Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
Imeboreshwa:
24 Januari 2026, 16:42:01

Dawa Guaifenesin
Guaifenesin ni dawa inayotumika kutibu kikohozi chenye makohozi, hasa pale ambapo makohozi ni mazito na magumu kutoka. Ni dawa ya kundi la dawa za kulainisha kikohozi, yaani dawa zinazosaidia kulainisha na kupunguza mnato wa makohozi ili yawe rahisi kutoka wakati wa kukohoa.
Hutumika sana katika maambukizi ya njia ya hewa ya juu na ya chini kama vile mafua, homa ya mapafu, bronkaitisi, na hali nyingine zinazosababisha uzalishaji wa makohozi mengi.
Majina ya kibiashara
Majina ya kibiashara ya Guaifenesin ni pamoja na;
Robitussin
Mucinex
Benylin Expectorant
Tussin
Glyceryl guaiacolate
Cheston
Actifed Expectorant (ikiwa mchanganyiko)
Guaifenesin ipo kundi gani la dawa?
Guaifenesin ipo katika makundi yafuatayo;
Dawa za kikohozi
Expectorants (dawa za kutoa makohozi)
Dawa zilizo kundi moja na Guaifenesin
Dawa zenye kazi zinazofanana au karibu na Guaifenesin ni;
Potassium citrate
Ammonium chloride
Sodium citrate
Carbocisteine (kwa kusaidia makohozi, ingawa ni mucolytic)
Fomu za dawa Guaifenesin
Guaifenesin hupatikana katika fomu zifuatazo;
Syrup (kioevu cha kunywa)
Kidonge
Kidonge cha kutolewa taratibu (extended-release tablets)
Poda ya kuchanganywa na maji (katika baadhi ya maandalizi)
Uzito (nguvu ya dawa Guaifenesin)
Guaifenesin hupatikana katika viwango mbalimbali kulingana na fomu;
100 mg
200 mg
300 mg
400 mg
600 mg (ya kufanyakazi muda mrefu)
1200 mg (ya kufanya kazi muda mrefu)
Guaifenesin hutibu nini?
Kikohozi chenye makohozi
Bronkitisi ya muda mfupi au sugu
Mafua yanayoambatana na makohozi
Maambukizi ya njia ya hewa ya juu
Maambukizi ya njia ya hewa ya chini
Hali yoyote yenye makohozi mazito yasiyotoka kirahisi
Namna Guaifenesin inavyofanya kazi
Guaifenesin hufanya kazi kwa kuongeza kiasi cha majimaji kwenye makohozi na kupunguza mnato wake, jambo linalosaidia makohozi kuwa mepesi na rahisi kutoka wakati wa kukohoa.
Dawa hii huchochea tezi za njia ya hewa kuzalisha ute mwepesi zaidi, hivyo kuimarisha ufanisi wa kikohozi chenye makohozi badala ya kikohozi kikavu.
Ufyozwaji wa dawa
Guaifenesin hufyonzwa haraka kupitia mfumo wa chakula baada ya kumezwa.
Huanza kufanya kazi ndani ya dakika 30
Athari hudumu kwa masaa 4–6 (kwa fomu ya kawaida)
Fomu ya kutolewa taratibu hufanya kazi kwa hadi masaa 12
Mwingiliano wa Guaifenesin na chakula
Guaifenesin inaweza kutumika pamoja au bila chakula. Hakuna mwingiliano mkubwa unaojulikana kati ya dawa hii na chakula.
Mwingiliano na pombe
Hakuna mwingiliano mkali uliothibitishwa kati ya Guaifenesin na pombe, lakini pombe inaweza kuongeza kizunguzungu au usingizi, hasa kama dawa ipo kwenye mchanganyiko na antihistamine.
Wagonjwa wasiopaswa kutumia Guaifenesin
Wagonjwa wenye mzio wa Guaifenesin
Watoto wadogo bila ushauri wa mtaalamu wa afya
Wagonjwa wenye kikohozi cha muda mrefu kisichojulikana chanzo (k.m. kikohozi cha TB, saratani, au pumu isiyodhibitiwa)
Utoaji taka wa Guaifenesin mwilini
Guaifenesin hubadilishwa (umetaboli) kwenye ini na hutolewa mwilini hasa kupitia mkojo kama mazao ya umetaboli. Nusu-maisha ya dawa ni mafupi, takribani saa 1.
Matumizi ya Guaifenesin kwa mama mjamzito
Hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonesha madhara kwa mama mjamzito au mtoto, lakini matumizi yake yanapaswa kufanyika chini ya ushauri wa mtaalamu wa afya, hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito(kipindi cha kwanza cha ujauzito).
Matumizi ya Guaifenesin kwa mama anayenyonyesha
Haijulikani kwa uhakika kama Guaifenesin hupita kwenye maziwa ya mama kwa kiwango kikubwa. Tafiti zilizopo hazijaonesha madhara makubwa kwa mtoto, hivyo inaweza kutumika kwa tahadhari.
Dawa zenye mwingiliano na Guaifenesin
Mwingiliano unaohitaji uangalizi
Antihistamines (chlorpheniramine, diphenhydramine)
Dawa za kuzuia kikohozi kikohozi (dextromethorphan, codeine)
Dawa za usingizi au pombe
Mwingiliano mdogo
Paracetamol
Antibiotics nyingi
Bronchodilators (salbutamol)
Maudhi madogo ya Guaifenesin
Kichefuchefu
Kutapika
Maumivu ya tumbo
Kuharisha
Kizunguzungu
Maumivu ya kichwa
Upele au muwasho (nadra)
Ufanye nini kama umesahau dozi yako?
Kama umesahau kutumia dozi yako, tumia mara tu unapokumbuka. Ikiwa muda wa dozi inayofuata umekaribia, ruka dozi uliyosahau na endelea na ratiba yako ya kawaida. Usitumie dozi mbili kwa wakati mmoja.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
24 Januari 2026, 16:42:01
Rejea za mada hii:-
