Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Peter A, MD
5 Novemba 2021 09:58:21
Magonjwa ya ulimi
Kuna zaidi ya magonjwa kumi ya ulimi, magonjwa hayo yanaweza kusababishwa na majeraha, maambukizi ya bakteria, fangasi au virusi pamoja na saratani. Sehemu hii imeorodhesha baadhi ya magonjwa yanayotokea sana kwenye ulimi;
​
Thrashi( fungasi kwenye ulimi)- husababishwa na maambukizi ya fangasi aina ya candida, hutokea kwa watu wenye kinga ya mwili iliyo dhaifu
Ulimi vinyweleo vyeusi- husababisha ulimi uonekane wenye vinyweleo vyenye rangi nyeusi bila maumivu yoyote. Tatizo hili hutokea pale endapo vinyweleo vya ulimi vimekuwa virefu na kuwavutia bakteria wa kinywa kufanya makazi na kuzaliana na kuanya ulimi uonekane mweusi wenye vinyweleo vingi. Visababishi vingine ni pamoja na matumizi ya dawa za antibayotiki, kutosafisha ulimi vema, kuvuta sigara, kunywa kahawa kwa wingi, na kutozalishwa kwa mate ya kutosha.
Vidonda vya kanka, hutokea sana kwenye kuta za kinywa na au kwenye ulimi, hupona ndani ya siku chache hadi wiki mbili, vidonda hivi huleta maumivu wakati wa kula au kunywa (bonyeza hapa kusoma zaidi)
Licheni planazi- ni harara zinazotokea kwa nadra sana, huonekana kama mwinuko wenye rangi nyeupe, miinuko hii huwa na ukubwa tofauti tofauti na huwa na sifa ya kungaa na hukaa kwenye ulimi au kwenye mashavu ya midomo. Tatizo hili huambatana na maumivu pamoja na vidonda kwenye kinywa na ulimi. Huweza kutibiwa kwa kutumia dawa za kunywa au kupaka. Endapo tatizo ni sugu huweza kupelekea kuwa saratani. Ugonjwa huu huweza kuathiri sehemu zingien za ngozi katika mwili pia.
Ulimi jiografia/ulimi ramani- Ulimi wa jiografia au ulimi ramani(ilimi kuwa na mabaka) kwa lugha ya kiingereza "geographic tongue" hutokana na ni michomo ya kinga za mwili ambayo huathiri sakafu ya juu au kwenye pembe za kushoto na kulia ya ulimi. Tatizo hili halina madhara yoyote kwa binadamu. Tafiti nyingi zimeonesha ulimi jiografia huambatana na matatizo ya pumu ya Ngozi, licheni planas na soriasisi (bonyeza hapa kusoma zaidi)
Saratani ya ulimi- Aina kadhaa za saratani zinaweza kuathiri ulimi na mara nyingi huanzia kwenye ukuta wa ngozi ya ulimi uliotengenezwa na seli za squamous. Matibabu na hatima ya saratani ya ulimi hutegemea aina ya saratani iliyoathiri ulimi. Visababishi vinaweza kuwa, uvutaji wa sigara, kunywa kupindukia(pombe) kukaa kweney jua kwa muda mrefu, historia ya saratani kwenye familia, maambukizi ya virusi vya HPV. (bonyeza hapa kusoma zaidi)
Vipele vya uongo- kutokana na historia, vipele hivi vinasemekana hutokea endapo mtu akisema uongo. Vipele hivi hutokana na shambulio la kinga za mwili kwenye ulimi na hutokea hata kama wewe unazungumza ukweli mtupu. Hupotea vyenyewe ndani ya siku kadhaa lakini husababisha hofu kwa mtu. Visababishi huweza kuwa ni mwitikio wa kinga za mwili dhidi ya chakula(aleji) au majeraha madogo kwenye ulimi kutokana na kujing’ata ulimi. Huhitaji matibabu lakini endapo maumivu ni makali unaweza kutumia dawa kuweka kinywani ili kupunguza maumivu. Soma hapo chini kuhusu ugonjwa wa kawasaki
Leukoplakia-Ulimi huonekana kuwa na rangi nyeupe kama maziwa mgando, ugonjwa huu hutokea kwa watu wenye kinga za mwili za chini kutokana na magonjwa yanayoshusha kinga za mwili, matumizi ya dawa za saratani n.k
Ugonjwa wa Kawasaki- huonekana kweye ulimi kwa kusababisha ulimi kuwa na rangi nyekundu sana na vipele vidogo- huu huwa dalili za awali za ugonjwa wa Kawasaki au homa ya skaleti
Upungufu wa vitamin B3- husababisha ulimi kuwa na rangi nyekundu lakini huwa mlaini na wenye kuuma.
Ulimi kuwa mkubwa kupita kiasi(makroglosia)
Ulimi uliopasuka/ulimi mifereji-Ulimi uliopasuka na kuwa na mifereji (ulimi kuchanika) ni tatizo linalojulikana sana, tatizo hili hutokana na matatizo asili ya kiuumbaji na hakuna kisababishi kinachofahamika kusababisha tatizo hili. Hata hivyo tatizo hili si saratani wala halina hatari ya kuwa saratani. (bonyeza hapa kusoma zaidi)
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 20:02:03
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada