1. HATI YA MAELEZO YA USHIRIKI WA UTAFITI
Maelezo haya yametolewa kueleza kwa nini utafiti huu unafanyika, jinsi taarifa zako zitakavyotumika, pamoja na faida, hatari au usumbufu wowote unaoweza kutokea kutokana na ushiriki wako. Ikiwa una swali au kuna jambo lolote halieleweki, una haki ya kuuliza kabla ya kuendelea.
1.1 Madhumuni ya Utafiti na Faida Zinazotarajiwa
Watu wengi nchini Tanzania hupata changamoto ya kupata taarifa za afya zilizo wazi na za kuaminika katika lugha wanayoielewa kikamilifu. Utafiti huu unalenga kuunda na kupima jukwaa la afya ya kidijitali linalotumia Akili Unde (AI) kwa Kiswahili ili kusaidia wagonjwa na wahudumu wa afya wa kada ya kati kupata taarifa sahihi na rahisi kueleweka.
Madhumuni ya utafiti huu ni:
Kuunda jukwaa la kidijitali linalotumia lugha rahisi ya Kiswahili na linalotumika kirahisi.
Kupima jinsi jukwaa linavyosaidia kuboresha uelewa wa Afya.
Kulinganisha jinsi wagonjwa na wahudumu wa afya wa kada ya kati wanavyotumia na kunufaika na jukwaa.
Huenda usipate faida ya moja kwa moja binafsi, lakini ushiriki wako utasaidia kuboresha elimu ya afya kwa Kiswahili kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.
1.2 Washiriki, Muda na Taratibu za Utafiti
Utafiti huu unahusisha takribani washiriki 380: wagonjwa watu wazima 190 na wahudumu wa afya wa kada ya kati 190. Muda wa ushiriki kwa kila mshiriki ni takribani dakika 15–20 na unahusisha matumizi ya jukwaa la afya la kidijitali na ujazaji wa dodoso mara moja.
Utafiti unafanyika mtandaoni kikamilifu na hakuna haja ya kufika kituoni.
1.3 Hatari, Faida, na Haki ya Kujiondoa
Utafiti huu una hatari ndogo sana. Hakuna hatari za kimwili. Usumbufu mdogo unaweza kutokea wakati wa kujibu maswali ya dodoso. Taarifa zote zitahifadhiwa bila majina na kwa usalama.
Ushiriki ni wa hiari kabisa. Unaweza kukataa kushiriki au kujiondoa wakati wowote bila madhara yoyote, na taarifa zako zitafutwa endapo utaamua kujiondoa.
Hakuna malipo, fidia, au zawadi zitakazotolewa kwa kushiriki katika utafiti huu.