top of page

Zaidi ya asilimia 80 ya maradhi huepukwa kwa kudhibiti Msongo| ULY CLINIC

Msongo ni mchakato wa mwili kupoteza uwezo wa kubadilika ili kukabiliana na mabadiliko ya hali au mazingira inayopelekea mabadiliko ya kisaikolojia na kibiologia, yanayochangia kusababisha magonjwa.Kwa maana nyingine ni hali ya mwili kuhisi umelemewa na jambo lililopo mbele na hivyo kushindwa kukabiliana nalo vema kibayolojia au kisaikolojia


Ili mwili upate msongo, lazima kuwe na kiamshi, ambacho huitwa kichocheo. Kuna aina nyingi za vichocheo vinavyoweza kusababisha msongo kama vile mahangaiko/mapambano ya kufanikiwa, kulemewa na kazi, kipato duni, malumbano ndani ya mahusiano au familia na mambo mengine yasiyoorodheshwa hapa.


Mahusiano ya msongo na magonjwa


Uhusiano wa msongo na kutokea kwa magonjwa ni tata, ikimaanisha hutegemea mtu na mtu na sababu mbalimbali kama sababu za kijeni, njia ya kukabiliana na msongo, aina ya utu na msaadamtu anapata kwenye jamii yake. Mtu anapopata kichocheo kwa kawaida, hujipima endapo kipo ndani ya uwezo wake au la. Endapo kichocheo kipo ndani ya uwezo wa mtu kikabiliana nacho, hukifanyia kazi na kikaisha, isipokuwa endapo kipo nje ya uwezo basi hupelekea mtu huyu kupata msongo wa muda mrefu na madhara kuonekana. Kutokana na maelezo haya, inamaanisha kuwa kichocheo kinachopelekea msongo wenye madhara kwa mtu mmoja kinaweza kisisababishe madhara kwa mtu mwingine na pia namna mtu anavyoitikia kukabiliana na kichocheo huchangia kutokea au kutotokea kwa madhara ya msongo.


Dalili za kiakili

 • Kukasirika haraka, kuchanganyikiwa na kuwa na hisia za kubadilika

 • Hisia za kutindikiwa kama vile kuona huna uwezo tena wa kudhibiti kitu Fulani, au kutaka kudhibiti kitu Fulani lakini

 • Kutokuwa na utulivu au kushindwa kutuliza akili

 • Kujihisi hufai, mpweke, usiye na thamani na mwenye mawazo mengi

 • Kujitenga na watu wengine

Dalili za kimwili

 • Kuishiwa nguvu

 • Maumivu ya kichwa

 • Mvurugiko wat umbo mfano choo kigumu, kuharisha na kichefuchefu

 • Maumivu , kubana na kuchomachoma kwa misuli

 • Maumivu ya kifua na mapigo ya moyo kwenda haraka

 • Kukosa usingizi

 • Kuugua mafua mara kwa mara na kupata maambukizi

 • Kukosa hamu au uwezo wa kufanya tendo la ndoa

 • Kukauka midomo na kushidnwa kumeza chakula

 • Kukaza kwa taya na kusagana kwa meno


Madhara ya msongo


Madhara ya muda mrefu wa msongo

Msongo wa muda mfupi si hali ya kutia hofu, endapo msongo unadumu zaidi ya muda wa miezi mitatu inatakiwa jamii itambue na kumsaidia mtu huyu kumuepusha na madhara makubwa yanayoweza kujitokeza. Madhara hayo baadhi yake ni;

 • Magonjwa ya akili

 • Magonjwa ya mfumo wa mishipa ya damu na moyo

 • Mabadiliko ya mwili

 • Kuongezeka uzito na matatizo mengine ya unene

 • Matatizo ya hedhi

 • Matatizo uzazi

 • Madhaifu ya ngozi


Namna ya kukabiliana na msongo


Kula na kunywa maji ya kutosha.


Watu wengi hujaribu kupunguza msongo kwa kutumia dawa za kulevya au kunywa pombe zaidi ya kawaida, kitendo hiki huharibu afya ya mtu zaidi na pia huwa hakisababishi kukabiliana na msongo. Ni vema ukiwa na msongo, unywe maji ya kutosha na mlo kamili ambao utakusaidia kukabiliana na msongo. Usitumie kahawa kwani inahusika kukuletea msongo mkubwa zaidi.


Fanya mazoezi yenye utaratibu maalumu


Mazoezi huwa na umuhimu kwenye afya ya mwili wako amoja na nguvu ya kupunguza msongo. Mazoezi mazuri si yale ya mashindano bali ni kama mazoezi ya viungo vya mwili, kunyanyua uzito, kujinyoosha pamoja na yoga. Mazoezi ya aerobic pia yanayohusisha kukimbia, kuogelea, kulima n.k husaidia mwili kujitengenezea homoni ya endorphin kwa wingi, homon inayosaidia kupunguza msongo, kukufanya uwe na mawazo chanya na kukupa usingizi mzuri.Usitumie tumbaku na mazao yake.


Watu watumiao 9tumbaku) sigara hupata pumziko la msongo wa muda mfupi, hata hivyo nicotine iliyo kwenye sigara huamsha na kufanya tatizo liwe kubwa zaidi mara baada ya kuacha. Dawa hizi pia hufanya mwili uwe mtumwa wa dawa hizo na ni ngumu kuziacha.


Soma na fanya matendo ya kupumzisha mwili na akili yako.


Kupata muda wa kupumzika kila siku hulinda mwili wako dhidi ya madhara ya msongo. Unaweza kutumia njia mbalimbali za kupumzisha mwili wako kama vile kupumua kwa kina, kupumzisha misuli kwa muda mrefu, kutengeneza picha ya vitu kwenye akili na kutafakari kwa kina.


Punguza vichocheo vya msongo


Maisha yako yanaweza kujawa na mahitaji mengi na matamanio mengi na ukawa na muda kidogo sana wa kupumzika, hata hivyo mara nyingi mahitaji haya ni yale ambayo sisi wenyewe tumeyachagua na hutuangaisha. Unaweza kujipa muda mwingi binafsi kwa kupunguza au kupanga muda wako vema na kupata muda wa kufanya kazi na muda wa kuwa na muda mwenyewe. Weka malengo yako na weka mipango ya kufikia malengo kisha fuata mpango mmoja baada ya mwingine kufikia malengo. Usitumie nguvu nyingi kupata mafanikio kwani mafanikio huja taratibu hatua kwa hatua.


Tambua kwanini upo duniani


Kutambua kwanini unaishi, na nini unataka katika maisha yako kutafanya uishi maisha yako ya kipekee na yasiyotegemea mvuto wa watu wengine. Kuishi maisha yaliyo madhumuni ya maisha yako duniani hufungua furaha, kuridhika na kujiamini wakati wote bila kuyumbishwa na mambo yanayopita.


Weka malengo yenye uhalisia


Ni vema na ni sawa kuwa si lazima kupata asilimia 100 ya matamanio yako katika maisha mara moja, hata hivyo unapoweka malengo fuata mipango uliyoiweka kutimiza malengo yako. Kubali vitu ambavyo unaweza kuvidhibiti na ambavyo usivyoweza kuvidhibiti.


Jisifie au jipongezekwa mafanikio uliyoyafikia


Unapohisi umelemewa na mzigo wa maisha, jikumbushe kuwa kuna mambo mengi umeshafanya katika maisha na unaendelea kufanya vema. Hii itaamsha kujikubali na kuondoa msongo wa mawazo.


Ongea na daktari wa akili


Kuongea na daktari wa magonjwa ya akili endapo unaona hupati msaada kwa njia zote zilizoorodheshwa hapa kutakusaidia kukupa mwanga wa nini ufanye. Wasiliana na daktari siku zote endapo unaishi dalili zozote zile za msongo. Endapo pia kuna ndugu yako ana dalili hizi ni vema ukamsaidia kupata msaada wa daktari.


Pata msaada wa kiroho


Onana na imamu au mchungaji wako kwa ushauri kuhusu mambo ya kiroho. Hii itasaidia kukupa Amani moyoni na kupunguza au kuondoa msongo wa mawazo. Shiriki maombi, jiamini na jiombee mwenyewe.


Kumbuka


Makala hii katika baadhi ya aya imetumia neno msongo kumaanisha msongo wa mawazo na kinyume chake ni kweli. Msongo na msongo wa mawazo imechukuliwa kuwa kitu kimoja kwa kuwa vyote hupelekea kuonekana kwa dalili kama zilivyoorodheshwa hapo juu.


Soma zaidi kuhusu makala hii kwa kubofya hapa.

Soma makala nyingine za wasiwasi na hofu liyopitiliza kwa kubofya hapa


Endapo una maswali zaidi na kutaka ufafanuzi wasiliana na daktari wako au daktari wa ULY CLINIC kwa kupitia mawasiliano chini ya tovuti hii.


Rejea za mada hii;


 1. Physiology, Stress Reaction. Brianna Chu, et al. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK541120/. Imechukuliwa 04.06.2021

 2. Life Event, Stress and Illness. Mohd. Razali Salleh. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3341916/. Imechukuliwa 03.06.2021

 3. Habib Yaribeygi, et al. The impact of stress on body function: A review. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5579396/. Imechukuliwa 02.06.2021

 4. Bruce McEwen et al. stress and your health. https://academic.oup.com/jcem/article/91/2/E2/2843213. Imechukuliwa 04.06.2021

 5. American Institute of Stress: "Effects of Stress.". https://www.stress.org/. Imechukuliwa 04.06.2021

 6. Stress Management for the Health of It. https://nasdonline.org/1445/d001245/stress-management-for-the-health-of-it.html#. Imechukuliwa 04.06.2021

 7. Stress. https://www.mentalhealth.org.uk/a-to-z/s/stress#:. Imechukuliwa 04.06.2021

64 views0 comments

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page