Mwandishi:
Dkt. Salome A, MD
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
23 Julai 2021, 18:39:35

Chakula kwa mjamzito
Matokeo mazuri ya ujauzito kwa mama na mtoto hutegemea mambo mengi ikiwemo lishe ya mama kabla ya kupata ujauzito na katika kipindi chote cha ujauzito, lishe nzuri ya mama hupelekea kupata mtoto mwenye afya njema na maisha marefu ya mama na mtoto.
Wajawazito wanahimizwa kula chakula bora chenye mlo kamili kwa kiwango kinachotakiwa, hata hivyo si vyakula vyote ni salama wakati wa ujauzito. Baadhi ya sumu zinazopatikana katika mazingira huingia katika baadhi ya vyakula, kama vyakula hivyo vikiliwa huleta matokeo mabaya ya ujauzito kama vile, watoto wenye kasoro za kimaumbile pamoja na maradhi kwa mama na mtoto.
Umuhimu wa elimu ya chakula kabla na wakati wa ujauzito
Bado kuna uelewa mdogo kuhusu lishe ya mjamzito hasa vyakula hatari wakati wa ujauzito ukilinganisha na elimu ya dawa hatari nk, kutokana na kukosa elimu ya ziada wakati wa kuhudhuria kliniki. Lakini pia baadhi ya vyakula vina madhara ambayo sio rahisi kuonekana kwenye vipimo na hivyo hupelekea madhara tu ambayo yanaweza kuzuilika endapo mama atapata elimu kuhusu vyakula hivyo na kuviepuka Lengo la makala hii ni kutoa elimu ya ziada kwa mjamzito kuhusu vyakula muhimu wakati wa ujauzito na vile ambavyo ni hatari.
Namna kijusi tumboni anavyopata chakula alichokula mama kwa afya yake
Mimba inapotungwa maendeleo ya ukuaji wa kijusi hutegemea chakula kupitia mishipa ya damu kutoka katika mirija ya uzazi na mji wa mimba mpaka kinapotimiza wiki 10, ambapo kinaanza kupata chakula kutoka kwenye damu ya mama kupitia kiunga mwana. Hivyo basi ni muhimu kwa mwanamke anayetarajia kubeba ujauzito kula chakula bora chenye mlo kamili kabla ya ujauzito na katika kipindi chote cha ujauzito.
Chakula na utengenezaji wa viungo vya kijusi
Katika kipindi cha wiki 11 na kuendelea za ujauzito, utengenezwaji wa viungo na mifumo ya mwili wa mtoto hufanyika, shughuli hizi zote huitaji nishati kutoka katika chakula vilevile huathiriwa na sumu kutoka kwenye mazingira zinazoingia mwilini kwa mjamzito kula chakula. Upungufu wa vyakula vyenye nishati au ulaji uliopitiliza wa vyakula vyenye nishati wakati huu kupelekea kasoro mbalimbali kama vile kudumaa, kuwa na uzito mdogo au mkubwa kupita kiasi, kasoro za kimaumbile nk. Kutokana na nadharia ya namna afya njema na magonjwa yanavyotokea, magonjwa mengi yanayojitokeza katika kipindi cha utu uzima chanzo chake ni katika kipindi cha ujauzito kwahiyo hiki ni kipindi maalumu sana ambacho kinaamua afya ya jamii ya hapo baadae. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wimbi la magonjwa yasioambukiza, magonjwa ya mzio, kuzaliwa kwa watoto wenye kasoro za kimaumbile na uzito ambao sio wa kawaida, yote haya yanahusishwa na sumu zitokanazo na baadhi ya vyakula lakini pia upungufu wa lishe bora kabla ya ujauzito na katika kipindi cha ujauzito na matumizi ya baadhi ya dawa.
Vyakula salama kwa mjamzito na faida zake
Mjamzito anapaswa kupata viinirishe na virutubisho kutoka vya vyakula vyenye;
Wanga
Nyuzinyuzi
Protini
Mafuta
Vitamin C
Vitamin D na kalisiamu
Vitamin E
Madini chuma
Madini joto
Vitamin Folate
Vyakula vya wanga
Ni chanzo cha kikuu cha nishati katika mwili na ubongo, sukari itokanayo na wanga hutoa nishati ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto. Mama anashauriwa kula vyakula venye wanga hasa kutoka kwenye nafaka ambazo hazijakobolewa, mboga za majani, matunda nk.
Vyakula vyenye nyuzi nyuzi
Ulaji wa vyakula vyenye nyuzi nyuzi unafaida nyingi ikiwamo kusaidia uzalishwaji wa bakteria ambao wanaozalisha kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta inayopunguza hatari ya kupata magonjwa ya mzio katika mfumo wa upumuaji wa mtoto baada ya kuzaliwa. Faida nyingine ni kupunguza ufyonzwaji wa lehemu kutoka katika tumbo, kurekebisha kiwango cha sukari katika mwili nk.Vyakula vyenye nyuzi nyuzi ni pamoja na parachichi, ndizi, karoti, shayiri nk.
Vyakula vya protini
Protini ni muhimu kwa ukuaji na utengenezwaji wa viungo vya mtoto.Vifuatavyo ni vyakula vyenye protini nyingi;
Nyama
Samaki
Mayai
Maziwa na mazao yatokanayo na maziwa
Maharagwe
Soya
Mafuta
Mjamzito anapaswa kula mafuta mazuri ambayo hayana cholesterol, na badala yake kula tindikali ya mafuta ya omega-3 Mafuta yenye tindikali ya mafuta ya omega-3 ni mazuri kwa kwa ukuaji mzuri wa ubongo na retina ya mtoto pia huzuia magonjwa ya mzio kwa mtoto katika siku za usoni. Tindikali ya mafuta ya omega-3 hupatikana kwa wingi katika samaki wa maji baridi, mbegu na karanga.
Vyakula vyenye vitamin C
Vyakula vyenye vitamin C husaidia kufyonzwa kwa madini chuma yaliyo kwenye chakula tumboni kuingia katika damu, pia vitamin C ina viuajisumu vinavyosaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya mzio kwa mtoto. Vyakula venye kiwango kikubwa cha vitamin C ni;
Matunda jamii ya malimao ikiwa pamoja na limao, ndimu
Nyanya
Brokoli
Machungwa
Pilipili
Stroberi
Viazi
Kabeji
n.k
Vyakula vyenye vitamin D na madini ya calcium
Vitamin D pamoja na calcium ni muhimu katika ukuaji wa mifupa ya mtoto hivyo kupunguza hatari ya magonjwa ya mifupa hasa mifupa dhaifu.
Upungufu wa vitamin D na kalisiamu wakati wa ujauzito hupelekea presha ya ujauzito, kisukari cha ujauzito, kupata uchungu kabla ya wakati na udhaifu wa mifupa ya kichanga. Kiwango kikubwa cha vitamin D hupatikana kwenye
Mafuta ya ini la samaki kodi pamoja na samaki wengine
Kiwango kidogo cha vitamin D hupatikana kwenye;
Mayai
Mafuta ya wanyama,
Vyanzo vingine vya Vitamin D
Kukaa kwenye jua la asubuhi huchochea ngozi kuzalisha wa vitamin D.
Vyanzo vikuu vya kalisiamu ni;
Maziwa pamoja na mazao yake
Mboga za majani zenye rangi ya kijani kama kale, okra na silio kwa kiwango kidogo
Mifupa ya samaki
Vinywaji vya soya vilivyotiwa kalisiamu
Mkate na mazao mengine yaliyotengeneza na unga ulioongezewa virutubisho
Vyakula vyenye vitamin E
Vitamin E inakiwango kikubwa cha viuajisumu ambavyo ni muhimu katika kuzikinga chembe hai dhidi ya msongo wa oksidesheni. Tafiti zinaonesha kuwa vitamin E hupunguza hatari ya watoto kupata pumu endapo mama atapata wakati wa ujauzito. Vyakula vingi vina vitamin E hata hivyo vitamin hii hupatikana kwa wingi kwenye;
Mbegu za alizeti
Lozi
Karanga
Mafuta ya kama vile mafuta ya wheat germ, rice bran, grapeseed na safflower
Parachichi
Spinach nk
Vyakula venye virutubisho vya madini joto
Madini joto ni kirutubisho muhimu na upungufu wake hupelekea kuharibika kwa mimba, vifo vya watoto wachanga, kasoro za kimaumbile, magonjwa ya mfumo wa fahamu na kuharibiwa kwa ubongo Virutubisho vya iodine hupatikana kwenye vyakula kama vile;
Samaki na sama kigamba
Matunda
Mboga za majani
Maziwa
Mayai
Nyama
Chumvi yenye madini joto
Vyakula vyenye madini chuma
Matumizi ya madini chuma katika mwili huongezeka sana katika kipindi cha ujauzito hivyo kupelekea upungufu wa madini haya kunako pelekea upungufu wa damu, hivyo kupelekea madhara kwa mama na mtoto. Kutokana na umuhimu wa madini chuma wajawazito hupewa dawa zeye madini haya muhimu, licha ya kupewa dawa hizi bado kuna umuhimu wa mjamzito kutumia vyakula venye madini chuma kwa wingi Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini chuma ni pamoja na;
Nyama
Mayai
Samaki
Matunda
Mboga za majani nk.
Vyakula vyenye vitamin Folate
Folate ni muhimu sana kwa ukuaji wa mfumo wa fahamu lakini pia huzuia tatizo la mogongo wazi kwa mtoto, mama hupewa vidonge vyenye virutubisho vya folate wakati wa kiliniki ambavyo huwa ni chanzo kikuu cha folate, lakini pia folate hupatikana katika vyakula vifuatavyo;
Vyakula jamii ya kunde
Mayai
Mboga za majani hasa spinachi
Matunda jamii ya malimao
Karanga
Ndizi
Maini ya ng’ombe nk
Vyakula vya hatari kwa mjamzito
Vyakula hatari kwa mjamzito vimegawanywa kwenye makundi yafuatayo ambayo yameelezewa kwenyemaelezo yanayofuata;
Vyakula zebaki kwa wingi
Vyakula vya kusindikwa
Vyakula vyenyemafuta mengi
Vyakula vyasukari nyingi
Vyakula visivyoiva vema
Vyakula vyenye zebaki kwa wingi
Zebaki ni elementi inayopatikana kwenye ardhi, anga na majini, vyakula vya baharini hupata elementi hii katika maji. Mjamzito anaweza kupata elementi hii kwa kula vyakula vya baharini Mjamzito anapokula vyakula vya majini vyenye elementi ya zebaki huweza kupata madhara, hata hivyo kutokea kwa madhara hutegemea na kiwango cha zebaki katika chakula, na kiwango cha ulaji. Jinsi samaki aishvyo muda mrefu na kuwa mkubwa ndivyo kiwango cha zebaki huongezeka kwani huwa na muda mrefu wa kupata elementi hii hatari kwa afya, zebaki haiwezi kuondolewa kwa kumpika samaki wa namna hii, kwahiyo njia salama ya kuepuka zebaki ni kula samaki wadogo na dagaa. Samaki wenye kiwango kikubwa cha zebaki hawafai kuliwa kabisa wakati wa ujauzito, wakati samaki walio na kiwango kidogo cha zebaki ni salama kuliwa milo michache bila kuleta madhara yoyote. orodha ya samaki wenye kiwango kikubwa na kiwango kidogo cha zebaki wameorodheshwa hapo chini;
Samaki wenye kiwango kikubwa cha zebaki
Jodari
Nguru
Sulisuli
Orange roughy
Sansuli
Papa
Samaki tile
Samaki wenye kiwango kidogo zebaki
Kambare
Anchovi
Codi
Heringi
Chaza
Polloki
Salmon
Dagaa
Shad
Uduvi
Sato
Trauti
nk
Madhara ya zebaki kwa mjamzito
Mama anapokula kiwango kikubwa cha mazao ya baharini yenye zebaki kwa muda mrefu, zebaki husafiri kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia kondo la nyuma na kusababisha madhara yafuatayo kwa mtoto;
Utindio wa ubongo
Kuwa na uwezo mdogo kiakili
Kutokuwa na kumbukumbu nzuri
Kupoteza umakini
Kukosa ujuzi laini wa kimota
Kukosa ujuzi wa spasho
Vyakula vya kusindika
Vyakula vingi vya kusindika hutumia viongezo vya chakula pamoja na vifungashio ambavyo huwa na kemikali aina ya bisphenol A (BPA). Mama anapopata kemikali za BPA wakati wa ujauzito husababisha madhara yafuatayo kwa mtoto katika siku za usoni;
Obeziti
Madhaifu ya kukosa utulivu kwa mtoto- ADHD
Wasiwasi uliopitiliza
Sonono
Vyakula vyenye mafuta mengi
Vyakula venye mafuta mengi hasa mafuta yaliyojaa (saturated fat)huwa na kiwango kikubwa cha lehemu ambayo ni hatari kwa afya.Mfano wa vyakula hivi nikama vile chips, nyama za kusindika kama soseji nk. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi wakati wa ujauzito husababisha madhara yafuatayo;
Magonjwa ya shikino la damu katika ujauzito
Kisukari cha mimba
Uchungu kabla ya wakati
Mtoto kudumaa akiwa tumboni
Kuzaliwa na uzito mkubwa uliopitiliza
Kujifungua kwa upasuaji
Vyakula vyenye sukari nyingi
Vyakula vyenye sukari nyingi wakati wa ujauzito huathiri shughuli za umetaboli na kuogeza hatari ya kupata madhara yafuatayo;
Kisukari cha mimba
Magonjwa ya shikino la damu katika ujauzito
Magonjwa ya moyo kwa mtoto katika siku za usoni
Vyakula ambavyo havijaiva au vyakula vibichi
Ulaji wa nyama au samaki ambao hawajapikwa au wabichi, maziwa ambayo hayajachemshwa, mayai mabichi pamoja na nyama zilizokaushwa kwa moshi ni hatari kwa afya ya mama na mtoto, kwani vyakula hivi hubeba vimelea mbalimbali wa magonjwa ambayo yana madhara katika ujauzito. Vimelea wa magonjwa wanaopatikana kwenye vyakula hivi ni kama ifuatavyo;
Listeria monocytogenes
Eschelichia coli
Campylobacter
Mycobacterium bovis
Salmonella
Toxoplasma gondii
Vimelea wa toxoplasma na listeria wana uwezo wa kupenya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia kitovu cha mtoto na kusababisha magonjwa yenye mdhara makubwa kwa mtoto kama yalivyoelezewa zaidi chini ya makala hii.
Madhara ya Salmonella, Campylobacter, Eschelichia coli na mycobacterium bovis Salmonella, Campylobacter na Eschelichia coli husababisha magonjwa ya homa ya matumbo na kuhara, wakati mycobacterium bovis husababisha kifua kikuu. Magonjwa haya humuathiri zaidi mama.
Ugonjwa wa listeriosis
Ugonjwa huu husababishwa na bacteria aitwaye listeria monocytogenes, mjamzito pamoja na mtoto aliyetumboni wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu mara 10 zaidi ya watu wengine, ugonjwa huu husababishwa na ulaji wa nyama mbichi au nyama ambayo haijava.
Bakteria huyu anauwezo wa kupenya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia kondo la nyuma na kusababisha madhara yafuatayo;
Kuharibu mimba
Mtoto kufia tumboni
Kupata uchungu kabla ya muda
Ugonjwa mkali kwa kichanga unaoweza kupelekea kifo
Ugonjwa wa toxoplasmosis
Ni ugonjwa unaosababishwa na parasaiti aitwaye toxoplasma gondii, ugonjwa huu husababishwa na ulaji wa nyama mbichi au nyama ambayo haijava. Ugonjwa huu husababisha madhara yafuatayo kwa mtoto;
Upofu
Uziwi
Utindio wa ubongo
Kiwango cha chakula kinachofaa kwa mjamzito
Hakuna kiwango maalumu cha chakula wakati wa ujauzito, mjamzito anapaswa kula mlo kamili kutoka katika makundi yote ya vyakula, hata hivyo lazima awe na tahadhari katika ulaji wa vyakula vyenye nishati nyingi. Vyakula vyenye nishati ni vyakula kutoka katika kundi la wanga, protini na mafuta. Lazima kuwe na uwiano wa ulaji wa vyakula hivi, kwani ulaji uliopitiliza na upungufu huleta utapiamlo na kusababisha madhara mbalimbali kama yalivyoelezewa hapa chini.
Madhara ya ulaji uliokithiri wa vyakula vyenye nishati kubwa
Kuongezeka uzito
Kuwa katika hatari ya kupata shinikizo la juu la damu
Kuwa katika hatari ya kupata kisukari cha mimba
Kuzaa kwa upasuaji kwasababu ya mtoto kuwa kubwa
Ugonjwa wa obeziti kwa mtoto
Madhara ya upungufu wa vyakula vyenye nishati
Mtoto kudumaa akiwa tumboni
Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo
Mtoto kuwa katika hatari ya kupata kisukari aina ya pili afikapo utu uzima
Je kuna vyakula maalumu kwa kipindi cha kwanza, pili na tatu cha ujauzito?
Kuna ongezeko kubwa la uhitaji wa virutubishi na viinilishe vya ziada kwa ajili ya uumbaji wa viungo mbalimbali vya kijusi katika kipindi cha kwanza cha ujauzito ambacho ni kipindi ndani ya wiki 12 za kwanza. Licha ya uhitaji huo mkubwa, mahitaji ya virutubisho hufanana katika vipindi vyote vya ujauzito. Virutubisho muhimu anavyopaswa kuvipata mjamzito vipindi vyote vitatu ni;
Vyakula vyenye vitamin B-9 au folik asidi au folate
Vyakula vyenye vitamin A, C, D, E
Vyakula vyenye protini
Vyakula vyenye madini kalisuamu kwa wingi
Vyakula vyenye madini chuma
Vyakula vyenye madini ya potasiamu
Tindikali mafuta ya omega-3 Mfano wa vyakula vizuri kipindi cha kwanza, pili na tatu cha ujauzito ni vile vyenye virutubisho na viinilishe kama vilivyotajwa hapo ni;
Nyama
Maziwa mgando
Mbaazi
Tunda kale, machungwa, ndimu
Mboga za kijani
Ndizi
Maharagwe
Tangawizi
Wapi utapata taariza zaidi?
Pata taarifa zaidi kuhusu chakula kwenye linki zingine za Vyakula na virutubisho ndani ya tovuti ya ULY CLINIC Usisahau kusoma pia kuhusu ujauzito na dawa, katika makala za matumizi ya dawa wakati wa ujauzito na kunyonyesha.
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
24 Desemba 2021, 05:59:40
Rejea za dawa
Sarah E Santiago, Grace H Park, and Kelly J Huffman. Consumption habits of pregnant women and implications for developmental biology: a survey of predominantly Hispanic women in California. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3704911.
EMILY OKEN et al. Diet During Pregnancy and Risk of Preeclampsia or Gestational Hypertension. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2532559/?report=reader
CDC mercury fact sheet.https://www.cdc.gov/biomonitoring/Mercury_FactSheet.html
Philip W. Davidson et l. Fish Consumption, Mercury Exposure, and Their Associations with Scholastic Achievement in the Seychelles Child Development Study. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2934742/?report=reader
Wolters Kluwer Health.Obstetrical & Gynecological Survey. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4949006/#!po=14.8352
Katherine Bowerse et al.A prospective study of prepregnancy dietary fat intake and risk of gestational diabetes. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3260071/?report=reader
Graham Devereux, et al. Low Maternal Vitamin E Intake during Pregnancy Is Associated with Asthma in 5-Year-Old Children.https://www.atsjournals.org/doi/10.1164/rccm.200512-1946OC?url_ver=Z39.882003&rfr_id=ori%3Arid%3Acrossref.org&rfr_dat=cr_pub++0pubmed&
Kirsten Herrick, David I. W. Phillips, Soraya Haselden, Alistair W. Shiell, Mary Campbell-Brown, Keith M. Godfrey. Maternal Consumption of a High-Meat, Low-Carbohydrate Diet in Late Pregnancy: Relation to Adult Cortisol Concentrations in the offspring.https://academic.oup.com/jcem/article/88/8/3554/2845229
High cholesterol foods.https://www.healthline.com/nutrition/high-cholesterol-foods#lowering-cholesterol
Alison N.Thorburn et al. Evidence that asthma is a developmental origin disease influenced by maternal diet and bacterial metabolites.https://www.nature.com/articles/ncomms8320
MK Javaid et al. Maternal vitamin D status during pregnancy and childhood bone mass at age 9 years:alongitudinal study.Published: January07,2006DOI:https://doi.org/10.1016/S0140-6736(06)67922-1
Healthline. 15 healthy foods that are high in folate (folic acid).https://www.healthline.com/nutrition/foods-high-in-folate-folic-acid#10.-Beef-liver
American Red Cross. Iron rich foods.https://www.redcrossblood.org/donate-blood/blood-donation-process/before-during-after/iron-blood-donation/iron-rich-foods.html
Medical news today.10 foods rich in vitamin E.https://www.medicalnewstoday.com/articles/324308