Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
12 Julai 2025, 06:55:10

Dawa Salbutamol
Ni dawa ya kupanua njia za hewa, inayotumika kutibu na kuzuia matatizo ya kupumua yanayosababishwa na magonjwa kama pumu, bronchitis, na ugonjwa sugu wa njia za hewa (COPD). Kazi yake kuu ni kufungua mirija ya hewa ili kurahisisha upumuaji.
Kundi la dawa
Salbutamol ni dawa ya kipanua njia ya hewa kutoka kwenye kundi la vichochea beta-2 adrenejiki . Hufanya kazi kwa kuchochea vipokezi vya beta-2 vilivyoko kwenye misuli laini ya njia ya hewa na kuisababisha kulegea, hivyo kupanua njia za hewa.
Sifa za dawa
Huanza kufanya kazi ndani ya dakika chache baada ya kuvutwa au kumezwa.
Hufanya kazi kwa muda mfupi.
Hupatikana kwa mfumo wa kuvuta (inhaler), sindano, tembe, au maji ya kunywa.
Rangi ya dawa ya kuvuta huwa mara nyingi bluu.
Huvutwa kupitia kifaa cha kupumulia kama inhaler au nebulizer.
Fomu ya dawa Salbutamol
Salbutamol hupatikana katika fomu zifuatazo:
Inhaler (100 mcg/spray)
Syrup (2mg/5ml)
Tembe (2 mg au 4 mg)
Sindano (500 mcg/ml)
Nebulizer solution (2.5 mg au 5 mg)
Utoaji taka mwilini wa Salbutamol
Huvunjwa kwa umetaboli katika ini
Huchujwa na kutolewa mwilini kupitia figo kwa njia ya mkojo
Salbutamol hutibu magonjwa gani?
Salbutamol hutumika kutibu au kupunguza dalili za:
Pumu (Asthma)
Bronkaitis
COPD (ugonjwa sugu wa kuziba kwa njia za hewa)
Kikohozi kinachoambatana na kubanwa kwa kifua
Kuzuia kuziba kwa bronkio kunakosababishwa na mazoezi (asthma inayoamshwa kwa mazoezi)
Salbutamol huathiri bakteria au virusi?
Hapana. Salbutamol sio antibayotiki — haina kazi ya kuua bakteria wala virusi, bali hufanya kazi kwa kupanua njia ya hewa tu.
Angalizo kwa watumiaji wa Salbutamol
Tumia dawa hii kwa tahadhari kwa watu wenye:
Shinikizo la juu la damu (hypertension)
Matatizo ya moyo kama pigo la moyo lisilo la kawaida
Kisukari – inaweza kuongeza sukari kwenye damu
Kiwango kikubwa cha homoni za tezi shingo kwenye damu (thairoidi)
Mzio kwa dawa hii au dawa nyingine ya kundi la vichochea beta
Dawa zisizopaswa kutumika pamoja na Salbutamol
Salbutamol haipaswi kutumika pamoja na dawa zifuatazo bila uangalizi wa daktari:
Beta-blockers (mf. propranolol) – hupingana na kazi ya salbutamol
Digoxin – salbutamol huweza kupunguza viwango vyake mwilini
Dawa za kuongeza mkojo – huongeza hatari ya matatizo ya moyo
Vizuia Monoamine oxidase(MAOIs) – huongeza maudhi yake kwenye ya moyo
Dawa kundi moja na Salbutamol
Terbutaline
Levalbuterol
Fenoterol
Formoterol (long-acting)
Salbutamol haipaswi kutumika kwa wagonjwa gani?
Wenye historia ya mzio mkali (anafailaksia) kutokana na dawa hii
Wenye matatizo makubwa ya moyo bila uangalizi wa daktari
Watu wasiokuwa na tatizo la kupumua lisilotakiwa kutumia vipanua njia ya hewa
Matumizi ya Salbutamol kwa wajawazito
Salbutamol inaweza kutumika wakati wa ujauzito endapo faida kwa mama ni kubwa kuliko madhara kwa mtoto. Daktari atapima hatari na faida kabla ya kutoa dawa.
Matumizi ya Salbutamol kwa wanaonyonyesha
Kiasi kidogo cha salbutamol huingia kwenye maziwa ya mama, lakini hakuna ushahidi wa madhara makubwa kwa mtoto anayenyonya. Inashauriwa kutumia kwa tahadhari chini ya uangalizi wa daktari.
Maudhi ya dawa Salbutamol
Baadhi ya madhara madogo ni pamoja na:
Kutetemeka mikono
Kuhisi mapigo ya moyo kwenda kasi
Kizunguzungu
Maumivu ya kichwa
Kichefuchefu
Kukosa usingizi
Mdomo kukauka
Maumivu ya kifua
Ufanye nini kama umesahau dozi yako?
Tumia mara tu unapokumbuka. Usitumie dozi mbili kwa wakati mmoja. Ikiwa muda wa dozi inayofuata umefika, ruka ile uliyosahau na uendelee na ratiba yako ya kawaida.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
12 Julai 2025, 06:55:18
Rejea za mada hii:-