Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Jumatano, 27 Januari 2021
Chunusi mithiri ya keloidi nyuma ya shingo
Makala hii imezungumzia tatizo la chunusi mithiri ya vipele au makovu nyuma ya shingo na kisogoni, linalofahamika na watu wengi kama makovu nyuma ya shingo na kitiba kama. Acne Keloidalis Nuchae?(AKN) au Folliculitis Keloidalis Nuchae(FKN).
Ni nini maana ya tatizo la AKN?
Ni ni tatizo la ngozi lenye sifa ya kutoa vipele vidogo kwa vikubwa kwenye mashina ya vinyweleo vya ngozi vyenye kufanana na makovu ya keloid, na mara nyingi hutokea maeneo ya nyuma ya shingo au kisogoni na kwa vijana wadogo wenye asili ya bara la Afrika na Amerika.
Vipimo vya histology ambavyo huangalia seli kutoka kwenye makovu hayo, huonyesha tatizo hili si keloid bali ni matokeo ya uvimbe unaotokea kama mwitikio wa kinga za mwili dhidi ya majeraha na maambukizi yanayotokea kwenye mashina ya nywele wakati wa kunyolewa.
Dalili za AKN
Dalili za tatio hili huwa pamoja na;
Kuota kwa vipele vidogo mithiri ya chunusi kwenye mashina ya nywele vinavyowashwa na kuwa vikubwa jinsi muda unavyoenda. Vipele hivi hutokea sana baada ya kunyoa nyweke fupi zaidi
Visababishi cha AKN
Kisababishi halisi hakifahamiki, hata hivyo tafiti zinaonyesha kwamba tatio hili linaweza kuchangiwa na;
Kunyoa nywele fupi zaidi- hii hupelekea majeraha kwenye mashina ya nywele yanayoleta uvimbe
Kuchokozwa mara kwa mara kwa ngozi kutokana na msuguano wa kola, helmeti au nguo kwenye ngozi nyuma ya shingo hupelekea kupata majeraha yanayopelekea uvimbe
Hali ya hewa ya ujoto na unyevu kidogo pia huweza pelekea tatizo kuwa na hali mbaya zaidi
Matumizi ya dawa aina Fulani kama za kutibu baridi yabisi, psoriasis na kifafa mfano cyclosporine n.k
Matatizo ya kijeni ya kuzaliwa nayo
Maambukizi sugu kwenye ngozi
Matibabu ya AKN
Matibabu ya AKN hutegemea aina na usugu wa tatizo, matibabu gani umeshayafanya na uchaguzi wako. Matibabu huhusisha dawa na tiba mionzi ya laser kutoa vinyweleo. Tatizo huweza kujirudia hata kama umepona baada ya matibabu ya mara ya kwanza.
Matibabu ya dawa
Matibabu yasiyo dawa
Matibabu ya dawa
Kwa tatizo lenye hatua za awali, dawa za kupaka au vidonge vya kunywa kudhibiti maambukizi huweza kusaidia. Hata hivyo mara nyingi hutaandikiwa na daktari kutumia dawa endapo tatizo ni dogo kwenye hatua za awali bali utafundishwa njia zingine za kujitibu kwa matibabu ya nyumbani.
Matibabu dawa huhusisha
Matibabu ya maambukizi ya fangasi, daktari atakupa dawa za kutibu maambukizi hayo pamoja na sabuni ya kuoshea nywele zako au shampoo ya kuogea
Matibabu ya maambukizi ya bakteria
Matibabu ya kuondoa uvimbe kutokana na uchokozi unaotokea wakati wa kunyolewa, hii utatumia kila baada ya kunyoa
Matibabu yasiyo dawa
Upasuaji mdogo kwa wale wenye vipele vikubwa au chunusi kubwa zaidi, vipele hivi vitapasuliwa ili kutoa usaha uliopo ndani yake ili kupunguza maumivu na kuharakisha uponyaji kutokea na kupunguza makovu.
Matibabu ya ya mwanga wa laser hutumika endapo matibabu mengine yote yameshindwa, matibabu haya hulenga kuondoa maambukizi na mashina ya vinyweleo. Matibabu ya laser, hutolewa kwenye baadhi tu ya hospitali na matibabu huwa ni ya gharama kubwa. Utafanyiwa matibabu haya katika vipindi ambavyo utapangiwa na daktari wako. Madhara madogo yanayoweza kutokea ni kama kupata makovu, kupata malengelenge na ngozi kubadilika rangi katika maeneo ambayo yanafanyiwa matibabu.
Matibabu ya AKN nyumbani
Jikande kwa kutumia maji ya uvuguvugu ambayo hayatakuunguza. Fanya hivi mara kwa mara kwa siku jinsi unavyoweza ili kupunguza muwasho. Kama ukiweza tengeneza maji yenye chumvi kijiko kimoja cha chai kwa kila robo lita ya maji ya uvuguvugu kisha jikanede kwa dakika 5 hadi kumi.
Tumia dawa za kupaka au mafuta kuzui maambukizi jamii ya antibiotic
Tumia losheni ya kulainisha maeneo hayo ili kuzuia muwasho na kujikwangua zaidi kunakosababisha uvimbe.
Nawisha eneo lenye tatizo mara mbili kwa siku kwa kutumia sabuni zinazoua bakteria. Usitumie nguvu kuzuia majeraha na baada ya kunawa tumia taulo kavu kuondoa majimaji kwa kugandamiza badala ya kufuta. Hakikisha hutumii taulo na mtu mwingine kuzuia kupata maambukizi.
Unashauriwa pia kutovaa nguo za mtu mwingine kuondoa hatari ya kupata maambukizi.
Acha au punguza kunyoa mara kwa mara. Kuacha kunyoa huondoa hatari ya kupata vipele na uvimbe, uashauriwa kulinda ngozi yako kwa kuacha kunyoa kama inawezekana au punguza kunyoa mara kwa mara. Tafiti zinaonyesha kuacha kunyoa au kupunguza kunyoa hupunguza ukali na kutokea kwa tatizo.
Kujikinga na AKN ufanyaje?
Fanya mambo yafuatayo ili kujikinga na tatizo hili;
Usikate nywele kuwa fupi sana
Usivae nguo zinazobana shingo yako au kuletamsunguano nyuma ya shingo
Usitumie mafuta yenye grisi au pomade yanayoziba nywele kutoka kwenye shina lake wakatiinaota
Usivae kofia au helmeti kwani huleta msuguani kwenye maeneo ya nyuma ya shingo
Safisha maeneo ya nyuma ya shingo na acha yawe makavu. Hakikisha hutumii nguvu kusafisha maeneo hayo ili kuepuka kuchokoza ngozi yako na kusababisha majeraha na uvimbe.