top of page

Ugonjwa wa monkeypox


Hutokea kwa nadra na huambukizwa kwa njia ya hewa, kushika majimaji ya vidonda au vipele vya mtu au mnyama mwenye ugonjwa. Homa, vipele, maumivu ya kichwa, misuli na mgongo, kuvimba mitoki na huwa miongoni mwa dalili.


Ni ugonjwa unaotokea kwa nadra uliogunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1958 kama mlipuko wa ugonjwa unaofanana na tetekuwanga kwa nyani waliokuwa wamehifadhiwa kwa ajili ya tafiti.
Mnamo mwaka 1970 mgonjwa wa kwanza kupata monkeypox alirekodiwa huko Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo.Tangu mwaka huo visa mbalimbali vya ugonjwa wa monkeypox vimeripotiwa katika nchi mbalimbali za Afrika ya kati na magharibi.


Monkeypox husababishwa na kirusi cha monkeypox kutoka jinus ya Orthopoxvirus na familia ya Poxviridae. Jinus Orthopoxvirus huwa na virusi wengine pia kama vile smallpox anayesababisha tetekuwanga.


Mtunzaji asili wa kirusi huyu bado hafahamiki mpaka leo, hata hivyo panya na nyani huweza kutunza kirusi huyu na kusambaza kwa binadamu.


Hali ya ugonjwa kwa sasa


Kwa sasa ugonjwa wa monkeypox umeonekana kwenye mataifa ambayo hakukuwa na historia ya ugonjwa.


Kuanzia mwezi Mei 13, shirika la afya duniani lililipoti visa kadhaa vya ugonjwa huu kwenye majimbo matatu ya WHO yanayohusisha nchi za Australia, Belgium, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Itali, Netherland, Portugol, Uhispania, Sweden, Marekani na United kingdom.


Katika visa hivyo, hakuna hakuna historia ya wagonjwa hao kusafiri kwemda kwenye nchi za afrika zenye ugonjwa huo.(WHO)


Baadhi ya wagonjwa waliopatikana ni wale ambao walikuwa na mahusiano ya jinsia moja kati ya mwanaume na mwanaume hata hivyo ugonjwa huu haujaripotiwa kienezwa kwa njia ya ngono.


Mpaka kufikia tarehe 21 mei, kulikuwa na visa 92 vya ugonjwa wa mankeypox, na visa vingine 28 ambavyo bado havijathibitika kwa vipimo. Hakuna kifp chochote ambacho kimeripotiwa mpaka muda huo.


Dalili na viashiria


Ugonjwa wa monkeypox hufanana dalili na ugonjwa wa tetekuwanga, utofauti ni kwamba monkeypox huwa na dalili kiasi pia husababisha kuvimba kwa mitoki.


Mara baada ya maambukizi ya kirusi, inachukua takribani siku 5-21 kuonyesha dalili za ugonjwa. Na mara baada ya dalili kuanza kuonekana, huchukua takribani wiki 2 hadi 4 kwa ugonjwa kuisha. Imeonekana kuwa kati ya watu 10 waliopata ugonjwa Afrika, mmoja hufa.


Dalili za ugonjwa huwa pamoja na;

 • Homa

 • Maumivu ya kichwa

 • Maumivu ya misuli

 • Maumivu ya mgongo

 • Kuvimba mitoki

 • Kutetemeka

 • Kuishiwa nguvu


Ndani ya siku 1 hadi 3 baada ya kuonekana kwa homa, mgonjwa hupata vipele vinavyoanzia usoni mara nyingi kisha kusambaa sehemu nyingine ya mwili. Vipele huanza kama baka kwenye ngozi, kisha kuwa kipele kidogo kabla ya kutengeneza malengelenge na kupata usaha. Upele unapokauka hutengeneza magamba yanayobanduka.


Namna ugonjwa unavyoambukizwa


Maambukizi ya ugonjwa hutokea endapo mtu amekutana na virusi kupitia mnyama, binadamu au vitu vyenye vimelea hao. Kirusi huingia mwilini kupitia ngozi iliyopasuka hata kama mpasuko hauonekani kwa macho. Pia huingia mwilini kupitia njia ya hewa, macho, pua na mdomo.


Maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu yanaweza kutokea kwa kukwanguliwa, kung’atwa , kula nyama porini au mzoga, kugusa majimaji au vidonda vya binadamu au mnyama anayeumwa, au vitu vyenye majimaji yenye virusi hao.


Maambukizi ya binadamu kwenda kwa binadamu hufikiriwa awali kuwa ni kwa njia ya hewa kupitia matone ya maji maji ya mfumo wa upumuaji yanayoweza kusafiri wakati wa kukohoa, kuongea, kupiga chafya, kuimba n.k. Maambukizi haya hutokea endapo mtu amekaa mita chache karibu na mgonjwa na kutizamana uso kwa uso.


Njia zingine pia ni kupitia kugusa vidonda au vitu vingine vyenye majimaji ya vipele au vidonda mfano nguo na matandiko yaliyotengenezwa kwa malighafi yza wanyama mfano ngozi nk.


Kinga


Kuna njia kadhaa unaweza kuzitumia ili kuzuia kupata maambukizi ya kirusi monkeypox ambazo ni:

 • Kuepuka kugusana na wanyama wanaofahamika kutunza ugonjwa huu ikiwa pamoja na wanyama wanaougua au waliokufa kutokana na ugonjwa katika maeneo ambayo ugonjwa huo umetokea.

 • Epuka kugusana na vitu kama vile mashuka ambayo yametumiwa na mgonjwa au vitu vinavyotandikwa kwa ajili ya mnyama kulala.

 • Kuwatenga wagonjwa na watu wengine ambao wana hatati ya kupata ugonjwa

 • Kunawa mikono mara baada ya kugusana na binadamu au mnyama anayeumwa. Tumia maji yanayotiririka na sabuni au kitakasa mikono.

 • Kutumia vifaa kinga unapobeba au kuhudumia mgonjwa au mnyama


Tiba


Mpaka sasa hakuna tiba iliyothibikika kuwa salama kutibu ugonjwa huu. Baadhi ya nchi hutumia chanjo ya tetekuwanga, dawa za kudhibuti virusi na vaccinia immune globulin (VIG) ili kudhibiti ugonjwa huu.


Rejea za mada hii


 1. Monkeypox. https://www.cdc.gov/poxvirus/monkeypox/treatment.html. Imechukuliwa 23.05.2022

 2. Small pox vaccine. https://www.cdc.gov/smallpox/vaccine-basics/index.html. Imechukuliwa 23.05.2022

 3. WHO. Mankeypox. https://www.who.int/emergencies/disease-outbreak-news/item/2022-DON385. Imechukuliwa 23.05.2022
54 views0 comments

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page