Varicocele ni ugonjwa unaotokana na kukua kwa mishipa ya vena inayotoa damu yenye oksijeni kidogo kutoka kwenye kifuko kinachobeba korodani. Varicocele hutokana na kutuwama kwa damu ndani ya mishipa hii badala ya kuwa kwenye mzunguko wa kawaida.
Ugonjwa huu mara nyingi huanza wakati wa kubarehe na ukubwa wa tatizo huendelea jinsi umri unavyoongezeka licha ya wenye tatizo kutoonyesha dalili wala madhara yoyote yale, hata hivyo huweza kusababisha maumivu na bughudha maeneo ya siri.
Madhara ya varicocele huweza kuwa pamoja na ukuaji duni wa korodani na uzalishaji duni wa manii, matatizo haya hupelekea ugumba.
Endapo kuna shaka au uwepo wa ugumba, upasuaji unaweza kufanyika ili kukabiliana na tatizo hili.
Dalili za varicocele
Maumivu. Maumivu huwa ya wastani, mithiri ya kuwasha na hutokea sana wakati wa kusimama au nyakati za jioni na hupungua kwa kulala.
Uvimbe wa ngozi ifunikayo korodani. Kama vena za kwenye kifuko cha korodani zikikuwa kupita kiasi, hutengeneza umbile mithiri ya kifuko kilichojaa minyoo. Varicocele ndogo ni rahisi kuonekana kwa kushika kuliko kutazama kwa macho.
Korodani kuwa na ukubwa tofauti. Korodani iliyoathirika huweza kuwa ndogo kuliko korodani nyingine.
Ugumba. Varicocele hupelekea ugumu wa kutungisha mimba kutokana na uzalishani duni wa manii. Hata hivyo si varicocele zote husababisha ugumba kwa mwanaume.
Wakati gani wa kuonana na daktari?
Ni vema watoto wanaokaribia kubarehe kufanyiwa uchunguzi wa korodani zao ili kutathmini afya yao kwa ujumla na kupata tiba au ushauri kwa wakati kama mabadiliko yataonekana.
Kwa sababu kuna hali na magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababisha maumivu na uvimbe kwenye korodani, inashauriawa kuonana na daktari mara moja kwa ushauri na tiba endapo utaona mabadiliko yoyote yale au kupata dalili zilizoorodheshwa hapo juu.
Visababishi vya varicocele
Ngozi ifunikayo korodani hupokea damu yenye oksijeni kutoka kwenye mishipa miwili, kila mshipa huingia kwenye korodani yake. Vivyo hivyo, kuna mishipa mikuu miwili ya vena inayotoa damu isiyo na oksijeni kutoka kwenye kila kifuko cha korodani ili kuirudisha kwenye moyo. Kwenye kila kifuko cha korodani pia kuna mkusanyiko wa mishipa midogomidogo ya vena inayokusanya damu isiyo na oksijeni na kuipeleka kwenye mishipa mikuu ya vena ya korodani. Varicocele hutokea endapo mishipa hii midogomidogo imevimba kwa kujaaa damu.
Kisababishi halisi cha varicocele hakifahamiki. Inafikiriwa kwamba udhaifu katika valvu za vena ya korodani husababisha damu ishindwe kusafiri hivyo hivyo kutuwama sehemu moja na kuleta uvimbe unaoitwa varicocele.
Mishipa ya vena ya kifuko cha korodani ya kushoto kwa kuwa huwa na njia tofauti ya kurudisha damu, hupelekea varicocele kutokea sana upande huu.
Vihatarishi
Hakuna visababishi vinavyoonekana kusababisha mtu apate varicocele.
Madhara ya varicocele
Kuwa na varicocele hufanya mwili ushindwe kudhibiti joto la mwili katika korodani hivyo hupelekea ongezeko la msongo na ongezeko la sumu. Madhara yafuatayo yanaweza kutokea kutokana na hili:
Korodani kuwa dhaifu: Kwa watoto wa kiume wanaokaribia kubarehe, varicocele huweza kuzuia ukuaji wa korodani, uzalishaji wa homoni na mambo mengine yanayotokana na kazi na afya ya korodani. Kwa wanaume waliokwisha kubarehe, varicocele huweza sababisha kusinyaa taratibu kwa korodani.
Ugumba. Ugonjwa wa varicocele mara nyingi huwa hausababishi ugumba, hata hivyo takribani asilimia 15 hadi 20 ya wanaume walio na varicocele hupata ugumu kubebesha mimba. Kati ya wanaume wote wenye varicocele, asilimia 40 huwa na varicocele.
Vipimo
Mtaalamu wa afya atagundua uwepo wa varicocele kwa kukuangalia kwa macho au kushika kifuko cha korodani. Uchunguzi huu hufanyika ukiwa umelala au kusimama.
Vipimo vya picha
Mtaalamu wa afya anaweza kuamua afanye kipimo kingine cha picha kama ultrasound ili kuchunguza zaidi kifuko cha korodani. Kipimo hiki kinaweza kusaidia mtaalamu huyu:
Kuthibitisha varicocele na kuangalia sifa zingine za varicocele
Kutofautisha varicocele na magonjwa mengine yenye dalili zinazofanana
Kutambua majeraha na mambo madhaifu mengine yanayoweza kuchangia kutokea kwa varicocele
Matibabu
Si lazima kupatiwa matibabu endapo una varicocele, hata hivyo endapo mwanaume ambaye ana tatizo la ugumba, upasuaji wa kuondoa varicocele huwa moja ya njia ya kutibu ugumba huu.
Kwa watoto wanaoelekea kubarehe na vijana wadogo wanaotafuta watoto, mara nyingi hushauriwa kufanya uchunguzi ili kubaini mabadiliko na upasuaji unaweza kuhitajika endapo kuna hali zifuatazo:
Kuchelewa kukua kwa korodani
Kiwango kidogo cha mbegu za kiume au kuwa na madhaifu ya kimaumbile
Maumivu makali yaliyoshindikana kudhibitiwa kwa dawa za maumivu
Upasuaji
Madhumuni ya upasuaji ni kufunga mishipa ya vena iliyoathirika na kuelekeza damu kusafiri kwenye mishipa mingine yenye afya.
Matokeo ya upasuaji huwa yafuatayo:
Korodani ikiyoathirika kurejea kwenye umbo lake la awali, endapo ni kijana mdogo, korodani hii itakuwa na kufanana na nyenzake.
Ongezeko la idadi ya manii
Ongezeko la manii na ubora wake
Madhara ya upasuaji
Matibabu ya varicocele kwa upasuaji huweza kupelekea hatari kidogo ya:
Kupata ngiri maji (hydrocele)
Kurejea kwa varicocele
Maambukizi kwenye korodani
Maumivu sugu ya korodani
Kuharibiwa kwa arteri za korodani
Kutuwama kwa damu katika korodani
Uchaguzi wa kufanya upasuaji hubadilika endapo lengo la matibabu ni kuondoa maumivu. Licha ya varicocele kuweza kusababisha maumivu, ni nadra sana kutokea. Maumivu ya korodani kwa mgonjwa mwenye varicocele yanaweza kusababishwa na magonjwa mengine pia yanayofahamika au kutofahamika. Endapo lengo la matibabu ya upasuaji ni kudhibiti maumivu, maumivu hayo yanaweza kuongezeka mara dufu au kubadilika tabia.
Kubadili mtindo wa maisha na matibabu ya nyumbani
Kama una maumivu ya varicocele yanayosababisha bugudha kiasi, lakini yasiyodhuru uzazi wako, waweza kufanya mambo yafuatayo kudhibiti maumivu:
Kutumia dawa za maumivu zisizohitaji cheti cha daktari kama parasetamo n.k
Kuzishikiria korodani kwa kuvaa nguo ya ndani yenye uwezo wa kuzibeba vema
Rejea za mada hii
Ferri's Clinical Advisor 2022. Elsevier; 2022. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 23.05.2022
Varicoceles. Urology Care Foundation. https://www.urologyhealth.org/urology-a-z/v/varicoceles. Accessed Nov. 16, 2021.
Eyre RC. Nonacute scrotal conditions in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 23.05.2022
Zundel S, et al. Management of adolescent varicocele. Seminars in Pediatriac Surgery. 2021; doi:10.1016/j.sempedsurg.2021.151084.
Brenner JS. Causes of painless scrotal swelling in children and adolescents. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 23.05.2022.
Partin AW, et al., eds. Campbell-Walsh-Wein Urology. 12th ed. Elsevier; 2021. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 23.05.2022.
Varicocele embolization. Radiological Society of North America. https://www.radiologyinfo.org/en/info/varicocele. Imechukuliwa 23.05.2022.
留言