Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin Lugonda, MD
11 Juni 2021 13:17:00
Kukojoa kitandani kwa mtu mzima
Kukojoa kitandani mara nyingi ni tatizo linalotokea kwa watoto wadogo na huisha jinsi anavyokuwa, hata hivyo baadhi ya watoto huendelea mpaka ukubwani. Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 1 hadi 2 ya watu wazima hukojoa kitandani, kukojoa kitandani kwa watu wazima huambatana na aibu naam hata ya kutafuta msaada kutoka kwa wataalamu wa afya.
Endapo utakojoa mara moja au mbili kwa mwaka inaweza kuwa bahati mbaya, na kutomaanisha kuwa kuna shida na hata hivyo hutokea kwa baadhi ya watu. Endapo mtu anakojoa mara kwa mara kitandani, anapaswa kufanyiwa uchunguzi ili kufahamu kisababishi ili kupata tiba sahihi. Mingoni mwa visababishi vya kukojoa kitandani kwa watu wazima ni;
Madhaifu ya mishipa ya mfumo wa fahamu
Kuziba kwa mfumo wa mkojo
Madhaifu ya kijeni
Maumbile yasiyo kawaida ya mfumo wa mkojo
Matumizi ya dawa
Kukatishwa kwa upumuaji wakati umelala
Maambukizi mfumo wa mkojo
Ugonjwa wa Kisukari
Ufanyaji kazi kupita kiasi wa misuli ya kibofu
Saratani kwenye mfumo wa mkojo
Uwezo mdogo wa kibofu kutunza mkojo
Madhaifu ya homoni
Mmaelezo zaidi kuhusu visababishi hivi yanapatikana kwenye aya zzinazofuata
Madhaifu ya homoni
Homon ADH hutuma ujumbe kwenye figo kupunguza uzalishaji wa mkojo wakati wa usiku. Homon hii huzalishwa wakati wa usiku ili kukuandaa kulala. Baadhi ya watu wanaokojoa kitandani inaonekana kuwa kiwango cha homoni ADH huwa kipo chini ya kiwango cha kawaida wakati wa usiku na hivyo figo zao huendelea kuzalisha mkojo kama ilivyo mchana , hii hupelekea baadhi ya watu kukojoa kitandani.
Kipimo cha ADH kinaweza fanyika hospitalini na endapo homon hii imeonekana ni kidogo, mgonjwa atapatiwa dawa.
Uwezo mdogo wa kibofu kutunza mkojo
Kuwa na uwezo mdogo wa kibofu kutunza mkojo haimaanishi mara zote kuwa na kibofu kidogo, bali humaanisha hisia za kibofu kijaa zinatokea mapema kabla ya kibofu kuwa na mkojo wa kutosha. Kwa wagonjwa wenye tatizo hili hufunzwa zoezi maalumu la kuongeza uwezo wa kibofu kukaa na mkojo. Soma namna gani kwenye maelezo ya matibabu yasiyo dawa.
Ufanyaji kazi kupita kiasi wa misuli ya kibofu
Misuli ya kibofu kwa jina la detrusor hutepweta pale mkojo unapoingia kwenye kibofu na kusinya wakati wa kukojoa ili kusukuma mkojo nje. Endapo misuli hii inafanya kazi kinyume, uwezo wa kutunza mkojo hupungua na kupelekea kukojoa kitandani. Hali hii inaweza kusababishwa na ufanyaji kazi usio kawaida wa mishipa ya fahamu kati ya bongo na kibofu. Visababishi vingine ni matumizi ya vinywaji vyenye kafeini, pombe na dawa aina fulani.
Saratani ya mfumo wa mkojo
Saratani ya kibofu cha mkojo au tezi dume huharibu mirija inayotoa mkojo nje ya kibofu, hii huambatana na kupoteza uwezo wa kudhibiti mkojo unaotoka haswa wakati wa usiku. Utambuzi wa saratani ni kwa kutumia vipimo vya uchunguzi wa awali wa mwili na daktari au vipimo vya biopsi au picha ya ultrasound na X-ray na kipimo cha damu.
Ugonjwa wa Kisukari
Ugonjwa wa kisukari ambao haujadhibitiwa vema huambatana na kupata kiu sana na kukojoa mara kwa mara, hii ni sababu figo huongeza kiwango cha mkojo ili kuhibiti kiwango sukari kwenye damu na hivyo kupelekea kukojoa mara kwa mara hata wakati wa usiku. Endapo utadhibiti sukari kwenye damu kwa njia ambazo umeambiwa na daktari wako. Tatizo hili litapungua au kuisha.
Kukatishwa kwa upumuaji usiku
Hali hii hutokea kwa baadhi ya watu, ni vigumu kutambua isipokuwa endapo unapata dalili( soma kwenye makala nyingine). Kukata kwa pumzi hutokea pale endapo upumuaji unasimama ghafla kwa sekunde kadhaa kisha kuanza wakati mtu amelala. Miongoni mwa visababishi vya tatizo hili ni magonjwa ya mfumo wa hewa, kuziba kwa njia ya hewa au kuziba kwa njia ya hewa na ute unaozalishwa kinywani, kulala pozi baya n.k. tafti zinaonyesha watu wenye shida hii hukojoa kitandnai wakati wa usiku. Kupata matibabu kutasaidia kupunguza au kuondoa tatizo la kukojoa.
Maambukizi mfumo wa mkojo
Maambukizi ya UTI yanafahamika sana kusababisha mtu kukojoa mara kwa mara wakati wa mchana au usiku. Kuwa na tatizo hili hupelekea hatari ya kujikojolea kitandani. UTI inatibika hivyo ni vema kupata uchunguzi kisha kupewa dawa. Endapo kisababishi ni UTI utapata dalii zingine za UTI na utakapopata matibabu tatizo litaisha.
Matumizi ya dawa
Baadhi ya dawa husababisha kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku kwa kuwa huongeza uzalishaji wa mkojo, na kuongeza hatari ya kukojoa kitandani wakati umelala. Baadhi ya dawa hizo dawa za usingizi, dawa jamii ya antisaikotiki, dawa za kupunguza maji mwilini jamii ya diuretiksi n.k. Endapo unadhani kuwa dawa ndo zinakupelekea kukojoa kitandani, wasiliana na daktari wako ili akubadilishie dawa kama kuna mbadala.
Madhaifu ya kijeni
Tatizo la kukojoa kitandani limeonekana kutembea kwenye famiilia yaani kurithiwa, hata hivyo wana sayansi bado hawajafanikiwa kufahamu ni jeni gani inayohusika kusafirisha tatizo hili kwenye familia au ukoo. Kabla daktari hajafika kusema hili linaweza kuwa tatizo la kurithi, atafanya vipimo vya kuangalia visababishi vingine kwanza. Hata hivyo endapo tatizo limefahamika kuwa ni la kurithi, matibabu yatahusisaha njia za kawaida za kubadilisha mtindo wa maisha kama ilivyoandikwa kwenye kipengele cha matibabu yasiyo dawa kwenye makala hii.
Maumbile yasiyo kawaida ya mfumo wa mkojo
Kwa kawaida mkojo huzalishwa kwenye figo kisha husafiri kupitia mirija ya ureta kuelekea kwenye kibofu cha mkojo na kisha kutoka nje ya mwili kupitia mrija wa yurethra. Endapo kuna shida katika mfumo huu wa kutoa mkojo kutokana na madhaifu kama makovu, kupinda au kuwa na maumbile yasiyo ya kawaida, mtu hupata dalili za kukojoa kwa shida, kukojoa mara kwa mara na hivyo kukojoa kitandani. Daktari atafanya vipimo vyaultrasound au X ray kuangalia kama kuna shida kwenye mfumo wa mkojo, endapo shida itaonekana na ukapata tiba, tatizo litaisha.
Madhaifu ya mishipa ya mfumo wa fahamu na Kuziba kwa mfumo wa mkojo
Madhaifu ya mishipa ya mfumo wa fahamu
Madhaifu yanayofahamika kutokea kwenye mfumo wa mkojo na kuathiri tabia ya ukojoaji ni ugonjwa wa multiple sclerosis na parkinson’s pamoja na madhaifu ya kifafa. Kupata matibabu sahihi ya matatizo haya husaidia kuondoa tatizo la kukojoa kitandani.
Kuziba kwa mfumo wa mkojo
Njia za mkojo zinaweza kuzibwa na mawe kwenye figo, kibofu au saratani kwenye mfumo wa mkojo. kuziba huku husababisha mkojo kupita kwa shida na hivyo huambatana na kukojoa mara kwa mara na kukojoa kitandani. Mawe kwenye kibofu au njia ya mkojo pia hupelekea misuli ya kibofu cha mkojo kufanya kazi kupitiliza. Kupata matibabu ya matatizo haya endapo yamegundulika hupelekea kupotea kwa shida ya kukojoa mara kwa mara na kukojoa kitandani.
Matibabu
Matibabu huhusisha matibabu yasiyo dawa, matibabu dawa na matibabu ya upasuaji kwa baadhi ya matatizo;
Matibabu yasiyo dawa
Matibabu haya hufanyika kwa watu wazima au watoto soma kwa maelezo zaidi
Kuzawadia
Njia hii hufanyika kwa kumpa zawadi mtoto endapo amefikia malengo fulani mliyokubaliana, mfano endapo mtoto ataenda chooni kabla ya kwenda kulala, au kukusaidia kutandika kitanda endapo amekojoa kitandani. Utaangalia ni zawadi gani utampatia mtoto mfano unaweza mpatia stika nzuri ambayo mtoto ataweka kwenye kalenda siku ambayo hajakojoa kitandani, kisha endapo amefikia malengo labda ya kuwa na zawadi ya stika 4 au 5 kwa wiki, atapatiwa zawadi nyingine ndogo. Njia hii ni nzuri kwa watoto wadogo tu.
Kukojoa kabla ya kulala na mida Fulani wakati wa usiku
Mtu mzima na Watoto wengi hupelekwa au huenda chooni muda kabla ya kulala, wazazi pia wanaweza kuwafunza watoto wao kuamka mara kadhaa wakati wa usiku ili kukojoa. Kufanya hivi kwa kujirudia rudia muda ule ule, kutamfunza mtoto kuwa na tabia ya kuamka muda huo kwenda chooni kukojoa mwenyewe.
Kutumia king’ora cha mkojo
Kuna aina tofauti za ving’ora vya kuamsha mtoto au mtu mzima kabla ya kujikojolea ambavyo huwekwa kwenye nguo ya ndani. King’ora cha mkojo hupiga kelele tone la kwanza linapotoka na hivyo mtu(mtoto) huacha kukojoa na kuamka.
Kwa siku za mwanzo, inaweza kuwa usumbufu kwa mama au mtoto kwa kuwa usingizi huwa unakatishwa na sauti za mara kwa mara za king'ora, hata hivyo baada ya muda kupita utazoea hali hiyo na mtoto au mtu mzima atakuwa na uwezo wa kuamka bila hata kutumia king’ora hiko. Vingor’a hivi vinapatikana sehemu nyingi na pia unaweza kununua kwa kuagiza mtandaoni.
Dhibiti kiwango cha maji kabla ya kulala
Baadhi ya wazazi huzuia watoto kukojoa kitandani kwa kuwazuia wasinywe maji mengi au kutotumia kabisa kimiminika chochote wakati karibu na kulala. Jambo hili ni jema, hata hivyo endapo mtoto ana kiu ya maji, mpatie maji ya kunywa. Zuia mtoto asitumie vinywaji vyenye sukari au kafeini kwa kuwa huongeza uzalishaji wa mkojo. Kwa ufanisi zaidi, usimpatie mtoto maji ya kunywa masaa mawili kabla ya kulala.
Kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo
Mafunzo ya kibofu kutunza mkojo na kuongeza uwezo wake wa kukaa na mkojo hulenga kuongeza kiwango cha mkojo kinachotunzwa na kibofu na hivyo kutunza mkojo mwingi wakati wa usiku. Hii hufanyika mchana kwa kumfunza mtoto(mtu mzima) kutokojoa pale anapopata hamu ya kwenda kukojoa, unaweza anza kuzuia mkojo dakika 10 kisha kuruhusu akojoe na kuongeza muda jinsi siku au wiki zinavyokwenda, wasiliana na daktari kufahamu namna gani ya kufunza kibofu na endapo inafaa kwako. Zoezi hili hupunguza tatizo la kukojoa kitandani. Njia hii ni nzuri endapo itaunganishwa na njia zingine.
Matibabu ya dawa
Dawa zinazotumika katika matibabu ya tatizo la kukojoa kitandani ni;
Desmopressin Acetate (DDAVP)
Hyosyamine (Levsinex)
Imipramine
Oxybutynin (Ditropan)
Matibabu upasuaji
Aina za upasuaji unaoweza kufanyika ni upasuaji wa;
Kuamshwa kwa mishipa ya sacral
Upasuaji wa kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo
Upasuaji wa kupunguza misuli ya kibofu ( detrusor)
Upasuaji wa kurekebisha henia ya viungo vya mwili kwa wanawake
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021 04:52:52
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Brown AM, et al. Adult obstructive sleep apnea with secondary enuresis.
ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC1303181/. Imechukuliwa 11.06.2021
2. Kuehhas FE, et al. Infantile enuresis: Current state-of-the-art therapy and future trends.
ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3151581/. Imechukuliwa 11.06.2021
3. McInnis RP, et al. CPAP treats enuresis in adults with obstructive sleep apnea. DOI:
10.5664/jcsm.6776. Imechukuliwa 11.06.2021
4. Shah AP.Polyuria.merckmanuals.com/professional/genitourinary-disorders/symptoms-of-genitourinary-disorders/polyuria. Imechukuliwa 11.06.2021
5. Sinha R, et al.Management of nocturnal enuresis – myth and facts. DOI:
10.5527/wjn.v5.i4.328. Imechukuliwa 11.06.2021
6. von Gontard A, et al.The genetics of enuresis: A review.
ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/11696807. Imechukuliwa 11.06.2021