Kupata mabadiliko ya harufu ya mwili wako wakati wa ujauzito ni kawaida na hutokea kwa wajawazito walio wengi. Mabadiliko haya mara nyingi husababishwa na ukuaji wa mtoto tumboni na mabadiliko ya homoni.
Kufahamu kwanini mabadiliko ya harufu ya mwili hutokea kutakuondolea hofu kuhusu mabadiliko hayo. Makala hii imeelezea kuhusu mabadiliko ya harufu wakati wa ujauzito, kwanini yanatokea na namna ya kukabiliaana nayo.
Kwanini mwili unatoa harufu kali wakagi wa ujauzito?
Mwili kutoa harufu kali au kuzidi kwa harufu ikiyokuwepo awali wakati wa ujauzito haswa kwenye maeneo yenye tezi nyingi za jasho kama kwapa na mapaja ni kawaida wakati wa ujauzito. Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha hali hii ambazo ni:
Ongezeko la ujazo wa damu mwilini
Wakati wa ujauzito, mwili hupata ongezeko la damu hadi asilimia 50 ya kiwango cha awali. Damu hii hupfanya kazi ya kubeba virutubisho na oksijeni kutoka kwa mama na kupeleka kwa mtoto kisha kutoa hewa ya Caboni dayoksaidi pamoja na uchafu mwingine wa kimetaboli na kuupeleka kwa mama ili upate kutolewa nje ya mwili. Ongezeko hili la damu huweza kuufanya mwili wako uhisi kuwa umeongezeka joto.
Wakati huu wa ongezeko la damu, mwili wako unaweza kutoa jasho jingi kama njia asili ya kushusha joto la mwili. Kutokwa na jasho jingi haswa kwenye maeneo ya kwapa na mapaja hupelekea mwili kutoa harufu kali au kuongezeka kwa harufu iliyokuwepo awali.
Ongezeko la homoni za jinsia
Esteojeni ni moja ya homoni ya jinsia inayoongezeka wakati wa ujauzito, mbali na kufanya kazi zingine kwenye ukuaji wa mtoto tumboni, estrojeni hufanya kazi ya kurekebisha joto la mwili na kutengeneza mazingira rafiki ya ukuaji wa kijusi. Estrojeni inapofanya kazi ya kurekebisha joto la mwili, huongeza kiwango cha jasho linalotoka haswa kwenye maeneo ya kwapa na mapajani.
Unaweza kupata dalili ya ongezeko la jasho na harufu kiasi cha kukuamsha usingizini wakati wa usiku, hii ni kawaida kutokea kwa baadhi ya wanawake na husababishwa na mabadiliko ya umetaboli pamoja na ongezeko kubwa la homoni kwenye damu linalotokea wakati wa usiku.
Ongezeko la homoni za tezi thyroid
Mara chache ongezeko la jasho wakati wa ujauzito hutokana na ongezeko la homoni zinazozalishwa na tezi thyroid. Homoni za tezi thyroid hufanya kazi ya kudhibiti joto la mwili, umetaboli, umeng’enyaji wa chakula na kazi zingine muhimu. Kama ongezeko litakuwa kubwa zaidi, linaweza kupelekea kukatokwa na jasho jingi haswa wakati umelala na kupelekea mwili wako kutoa harufu kali.
Wakati gani wa kuwasiliana na daktari?
Kama hali ya kutokwa jasho imebadilika kiasi cha kukupa hofu, wasiliana na daktari wako kwa uchunguzi zaidi.
Wasiliana na daktari haraka pia endapo harufu kali na kutokwa jasho kumeambatana na dalili zifuatazo ambazo huashiria ugonjwa wa Graves’( unaosababishwa na kuzalishwa kupita kiasi kwa homoni za tezi thyroid):
Mapigo ya moyo kwenda kasi
Kupoteza uzito bila sababu
Mijongeo ya mara kwa mara ya tumbo
Kudhoofika kwa misuli
Ngozi kuwa nyembamba
Nywele kukatika kirahisi
Kupanda kwa shinikizo la damu
Macho kuongeza hisia kwenye mwanga (kuumizwa na mwanga)
Kukanganikiwa
Kukosa utulivu wa kiakili
Wakati gani harufu mbaya hutokea?
Dalili ya mwili kutoa harufu kali inaweza kutokea mapema zaidi haswa kipindi cha kwanza cha ujauzito yaani miezi mitatu ya awali. Dalili hii pia inaweza kutokea kwenye vipindi vya ujauzito vinavyofuata.
Visababishi vya ongezeko la jasho na harufu kipindi cha pili na cha tatu cha ujauzito huchagiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la ujazo wa damu.
Wakati gani harufu mbaya hupotea?
Ongezeko la harufu na kutokwa jasho wakati wa ujauzito mara nyingi hupotea baada ya kujifungua. Hata hivyo imeonekana kuwa dalili hii inaweza kupotea na kurudi wakati wowote kwa baadhi ya wajawazito.
Namna ya kukabiliana na mwili kutoa harufu mbaya kwenye ujauzito
Kwa kuwa mabadiliko mbalimbali ya mwili wakati wa ujauzito ni kawaida kutokea na hutokana na ukuaji wa mtoto tumboni. Si wakati wote unaweza kutumia njia yoyote kuzuia dalili kwa kuwa huenda si salama kwa ujauzito wako. Unaaweza kupunguza dalili ya mwiliKutoa harufu kali wakati wa ujauzito kwa kufanya mambo yafuatayo:
Oga kila siku na pale unapopatwa na jasho
Kutumia vizuia jasho (deodorant) vya kupaka au kupulizia kwapani
Kuvaa nguo zisizobana
Kuvaa nguo zilizotengenezwa kwa pamba ili kufyonza kirahisi unyevu na jasho kwenye ngozi
Kupaka poda kwenye miguu inayotoa jasho au harufu kali
Kula mlo kamili
Kunywa maji ya kutosha
Makala hii imejibu pia kuhusu
Kutokwa na jasho jingi kwa mjamzito
Harufu ya jasho kwa mjamzito
Kunuka kikwapa kwa mjamzito
Kunuka mapajani kwa mjamzito
Kukabiliana na harufu mbaya wakati wa ujauzito
Kukabiliana na jasho jingi wakati wa ujauzito
Kukabiliana na kunuka kikwapa kwa mjamzito
Rejea za mada hii
Marx, Helen et al. “Hyperthyroidism and pregnancy.” BMJ (Clinical research ed.) vol. 336,7645 (2008): 663-7. doi:10.1136/bmj.39462.709005.AE
Bhatia, Pradeep, and Swati Chhabra. “Physiological and anatomical changes of pregnancy: Implications for anaesthesia.” Indian journal of anaesthesia vol. 62,9 (2018): 651-657. doi:10.4103/ija.IJA_458_18
Vora, Rita V et al. “Pregnancy and skin.” Journal of family medicine and primary care vol. 3,4 (2014): 318-24. doi:10.4103/2249-4863.148099
Cameron EL. Pregnancy and olfaction: A review. frontiersin.org/articles/10.3389/fpsyg.2014.00067/full
Charkoudian N, et al. (2015). Sex hormone effects on autonomic mechanisms of thermoregulation in humans. pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/26674572/
Laurberg P, et al. Endocrinology in pregnancy: Pregnancy and the incidence, diagnosing and therapy of Graves’ disease. eje.bioscientifica.com/view/journals/eje/175/5/R219.xml
Soma-Pillay P, et al. Physiological changes in pregnancy. ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4928162/
Comments