Tangazo la mwaliko wa kushiriki Utafiti
Unaalikwa kushiriki katika utafiti unaotathmini jukwaa la afya ya kidijitali linalotumia Akili unde (ULY Clinic AI) kwa lugha ya Kiswahili. Jukwaa(tovuti) hili limeundwa kuboresha uelewa wa afya kwa wagonjwa na kusaidia maendeleo endelevu ya kitaaluma kwa wahudumu wa afya wa kada ya kati nchini Tanzania.
Mada ya Utafiti
Uundaji, Utekelezaji, na Tathmini ya Athari ya Jukwaa la Afya ya Kidijitali linalotumia Akili Unde (AI) kwa Kiswahili ili kuongeza uelewa wa Afya miongoni mwa Wagonjwa na Wahudumu wa Afya wa ngazi ya kati nchini Tanzania
Madhumuni ya Utafiti
Lengo la utafiti huu ni kutathmini urahisi wa matumizi, manufaa, na athari za jukwaa la afya la kidijitali linalotumia AI kwa Kiswahili katika:
-
Uelewa wa taarifa za afya miongoni mwa wagonjwa watu wazima
-
Kujifunza na kuimarisha maarifa ya kitaaluma miongoni mwa wahudumu wa afya wa kiwango cha kati
Nani anaweza kushiriki
Wagonjwa
-
Wenye umri wa miaka 18 au zaidi
-
Wanaoweza kusoma na kuelewa Kiswahili
-
Waliowahi kutembelea tovuti ya ULY Clinic au kutumia Msaidizi Akili Unde angalau mara moja
Wahudumu wa Afya ngazi ya kati
-
Wanaofanya kazi kwa sasa nchini Tanzania (mf. wauguzi, maafisa tabibu, wahudumu wa msingi wa afya, wahudumu wa sayansi shirikishi za afya)
-
Wanaoweza kusoma na kuelewa Kiswahili
-
Waliotumia au wanaotarajia kutumia jukwaa la kidijitali la mafunzo la ULY Clinic
Utafiti unalenga kukusanya jumla ya washiriki 380, wakiwemo wagonjwa 190 na wahudumu wa afya ngazi ya kati 190 nchini Tanzania.
Ushiriki unahusisha nini
-
Kusoma taarifa za afya na/au kuwasiliana na Msaidizi Unde kupitia jukwaa la ULY Clinic
-
Kujaza dodoso la mtandaoni kuhusu urahisi wa matumizi, uelewa wa taarifa za afya, na uzoefu wa jumla wa utumiaji.
-
Dodoso litachukua takribani dakika 15–20 kukamilika.
Hatari na Faida
-
Utafiti huu una hatari ndogo sana na hauhusishi matibabu yoyote au afua za kitabibu.
-
Hakuna faida ya moja kwa moja binafsi kutokana na kushiriki katika utafiti huu.
-
Hata hivyo, unaweza kupata faida zisizo za moja kwa moja kama vile kupata taarifa za afya kwa Kiswahili na kujifunza jinsi ya kutumia jukwaa la afya linalotumia AI.
-
Taarifa utakazotoa zitasaidia kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za afya kwa Kiswahili kwa wagonjwa na wahudumu wa afya nchini Tanzania.
Ushiriki wa hiari
Ushiriki wako ni wa hiari kabisa. Unaweza kuchagua kutoshiriki au kujiondoa wakati wowote bila adhabu au kupoteza manufaa yoyote.
Malipo au motisha
Hakuna malipo ya kifedha kwa kushiriki katika utafiti huu.
Wahudumu wa afya wa ngazi ya kati wanaweza kupokea cheti cha kidijitali cha ushiriki.
Usiri wa Taarifa
-
Hakuna taarifa binafsi za utambulisho zitakazokusanywa
-
Majibu yote yatawekwa bila utambulisho na kutumika kwa madhumuni ya utafiti pekee
Jinsi ya Kushiriki
Washiriki wanaostahili wanaweza kujiunga na utafiti kupitia ujumbe wa mwaliko utakaojitokeza kwenye tovuti ya ULY Clinic, machapisho yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya ULY Clinic ikiwemo Facebook na WhatsApp, pamoja na mialiko ya moja kwa moja isiyo ya kulazimisha inayosambazwa kupitia mitandao ya kitaaluma ya wahudumu wa Afya wa ngazi ya kati.
Ushiriki unahusisha kufungua kiungo cha mtandaoni kinachowaelekeza washiriki kwenye ukurasa wa ridhaa ya kielektroniki na dodoso la mtandaoni.
Kurasa ya Ushiriki
Bofya hapa kwenda kwenye dodoso kushiriki utafiti huu.
Ratiba ya Ushiriki
Utafiti umeanza tarehe 20 Januari 2026 na utamalizika Tarehe 20 Januari 2027.
-
Mtafiti Mkuu: Kim Do-Hwan
-
Taasisi: Korea University, Graduate School of Medicine (Medical Education)
-
Mtafiti: Sospeter Benjamin Mangwella
-
Barua pepe: ulyclinic.research@gmail.com
