top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dkt. Glory, MD

ULY CLINIC

20 Novemba 2025, 15:35:44

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Dawa ya PID ya hospitali

PID (michomokinga ya via ndani ya nyonga) ugonjwa unaotokana na kutotibiwa vema kwa magonjwa ya zinaa hutibiwa kwa mchanganyiko wa antibiotiki ili kuangamiza bakteria wa magonjwa ya zinaa ambao ni Neisseria gonorrhoeae, Chlamydia trachomatis, na bakteria jamii ya anaerobik. Dawa hutolewa kulingana na ukali wa dalili na matibabu hugawanywa kwenye makundi mawili yaani matibabu ya wagonjwa wa nje ya hospitali au matibabu ya wagonjwa wa ndani ya hospitalini (wanaolazwa).


Kumbuka
ree

Kabla ya kutumia dawa yoyote, wasiliana na daktari wako kabla ya kutumia dawa yoyote kuepuka madhara na usugu wa vimelea kwenye dawa. ULY CLINIC haitahusika na madhara yoyote yatakayotokea endapo hutafuata ushauri wa daktari wako.


Dawa ya PID kwa wagonjwa wa nje (Maambukizi ya wastani au madogo)

Dawa zifuatazo hutumika katika matibabu ya wagonjwa ambao hawatarajii kulazwa hospitali kwa sababu ya PID, dawa nyingi hutumika kwa njia ya kunywa isipokuwa ceftriaxon:

  • Ceftriaxone

  • Doxycycline

  • Metronidazole


Matibabu mbadala ya dalili kali za PID

Cefoxitin 2g IM  na Probenecid 1g


Dawa za PID kwa wagonjwa wa kulazwa (Maambukizi makali)

Wagonjwa wa kulazwa hupewa dawa za kuchoma kwenye misuli au mishipa, miongoni mwa dawa hizo ni;

  • Ceftriaxone

  • Doxycycline na

  • Metronidazole


Matibabu mbadala wakw kwa wagonjwa wenye mzio na dawa jamii ya  β-lactam ni

  • Clindamycin na

  • Gentamicin IV


Tahadhari za kutumia dawa ya PID ya hospitali

Wakati wa kutumia antibiotiki za kutibu Pelvic Inflammatory Disease (PID), ni muhimu kuzingatia tahadhari zifuatazo:


Maudhi ya dawa ya PID ya hospitali


Ceftriaxone

Inaweza kusababisha mzio, maumivu kwenye sehemu ya kuchoma sindano, kuhara, au mabadiliko ya ini.


Doxycycline

Inaweza kusababisha kichefuchefu, kuhara, kuongezeka kwa hisia ya ngozi kwenye mwanga wa jua, na uharibifu wa meno kwa wajawazito na watoto chini ya miaka 8.


Metronidazole

Inaweza kusababisha kichefuchefu, ladha mbaya mdomoni, na haipaswi kutumiwa na pombe kwani inaweza kusababisha madhara makali kama vile mwitikio wa disulfiram.


Gentamicin

Inaweza kusababisha kuferi ghafla kwa figo na upotevu wa kusikia.


Uwezekano wa Mzio na mzio mkali

Wagonjwa wenye mzio na dawa jamii ya penicillin au cephalosporins wanapaswa kuwa waangalifu wanapotumia Ceftriaxone au Cefoxitin. Dalili za mzio mkali ni pamoja na uvimbe kwenye uso, kushindwa kupumua, na mshtuko wa mwili.


Matumizi sahihi ya dawa ya PID ya Hospitali

Wakati unatumia dawa hizi ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo kwa matokeo mazuri ya matibabu na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza:

  • Kuhakikisha mwenza wako anapata matibabu ili kuzuia maambukizi tena.

  • Kuepuka kushiriki ngono hadi matibabu yatakapo kamilika.

  • Kufuatilia maendeleo yako ili kuhakikisha kama dalili zinapungua.

  • Tumia dawa zote kwa muda uliopendekezwa hata kama dalili zimepungua ili kuepuka usugu wa bakteria.

  • Usimeze Doxycycline kbila chakula – kula chakula ili kupunguza maudhi ya tumbo.

  • Epuka pombe wakati wa kutumia Metronidazole ili kuepuka maudhi makali ya dawa hii.


Maswali 10 yaliyoulizwa mara kwa mara

1. Najuaje kama PID yangu imetulia na matibabu yanafanya kazi?

Dalili kama maumivu ya tumbo la chini, homa, na maumivu wakati wa ngono au kukojoa hupungua ndani ya siku 48–72. Ikiwa hakuna mabadiliko baada ya muda huo, maambukizi yanaweza kuwa sugu, dawa zinaweza kuwa hazifanyi kazi, au kuna tatizo lingine la uzazi linalofanana na PID linalohitaji uchunguzi zaidi (mfano, ugonjwa wa kidole wa kidole tumbo au kujisokota kwa ovari).

2. Kwa nini PID huhitaji dawa zaidi ya moja kwa wakati mmoja?

PID husababishwa na mchanganyiko wa bakteria tofauti, hivyo dawa moja haitoshi. Mchanganyiko wa antibiotiki hufunika bakteria wa zinaa, anaerobes, na vimelea vingine vinavyosababisha maambukizi kuendelea.

3. Je, PID inaweza kutokea bila mtu kuwa na magonjwa ya zinaa?

Ndiyo. Ingawa mara nyingi hutokana na chlamydia au kisonono, inaweza pia kutokana na:

  • Bakteria wa kawaida wa uke kupenya ndani,

  • Upasuaji wa kizazi,

  • Kuingiza IUD,

  • Kuzaa au kutoa mimba.

4. Je, PID ikitibiwa mapema inaweza kuathiri uzazi?

Matibabu ya mapema hupunguza hatari ya uharibifu wa mirija ya uzazi. Ikiwa imechelewa au imetokea mara kwa mara, inaweza kusababisha:

  • Uzazi mgumu (Ugumba)

  • Mimba nje ya mfuko

  • Maumivu ya nyonga ya kudumu

5. Kwa nini inasisitizwa mwenza kutibiwa pia?

Kwa sababu vimelea wanaosababisha PID huambukizwa kimwili. Hata kama mwenza hana dalili, anaweza kubeba maambukizi na kukurudishia baada ya matibabu yako kukamilika (reinfection).

6. Je, ninaweza kupata PID tena hata nikitibiwa vizuri?

Ndiyo. Vyanzo kama kutopona kwa mwenza, kuwa na wapenzi wengi bila kutumia kinga, au historia ya PID huongeza hatari ya kupata tena.

7. Kwa nini Metronidazole haipaswi kuchanganywa na pombe?

Mchanganyiko wake husababisha reaction kali kama ya disulfiram, ikijumuisha kutapika, mapigo ya moyo kwenda mbio, na maumivu ya kichwa, ambayo yanaweza kuwa hatari.

8. Je, ninaweza kuendelea kunyonyesha nikiwa natumia dawa za PID?

Ndiyo, kwa baadhi ya dawa. Hata hivyo, Doxycycline haitakiwi kutumiwa kwa muda mrefu kwa mama anayenyonyesha kwa sababu huweza kuathiri ukuaji wa mifupa ya mtoto. Daktari hutoa mbadala salama kwa mama wajawazito au wanaonyonyesha.

9. Kwa nini baadhi ya wagonjwa hulazwa hospitalini wakati wengine hutibiwa nyumbani?

Kulazwa hutokea endapo kuna:

  • Homa na maumivu makali

  • Kutapika hadi kushindwa kumeza dawa

  • Maambukizi kuenea kwenye damu

  • Mimba (PID wakati wa ujauzito)

  • Kutokuwa na uhakika wa utambuzi

10. Je, matumizi mabaya ya antibiotiki yana madhara gani kwa PID?

Kutokumaliza dawa au kutumia bila ushauri husababisha:

  • Usugu wa bakteria

  • Kutokutibika kikamilifu

  • Uharibifu wa mirija ya uzazi

  • PID sugu au kurudia mara kwa mara

11. Ukiwa unapona PID, dalili zake huwa zinabadilika au kuonekana vipi?

Wakati PID inaanza kupona, dalili huwa zinapungua hatua kwa hatua ndani ya siku 3–5 baada ya kuanza dawa sahihi. Badala ya maumivu makali ya tumbo la chini, mgonjwa hupata maumivu madogo yanayopungua siku hadi siku. Homa na uchovu hupungua, na uchafu ukeni hupungua kwa wingi na harufu. Wakati wa uponaji, mwili haupaswi kuwa na maumivu makali ya ghafla, kutokwa damu kusiko kawaida, au homa mpya—ikiwa hayo yanatokea, ni dalili kuwa maambukizi hayajapungua au yametatiza mirija ya uzazi, hivyo unapaswa kurudi hospitalini haraka.


Rejea za mada hii:
  1. Mediscape. Pelvic Inflammatory Disease Treatment & Management. https://emedicine.medscape.com/article/256448-treatment#:. Imechukuliwa 15.03.2025

  2. Pelvic Inflammatory Disease CDC. (PID).https://www.cdc.gov/std/treatment-guidelines/pid.htm. Imechukuliwa 15.03.2025

  3. ULY CLINIC. Ugonjwa wa PID. https://www.ulyclinic.com/magonjwa-na-saratani/ugonjwa-wa-pid. Imechukuliwa 15.03.2025.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page