Imeandikwa na ULY CLINIC
Namna ya kupima joto la mwili
Kabla ya kupima joto hakikisha
Kabla ya kupima joto la mwili hakikisha una kipimajoto kisafi na endapo kinatumika kwa mtu zaidi ya mmoja, hakikisha kuwa kimetakaswa. Joto la mwili hupimwa kwenye maeneo makuu matano ambayo ni mdomo paji, njia ya haja kubwa, kwapa na kwenye sikio
Njia muimu ambayo inatumika kutakasa kipima joto ni kutumia vitakasa mikono au pamba iliyochovywa kweney spititi. Wakati wa kutakasa kifa chako utatakiwa kuwa na pamba pamoja kitakasa mikono au spiriti, chovya pamba yako kwenye kitakasa mikono au spiriti kisha futa kipimajoto chako. Kipima joto ambacho hakigusi mwili yaani kile cha infrared hakipaswi kutakaswa.
Fuata maelekezo ya muuzaji kuhusu namna ya kutakasa kifaa chako kwa ufanisi zaidi.
Kumbuka pia
-
Baada ya majibu kuwa tayari yasome mara moja ili kuzuia kupata majibu yasiyo sahihi
-
Kifaa cha analogia (glasi) kinatikiswa ili mercury au silver iliyo ndani ya glasi iingie kwenye bulbu kabla ya kutumika. Wakati wa kutikisa hakikisha unashika upande usio na ncha kisha tikisa mara tatu hadi nne, kuwa mwangalifu ili usipasue kipimajoto chako. Siku zote fuata maelekezo ya matumizi ya kifaa chako yaliyoandikwa na mtengenezaji wa kifa hiko.
Joto la mwili wa binadamu linaweza kutambuliwa kwa kupimwa kwenye maeneo tofauti ambayo ni;
Mdomo
Hapa utatakiwa kuweka ndani ya midomo kipima joto kilicho takaswa, kifaa cha kidigitali au cha analogia kinaweza kutumika. Hata hivyo endapo unatumia njia hii, hakikisha kifaa chako ni kisafi au kitumiwe na mtu mmoja tu la sivyo ufuate kanuni za kutakasa ili kuzuia kusafirisha maambukizi ya kinwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Ingiza ncha ya kipimo iingiea na kuvuka meno kidogo kisha bana(bumba) midomo yako kwa dakika tano endapo unatumia kifaa cha analogia au mpaka muito usikike kwa kifaa cha kidigitali. Joto linalopimwa kwa njia hii huchukuliwa kama joto rejea. Joto la kawaida huwa ni nyuzi joto la Celsius 37 au Fahrenheit 98.6
Haja kubwa
Njia hii hupima joto la katikati ya mwili, ni njia nzuri sana ingawa inakera kwa sababu maeneo haya watu hawapendi kuyachokoza hata hivyo pia kuingiza kitu kigeni maeneo haya hufanya mtu ajihisi vibaya. Ingiza ncha ya kipimo kwenye njia ya haja kubwa kiasi kwamba ivuke kwenye misuli ya tungu huku ukiwa umelala upande mmoja. Utofauti wa joto la mwili linalopimwa kwenye njia ya haja kubwa na mdomoni ni ongezeko la nyuzi joto za Celsius 0.3-0.6 zaidi kwenye kipimo cha njia ya haja kubwa.
Kwapa
Njia hii ni njia inayofahamika sana kwa watu wengi afrika, watu wengi waliowahi kufika hospitali wakiwa wanaumwa wameshawahi kutumia njia hii kupimwa joto la mwili. Weka ncha ya kipimajoto kikae katikati ya kwapa kisha bana kwapa. Endapo kipimajoto cha kidigitali kitatoa sauti basi kitoe kisha soma majibu hapo hapo. Kwa kifaa cha analogia kiache kikae kwa dakika tano kisha kitoe na soma majibu hapo hapo. Joto linalopimwa kwa njia hii huwa na upungufu wa nyuzi joto za Celsius 0.3 hadi 0.6 dhidi ya joto linalopimwa mdomoni.
Sikio (paji la uso)
Njia hii haitumiki sana na watu wengi lakini ni njia ambayo inatumika kupima joto la katikati ya mwili (joto la viungo vya ndani ya mwili)
Ngozi
Njia hii hutumika kusoma joto la mwili kwa njia ya ngozi haswa maeneo ya paji la uso, kipima joto maalumu kama tochi ambacho hakigusi mwili wa mtu hutumika, kipima joto hiki hutumia mionzi ya infrared ili kukiwezesha kusoma joto la mwili. Joto linalopimwa kwa njia hii huwa pungufu kwa njuzi joto za Celsius 0.3- 0.6 dhidi ya joto linalopimwa kwenye kwapa.
Imeboreshwa, 2.1.2021
Rejea za mada hii
-
John Hopkins medicine. Vital Signs (Body Temperature, Pulse Rate, Respiration Rate, Blood Pressure). https://www.hopkinsmedicine.org/health/conditions-and-diseases/vital-signs-body-temperature-pulse-rate-respiration-rate-blood-pressure. Imechukuliwa 31.12.2020
-
CDC. VItal Signs. https://www.cdc.gov/vitalsigns/index.html. Imechukuliwa 31.12.2020
-
Vitals signs in children. https://www.mottchildren.org/health-library/abo2987. Imechukuliwa 31.12.2020