzo, hivyo si vizuri kutumia dawa za aina mbalimbali bila utambuzi.

10. Ni wakati gani maumivu wakati wa kujisaidia yanakuwa ishara ya hatari?

Maumivu yanakuwa ya kuhitaji uchunguzi wa haraka zaidi ikiwa yanaambatana na damu nyingi au inayojirudia, homa, uchafu au usaha kutoka njia ya haja kubwa, uvimbe mpya, maumivu makali ya tumbo au mgongo, kupungua uzito bila sababu au mabadiliko makubwa ya namna ya kupata haja kubwa.


Pia, mtu mwenye maumivu yanayoendelea zaidi ya muda unaotarajiwa kupona au yanayozidi badala ya kupungua anapaswa kufanyiwa uchunguzi. Dalili zinazohusiana na ngono, kama maumivu ya tendo la ndoa, uchafu usio wa kawaida au historia ya ngono bila kinga, zinaweza kuonyesha hitaji la kupima maambukizi ya zinaa.


Kwa ujumla, maumivu wakati wa kupitisha haja kubwa yana sababu nyingi na nyingi zinaweza kutibika. Hata hivyo, kutambua chanzo ni muhimu kwa sababu matibabu ya bawasiri, mpasuko, maambukizi, magonjwa ya uchochezi wa utumbo na matatizo mengine hayafanani. Makala hii inaeleza kuwa dalili hii inaweza kutokana na hali mbalimbali, zikiwemo mpasuko, bawasiri, haja ngumu, kuhara, IBD, endometriosis na baadhi ya maambukizi ya zinaa.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

4 Septemba 2021, 17:33:29

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

​

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada hii:

  1. FDA approves expanded use of Gardasil 9 to include individuals 27 through 45 years old. fda.gov/NewsEvents/Newsroom/PressAnnouncements/ucm622715.htm. Imechukuliwa 04.09.2021

  2. Cleveland clinic. Hemorrhoids. my.clevelandclinic.org/health/diseases/15120-hemorrhoids. Imechukuliwa 04.09.2021

  3. CDC. Human papillomavirus (HPV) treatment and care. cdc.gov/std/hpv/treatment.htm. Imechukuliwa 04.09.2021

  4. Mayo Clinic Staff. Anal fissure. mayoclinic.org/diseases-conditions/anal-fissure/symptoms-causes/syc-20351424. Imechukuliwa 04.09.2021

  5. Mayo Clinic Staff. Constipation. mayoclinic.org/diseases-conditions/constipation/symptoms-causes/syc-20354253. Imechukuliwa 04.09.2021

  6. NIH. Proctitis. niddk.nih.gov/health-information/digestive-diseases/proctitis. Imechukuliwa 04.09.2021

  7. Cleveland clinic. Rectal bleeding. my.clevelandclinic.org/health/symptoms/14612-rectal-bleeding. Imechukuliwa 04.09.2021

  8. Cancer gov. Regorafenib. cancer.gov/about-cancer/treatment/drugs/regorafenib?redirect=true. Imechukuliwa 04.09.2021

  9. Mayo Clinic Q and A: Painful bowel movements may be due to anal fissure. newsnetwork.mayoclinic.org/discussion/mayo-clinic-q-and-a-painful-bowel-movements-may-be-due-to-anal-fissure/%0A/. Imechukuliwa 04.09.2021

  10. CDC. What is inflammatory bowel disease (IBD)?. cdc.gov/ibd/what-is-IBD.htm. Imechukuliwa 04.09.2021

bottom of page