top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Dkt. Sospeter M, MD

Dkt. Charles W, MD

9 Juni 2020 10:34:23

Madhara ya kisukari

Madhara ya kisukari

Kisukari kina madhara ya muda mfupi na yale ya muda mrefu, madhara ya muda mfupi ni kama vile kushuka kwa kiwango cha sukari, DKA, HHS. Madhara ya muda mrefu ni kama vile kuferi kwa figo, kiharusi na magonjwa mengine ya mishipa ya damu. Sehemu hii utajifunza madhara mengi yanayotokea mwilini kwa agonjwa wa kisukari. MAdhara haya yameonekana kwenye tafiti mbalimbali za wagonjwa wa kisukari.


Madhara ya muda mfupi (madhara ya ghafla)


1.Kushuka kwa sukari

Sukari kushuka chini ya kiwango cha kawaida (chini ya 3.5mmol/L), tatizo hili linatokana na matumizi ya dawa hasa aina ya sulphonyurea au sindano za insulin kuliko kusababishwa na ugonjwa wenyewe. Pia pombe, mazoezi makali, kutokula chakula, kula chakula kidogo au kutofuata ratiba ya kula.


Kushuka kwa sukari hutokea sana pale, kabla ya kula, unapokuwa unafanya mazoezi, mda mfupi baada ya kujichoma sindano ya homoni insulin, kiwango cha pombe kikiongezeka wakati kiwango cha chakula kimebaki kilekile. Pia wakati wa usiku ambapo mchana wake ulikuwa na mazoezi mengi au umejidunga insulin nyingi kabla ya kulala au ulkula kidogo au hukula kabisa.


Dalili zake huwa kati ya hizi;

 • Kutokwa na jasho mwilini

 • Njaa kali

 • Mwili Kutetemeka

 • Kuwa na hwasiwasi sana

 • Moyo kudunda kwa nguvu

 • Kuchanganyikiwa

 • Kushindwa kuongea

 • Kulegea sana kwa mwili

 • Kushindwa kumanikia jambo


Pia dalili zingine zisizo rasimi ni kama kichefuchefu, kuchoka mwili na kichwa kuuma

Kumbuka:


Si kila mtu anapata dalili zote hizo, ni baadhi tu, na pia ni vema kuangalia wewe unapata dalili gani. Kumbuka kupima kiwango cha sukari katika damu kwa utaratibu maalumu (inashauriwa mtu mwenye kisukari aina ya 1 kupima mara 4 hadi 5 kwa siku, kabla ya kula mlo wowote, na wakati wa usiku mida ya sa nane au tisa- mara moja kwa wiki)


Kwa jinsi unayopima sukari yako katika dam undo jinsi unavyojua kiwango chako na kuwa na uwezo wa kudhibiti kama imeshuka au kupanda. Usisahau kuweka rekodi katika kitabu chako pale unapopima sukari.


Hakikisha umeongea na ndugu na jamaa wanaoishi nawe ili waweze jua dalili za sukari kushuka chini ya kiwango ili waweze kukusaidia endapo wewe utakuwa hujitambui au kushindwa kuongea wakati huo. Kama ukishindwa kutambua kushuka kwa sukari ubongo ukikosa sukari unaweza kupata matatizo makubwa na utapoteza fahamu. Pia kumbuka kubeba kiutambulisho kwamba wewe unakisukari.


Kukabiliana na tatizo la kushuka na sukari kwenye damu

Unaweza kufanya haya mara sukari yako inappokuwa imeshuka chini ya 3mmol/L


 • Chukua maji safi na kuweka glukosi vijiko viwili kisha kunywa au kuweka sukari vijiko viwili na kunywa kama huduma ya kwanza

 • Kunywa soda kama ipo karibu

 • Kunywa gramu 3 au tano za kidonge cha sukari

 • Kula zabibu wingi wa kiganja kimoja cha mkono

 • Kunywa vijiko viwili vya asali

 • Maziwa yasiyo na mafuta glasi moja na pia waweza kula biskuti

 • Kula pipi sita


2. Diabetic ketoacidosis-DKA

Hili ni tatizo linaloambatana na kiwango kikubwa cha kemikali za ketone na sukari katika damu kwa sababu ya kukosekana kwa homoni ya insulin kwenye damu, hutokea sana kwa wagonjwa wenye kisukari aina ya 1.


Tatizo la DKA mara nyingi huwa na visababishi, mara nyingi huwa ni hivi vilivyoambatanishwa chini;


 • Kusahau kujichoma dozi yako ya insulin

 • Kusahau dozi mojawapo ya insulin

 • Kutoongeza dozi ya insulin wakati unaugua

 • Maambukizi kwenye mwili (kama maambukizi ya malaria, bakteria kwenye damu, maambukizi ya njia ya mkojo)


3. DKA huambatana na dalili hizi;

 • Dalili za kisukari( kiu ya mara kwa mara, kukojoa mara kwa maraji

 • Dalili za kuishiwa maji mwilini kama vile kukauka midomo, na ngozi kuwa kavu

 • Maumivu makali ya tumbo maeneo ya kuzunguka kitovu- kukosa hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika

 • Kupooza kwa matumbo

 • Mapigo ya moyo kwenda kasi

 • Kushuka kwa shinikizo la damu unapokuwa umesimama

 • Uwezo wa kiakili kupungua- uwezo wa kujitambua

 • Kupumua kwa kina zaidi na kwa haraka sana

 • Kutoa harufu nzuri kinywani

 • Kupoteza fahamu

 • Sukari kupanda zaidi ya 33 endapo utapima kwenye kipimo(au huweza kuonyesha HIGH pasipo kuonyesha namba)

 • Mwili kuwa dhaifu sana

 • Kuonekana kwa ketone kwenye mkojo ukipimwa


Mgonjwa huyu atahitaji matibabu ya haraka sana hospitali kwenye chumba chenye uangalizi wa makini (ICU)

Matibabu ya awali unayoweza kufanya wakati unampeleka hospitali ni

4. HHS

Ni aina ya tatizo linalotokea kwenye wagonjwa wenye kisukari aina ya 2 huwa na dalili chache za awali na huambatana na dalili hizi;


 • Kukojoa sana

 • Dalili za kuishiwa maji mwili (kukauka kwa midomo, ngozi kuwa kavu)


Hatua za mwisho ni kama kupigwa na degedege, kuzimia, au kifo cha ghafla.


Vihatarishi/visababishi vyaweza kuwa;

 • Kuugua

 • Kushindwa kudhibiti kiwango cha sukari mwilini kwa mda mrefu

 • Msongo wa mawazo

 • Dawa na chakula- kama vile vunywaji vyenye kahawa, pombe na dawa aina ya diuretics zinazotumika kutibu shinikizo la juu la damu, dawa aina ya steroid, cimetidine, na dawa ya aina ya phenytoin

 • Wagonjwa wa figo wanaofanyiwa dialysis


HHS yaweza kuzuiliwa kwa kupima sukari yako mara kwa mara kulingana na ulivyoshauriwa na daktari wako, haswa pale ukiwa unaumwa waweza kupima zaidi ya mara mbili kwa siku.

Kumbuka


Endapo umetambua mgonjwa mwenye tatizo hili basi ni vema kumuwahisha hospitali haraka akapate matibabu


Madhara sugu


Kuna baadhi ya mambo ya kijeni na uwezo wa kudhibiti sukari yanayoweza kutabiri mtu gani atapata madhara ya kisukari hapo mbeleni. Mtu aliyedhibiti sukari yake kwa kiwango kinachoshauriwa huishi vema kama mtu asiye na kisukari.

Kutokea kwa madhara hutokana na kubadilishwa kwa glukosi kwenda sorbitol kwenye damu, kemikali hii ni sumu kwenye tishu mbalimbali mwilini.

Kuna ushahidi wa kisayansi kwamba kudhibiti vizuri sukari huweza kuzuia madhara mengi yanayoweza kutokea kutokana na kisukari.

Wasiwasi uliopitiliza


Ni kawaidakupata wasiwasi au hofu wakati Fulani katika maisha na kila mtu huwa na hali hii, wasiwasi wa kiasi huweza kuwa ni vema kwa sababu hukusaidia kupambana na hatari mbaya na huweza kukupa hamasa ya kufanya vizuri shuleni au kazini.


Lakini kama una wasiwasi mara nyingi bila sababu na wasiwasi huo unaathiri maisha yako, basi una tatizo la wasiwasi. Tatizo la wsiwasi linaweza kusababisha hofu iliyopitiliza na zisizo za kweli dhidi ya hali mbalimbali za kimaisha bila kuwa na kisababishi kinachojulikana.


Mahusino kati ya tatizo la wasiwasi na kisukari haufahamiki vema, lakini tafiti zinaonyesha kuwa kiwango cha wasiwasi kwa watu wenye kisukari huwa kikubwa. Wasiwasi kwa watu wenye kisukari huweza kusababisha tatizo katika kudhibiti kiwango cha sukari katika damu.


Dalili za mtu mwenye tatizo la wasiwasi huwa kama hizi

 • Kutotulia

 • Kujihisi mwenye fadhaa au umefikia ukomo

 • Kuhisi uvimbe kwenye koo lako

 • Kushindwa kutulia kwenye jambo moja kimawazo

 • Kuchoka

 • Kutokuwa mvumilivu

 • Kupotezwa kimawzo haraka na jambo fulani

 • Misuli kukaza

 • Kutopata usingizi au kushindwa kuendelea kulala

 • Kutokwa na jasho jingi

 • Kuishiwa pumzi

 • Maumivu ya tumbo

 • Kuharisha

 • Kichwa kuumaMatibabu ya wasiwasi huhusisha matibabu ya dawa na maongezi maalumu, huweza kutumika kwa pamoja au unaweza kupewa aina moja ya matibabu.


Ongea na daktari wako endapo unahisi kwamba unatatizo la wasiwasi kwa ushauri na matibabu.


Ugonjwa wa celiac


Tatizo hili huonekana sana kwa watu wenye kisukari aina ya 1 kuliko kwa watu wengine, hutokea kwa asilimia 4 hadi 9 ya watoto wenye kisukari aia ya 1 na kati yao asilimia zaidi ya 50 huwa hawana dalili. Watoto wenye kisukari aina ya 1 wanahatarishi ya kupata ugonjwa huu.


Nini maana ya Ugonjwa wa celiac?

Ni tatizo linalotokana na kinga za mwili kupambana dhidi ya protini ya gluten inayopatikana kwenye ngano. Ngano hutumiwa katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama mkate, sambusa, maandazi n.k. kama una ugonjwa wa celiac basi ukitumia vitu viilivyoengenezwa kwa ngano kinga yako ya mwili utapambana nayo na kuababisha uharibifu kwenye kuta za tumbo lako na hivyo ufyonzwaji protini, mafuta, wanga,vitamin, na madini hupungua.


Tatizo hili la celiac hurithiwa kutoka. Ndugu wa damu wa karibu (dada, kaka, watoto wa dada) wa mtu mwenye tatizo la celiac huwa na hatari ya kupata tatizo hili pia bila hata kutambulika. Huweza kuonekana kwenye kipindi chpchote kile cha maisha ya mtu, na hurithiwa. Sababu za kimazingira kama msongo wa mawazo, ujauzito, upasuaji, maambukizi(nimonia, kuhara) huweza kuamsha tatizo hili la celiac.


Dalili

Mara nyingi watu wenye tatizo la celiac huwa hawana dalili kabisa, ndio maana tatizo huwa halitambuliwi. Kama watu wakipata dalili huhusiana na mambo ya mmengenyo kama kuharisha sana pia hupata dalili za kimsongo wa mawazo na mabadiliko ya tabia.

Dalili zingine ni kama

 • Gesi

 • Maumivu ya tumbo, kusokota kwa tumbo na tumbo kuja

 • Chakula kukaa mda mrefu tumboni na kichefuchefu

 • Kuhara sana

 • Kinyesi kunuka kama kitu kilichooza

 • Kutoongezeka uzito kwa shida

 • Upungufu wa damu kutokana na kutofyonzwa kwa madini chuma, folate na vitamin B12

 • Kuchoka sana na mwili kuwa dhaifu

 • Kiwango cha chini sana cha sukari kisichokuwa na sababu kwa watu wenye kisukari aina ya 1

 • Kutokwa na vipele au harara zinazowasha sana

 • Kutopata choo

 • Kuhara au kutopata choo

 • Kuchanika midomo


Dalili za ziada kwa watoto wadogo ni

 • Kuchelewa kukua

 • Kubadilika tabia na kuwa msumbufu

 • Kutapika

 • Kuchelewa kubalehe

 • Matatizoya meno na fizi


Utambuzi

Kipimo cha kuchukua kinyama kidogo kutoka kwenye kuta za utumbo huwa kipimo kitambuzi cha kepee


Matibabu

Bila matibabu, ugonjwa huu hupelekea upungufu wa lishe (utapiamlo), upungufu wa damu, mifupa isiyo imara, ugumba, na kwa watu wenye kisukari aina ya 1 hupata tatizo la kiwango cha chini cha damu.


Matibabu pekee ni kujiepusha na vyakula vyenye protini ya gluteni ambayo hupatikana kwenye ngano. Hivyo mtu anatakiwa kuepuka vitu vilivyotengenezwa kwa ngano kama mkate, maandazi n.k


Mtaalamu wa lishe atakusaidia kujua vyakula vvisivyo na protini ya gluten, au unaweza kuangalia katika mtandao wetu wa ULY-CLINIC.


Huzuniko


Dalili ya huzuniko huonekana kwa asimilia 30 kwa wagonjwa wenye kisukari, asilimia 10 kati ya hizi 30 hupata dalili kuu za huzuniko. Hali ya Huzuniko husababisha mtu kuwa dhaifu kiakili na kimwili na husababisha ugumu zaidi kwenye matibabu ya kisukari na kupelekea


 • Kushindwa kudhibiti sukari

 • Kutokea kwa matatizo mengine yanayodhuru afya ya mwili yanayoambatana na kisukari

 • Kupungua kwa ubora wa maisha ya mtu

 • Kuongezeka kwa matatizo ya kifamilia na kuongezeka kwa gharama za matibabu

Uhusiano kati ya huzuniko na kisukari haujaweza kufahamika vema. Huzuniko huweza kutokea kwa sababu ya msongo wa mawazo na hofu inayotokea mtu akiwa katika matibabu ya kisukari. Kwa mara nyingi ni vigumu kutambua mtu mwenye huzuniko na hivo ni vigumu kutibu pia. Ni kazi ya wataalamu wa afya kuweza kuwa na utaratibu maalumu wa kuwachunguza wagonjwa wa kisukari dhidi ya matatizo ya kisaikolojia ili kuweza kutambua endapo wana huzuniko na kuwapatia matibabu yanayotakiwa.


Matibabu

Kutibu huzuniko kunahusisha matibabu ya maongezi ya kisaikolojia, madawa au vyote viwili, matibabu haya huweza kuimarisha afya ya mtu na kuweza kudhibiti kisukari. Kwa watu wenye huzuniko na kisukari kwa pamoja,tafiti za wanasayansi zimeonyesha matibabu ya maongezi ya kisaikolojia na dawa dhidi ya huzuniko husaidia kuimarisha afya ya mtu na kudhibiti kupanda kwa kisukari. Dawa dhidi ya huzuniko hufanya kazi vema, na aina Fulani ya matibabu ya kisaikolojia husaidia kutibu huzuniko ingawa matibabu ya huzuniko huwa ya mtu mrefu. Madawa dhidi ya huzuniko huweza kutumia wiki kadhaa kupambana na huzuniko na huweza kuhitaji kuchanganya matibabu ya dawa na maongezi ya kisaikolojia. Pia miili hutofautiana katika kusikia dawa, hivyo mtu anaweza kuongezewa dozi, kupunguziwa au kubadilishiwa dawa na daktari ili kukabiliana na huzuniko.


Kwa matumizi ya dawa za asili kwa ajili ya kutibu huzuniko, lazima uombe ushauri wa daktari ili kujua kama yana mwingiliano na dawa zingine za kisukari. Matumizi ya dawa za asili yanaweza kufanya dawa za kisukari zisifanye kazi vema na huweza kuleta madhara ikiwemo kifo.


Magonjwa ya moyo na kiharusi


Watu wenye kisukari wapo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo na kiharusi, kwa jina jingine ikifahamika kama magonwa ya mishipa ya moyo na ubongo.

Mgonjwa wa kisukari anawez kupatwa na magonjwa ya moyo miaka 10 au 15 mapema zaidi ukilinganisha na mtu asiye na kisukari


Ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo(coronary artery) huongeza kwa kutokea kama ugonjwa wa moyo. Hutokea pale mishipa hii inapokuwa inapungua kizio (kupungua kwa ukubwa wa tundu ka mshipa wa damu) cha ndani na kupelekea kutofika kwa damu sehemu zingine za moyo kwa sababu damu haipiti ya kutosha au haipiti kabisa. Kupungua kwa kizio kunaweza kutokana na kuganda kwa mafuta(rehamu) ndani ya mishipa ya damu. Tendo hili huitwa “kuganda kwa mishipa ya ateri” kama mishipa ya damu inayolisha ubongo itaganda basi mtu anaweza kupata kiharusi.


Kiwango kikubwa cha sukari katika damu ni kihatarishi kimojawapo cha kupata kiharusi, lakini watuwenye kisukari huwa na vihatarishi vingine ambata. Vihatarishi hivyo vinahusisha uzito mkubwa kuputa kiasi(na haswa kwa mtu mwenye mafuta mengi maeneo ya kiunoni), kutoshughulisha mwili, shinikizo la juu la damu, na kuwa na kiwango cha juu cha rehani kwenye damu. Watu wanaovuta sigara au wenye historia kwenye familia ya kuwa na kiharusi au magonjwa ya moyo huonekana kuwa na wana kiharatishi kikubwa cha kupata magonjwa ya mishipa ya damu na ubongo.


Kupunguza Vihatarishi


Habari njema ni kwamba watu wenye kisukari wanaweza kupunguza vihatarishi vya magonjwa ya moyo na kiharusi kwa kuzingatia na kuweka umakini kwenye vihatarishi walivyonavyo. Kushirikiana na timu yako ya tiba kufikia malengo yafuatayo yataweza kukusaidia kudhibiti sukari na magonjwa ambata. Kupata uzito wa kiafya ,kula vyakula vyenye afya bora na kuushughulisha mwili kwenye mazoezi ni muhimu. Watu wenye wenye kisukari huweza kuhitaji nyongeza ya dawa ili waweze kufikia malengo hayo


Unafahamu kuhusu ABCDEs?

Ni kifupisho cha vitu unavyotakiwa kuzingatia au kufanya ili kupunguza vihatarishi vya magonjwa ya moyo na kiharusi. Mchanganuo umefanyikahapo chini kuhusu ABCDEs kwa kila herufi


 1. A-A1C- lengo la A1C liwe asilimia 7%* au pungufu (AIC imeelezewa kwenye kitabu hiki hivyo fanya rejea)

 2. B- Dhibiti shinikizo la damu( liwe pungufu ya 130/80*)

 3. C- Cholesterol/rehamu ainaya LDL(rehamu mbaya) kiwango kiwe 2*mmol/L au pungufu

 4. D- Dawa za kulinda moyo. Madawa ya kutibu shinikizo la damu la juu jamii ya ACE au ARBs, dawa za kupunguza rehamu mbaya kwenye damu, aspirini au clopidogrel. Ongea na daktari wako kuhusu madawa haya ya kukuzuia na kisukari pamoja na kiharusi ili upate ushauri.

 5. E- Mazoezi.Mazoezi endelevu, kuushughulisha mwili, pamoja na chakula bora. Zingatia uzito unaoshauriwa kutokana na mwili wako*

 6. S- Sigara na msongo wa mawazo/stress – acha kuvuta sigara na kabiliana na msongo wa mawazo ipasavyo


* Ongea na mtaalamu wako wa afya ili akushauri kiwango halisi kwako. Kumbuka malengo ya kiwango cha A1C ya mwanamke mjamzito, watoto wenye umri chini ya miaka 12 na mzee huwa tofauti tofauti.

Mwisho unaweza kuongea na daktari wako kuhusu mambo haya unayoshauriwa na namna ya kufikia malengo.


Madhara katika macho


Matatizo katika retina ya jicho sehemu inayopokea mwanga unaoingia katika jicho matatizo haya hutokana na uzalishaji wa mishipa ya damu mingi kupita kiasi, matokeo yake ni kuziba sehemu hii ya jicho na kusababisha dalili za kuona ukungu au kushindwa kuona. Tatizo hili linaweza kusababishwa na magonjwa mengine kama shinikizo la damu la juu.


Baada ya miaka 10 ya kuwa na kisukari, nusu ya wagonjwa hupata udhaifu katika retina unaosababisha kushindwa kuona, zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wa kisukari watapata tatizo hili ndani ya miaka 15 ya kuwa na ugonjwa wa kisukari.

Tatizo hili huweza kupelekea kupungua uwezo wa kuona au kutoona kabisa kusikotibika kwa sababu ya kunyofoka kwa retina katika sehemu yake kwenye jicho.


Matibabu

Matibabu ya mwanga wa laser, huharibu tishu zilizozalishwa kwa wingi na kujikusanya katika retina na kupelekea kutoona, matibabu haya husaidia kuingia kwa hewa safi ya oksijeni kwenye retina na kuona vizuri.

Kumbuka matibabu haya yanatakiwa kufanyika mapema kabla retina ya jicho haijafunikwa kabisa.


Mtoto wa jicho.


Hutokea kwa watu wa kisukari kwa sababu ya kemikali ya sorbitol, Ili kutambua mapema tatizo hili ni vema kila mwaka mtu mwenye kisukari apime macho yake akiwa anaenda kliniki.


Matatizo ya figo


Kisukari huchangia matatizo ya figo kwa namna tatu,kwa kuharibu tishu za uchujaji mkojo na kemikali katika figo, kusababisha kuziba kwa mishipa ya damu na kupanda kwa maambukizi kwenye mfumo wa juu wa mkojo(kwa sababu ya kinga ya chini ya mwili inayosababishwa na kiskari kisichodhibitiwa).


Tatizo hili Hutokea miaka 15 hadi 25 baada ya kutambuliwa na ugonjwa wa kisukari na asilimia 25- 30 ya watu wametambuliwa na tatizo hili wakiwa na umri chini ya miaka 30. Tatizo hili huongoza kwa kusababisha vifo kwa vijana wadogo wenye kisukari.


Kuziba kwa mishipa ya damu na matatizo ambata


Majeraha na kukakamaa katika mishipa ya damu ya ateri huweza kusababishwa na kisukari. Mwonekano hufanana na ule unaoletwa na shinikizo la juu la damu la juu ila hupelekea magonjwa ya kuziba kwa mishipa ya damu hivo hewa safi kushindwa kufika katika figo na hatimaye chembe na tishu hai katika figo hufa na huambatana na dalili kadhaa.


Maambukizi ya kupanda katika mfumo wa mkojo hutokea kutokana na kutuwama sana kwa mkojo ndani ya kibofu. Kutuwama huku hutokea kwa sababu ya kuharibika kwa mishipa ya fahamu kulikosababishwa na kisukari. Kibofu hushindwa kutanuka na kusinyaa ili kutoa mkojo nje na maambukizi kwa vile hupenda maji yaliyotuwama huvamia kibovu na huweza kupanda hadi kwenye figo. Cha kushangaza tatizo hili hutokea sana kwa wanawake kwa sababu za kimaumbile Soma hapa


Matibabu

Matibabu halisi ya maambukizi ya kupanda ni kuzuia kuharibika kwa mishipa ya fahamu ya kibofu kwa kudhibiti kiwango cha sukari mwilini. Kama sehemu ya matibabu ya kisukari vipimo vya protini ndogo zinazotolewa na figo na kuignia katika mkojo hutakiwa kipimwa kila mwaka ili kugunduliwa mapema zaidi ili kuzuia tatizo kuwa kubwa la figo kutoa protini kubwa kwenye mkojo kwa kufanya yafuatayo mara baada ya kutambuliwa


 • Kudhibiti sukari mwilini

 • Kudhibiti shinikizo la juu la damu

 • Kutumia dawa jamii ya ACE au ARBs

 • Kutumia dawa za kushusha mafuta mwilini

 • Dawa jamii ya ACE huzuia kuonekana kwa protini kubwa kwenye mkojo na huzuia kuendelea kuharibiwa kwa figo kunakotokana na protini hizi kwa watu wenye kisukari aina ya 1 na 2.


Kuharibika kwa mishipa ya fahamu kwenye miguu na mikono


Tatizo hili Hutokea mapema zaidi kuliko matatizo mengine kama madhara ya kisukari, pia hutokea kwa watu wengi na hudhuru asilimia 30 ya wagonjwa wa kisukari, huwa haiambatani na dalili kwa watu wengi wenye kisukari.


Kisukari hupelekea kupanuka mishipa ya fahamu na kuharibu kwa kuta za mishipa ya fahamu, pia husababisha kuganda kwa damu kwenye uwazi wa mshipa mmoja wa fahamu na mwingine na hivyo kupelekea kutosafilishwa kwa taarifa muhimu za mfumo wa fahamu kama hisia za kuguswa n.k

Uhaibifu huweza tokea upande mmoja wa mwili au kutokea pande zote za mwili haijalishi miguu au mikono.


Dalili

 • Maumivu ya miguu na ganzi (maumivu huwa sio makali sana, ya kuchoma na huwa makali wakati wa usiku na huhisiwa sehemu ya mbele ya mguu.

 • Kuhisi hali ya kuungua katika kanyagio na huambatana na kuhisi ganzi kwenye mguu


Viashiria

 • Kupungua hisia dhidi ya mitetemo katika miguu

 • Kupoteza fahamu zote miguuni kama mtu aliyevaa soksi

 • Vidole vya miguu kubadilika maumbile na kuwa vigumu sehemu za misuguano


Kuisha kwa misuri upande mmoja wa mwili


Hutokea kama madhara makali ya kisukari, upande mmoja wa mwili huisha na kuwa mwembamba sana, hutokea sana kwenye mguu ingawa huweza kutokea kwenye mikono pia. Huambatana na maumivu makali sana na kupata ganzi au hisia za maumivu makali endapo utaguswa au kukanyaga chini, maumivu haya hutokea mbele ya mguu.


Kuharibiwa kwa mshipa ya fahamu


Mshipa wa macho namba 3 na 6 hudhurika sana na kupelekea tatizo la kuona kitu kimoja kama viwili, mshipa wa sciatic na femoral hudhulika pia na kusababisha dalili za ganzi na maumivu.


Kuharibika kwa mishipa inayoongoza matendo yasiyo ya hiari


Kwenye moyo- kushuka kwa shinikizo la damu unaposimama, hupelekea mtu kuzimia, husababisha pia mapigo ya mwendo kwenda kwa kasi wakati umekaa


Mfumo wa chakula- kushindwa kumeza kwa sababu mrija wa kimeleo hausinyai na kutanuka, kutokwenda haja kubwa mda mrefu, hisia za tumbo kujaa, kichefuchefu na kutapika (utumbo kupooza)


Mfumo wa mkojo na uzazi- kushindwa kuzuia mkojo kutoka, kushindwa kusimamisha uume/mboo wakati wa tendo la kujamiiana, kutotoa shahawa wakati wa tendon a shahawa kuingia kwenye kibofu. Matatizo hayo huweza kutibiwa kwa dawa hivyo ni vema kuwasiliana na daktari wako mapema zaidi ili kupata tiba sahihi.


Mfumo wa misuli- Kuhisi baridi katika miguu


Mboni- Kupungua kwa ukubwa wa mboni, usungu kwenye dawa aina ya myridiatic, kutoitikia kwenye mwanga haraka au kutoitika kabisa.


Matibabu

 • Kudhibiti sukari iwe katika kiwango kinachoshauriwa

 • Kutibu dalili

 • Maumivu hutibiwa na dawa jamii ya TCA

 • Kutopata choo mda mrefu hutibiwa kwa madawa ya kulainisha kinyesi

 • Na tatizo la kutosimamisha uume hutibiwa kwa dawa jamii ya phosphodiesterase 5 inhibitor mfano wa sildenafil


Magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo


Hutokea mapema sana kwa wagonjwa wa kisukari, wanawake hudhurika sawa na wanaume ambapo kwa watu wasio na kisukari inaonekana wanawake hawadhuriki sana kwa sababu za kijinsia na homoni. Magonjwa ya kuziba kwa mishipa ya damu na kufa kwa chembe za moyo huwa hayana dalili mara nyingi kwa wagonjwa wa kisukari, hivyo huweza kusababisha vifo vya ghafla bila hata mgonjwa kuwa na dalili yoyote ile. Wagonjwa hawa hupata dalili za kufeli kwa moyo, kama madhara ya matokeo ya uharibifu kwenye moyo yanayotokana na kisukari.


Madhara mengine


 • Kujikunja na kukakamaa kwa vidole vya mikono au miguu (charcot’s joint)

 • Kupatwa na maambukizi ya bakteria aina ya pseudomonas, maambukizi kwenye mfumo wan je wa masikio na kupungua kwa ufahamuImeboreshwa

11 Desemba 2021 13:58:41

Uly clinic inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote dhidi ya afya yako.

Wasiliana na daktari wa ULY clinic kwa kubonyeza 'Pata Tiba' au kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii.

Rejea za mada hii;

 1. Tessier D, Meneilly GS. Diabetes management in the elderly. In: Gerstein HC, ed. Evidence-based diabetes care. Hamilton: BC Decker Inc., 2001, pg. 370–9.

 2. Lipska KJ, De Rekeneire N, Van Ness PH, et al. Identifying dysglycemic states in older adults: Implications of the emerging use of hemoglobin A1c. J Clin Endocrinol Metab 2010;95:5289–95.

 3. Crandall J, Schade D, Ma Y, et al. The influence of age on the effects of lifestyle modification and metformin in prevention of diabetes. J Gerontol A Biol Sci Med Sci 2006;61:1075–81.

 4. Chiasson JL, Josse RG, Gomis R, et al. Acarbose for prevention of type 2 diabetes mellitus: The STOP-NIDDM randomised trial. Lancet 2002;359:2072–7.

 5. DREAM (Diabetes REduction Assessment with ramipril and rosiglitazone Medication) Trial Investigators, Gerstein HC, Yusuf S, et al. Effect of rosiglitazone on the frequency of diabetes in patients with impaired glucose tolerance or impaired fasting glucose: A randomised controlled trial. Lancet 2006;368:1096– 105.

 6. Inzucchi SE, Viscoli CM, Young LH, et al. Pioglitazone prevents diabetes in patients with insulin resistance and cerebrovascular disease. Diabetes Care 2016;39:1684–92.

 7. Kronsbein P, Jorgens V, Muhlhauser I, et al. Evaluation of a structured treatment and teaching programme on non-insulin-dependent diabetes. Lancet 1988;2:1407–11.

 8. Wilson W, Pratt C. The impact of diabetes education and peer support upon weight and glycemic control of elderly persons with NonInsulin Dependent Diabetes Mellitus (NIDDM). Am J Public Health 1987;77:634–5.

 9. Braun AK, Kubiak T, Kuntsche J, et al. SGS: A structured treatment and teaching programme for older patients with diabetes mellitus–a prospective randomised controlled multi-centre trial. Age Ageing 2009;38:390–6.

 10.  Fagan PJ, Schuster AB, Boyd C, et al. Chronic care improvement in primary care: Evaluation of an integrated pay-for-performance and practice-based care coordination program among elderly patients with diabetes. Health Serv Res 2010;45:1763–82.

 11. McGovern MP, Williams DJ, Hannaford PC, et al. Introduction of a new incentive and target-based contract for family physicians in the UK: Good for older patients with diabetes but less good for women? Diabet Med 2008;25:1083–9.

 12. Maar MA, Manitowabi D, Gzik D, et al. Serious complications for patients, care providers and policy makers: Tackling the structural violence of First Nations people living with diabetes in Canada. Int Indigenous Policy J 2011;21:http://ir.lib.uwo.ca/iipj/vol2/iss1/6. Article 6.Imechukuliwa 05.06.2020

 13.  Jacklin KM, Henderson RI, Green ME, et al. Health care experiences of Indigenous people living with type 2 diabetes in Canada. CMAJ 2017;189:E106– 12.

 14. Chandler MJ, Lalonde C. Cultural continuity as a protective factor against suicide in First Nations Youth. Horizons 2008;10:68–72.

 15. Oster RT, Grier A, Lightning R, Mayan MJ, Toth EL. Cultural continuity, traditional Indigenous language, and diabetes in Alberta First Nations: A mixed methods study. Int J Equity Health 2014;13:92. doi:10.1186/s12939-014- 0092-4.

 16. Truth and Reconciliation Commission of Canada. Truth and reconcilliation commission of Canada: calls to action. Winnipeg, MB: Truth and Reconciliation Commission of Canada 2012. 2015. http://www.trc.ca/websites/ trcinstitution/File/2015/Findings/Calls_to_Action_English2.pdf.Imechukuliwa 05.06.2020

 17.  Yu CH, Zinman B. Type 2 diabetes and impaired glucose tolerance in aboriginal populations: A global perspective. Diabetes Res Clin Pract 2007;78:159– 70.

 18. Gracey M, King M. Indigenous health part 1: Determinants and disease patterns. Lancet 2009;374:65–75.

 19. Chronic Disease Surveillance and Monitoring Division, Centre for Chronic Disease Prevention and Control. Diabetes in Canada: Facts and figures from a public health perspective. Ottawa, ON: Public Health Agency of Canada, 2011 http://www.phac-aspc.gc.ca/cd-mc/publications/diabetes-diabete/facts -figures-faits-chiffres-2011/index-eng.php. Imechukuliwa 05.06.2020

 20. Turin TC, Saad N, Jun M, et al. Lifetime risk of diabetes among first nations and non-first nations people. CMAJ 2016;188:1147–53.

 21. Singer J, Putulik Kidlapik C, Martin B, et al. Food consumption, obesity and abnormal glycaemic control in a Canadian Inuit community. Clin Obes 2014;4:316– 23.

bottom of page