Kuhusu mwandishi
Imeandikwa na Dkt Mangwell sospeter/MD
​
Mwandishi wa kitabu hiki ni Daktari wa wagonjwa ya binadamu, amekuwa akihudumia wagonjwa wa kisukari na kukutana nao wakiwa kwenye hatua mbalimbali za ugonjwa. Pia amekuwa akifanya tafiti ili kujua kuhusu kwanini watanzania wenye kisukari wanapata madhara yanayojulikana kutokea kwa upesi zaidi ukilinganisha mataifa mengine. Sababu kubwa iliyoonekana ni uelewa duni kuhusu ugonjwa wa kisukari. Uelewa duni umesababishwa kwa sababu ya kukosa Elimu inayohusu kisukari kwenye jamii na pia kwenye sehemu elimu ilipokuwa inatolewa, ilikuwa haikidhi mahitaji hivyo watu/wagonjwa wachache walipata ufahamu kidogo.
​
Mwandishi aliamua kuandika Makala haya ya “Jikinge na dhibiti kisukari” ili kusaidia wale ambao watasoma kitabu hiki si tu waweze kuishi na kisukari bali kuwasaidia wale wasio na kisukari waweze kujikinga na kisukari kwa kujua yale mambo hatarishi yanayozuilika,yanayopelekea mtu kupata kisukari.
​
Historia ya kisukari
​
Kisukari ni moja kati ya magonjwa ya kwanza kabisa kutambuliwa na kuandikwa kwenye maandishi miaka 1500KK huko misri ikielezea ni tatizo la “kukojoa sana” wataalamu wa magonjwa tiba wa kihindi kwenye miaka hiyo hiyo walielezea tatizo hili kuwa ni “Mkojo wa asali’ kwa sababu mkojo aina hii uliwavutia sana sungusungu. Kwa lugha ya kigeni huitwa “diabetes mellitus”, diabetes ikimaanisha kupitisha na mellitus ikimaanisha kutoka “kwenye asali” . Miaka ya 1600KK mtaalamu wa mambo ya afya bwana Thomas willis alitofautisha kisukari hiki na kile cha diabetic inspidus ambacho nacho kinahusiana na kukojoa sana lakini mkojo huwa hauna sukari. Katika kitabu hiki tumezungumzia kisukari cha asali yaani DM na kila msomaji msomaji wa kitabu hiki anapaswa kuelewa hivyo hapa mwanzoni.
​
Kisukari ni nini?
​
Ni jambo la msingi tukijikumbusha ni nini maana ya kisukari na hutokeaje. Kisukari (Diabetes mellitus) ni kundi la magonjwa sugu yasiyoambukizwa, hutokana na kuathirika kwa mfumo wa uchakatuaji na utumiaji glukosi mwilini. Glukosi ni chanzo cha nishati-nguvu mwilini, na huwa na umuhimu katika kuendeleza maisha ya chembe hai. Ubongo hupata nguvu za kufanya kazi kwa asilimia kubwa kutoka kwenye nishati inayotolewa na glukosi. Glukosi isipokuwepo kwenye damu kwa kiwango cha kutosha mtu huweza kupata madhara kama kuzimia n.k kama ishara kwamba ubongo umekosa sukari kwa kiwango kinachohitajika.
Mtu akiwa na kisukari(DM) haijalishi ni aina gani, kinachotokea ni kwamba mtu huyu huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye mzunguko wa damu. Kuwa na sukari nyingi kwa mda mrefu huweza kuleta madhara makubwa kwenye ogani mbalimbali ndani ya mwili(sana sana kwenye macho, figo, mishipa ya damu, moyo) yanayoweza kuwa ya ghafla yanayodumu kwa kwa mda mfupi au sugu.
Aina mbalimbali za tatizo la kisukari
Kujua aina ya kisukari kinachokusumbua husaidia kufungua njia kwenye matibabu yako, kwa kuwezesha kufanya maamuzi ya kujua utumie dawa? na kama kutumia dawa ni dawa gani unatakiwa kutumia?
​
Tatizo sugu la kisukari limegawanyika katika sehemu mbili, kisukari cha kupanda aina ya 1 na cha aina ya 2 (DM1 na DM2)
Kipo kisukari kinachotokea wakati wa ujauzito ambacho huitwa “kisukari cha ujauzito”, kisukari hiki huweza kuisha baada ya ujauzito au huweza kuendelea baada ya ujauzito lakini huwa katika kundi la aina ya kisukari kinachoweza kuonekana kwenye mkojo. Kwenye kurasa inayofuata tutazungumzia sana kuhusu kisukari aina ya 1 na 2
​
1.Kisukari aina ya 1 (Diabetes mellitus type1-DM1)
Kisukari aina ya kwanza ni ugonjwa unaotokana na kushindwa kuzalishwa kwa homoni ya insulin kwa sababu ya kuharibiwa kwa chembe hai ndani ya kongosho zinazotengeneza homoni hii, chembe chembe za kinga ya mwili wa mtu huhusika kufanya uharibifu huu kwa asilimia 90 ya wagonjwa. Asilimia 10 ya wagonjwa sababu bado hazijulikani .
Uhalibifu wa kinga za mwili unaweza kusababishwa na sababu mablimbali zikiwezo za kijeni(ambapo hutokea kwa robo ya wagonjwa tu) au za kimazingira kama maambukizi ya virusi vya rubella, Mumps na Cocksackie virus B. Pia inasemekana matumizi ya maziwa ya ng’ombe mapema zaidi, mtoto anapozaliwa
Kisukari aina hii huanza utotoni, kwa asilimia zaidi ya 80 lakini unaweza kuanza pia kwenye umri wa miaka 30 au 40.
Kisukari aina ya kwanza kimeonekana kuhusianishwa na maambukizi ya kirusi cha enterovirus kwa kuwa watoto wengi walioonekana kuwa na maambukizi haya huko taiwan walikuwa na kisukari aina ya kwanza kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na watoto ambao hawakuathiriwa na virusi hao.
Dalili za kisukari aina ya 1
-
Kula sana(kwa sababu ya kuhisi njaa mara kwa mara)
-
Kunywa maji sana kutokana na kupata kiu kupita kiasi,
-
Kukojoa sana
-
Kupungua uzito
Dalili zingine ni kuhisi mwili kuchoka, kichefuchefu na kutoona vema.
2. Kisukari aina ya 2 (Diabetes mellitus type 2- DM2)
Kisukari aina ya pili hutokea kutokana na udhaifu unaotokea kwenye seli hai zinazochakatua sukari mwilini. Udhaifu huu huweza kusababishwa na upinzani wa homoni ya insuline kufanya kazi au kutozalishwa kwa wingi kwa homoni hii au uzalizashi wa kiwango kikubwa cha homoni ya glukagoni kisichotakiwa mwilini. Madhara ya udhaifu huo wote hupelekea mwili kushindwa kutumia sukari iliyo kwenye damu na hivyo kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu.
Kisukari aina hii hutokea kwa watu wazima yaani watu wenye umri zaidi ya miaka 35 na kuendelea. Cha kushangaza kisukari aina ya 2 kimeanza kuongezeka kwa kasi kwa vijana wadogo kwa sababu ya kubadilika kwa mtindo wa maisha na sababu zingine zinazoelezewa hapo chini
​
​
Wasiliana na daktari wako siku zote kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatu yoyote
​
​
Imeboreshwa 12.03.2020
​
Rejea​
​