top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

13 Agosti 2023 11:53:50

Je, wamsaidiaje daktari kutambua ugonjwa kwa dalili?

Je, uelezeaje dalili kuu ya ugonjwa kwa daktari wako?

Ili kuwasiliana vema na daktari na kumwezesha atambue tatizo lako na kufanya vema uchunguzi na tiba unapaswa kuelezea vema dalili kuu na dalili ambata.


Tambua dalili kuu

Watu wengi wanapozungumza na wataalamu wa afya(daktari) hudhani kuwa kuipa kila dalili uzito mkubwa au kuelezea kila dalili ni kuu humsaidia daktari kutambua ugonjwa na kuwapa matibabu mazuri, la hasha, kufanya hivyo kutamchanganya daktari ashindwe kufahamu vema ugonjwa wako ulivyo. Ni vema ukatambua dalili kuu na dalili zingine.


Dalili kuu ni nini?

Kwa maelezo mafupi, dalili kuu ni dalili iliyokufanya ushindwe kuvumilia na kutafuta msaada wa daktari. Dalili kuu inaweza kutokea wakati wowote wa ugonjwa, yaani inaweza kutokea mwanzoni, katikati au mwishoni mwa ugonjwa kabla ya wewe kutafuta msaada wa matibabu kutokana na kutoivumilia.


Eleza vema mlolongo wa kutokea kwa dalili

Mara nyingi ugonjwa huanza na dalili fulani kwanza ndipo dalili zingine hufuatia ambazo katika tiba huitwa dalili ambatana (dalili zinazoambatana na dalili kuu). Hivyo ili uweze masaidia daktari kutambua ugonjwa wako na kuweka mpango mzuri wa matibabu ni lazima uweze kueleza vema dalili ipi iliyoanza na kueleza dalili zilizotokea baada ya dalili kuu. Mfano, mgonjwa amekuja na shida ya kutokwa usaha sehemu za siri, dalili ya kwanza inaweza kuwa muwasho kwenye mrija wa mkojo ambao ulidumu kwa siku 4 kisha uteute kiasi ukawa unatoka kwenye uume na baadae yakafuatia maumivu wakati wa kukojoa na maumivu ya korodani.


Namna ambayo si njema ya kumweleza daktari ni kusema kuwa una dalili zote hizo. Ikumbukwe pia kuwa, ugonjwa unaweza kuanza sehemu moja na usambaa sehemu nyingine ya mwili hivyo hakikisha kuwa umemweleza daktari mlolongo wa matukio ili atambue haswa ugonjwa ulipoanzia na kukupa mpango mzuri wa uchunguzi wa mwili na tiba ambao utakuwa na ufanisi na gharama nafuu.


Aina za dalili

Kuna aina kuu tatu za dalili

 • Dalili za kuisha. Hizi ni dalili zinazotokea na kuisha zenyewe bila kupata matibabu, mfano mafua ya baridi huweza kutokea kwa siku kadhaa na kuisha yenyewe ndani ya siku kadhaa pasipo matibabu.

 • Dalili sugu.

  Hizi ni dalili zinazodumu kwa muda mrefu au kujirudia rudia mara kwa mara. Dalili sugu au za kujirudia rudia mara nyingi hutokea kwenye magonjwa sugu kama kisukari, pumu ya kifua na saratani.

 • Dalili za rejevu. Hizi ni dalili ambazo ziliwahi tokea hapo zamani na kuisha na kisha kurudi tena baada ya muda mrefu kupita. Mfano wa dalili ni dalili za sonona ambazo huweza potea kwa miaka kadhaa kabla ya kurudi tena.

Mambo mengine unapaswa kufahamu

Mbali na historia ya dalili, kuna mambo mengine unapaswa kumweleza daktari wako vema na kwa usahihi, mambo hayo yameelezwa sehemu nyingine katika tovuti hii;

 • Historia inayoendana na ugonjwa uliopo sasa

 • Historia ya matibabu yaliyopita

 • Historia ya kijamii inayohusiana na ugonjwa

 • Historia ya kifamilia inayohusiana na ugonjwa

 • Dalili zingine zozote ambazo hazihusiani na ugonjwa

 • Uchunguzi wa awali wa mwili


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeboreshwa,

13 Agosti 2023 13:58:18

Rejea za mada hii

 1. Medical history. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK534249/#:. Imechukuliwa 13.08.2023

 2. Hampton JR, Harrison MJ, Mitchell JR, Prichard JS, Seymour C. Relative contributions of history-taking, physical examination, and laboratory investigation to diagnosis and management of medical outpatients. Br Med J. 1975 May 31;2(5969):486-9.

 3. Peterson MC, Holbrook JH, Von Hales D, Smith NL, Staker LV. Contributions of the history, physical examination, and laboratory investigation in making medical diagnoses. West J Med. 1992 Feb;156(2):163-5.

 4. Litzau M, Turner J, Pettit K, Morgan Z, Cooper D. Obtaining History with a Language Barrier in the Emergency Department: Perhaps not a Barrier After All. West J Emerg Med. 2018 Nov;19(6):934-937.

 5. Dunne C, Dunsmore AWJ, Power J, Dubrowski A. Emergency Department Presentation of a Patient with Altered Mental Status: A Simulation Case for Training Residents and Clinical Clerks. Cureus. 2018 May 04;10(5):e2578.

 6. Toney-Butler TJ, Unison-Pace WJ.  StatPearls [Internet]. StatPearls Publishing; Treasure Island (FL): Aug 29, 2022. Nursing Admission Assessment and Examination.

 7. Ohm F, Vogel D, Sehner S, Wijnen-Meijer M, Harendza S. Details acquired from medical history and patients' experience of empathy--two sides of the same coin. BMC Med Educ. 2013 May 09;13:67.

bottom of page