top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Jumanne, 6 Aprili 2021

Gauti

Gauti

Gauti ni la Kiswahili linalotokana na neno tiba ni mojawapo ya magonjwa ya maungio ya mwili yanayosababishwa kwa kupanda kwa kiwango cha uric acid kwenye damu ikifahamika kwa jina jingine la hyperuricemia. Ugonjwa huu unaofahamika sana kwa watu wengi unaweza kumdhuru mtu yeyote yule.


Dalili za maumivu makali ya ghafla, kuvimba na kubadilika rangi kwa maungio ya mwili, haswa maugio ya kidole gumba cha mguu huwa ni dalili kuu ya ugonjwa wa gaout.


Endapo ugonjwa umegunduliwa mapema na kupatiwa matibabu yanayostahili, mgonjwa ataishi maisha ya kawaida kama watu wengine wasio na ugonjwa. Hata hivyo baadhi ya wagonjwa huwa hawapati nafuu kabisa kwa sababu ya kutopata elimu ya kutosha, utumiaji wa kupindukia wa pombe na kupata matibabu chini ya kiwango kutoka hospitali.


Dalili za Gauti


Unaweza kuamshwa usiku kwa dalili za maumivu ya makali ya ghafla ya umoto. Endapo utajishika maeneo yenye maumivu utahisi ni ya moto, yamevimba na kuwa na maumivu. Dalili hizi huonekana na kutoweka katika kipindi cha ugonjwa. Maelezo Zaidi ya dalili yapo hapa chini;


 • Hisia za maumivu makali sana ya maungio ya kidole gumba cha mguu, goti, kiwiko, vidole vya mikono na maungio ya kiganja cha mkono au maungio mengine ya mwili. Maumivu haya kwa mara ya kwanza huanzia kwenye maungio ya kidole gumba kisha hutokea maeneo ya maungio mengine

 • Maumivu makali sana kipindi cha masaa 12 toka yametokea

 • Baada ya kuisha kwa maumivu makali, utahisi maungio ya mwili yako hayapo vema na maumivu yakija mara nyingine yanaweza kuwa makali zaidi na kudhuru maungio mengine zaidi

 • Kuonekana kwa dalili za inflammation ambazo ni kuvimba, kuongezeka joto, maumivu na wekundu kwenye maungio yaliyoathiriwa

 • Kushindwa kujongesha kiungo cha mwili katika uelekeo asili wa kiungo


Wakati gani wa kumwona daktari unapokuwa na Gauti?


Mwone daktari wako kwa ushauri na tiba endapo


 • Unapata maumivu makali sana, ya ghafla ili upate matibabu, ukizembea kuna hatari ya kuharibika kwa anatomia ya maumbile ya maungio ya mwili wako.

 • Endapo maumivu yanaambatana na homa na kuongezeka joto kwenye maungio na uvimbe ambapo inamaanisha dalili ya maambukizi


Namna Gauti inavyotokea


Kwa kawaida mwili huzalisha kemikali ya uric acid kwenye damu kutokana na kuvunjwa vunjwa kwa seli na vyakula tunavyokula. Kiwango cha uric acid kwenye damu hudhibitiwa na figo kwa kutolewa nje ya mwili kupitia mkojo. Endapo kiwango kinachozalishwa ni kikubwa zaidi ya kiwango kinachotolewa kwenye mkojo, kiwango cha uric acid huongezeka mara dufu zaidi kwenye damu na kusababisha kuingia kwa uric acid kwenye maungio kisha kutengeneza madini ya urate yenye ncha za sindano na hivyo kuleta dalili za inflammation pamoja na maumivu makali.


Visababishi vya gauti


Kisababishi cha gauti ni kufanyika kwa madini chumvi yenye jina la urate kwenye maungio ya mwili, madini chumvi haya yanapokusanyika kwenye maungo ya mwili husababisha inflammesion na maumivu makali ya gauti. Kufanyika kwa madini chumvi kwenye maungo ya mwili huchangiwa na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uric acid kwenye damu kutokana na kuvunjwavunjwa kwa purine mwilini. Purine hutokana na vyakula unavyokula na seli zilizo ndani ya mwili.


Baadhi ya vyakula vilivyo na purine kwa wingi ni;


 • Nyama- haswa nyama nyekundu kama nyama ya mbuzi

 • Vyakula vya viungo vya ndani ya wanyama(ini n.k)

 • Vyakula vya viumbe wa baharini

 • Vyakula vinavyochochea utengenezaji kwa wingi wa uric acid ni

 • Vinywaji vyenye kilevi haswa bia

 • Vinywaji vitamu vyenye sukari aina ya fructose kama soda, juisi za kusindikwa n.k


Vihatarishi vya kupata gauti


Mtu anakuwa na hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa gauti endapo;


 • Unakula vyakula vyenye nyama kwa wingi, vyakula vya viumbe wa baharini, kunywa bia na vinywaji vyenye sukari ya fructose

 • Una uzito mkubwa kupita kiasi au ugonjwa wa obeziti- hii ni kutokana kuwa mwili wa wagonjwa wa obeziti huzalisha uric acid kwa wingi sana.

 • Unaugua ugonjwa wa presha ya juu( shinikizo la juu la damu), kisukari, magonjwa ya kimetaboliki, moyo na figo

 • Unatumia dawa jamii ya thiazide kutibu shinikizo la juu la damu, aspirini, dawa za kushusha kinga za mwili kama corticosteroid kwa wagonjwa waliopandikiziwa viungo kutoka kwa mtu mwingine

 • Kuwa na historia ya ugonjwa wa gauti katika familia yako ya damu moja

 • Kuwa mwanaume na umri kati ya miaka 30 hadi 50

 • Kuwa mwanamke katika kipindi baada ya komahedhi

 • Kufanyiwa upasuaji au kupata majeraha ya ajali


Vipimo na utambuzi wa ugonjwa wa Gauti


Utambuzi wa ugonjwa hutegemea historia ya ugonjwa inayopatikana kwa kuulizwa maswali na mtaalamu wa afya kuhusu vihatarishi na visababishi pamoja na dalili ulizonazo na vipimo vya maabara kuangalia kiwango cha uric acid kwenye damu na chumvi urate kwenye maungio yaliyoathiriwa.


Kipimo tambuzi kinachoonyesha tatizo ni kile cha kupima uwepo wa chumvi urate kwenye ute unaotoka kwenye maungio ya mwili yalio na tatizo.


Kipimo cha kupima kiwango cha uric acid kwenye damu huweza kufanyika pia lakini katika hatua za awali za ugonjwa kinaweza onyesha kiwango kuwa cha kawaida, endapo kiwango kwenye damu kitazidi miligramu 6.8 kwa kila decilita (6.8md/dL) na mtu akawa na dalili za gout basi itasemekana kuwa mtuu huyu ana madhaifu ya gout.


Kipimo kimojawapo pia kati ya xray, ultrasound na CT scan pia huweza agizwa fanyika ili kuangalia hatua za ugonjwa na uharibifu ambao umeshatokea kwenye maungo ya mwili


Matibabu


 • Matibabu ya gauti huhusisha matumizi ya dawa za kupunguza maumivu jamii ya NSAID, colchicine, corticosteroid na interleukins-1 antagonist

 • Utapewa dawa pia za kukinga kutokea kwa dalili na kukinga kutengenezwa kwa chumvi ya urate kwenye maungio ya mwili na kuondoa uvimbe kutokana na tatizo hili

 • Matibabu pia yanahusisha matibabu ya magonjwa mengine aliyonayo mgonjwa kama shinikizo la juu la damu, obeziti na kisukari pamoja na kupewa elimu ya vyakula vya kula a vya kutokula.

 • Kuhusu matibabu Zaidi soma kwenye Makala zinazohusi dawa za kutibu gauti.


Madhara ya Gauti


Gauti inaweza kuleta madhara endapo dalili zinajirudia rudia mara kwa mara. Kujirudia kwa dalili husababisha


 • Kuharibika kwa anatomia ya maungio

 • Kufanyika kwa vimbe kwenye maungio ya mwili

 • Kufanyika kwa mawe kwenye figo


Namna ya kujikingana Gauti


Ili kuweza kujikinga a madhara au kupata gauti unaweza kufanya mambo yafuatayo;


 • Kunywa maji ya kutosha kila siku hii inasaidia mwili kuondoa kiwango cha uric acid kwenye damu na kuondoa uwezekano wa kupata gauti

 • Dhibiti kiwango cha matumizi ya vinywaji vitamu vya kusindikwa haswa vyeye sukari ya fructose mfano juisi, soda, ice cream, na pipi. Kuwa na tabia ya kusoma kilichomo ndani ya kinywani ni nini.

 • Dhibiti kiwango cha kilevi uanchotumia, kunywa katika kiwango kinachoshauriwa kitalamu, chagua kinywaji ambacho ni salama kwako, hata hivyo tafiti zinaonyesha unywaji wa bia unaongeza hatari ya kupata gauti

 • Endapo unahitaji chakula cha protini, kipate kutoka kwenye maziwa yaliyopunguzwa mafuta

 • Dhibiti kiwango cha nyama, samaki na viumbe jamii ya ndege kama kuku, tumia kwiango kidogo endapo una tatizo la gauti kwani mwili wako unaweza kustahimili.

 • Usitumie nyama ya mbuzi, kondoo au nguruwe

 • Usile nyama za ndnai ya kiumbe kama ini, figo, tezi au kongosho

 • Usitumie samaki aina ya sardine, lobster, mussels, anchovies na shellfish

 • Kuwa na uzito kwenye unaotakiwa kiafya kwa kula vyakula vinavyokufanya usiongezeke na kuwa na uzito wa kiafya. Jifunze Zaidi kuhusu kupunguza uzito na kuwa na uzito wa kiafya katika Makala zingine ndani ya tovuti hii ya ULYCLINIC

 • Acha kufunga na kupunguza uzito kwa haraka kwani wakati wa kufunga kiwango cha uric acid huzalishwa kwa wingi Zaidi kutoka kwenye uvunjwaji wa protini kutoka kwenye mwili wako.


Vyakula vinavyofaa kwa mgonjwa mwenye gauti


Vyakula vipo vingi ambavyo anapaswa kutumia mgonjwa wa gauti, vyakula vilivyoorodheshwa hapa chini ni vizuri kwa sababu huwa havina purine na hupunguza hatari ya kupanda kwa kiwango cha uric acid kwenye damu kutokana na kuvunjwa kwa protini ndani ya mwili.


 • Maziwa yaliyopunguzwa mafuta kama maziwa mtindi

 • Matunda aina mbalimbali

 • Mboga za majani za aina mbalimbali

 • Karanga, siagi ya karanga na vyakula vya mbegu

 • Mafuta

 • Mayai kwa kiwango kidogo

 • Nyama ya samaki, kuku na nyama nyekundu kwa kiasi cha gramu 100 hadi 170 kwa siku

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

26 Oktoba 2021 21:05:59

Rejea za mada hii:

1. Hochberg MC, et al. Clinical gout. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 29.11.2020

2. Centers for Disease Control and Prevention. Gout. https://www.cdc.gov/arthritis/basics/gout.html. Imechukuliwa 29.11.2020

3. American College of Rheumatology Gout. http://www.rheumatology.org/Practice/Clinical/Patients/Diseases_And_Conditions/Gout/ . Imechukuliwa 29.11.2020

4. National Institute of Arthritis and Musculoskeletal and Skin Diseases . Questions and answers about gout. http://www.niams.nih.gov/Health_Info/Gout/default.asp. Imechukuliwa 29.11.2020

5. Prevention of recurrent gout . Becker MA. Pharmacologic urate-lowering therapy and treatment of tophi. https://uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 29.11.2020

6. National Center for Complementary and Integrative Health. Relaxation techniques for health. https://nccih.nih.gov/health/stress/relaxation.htm. Imechukuliwa 29.11.2020

7. Becker MA. Treatment of acute gout. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 29.11.2020

8. Becker MA. Prevention of recurrent gout: Lifestyle modification and other strategies for risk reduction. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 29.11.2020

9. Natural Medicines. Coffee. https://naturalmedicines.therapeuticresearch.com. Imechukuliwa 29.11.2020

10. Web md. Gout Diet: Foods to Eat and Those to Avoid .https://www.webmd.com/arthritis/gout-diet-curb-flares

11. 2020 American College of Rheumatology Guideline for the Management of Gout. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/32391934/. Imechukuliwa 29.12.2020

12. MSD manual for professional. https://www.msdmanuals.com/professional/musculoskeletal-and-connective-tissue-disorders/crystal-induced-arthritides/gout. Imechukuliwa 29.12.2020

bottom of page