Hemophilia ni ugonjwa unaotokea kwa nadra, mwili hukosa uwezo wa kugandisha damu baada ya kupata jeraha kutokana na kukosa au kupungua kwa vigandisha damu. Vigandisha damu ni protini maalumu zinazozalishwa ndani ya mwili.
Wagonjwa wa hemophilia huwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda mrefu kuliko kawaida baada ya kupata jeraha. Watu wenye ugonjwa mkali, hofu kubwa huwa ni kuvia kwa damu ndani ya mwili haswa kwenye magoti, kiwiko cha mkono na mguu. Kuvia damu ndani ya mwili huweza sababisha uhalibifu ndani ya tishu na kupoteza maisha ya mtu.
Hemophilia kwa kuwa mara nyingi hutokana na madhaifu katika vinasaba, matibabu yake huhusisha kurejesha vigandisha damu vilivyokosekana au kupungua. Matibabu mapya yasiyohusisha kuongezewa vigandisha damu yapo na hutumika pia.
Dalili za hemophilia
Dalili za ugonjwa hutofautiana kwa mtu na mtu na hutegemea aina ya vigandisha damu vilivyopungua. Endapo vigandisha damu vimepungua kwa kiasi kidogo, mgonjwa hutoka damu isivyo kawaida akifanyiwa upasuaji au kupata jeraha. Kama vigandisha damu vimepungua kwa kiasi kikubwa, mgonjwa hutoka damu pasipo sababu ya msingi.
Dalili za kutokwa damu bila sababu zinajumuisha:
Kutokwa damu nyingi bila sababu baada ya kupata jeraha, kufanyiwa upasuaji au kung’olewa jino.
Mvio mkubwa wa damu chini ya ngozi au kuwa na mabaka mengi kutokana na kuvia kwa damu.
Kutokwa damu nyingi baada ya kuchoma sindano
Kuvimba au hisia za kukaza kwenye maungio ya mwili
Kutokwa damu puani pasio sababu
Kuvia kwa damu ndani ha ubongo
Jeraha dogo la kugonga au kupigwa kichwani huweza sababisha kuvia damu ndani ya fuvu kwa watu walio na hemophiloa kali. Dalili zinazoweza kutokea ni pamoja na:
Maumivu makali ya kichwa yaliyo endelevu
Kutapika kuliko endelevu
Kusinzia au kuishiwa nguvu
Kuona vitu viwiliviwili
Kupo oza ghafla au misuli kuwa dhaifu
Degedege
Wakati gani wa kumwona daktari?
Tafuta msaada wa haraka endapo una:
Dalili au viashiria vya kuvia damu ndani ya ubongo
Jeraha lolote lisilokatika damu
Vimba maungio ya mwili kunakoambatana na maumivu
Visababishi
Ugonjwa wa hemophilia hutokea pale mwili unapokosa au kupungua kwa vigandisha damu ambavyo hufanya damu igande kwa wakati baada ya kupata jeraha.
Hemophilia ya kurithi
Hemophilia mara nyingi huwa tatizo la kurithi, ikiwa na maana mtu anazaliwa akiwa tayari na tatizo. Hemophilia ya kurithi imegawanywa kwenye makundi mbalimbali yanayotegemea kigandisha damu kilichopungua.
Aina ya hemophilia ya kurithi inahotokea sana ni hemophilia A, aina hii husababishwa na ukosefu wa kigandisha damu namba 8, wakati hemophilia B, husababishwa na ukosefu wa kigandisha damu namba 9.
Hemophilia isiyorithika
Baadhi ya watu hupata hemophilia lakini hawana historia hiyo kwenye familia, tatizo hili hufahamika kama hemophilia isiyorithika. Hemophilia isiyorithika hutokea endapo magonjwa na hali mbalimbali zinaharibu vigandisha damu namba 8 na 9 vilivyo kwenye damu. Hali na magonjwa yanayoweza kuambatana na hemophilia isiyorithika ni:
Ujauzito
Magonjwa ya kujishambukia kwa mfumo wa kinga ya mwili
Saratani
Sclerosis iliyo sambaa
Mwitikio wa dawa
Urithishaji wa hemophilia
Udhaifu wa DNA unaopelekea hemophilia huwa kwenye kromozomu X. Binadamu huwa na kromozomu mbili XX au XY. Mwanamke ametengenezwa kwa kromozomu XX ambapo hupata X moja kutoka kwa baba na nyingine kutoka kwa mama, wakati mwanaume hupokea X kutoka kwa mama na kromozomu Y kutoka kwa baba. Hii huwa na maana kuwa karibia mara zote ugonjwa wa hemophilia hutokea kwa wanaume, wanawake huwa wabebaji tu wa kromozomu yenye ugonjwa na huwa hawapati dalili isipokuwa endapo wana ugonjwa wa wastani. Maelezo zaidi kuhusu urithishaji yanapatikana kwenye picha inayofuata:
Picha inayoelezea namna urithishaji wa hemophilia unavyotokea kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto
Ufunguo:
U humaanisha kuwa mtu asiyebeba kinasaba cha ugonjwa au asiye na ugonjwa, C humaanisha mtu aliyebeba kinasaba chenye ugonjwa na H ni mtu anayeugua ugonjwa wa hemophilia.
Vihatarishi
Kihatarishi kikubwa cha kupata hemophilia ni kuwa na historia ya ugonjwa huu kwenye ndugu wa damu moja. Wanaume wana hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu.
Madhara
Madhara ya hemophilia hujumuisha:
Kuvia kwa damu ndani ya mwili. Kuvia damu ndani ya misuli husababisha kuvimba kwa kiungo chenye msuli huo. Uvimbe wa damu pia unaweza kusababisha mgandamizo katika mishipa ya fahamu na kupelekea dalili ya kupatq ganzi au maumivu kwenye eneo linalohudumiwa na mshipa husika. Madhara ya kuvia damu hutegemea sehemu iliyoathirika, wakati mwingine kifo huweza kutokea kutokana na kuvia damu.
Kushindwa pumua vema au kupumua kwa shida. Kuvia damu ndani ya koo au shingoni huathiri uwezo wa mtu kupumua.
Uharibifu wa maungio ya mwili. Mvio wa damu ndani ya maungio ya mwili huongeza mgandamizo ndani ya maungio na kupelekea maumivu. Endapo mtu asipopata matibabu na kuvia huko kukiwa ni kwa mara kwa mara, ugonjwa wa athritis hutokea na wakati mwingine hupelekea kiharibika kwa maungio.
Maambukizi. Endapo matibabu ya kuongeza vigandisha damu ni kwa njia ya kuongezewa damu kitoka kwa mtu mwingine, kuna hatari kidogo ya kupata magonjwa ya virusi kama hepatitis C. Hatari hii mi kidogo kwa sasa kutokana na kufanyika kwa uchunguzi kabla ya kuongezewa damu.
Mzio mkali. Kwa baadhi ya watu wenye hemophilia kali, mfumo wao wa kinga huwa na mwitikio hasi dhidi ya vigandisha damu vinavyoongezwa mwilini kwa ajili ya tiba. Mfumo wa kinga hutengeneza protini zinazothibiti na kuondoa vigandisha damu vilivyoongezwa na kufanya ufanisi wa matibabu upungue.
Utambuzi
Ugonjwa mkali wa hemophilia mara nyingi hutambulika ndani ya mwaka wa kwanza wa maisha. Hemophilia ya wastani huweza kuonekana ukubwani. Watu wengi hutambulika kuwa wana hemophilia baada ya kutoka damu nyingi wakati wa upasuaji. Baadhi ya vipimo vinavyoweza kutambua tatizo hili ni:
Kipimo cha kiwango cha vigandisha damu
Hutambuwa kiwango cha vigandisha damu na kuonyesha ukubwa wa tatizo.
Kipimo cha DNA
Hufanyika kwa wagonjwa wenye historia ya ugonjwa kwenye familia, lengo ni kutambua kama umebeba vinasaba ili kufanya maamuzi ya kubeba mimba. Kipimo hiki kinaweza kufanyika kwa mtoto aliyetumboni hata hivyo huwa na hatari ya kuharibu mimba.
Matibabu
Matibabu ya ugonjwa mkali wa hemophilia huhusisha kuongezewa vigandisha damu kupitia mishipa ya damu ya vena. Matibabu ya aina hii huweza tumika kama tiba ya dalili iliyopo ya kutokwa damu ama kinga. Vigandisha damu vinavyoongezwa huweza kutoka kwenye damu ya mtu mwingine au kutengenezwa maabara.
Matibabu mengine
Matibabu mengine huhusisha:
Matumizi ya dawa
Desmopressin
Emicizumab
Epsilon Amino caproic acid
Dawa za kugandisha damu
Evicel
Upasuaji
Hupunguza dalili za kuvia damu katika maungio ya mwili, uharibifu kama ni mkubwa huhitaji upasuaji wa kurekebisha ungio lililoharibika.
Matibabu ya nyumbani na kubadili mtindo wa maisha
Ili kuzuia kutokwa damu nyingi unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:
Fanya mazoezi yenye mpangilio. Mazoezi kama kuogelea, kuendesha baiskeli hufanya mwili uchangamke na kuwa na afya njema. Mazoezi yanayohusisha kugusana kama vike mpira wa miguu, mieleka, ngumi n.k hayafai kwa mgonjwa wa hemophilia.
Kuepuka matumizi ya baadhi ya za maumivu. Baadhi ya dawa kama vile aspirin, ibuprofen, n.k hufanya damu isigande mapema hivyo kuzidisha ugonjwa wa hemophilia. Ongea na daktari wako kufahamu dawa gani inayokufaa endapo kuna uhitaji wa kutumia dawa kama hizo.
Jiepushe na dawa za kuyeyusha damu. Dawa zinazoyeyusha damu huzuia damu kuganda kwa wakati na hivyo kupelekea kupoteza damu nyingi na kupatwa na majeraha kirahisi, mfano wake ni heparin, warfarin, clopidogrel, prasugrel, ticagrelor, rivaroxaban, apixaban, edoxaban, dabigatran n.k.
Zingatia usafi wa kinywa. Usafi wa kinywa hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya kinywa yanayoweza kusababisha kutokwa na damu nyingi.
Pata chanjo kwa wakati. Watu wenye hemophilia hupaswa kupata chanjo kama watu wengine kuzingatia umri. Chanjo zingine anazopaswa kupata mgonjwa ni chanjo ya hepatitis A na B. Hata hivyo sindano ndogo inapaswa kutumika na pia baada ya kuchomwa, mgandamizo unapaswa kuwekwa kwa dqkika 3 hadi 5 pia kipande cha barafu kinaweza tumika kugandamizia eneo hilo ili kugandisha damu haraka na kuzuia damu nyingi kutoka.
Jikinge na majeraha. Haiikisha mazingira unayokaa na kufanyia kazi ni salama kwa kutunza bema vifaa vyenyenncha kali, kuvaa helmet na vifaa vingine vya kuzuia majeraha mwilini. Funga mkanda unapotumia chombo cha usafiri, fanya hivyo kwa mwanao pia.
Huduma ya kwanza kwa mgonjwa wa hemophilia
Endapo unatokwa damu, weka mgandamizo kkwa dakika 3 hafi 5 mfululizo kwenye eneo linalotoka damu. Hii itasaidia damu kukatika. Kama unatokwa damu chini ya ngozi, tumia kipande cha barafu kukanda. Kipande cha barafu pia kinaweza kudhibiti kutoka damu ndani ya kinywa kutokana na majeraha madogo ndani ya kinywa.
Rejea za mada hii
Bleeding disorders. National Heart, Lung, and Blood Institute. https://www.nhlbi.nih.gov/health-topics/bleeding-disorders. Imechukuliwa 25.05.2021
Hoots WK, et al. Hemophilia A and B: Routine management including prophylaxis. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 25.05.2021
Hemophilia. Merck Manual Professional Version. https://www.merckmanuals.com/professional/hematology-and-oncology/coagulation-disorders/hemophilia?query=hemophilia#. Imechukuliwa 25.05.2021
Weyand AC, et al. New therapies for hemophilia. Blood. 2019; doi:10.1182/blood-2018-08-872291.
What is hemophilia? Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/ncbddd/hemophilia/facts.html. Imechukuliwa 25.05.2021
Hoots WK, et al. Treatment of bleeding and perioperative management in hemophilia A and B. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 25.05.2021
Opmerkingen