Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Sospeter B, MD.
31 Machi 2025, 12:05:26

Jinsi ya kutunza kidonda cha upasuaji wa kujifungua nyumbani
Upasuaji wa kujifungua (Caesarean Section) ni njia inayotumika kumtoa mtoto tumboni mwa mama pale ambapo kujifungua kwa kawaida kunashindikana kutokana na sababu mbalimbali. Baada ya upasuaji na kuruhusiwa kurudi nyumbani ni muhimu kutunza kidonda vizuri ili kuzuia maambukizi na kuharakisha uponaji.
Makala hii imeelezea mbinu mbali mbali za utunzaji wa kidonda pamoja na dalili na viashiria vya maambukizi katika kidonda.
Utunzaji wa kidonda
Ili kuhakikisha kidonda kinabaki safi bila maambukizi mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia;
Usafi wa kidonda
Epuka maji kugusa kidonda wakati wa kuoga kwa muda wa siku 7 kamili.
Unaweza kuanza kuoga kwa kutumia maji kidogo kwa kufuta mwili kwa taulo safi huku ukifunika kidonda kwa kitambaa kisafi juu ya bandeji ili kuhakikisha maji hayagusi kidonda. Baada ya siku hizo kidonda kinakuwa kimepona kwa kiwango kikubwa na unaweza kuoga kwa maji mengi huku ukisafisha eneo la kidonda taratibu kwa maji safi na sabuni na kukausha kwa kitamba safi.
Miongozo ya kuoga na utunzaji wa kidonda hutofautiana kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea. Katika nchi zinazoendelea upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na bandeji zisizoruhusu maji kuingia kwenye kidonda ni changamoto, hivyo mbinu ya kuzuia kidonda kuingia maji kabla ya siku 7 hutumika kuhakikisha mama hapati maambukizi. Katika nchi zilizoendelea wagonjwa huoga mapema bila kuhatarisha uponaji wa kidonda.
Epuka kugusa kidonda mara kwa mara
Kugusa kidonda mara kwa mara hususani ukiwa hujanawa kwa maji na sabuni kunaweza kuleta vijidudu vinavyosababisha maambukizi.
Badilisha bandeji
Shughuli zote za kubadilisha bandeji zinatakiwa kufanyika hospitali kwa kufuata utaratibu utakaopewa wakati wa kuruhusiwa kurudi nyumbani.Usichukue uamuzi wa kubadilisha bandeji nyumbani hata kama imelowa bila kupata ushauri na maelekezo ya daktari wako na ikiwa kidonda kimekauka na daktari ameshauri kukiacha wazi, usifunikie ili kisaidie kupona haraka.
Tumia dawa ulizopewa kwa usahihi
Wakati wa kuruhusiwa kurudi nyumbani mama hupewa dawa za antibayotiki na dawa za maumivu, lengo ni kukinga kidonda dhidi ya maambuki na kupunguza maumivu. Ili dawa zifanye kazi vizuri zingatia dozi na muda sahihi wa kunywa kama ulivyoandikiwa na daktari.
Kufanya mazoezi
Kufanya mazoezi baada ya upasuaji wa kujifungua husaidia kupunguza maumivu, kuimarisha misuli, kusaidia kurudi kwa mji wa mimba katika hali yake ya kawaida, kusaidia utoaji wa uchafu wa uzazi (lochia), kuimarisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na njia ya mkojo, pamoja na kuharakisha uponaji wa kidonda. Si hivyo tu pia husaidia kupunguza hatari ya kuganda kwa damu baada ya upasuaji.
Mazoezi muhimu yaliyopendekezwa ni pamoja na: Mazoezi ya kegeli, kutembea, mazoezi ya kupumua, na kunyoosha mwili taratibu. Unaweza kufunga mkanda wa tumbo ili kuzuia mtikisiko wa tumbo ambao unaweza kuleta maumivu wakati wa mazoezi.
Licha ya umuhimu wa mazoezi katika uponaji wa kidonda unapaswa kuwa muangalifu na epuka mambo yafuatayo;
Epuka kuinua vitu vizito: Katika wiki 2 hadi 3 za kwanza baada ya upasuaji, usiinue vitu vizito zaidi ya mtoto wako ili kuepuka msongo kwenye mshono kuna koweza kusababisha nyuzi kulegea na mshono kuachia
Usifanye mazoezi kupitiliza: Pata muda wa kutosha kupumzika na usifanye mazoezi kupita kiwango unachoweza kustahimili.
Usibane tumbo kwa kukaza sana: Kubana tumbo kwa kukaza sana husababisha msongo kwenye kidonda hivyo kupelekea kuachia kwa nyuzi na kutoka damu
Kula mlo kamili
Unapaswa kula mlo kamili wenye kiwango kikubwa cha vyakula vyenye protini, vitamini C na nyuzi nzuzi. Protini husaidia katika uponaji wa tishu, Vitamini C huongeza kinga ya mwili na huchangia kuharakisha uponyaji wa kidonda wakati nyuzi lishe zina mchango mkubwa katika kuzuia tumbo kujaa na kukosa choo, tatizo ambalo ni la kawaida baada ya upasuaji, pia husaidia kuboresha mmeng’enyo wa chakula na kuwezesha kinyesi kupita kwa urahisi, hivyo kupunguza usumbufu na maumivu wakati wa kujisaidia
Usafi wa mwili
Hakikisha mwili wako, nguo na mazingira yanayokuzunguka yapo katika hali ya usafi. Oga vizuri, safisha sehemu za siri na eneo la haja kubwa kila siku ili kudumisha usafi na kuondoa uchafu wenye harufu mbaya unaoweza kujikusanya kwenye nyufa za labia. Usafi huu husaidia kupunguza hatari ya maambukizi na kuhakikisha uponyaji mzuri baada ya upasuaji.
Dalili za Maambukizi ya Kidonda
Ikiwa utapata dalili zozote kati ya hizi, wasiliana na mtoa huduma wako wa afya mara moja.
Kuvimba au kuwa na wekundu unaoongezeka kwenye eneo la kidonda
Kutoka usaha au majimaji yenye harufu mbaya kutoka kwenye kidonda
Homa au ongezeko la joto mwilini
Maumivu makali yanayoendelea au kuongezeka
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
31 Machi 2025, 14:30:59
Rejea za dawa
An integrative review of home care recommendations for women after caesarean section. National Institutes of Health (NIH) (.gov). https://pmc.ncbi.nlm.nih.gov/articles/PMC10965751/. Imechukuliwa 30.03.2025
6 Tips for a Fast C-Section Recovery. Healthline. https://www.healthline.com/health/pregnancy/c-section-tips-for-fast-recovery. Imechukuliwa 30.03.2025
C-section recovery: What to expect - Mayo Clinic. https://www.mayoclinic.org/healthy-lifestyle/labor-and-delivery/in-depth/c-section-recovery/art-20047310. Imechukuliwa 30.03.2025
C-Section Recovery - What to Expect: Walking, Blood Clots… WebMD. https://www.webmd.com/baby/recovery-after-c-section. Imechukuliwa 30.03.2025