Mwandishi:
Mhhariri
Dkt Benjamin L, MD
Dkt. Adolf S, MD, Dkt. Sospeter M, MD
Ijumaa, 17 Septemba 2021
Homa ya uti wa mgongo
Watu waishio katika ukanda wa homa ya uti wa mgongo Afrika hupata mlipuko wa homa hiyo kutokana na kuambukizwa kwa njia ya hewa bakteria Neisseria meningitidis. Baadhi ya dalili zake ni homa ya ghafla, maumivu makali ya kichwa, kukakamaa kwa shingo, kichefuchu na kutapika. Ili kutopoteza maisha, fika kituo cha afya karibu nawe kwa tiba ya haraka.
Homa ya uti wa mgongo kwa jina la kitiba meninjaitiz hutokana na michomo kinga kwenye maji au ukuta unaofunika mfumo wa kati wa fahamu inayoamshwa na maambukizi ya vimelea vya maradhi vinavyoweza kuwa bakteria, virusi, fangasi n.k
Mfumo wa kati wa fahamu umetengenezwa kwa ubongo na uti wa mgongo uliofunikwa kwa ukuta wa meninjo. Ndani ya ukuta huu kuna maji ya uti wa mgongo. Ukuta na maji haya hulinda ubongo na uti wa mgongo dhidi ya mitikisiko, majeraha na maambukizi yanayoweza kupenya na kuingia kwenye mfumo wa kati wa fahamu.
Maambukizi mengi ya meninjaitiz katika nchi za afrika husababishwa na maambukizi ya bakteria na katika nchi za watu weupe husababishwa na virusi. Fangasi na vimelea wanyonyaji huchangia kwa kiasi kidogo kusabaisha ugonjwa huu.
Baadhi ya wagonjwa wa homa ya uti wa mgongo wanaweza kupona bila matibabu ndani ya wiki chache hata hivo wengi wao wanahitaji tiba inayohusisha matumizi ya dawa zenye uwezo kuingia kwenye mfumo wa kati wa fahamu.
Kama una dalili zozote za homa ya uti wa mgongo, unapaswa kuonana na daktari haraka kwa matibabu.
Dalili
Dalili za homa ya uti wa mgongo awali huweza fanana na homa ya mafua. Dalili zinaweza kutokea taratibu na kuongezeka kwa kasi na hutofautiana pia kwa mtu mzima na watoto;
Umri wa miaka 2 na kuendelea huwa na dalili za;
Homa ya ghafla
Shingo kuwa ngumu
Maumivu makali ya kichwa yasiyo ya kawaida
Maumivu ya kichwa yanayoambatana na kichefuchefu na kutapika
Kukanganyikiwa na kupoteza uwezo wa kutulia kwenye wazo moja
Degedege
Kushindwa tembea
Kukosa usingizi
Macho kuumizwa na mwanga
Kukosa hamu ya kula
Kukosa kiu
Harara kwenye ngozi
Dalili kwa watoto chini ya miaka 2
Homa kali
Kulia lia wakati wote
Kukosa usingizi
Kutotulia
Kushindwa kuamka kutoka usingizini
Kutulia au Kupooza
Kula kwa shida
Kutapika
Kuvimba kwa utosi
Kukakamaa kwa mwili haswa shingo
Kushindwa bembelezeka na kulisa sana kama wakibebwa
Muda sahihi wa kuonana na daktari
Onana na daktari haraka kama ukipata dalili zifuatazo;
Homa
Maumivu makali ya kichwa yaliyo makali kupita kiasi
Kuchanganyikiwa
Kutapika
Kukakamaa kwa shingo
Meninjaitiz ya bakteria inaweza kuwa kali zaidi na kusababisha kifo kama mtu asipopata matibabu ya haraka. Matibabu ya haraka hupunguza kuharibiwa kwa ubongo na kifo.
Kama ndugu yako au rafiki ana dalili zilizotajwa hapo juu, unapaswa kumpeleka hoapitali akapate uchunguzi na tiba.
Ugonjwa mkali wa homa ya uti wa mgongo
Homa ya uti wa mgongo kutokana an bakteria hutishia maisha ya mtu na hivyo mtu yeyote anayeshukiwa kuwa na maambukizi haya hutibiwa kwa dawa za antibayotiki haswa katika nchi ambazo hazina uwezo wa kutambua haraka maambukizi hayo kwenye maji ya uti wa mgongo.Baadhi ya bakteria wanaosababisha homa kali ya uti wa mgongo ni;
Streptococcus pneumoniae (pneumococcus)
Neisseria meningitidis (meningococcus)
Meningococcal meninjaitiz
Haemophilus influenza (haemophilus)
Listeria monocytogenes (listeria)
Ugonjwa sugu wa homa ya uti wa mgongo
Vimela wanaozaliana kwa taratibu kama vile fangasi na bakteria Mycobacterium tuberculosis huweza vamia kuta ya meninjezi na kupelekea homa sugu ya uti wa mgongo.
Homa sugu ya uti wa mgongo huanza kuonekana kwa muda wa wiki mbili au zidi. Dalili za homa ya uti wa mgongo ya namna hii ni pamoja na maumivu ya kichwa, homa, kutapika na kukanganyikiwa.
Visababishi
Kisababishi kikuu cha homa ya uti wa mgongo ni maambukizi ya virusi ikifuatiwa na bakteria na kwa kiasi kidogo huchangiwa na fangasi au vimelea wanyonyaji. Fangasi na vimelea wanyonyaji husabisha mara nyingi homa sugu ya uti wa mgongo wakati huo ugonjwa mkali wa homa ya uti wa mgongo hutokana na uambukizo wa bakteria.
Homa ya uti wa mgongo kutokana na bakteria
Vimelea vya bakteria vilivyoingia kwenye damu vinaweza kupita na kuingia kwenye ubongo na uti wa mgongo na kusababisha maambukizi makali ya homa ya uti wa mgongo. Hata hivyo huweza tokea pia kama vimelea hao wameingia moja kwa moja kupitia sinaiz, masikio, fuvu lililopasuka kwa ajali na baadhi ya upasuaji.
Kuna aina kadhaa za bakteria wanaosababisha homa ya uti wa mgongo, wanaoongoza ni;
Streptococcus pneumoniae (pneumococcus)
Huongoza kusababisha maambukizi ya uti wa mgongo kwa vichanga na watoto wadogo. Bakteria huyu husababisha pia nimonia na maambukizi kwenye sikio.
Neisseria meningitidis (meningococcus).
Bakteria huyu husababisha homa ya uti wa mgongo pia magonjwa ya mfumo wa juu wa upumuaji. Homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na bakteria huyu hutokea kama kimelea kutoka kwenye mfumo wa juu wa upumuaji ataenya na kuingia kwenye damu na hufahamika kwa jina jingine la meningococcal meninjaitiz.
Meningococcal meninjaitiz
Ni ugonjwa unaosambukizwa kwa kasi na unaweza kusababisha homa ya uti wa mgongo ya mlipuko kwa watoto na vijana wadogo waliopo mashuleni, chuoni na shule za kulala. Mtu yeyote mwenye maambukizi haya anapaswa kupata matibabu ya antibayotiki hata kama amepata chanjo ya bakteria huyu.
Haemophilus influenza (haemophilus)
Bakteria Haemophilus influenzae aina B (Hib) awali alikuwa anaongoza kusababisha homa ya uti wa mgongo kutokana na bakteria kwa watoto. Chanjo ya Hib imesaidia kupunguza idadi ya watoto wanaougua homa hii.
Listeria monocytogenes (listeria)
Bakteria huyu hupatikana kwenye maziwa ambayo hayajachemshwa. Wajawazito, vichanga na wazee huwa hatarini kupata homa hii kutokana na kuwa na kinga ya mwili dhaifu. Kimelea huyu anaweza kupenya na kuingia kwa kichanga tumboni na kusababisha kifo kwa mtoto.
Homa ya uti wa mgongo kutokana na Virusi
Homa ya uti wa mgongo kutokana na virusi huwa ya wastani. Vrusi wanaoongoza kusababisha homa hii ni enteroviruses, kirusi herpes simplex,Kirusi HIV, kirusi mumps, kirusi West Nile na wengine pia.
Homa ya uti wa mgongo kutokana na fangasi
Homa ya uti wa mgongo ya fangasi ni nadra sana kutokea. huweza kufanana na dalili za homa kali ya uti wa mgongo, huenezwa kwa kupuva pumzi yenye vimelea vya fangasi kwenye udongo, mbao zilizooza na mavi ya ndege. Huwapata sana watu wenye upungufu wa kinga mwilini. Fangasi Cryptococcal, huongoza kusababisha homa ya uti wa mgongo kutokana na fangasi kwa wagonjwa wenye UKIMWI. Pasipo matibabu mgonjwa anaweza kupoteza maisha kirahisi na pia ugonjwa unaweza kujirudia hata baada ya matibabu ya kutumia dawa za fangasi.
Homa ya uti wa mgongo kutokana na fangasi
Homa ya uti wa mgongo ya fangasi ni nadra sana kutokea. Dalili zake huweza fanana na dalili za homa kali ya uti wa mgongo, huenezwa kwa kuvuta pumzi yenye vimelea vya fangasi kwenye udongo, mbao zilizooza na mavi ya ndege. Huwapata sana watu wenye upungufu wa kinga mwilini. Fangasi Cryptococcal, huongoza kusababisha homa ya uti wa mgongo kutokana na fangasi kwa wagonjwa wenye UKIMWI. Pasipo matibabu mgonjwa anaweza kupoteza maisha kirahisi na pia ugonjwa unaweza kujirudia hata baada ya matibabu ya kutumia dawa za fangasi.
Homa ya uti wa mgongo ya vimelea wanyonyaji
Vimelea wanyonyaji ( parasaiti) husababisha homa ya uti wa mgongo kwa nadra sana, homa yao hufahamika pia kama meninjaiitiz ya eosinophilic, hii ni kutokana na mwili kuzalisha chembe za ulinzi eosinophil ili kupambana na kimelea huyu. Baadhi ya vimelea wanyonyaji ni tapeworm (anayesabanisha sistiserkosis) na kimelea cha malaria anayesababisha malaria ya kichwani.
Kimelea cha amoeba pia kinaweza sababisha homa ya uti wa mgongo lakini kwa nadra sana. Mtu anaweza kupata maambukizi kutoka kwenye dimbwi la kuogelea na kula chakula chenye vimelea na huenezwa kati ya mtu mmoja na mwingine pamoja na wanyama.
Visababishi vingine vya homa ya uti wa mgongo
Kuna sababu zingine zisizohusiana na vimelea zinazoweza kupelekea homa ya uti wa mgongo kama vile mwitikio wa mwili kwenye kemikali, dawa na aina fulani ya saratani na magonjwa ya michomo kwa mfano sarcoidosis.
Vihatarishi
Vihatarishi vya kupata homa ya uti wa mgongo ni pamoja na;
Kutopata chanjo au kuruka chanjo wakati wa utoto au utu uzima
Umri chini ya miaka 5 kwa homa ya kirusi au umri chini ya miaka 20 kwa homa ya bakteria
Kuishi kwenye mkusanyiko wa watu mfano chuoni, shuleni, jeshini, kwenye hosteli shule za kulala.
Maeneo haya huongeza hatari ya kuambukizana homa ya uti wa mgongo ya meningococcal kwa kuwa huambukizwa kwa njia ya hewa
Ujauzito. Huongeza hatari ya kupata homa ya uti wa mgongo ya listeriosis. Listeriosis huongoza hatari ya mimba kutoka, kujifungua mtoto mfu na kabla ya wakati.
Upungufu wa kinga mwilini. Upungufu wa kinfa mwilini kutokana na magonjwa kama kisukari, pombe, dawa za kushusha kinga na HIV huongeza hatari zaidi ya kupata maambukizi
Utambuzi
Daktari anaweza kutambua kama mgonjwa ana homa ya uti wa mgongo kwa kuulizwa maswali na kufanya uchunguzi wa mwili kabla ya kufanya kipimo.
Vipimo
Baadhi ya vipimo tambuzi vinavyofanyika ni;
Kipimo cha gramu stain
Kuotesha damu
Kipimo cha Computerized tomography (CT) ya kifua au uti wa mgongo
Kipimo cha magnetic resonance imaging (MRI) ya kichwa
Picha ya mionzi ya kifua
Kipimo kingine huhusisha kupima maji kutoka kwenye uti wa mgongo kwa kutumia sindano ndogo inayochomwa chini ya mgongo. Maji hayo hufanyiwa vipimo vifuatavyo;
Kiwango cha Glukosi
Kiwango cha protini
Kiwango cha chembe nyeupe za damu
Kuotesha bakteria
PCR
Matibabu
Matibabu ya homa ya uti wa mgongo hutegemea kisabababishi, hata hivyo katika vituo vya afya au taasisi za tiba zisizo na vipimo tambuzi vya haraka zinaweza kutibu kwa kulenga kupewa dawa zinazoweza kutibu homa ya uti wa mgongo kutokana na bakteria, virusi na fangasi.
Matibabu ya homa ya uti wa mngongo kutokana na bakteria
Maambukizi makali huhusisha matumizi ya;
Corticosteroid ya kuchoma kwenye mishipa ili kupunguza michomo kinga. Kuchomwa dawa hii hupunguza madhara yanayoweza kujitokeza
Dawa za antibayotiki bakteria vimelea wanaodhuriwa na dawa hii
Kama una maambukizi wkenye sinus, daktari atafanya upasuaji mdogo kuondoa uchafu kwenye sinus na fupa mastaoid
Homa ya uti wa mgongo kutokana na virusi
Homa ya uti wa mgongo kutokana na virusi huisha pasipo matibabu ndani ya wiki chache. Matumizi ya dawa za antibayotiki huwa hayana faida na haziwezi kutibu maambukizi ya virusi. Kwa nchi zisizojiweza kutambua haraka kisababishi, mara nyingi hutumia dawa za antibayotiki. Kama homa ya uti wa mgongo imesababishwa na kirusi, matibabu huhusisha;
Kupumzika
Kunywa maji ya kutosha
Matumizi ya dawa ya kupunguza maumivu
Matumizi ya dawa jamii ya corticosteroid ili kupunguza michomo katika mfumo wa kati wa fahamu kutokana na virusi
Kama unapata degedege, utapata dawa za kuzuia degedege
Dawa za virusi pia zinaweza kutumiaka kama homa ya uti wa mgongo imesabishwa na vkirusi herpes
Matibabu ya homa ya uti wa mgongo isiyosababishwana maambukizi
Kama kisababishi hakifahamiki, daktari atakutibu kwa kutumia dawa za virusi pamoja na dawa za antibayotiki, ni bora zaidi kutumia dawa hizi kuliko kuchelewa ili kuokoa maisha. Dawa za fangasi pia hutumika katika matibabu ya homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na fangasi. Homa ya uti wa mgongo kutokana na kimelea cha Kifua kikuu hutibiwa kwa kutumia dawa za kifua kikuu.
Hata hivyo matibabu ya homa ya uti wa mgongo kutokana na TB au fangasi yanaweza kuanzishwa baadaye baada ya majibu ya vipimo kurejea
Homa ya uti wa mgongo kutokana na saratani hutibiwa kwa kutumia dawa za kuondoa chembe za saratani.
Kinga na chanjo
Kwa sababu vimelea wengi wanaosababisha homa ya uti wa mgongo iliyo kali inaweza kuenezwa kwa njia ya kukohoa, kupiga chafya, kubusu, kushiriki vyombo vya kulia, mswaki na sigara, kwa kufanya njia zifuatazo unaweza kupunguza hatari ya kupata homa ya uti wa mgongo.
Safisha mikono yako
Nawa mikono kwa maji safi au vitakasa mikono kuzuia kueneza vimelea au kupata vimelea kabla na baada ya kula, baada ya kutoka eneo lenye mkusanyiko wa watu na kwenye malisho ya wanyama.
Kuwa msafi
Usishiriki kutumia vyombo vya mtu mwenye maambukizi--mfano besini, sahani n.k pia epuka kutumia vitu vya mtu mwingine kama lipbam, mswaki n.k. wafundishe watoto pia kutofanya hivyo.
Ishi kiafya
Ili kufanya kinga ya mwili wako kuwa imara, unatakiwa kupata usingizi wa kutosha, kula mlo kamili( kutoka kwenye makundu matano ya chakula) na kufanya mazoezi
Funika midomo wakati wa kukohoa
Tumia tishu au kiwiko cha mono wakati wa kukohoa na kupiga chafya badala ya kutumia mikono yako
Kuwa makini na vyakula
Kwa mjamzito, unapasws akuwa makini na vyakula ili kuepuka hatari ya kupata maambukizi ya listeria kwa kula vyakula vilivyopoa. Epuka kula mazao ya maziwa na maziwa yasiyochemshwavema.
Chanjo
Kuna baadhi ya chanjo zinapatika na zinatumika katika kinga ya homa ya uti wa mgongo kutokana na bakteria kama vile
Chanjo ya Haemophilus influenzae aina b (Hib) inayotolewa utotoni
Chanjo ya Pneumococcal conjugate (PCV13)
Chanjo ya Pneumococcal polysaccharide (PPSV23)
Chanjo ya Meningococcal conjugate