Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
Imeboreshwa:
23 Januari 2026, 14:00:23

Dawa Ketoprofen
Ketoprofen ni dawa ya kupunguza maumivu, uvimbe na homa, inayotumika sana katika vituo vya afya na hospitali nchini Tanzania. Licha ya matumizi yake kuwa ya kawaida, wagonjwa wengi huitumia bila kuelewa aina ya dawa, hatari zake na nani hapaswi kuitumia.
Makala hii ya ULY CLINIC inalenga:
Kutoa elimu sahihi kuhusu Ketoprofen
Kusaidia jamii kutofautisha matumizi sahihi na hatarishi
Kuwa chanzo cha rejea kwa makala nyingine za dawa za maumivu
Ketoprofen ni Dawa Gani?
Ketoprofen ni dawa kutoka kundi la NSAID.
Kitaalamu:
Hupunguza maumivu
Hupunguza uvimbe
Hupunguza homa
Inafanya kazi kwa kuzuia prostaglandins, kemikali zinazohusika na maumivu na uvimbe mwilini.
Ketoprofen hutumika kutibu nini?
Ketoprofen hutumika kutibu:
Maumivu ya viungo (arthraitis)
Maumivu ya mgongo
Maumivu baada ya upasuaji
Maumivu ya meno
Maumivu ya hedhi
Maumivu ya misuli na majeraha
Haitibu chanzo cha ugonjwa, bali hupunguza dalili.
Fomu na Aina za Ketoprofen
Ketoprofen hupatikana katika:
Vidonge (Tembe/vidonge)
Sindano ( hospitalini)
Jeli au krimu (kwa baadhi ya nchi)
Sindano hutolewa chini ya uangalizi wa mtaalamu wa afya.
Ketoprofen inafanya kazi vipi mwilini?
Huzuia kimeng’enya cyclooxygenase (COX)
Hupunguza uzalishaji wa homoni prostaglandin
Matokeo: maumivu na uvimbe hupungua
Ndiyo maana inaweza kusaidia haraka, lakini pia kuleta madhara kwenye tumbo.
Maudhi na Madhara ya Ketoprofen
Maudhi madogo
Maumivu ya tumbo
Kichefuchefu
Kiungulia
Kizunguzungu
Madhara makubwa:
Vidonda vya tumbo
Kutokwa damu tumboni
Shinikizo la damu kuongezeka
Kuathiri figo
Hatari huongezeka kwa matumizi ya muda mrefu.
Nani hapashwi kutumia Ketoprofen?
Ketoprofen haifai kwa:
Wenye vidonda vya tumbo
Wagonjwa wa figo au ini
Watu wenye pumu inayochochewa na dawa za kundi la NSAID
Wanawake wajawazito (hasa miezi ya mwisho)
Wazee bila uangalizi maalum
Ketoprofen na mwingiliano wa dawa zingine
Ketoprofen inaweza kuingiliana vibaya na:
Aspirin
Dawa nyingine za kundi la NSAID
Dawa za kupunguza damu kuganda( Za kuyeyusha damu)
Pombe
Mchanganyiko unaweza kuongeza hatari ya kutokwa damu.
Matumizi ya Ketoprofen kwa Mjamzito na Mama Anayenyonyesha
Ketoprofen kwa mwanamke Mjamzito
Ketoprofen haipendekezwi kutumiwa bila ushauri wa daktari kwa mwanamke mjamzito, hasa katika:
Kipindi cha tatu cha ujauzito
Inaweza:
Kufunga mapema mshipa wa damu wa mtoto (daktasi ateriosas)
Kusababisha matatizo ya figo kwa mtoto
Kuongeza hatari ya matatizo wakati wa kujifungua
Kipindi cha kwanza na cha pili cha ujauzito
Inaweza kutumika tu kama faida ni kubwa kuliko hatari, na kwa:
Dozi ndogo
Muda mfupi
Chini ya uangalizi wa daktari
ULY CLINIC inasisitiza: Mjamzito asitumie Ketoprofen kwa hiari, hata kama alishawahi kuitumia kabla.
Ketoprofen kwa Mama Anayenyonyesha
Ketoprofen hupita kwa kiasi kidogo kwenye maziwa ya mama.
Kwa ujumla:
Inaweza kutumika kwa muda mfupi
Kwa dozi ndogo
Chini ya ushauri wa mtaalamu wa afya
Tahadhari:
Epuka matumizi ya muda mrefu
Fuata maelekezo ya daktari
Fuatilia mtoto kama ana:
Kusinzia kupita kiasi
Kutapika
Kukosa kunyonya vizuri
Ikiwa kuna mbadala salama zaidi (mf. Paracetamol), hupewa kipaumbele.
Namna Sahihi ya Matumizi ya Ketoprofen
Tumia baada ya chakula
Usizidishe dozi
Epuka matumizi ya muda mrefu bila tathmini
Usitumie dawa mbili jamii ya NSAID kwa pamoja
Nifanye nini nikisahau dozi ya Ketoprofen?
Ikiwa umesahau kutumia dozi ya Ketoprofen:
Tumia dozi mara tu utakapoikumbuka, kama bado kuna muda kabla ya dozi inayofuata
Usitumie dozi mbili kwa wakati mmoja ili kufidia uliyosahau
Kama muda wa dozi inayofuata uko karibu, ruka dozi uliyosahau na endelea na ratiba ya kawaida
Hitimisho
Ketoprofen ni dawa yenye manufaa makubwa katika kupunguza maumivu na uvimbe, lakini pia ina hatari kubwa ikitumiwa vibaya.Matumizi salama ya Ketoprofen yanahitaji elimu, tahadhari na ushauri wa kitaalamu.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Je, Ketoprofen ni kali kuliko Ibuprofen?
Kwa baadhi ya watu, ndiyo — lakini hutegemea dozi na hali ya mgonjwa.
2. Ketoprofen inatibu homa?
Inaweza kupunguza homa, lakini si dawa ya kwanza kwa homa rahisi.
3. Je, Ketoprofen inafaa kwa maumivu ya mgongo?
Ndiyo, hasa ya uvimbe, lakini kwa muda mfupi.
4. Naweza kutumia Ketoprofen kila siku?
Hapana bila ushauri wa daktari.
5. Ketoprofen na Paracetamol zinaweza kutumiwa pamoja?
Ndiyo, kwa ushauri wa mtaalamu.
6. Je, sindano ya Ketoprofen ni salama?
Ni salama chini ya uangalizi wa kitaalamu.
7. Ketoprofen huathiri tumbo?
Ndiyo, hasa ikitumiwa bila chakula.
8. Wazee wanaweza kutumia Ketoprofen?
Ndiyo, lakini kwa tahadhari kubwa.
9. Ketoprofen inaruhusiwa Tanzania?
Ndiyo, ipo kwenye matumizi ya kawaida ya kitabibu.
10. Nifanye nini nikipata maumivu makali ya tumbo?
Acha dawa na muone mtaalamu wa afya haraka.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
23 Januari 2026, 14:00:23
Rejea za mada hii:-
