Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dr.Sospeter Mangwella, MD
ULY CLINIC
15 Juni 2025, 09:37:03
Kubadilika kwa majibu ya kipimo cha UKIMWI
Swali
Watu wengi huuliza maswali haya yanapofanya kipimo cha haraka cha UKIMWI aina ya SD Bioline au vingine vya aina hiyo. Maswali yanayojitokeza mara kwa mara ni:
Je, kwa nini mistari ya ziada huonekana kwenye kipimo cha SD Bioline baada ya zaidi ya nusu saa?
Je, kwa nini majibu hubadilika ndani ya masaa 24?
Je, mstari unaojitokeza baada ya muda mrefu una maana gani?
Je, kubadilika kwa majibu kunaonyesha uwepo wa maambukizi ya UKIMWI?
Mstari wa ziada una maana gani kisayansi?
Makala hii inakupa majibu ya maswali hayo kwa kutumia ushahidi wa kisayansi na miongozo ya watengenezaji wa vipimo hivi.

Majibu
Majibu Sahihi ya Kipimo cha UKIMWI Yanasomwaje?
Majibu ya vipimo vya haraka vya UKIMWI, kama vile SD Bioline, ni sahihi tu ikiwa yamesomwa ndani ya muda uliowekwa na mtengenezaji wa kipimo – kwa kawaida ndani ya dakika 15 hadi 20, lakini si zaidi ya dakika 30. Ukisoma majibu baada ya muda huo kupita, si sahihi na yanaweza kupotosha.
Kwanini mistari ya ziada inatokea?
Watengenezaji wa SD Bioline hawajatoa sababu maalum ya kisayansi kuhusu kwanini mistari ya ziada (hasa mstari hafifu kwenye eneo la T – Test Line) hujitokeza baada ya dakika nyingi au masaa.
Hata hivyo, wataalamu wa maabara na tafiti mbalimbali zimeeleza sababu zifuatazo:
Kuvuja kwa kemikali za kipimo kutoka kwenye eneo la mistari ya majibu baada ya muda mrefu
Mmwitikio wa kuchelewa wa antibodi na antijens unaochora mstari bila kuwa sahihi
Ukaushaji wa sampuli kwenye kipimo baada ya muda mrefu wa kupigwa hewa
Matari wa mnunurisho – mistari inayoonekana kwa sababu ya kukauka kwa sehemu ya kipimo
Mistari hii siyo ya kuaminika kiafya na haihusiani moja kwa moja na uwepo wa VVU.
Je, kuongezeka kwa mstari wa ziada baada ya muda wa kusoma majibu kunamaanisha nina maambukizi?
Hapana. Ikiwa mstari umeonekana baada ya dakika 30 au zaidi, haumaanishi kuwa una maambukizi ya VVU. Huo ni mstari batili ambao haupaswi kuzingatiwa.
Ikiwa una wasiwasi:
Rudia kipimo ukifuata muda wa kusoma majibu kama ilivyoelekezwa
Tumia kipimo cha aina nyingine kama Unigold au Determine
Fanya kipimo cha maabara cha PCR au Western blot ikiwa majibu yana utata
Utaratibu Bora wa Kusoma Majibu
Soma majibu ndani ya dakika 15–30
Ikiwa mstari wa "C" pekee umeonekana = Huna VVU
Ikiwa mistari miwili ya “C” na “T” inaonekana = Una VVU (Positive)
Mstari wa “T” pekee au majibu baada ya dakika 30 = Majibu batili
Mambo muhimu ya kukumbuka
Baada ya kusoma majibu ndani ya muda sahihi, kipimo kinapaswa kutupwa
Hakuna ulazima wa kuendelea kukiangalia kipimo hicho baadaye
Majibu yanayojitokeza baada ya muda hayaaminiki na hayawezi kutumiwa kama ushahidi wa maambukizi
Wapi unaweza kupata maelezo zaidi?
Kupata maelezo zaidi soma makala zifuatazo kwenye tovuti ya ULY CLINIC
Dawa za kutibu UKIMWI
Dalili za UKIMWI
UKIMWI hutambuliwa baaa ya muda gani?
Pia unaweza kuwasiliana na daktari wako kwa melezo zaidi, au kuwasiliana na daktari wa ULY Clinic kupitia kiungo cha wasiliana nasi chini ya tovuti hii.
Video kuhusu kipimo cha UKIMWI
Video ya dalili za awali za UKIMWI
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
