Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Jumatatu, 5 Aprili 2021

Kuvunjika uume
Watu wengi wanashangaa kama kweli uume unaweza kuvunjika, hii ni kwa sababu inafahamika kuwa kitu kinachovunjika ni kile chenye mifupa tu. Ni kweli kwamba uume hauna mfupa lakini unaweza kuvunjika pale unapopata ghasia wakati umesimama.
Ni nini ndani ya uume huvunjika?
Uume husimama pale damu nyingi imeingia ndani ya silinda zinazobeba damu ndani ya uume zenye jina la corpora cavernosa zilizofunikwa kwa ukuta wenye jina la tunica albuginea. Endapo silinda hizi zenye damu iliyo na shinikizo zitapindishwa ghafla au kwa lazima, kuta ya silinda mojawapo au zote mbili huweza pasuka na kupelekea tatizo la kuvunjika. Kwa maelezo zaidi kuhusu silinda za uume ingia katika sehemu nyingine ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC kusoma kuhusu maumbile ya uume.
Nini kinaweza kusababisha uume kuvunjika?
Kuvunjika uume kunaweza kusababishwa na sababu mbalimbali ambazo ni;
Kuchomoka kwa uume ndani ya uke kisha kujigaongesha kwenye fupanyonga kwa bahati mbaya
Kujichua kwa kutumia nguvu
Kukunja uume
Dalili
Dalili kuu ya uume uliovunjika nikupinda kwa uume au kuonekana kwa uvimbe katika mpini wa uume unaoonekana kuwa na rangi ya zambarau. Dalili zingine ni
Maumivu makali kwenye uume yanayoanza ghafla
Sauti ya kuvunjika kitu kwenye uume
Uume kusinyaa ghafla
Kuvimba kwa mpini wa uume
Kubadilika rangi kwa mpini wa uume
Kutokwa damu kwenye mrija wa uume(kwa baadhi ya nyakati endapo mrija wa mkojo pia umepasuka)
Mapozi hatarishi kuvunjika uume
Mapozi ya kujamiana yenye uhusiano mkubwa na uuume kuvunjika
Tafiti zinaonyesha mapozi yafuatayo huhusiana na uume kuvunjika
Kujamiana pozi ya mbwa kati ya mwanamke na mwanaume
Kujamiana mwanamke akiwa amelala juu ya mwanaume
Ni nini cha kufanya endapo uume umevunjika?
Endapo uume wako umevunjika, utahitaji matibabu ya haraka sana ili kuokoa uume wako. Daktari atakuona na kutambua tatizo lako kwa kufanya uchunguzi wa mwili wako na baadhi ya vipimo kama vitahitajika. Endapo vipimo vitahitajika, vifuatavyo hufanyika;
Kipimo cha ultrasound
Matibabu
Matibabu ya uume uliovunjika ni upasuaji wa kuunga mirija iliyopasuka. Upasuaji huuu hufanyika kwa kufungua uume kisha kukagua mrija uliopata shida na kuushona
Madhara
Endapo hautapata matibabu, uume uliovunjika unaweza kusababisha uume wako kupinda au tatizo la kudumu la uume kushindwa simama au kujaa vema kwa tendo la kujamiana.