top of page
Fangasi wa mokononi- ulyclinic

Imeandikwa na ULY CLINIC

Tinea manuum

(Ugonjwa wa Fangasi wa mikono)

Utangulizi

Makala hii imezungumzia kuhusu ugonjwa wa fangasi mikononi kwa jina jingine la Tinea manuum. Tinea manuum ni jina la ugonjwa wa fangasi unaodhuru mikono tu na hutokea kwa nadra sana ukilinganisha na fangasi wa kanyagio wenye jina la Tinea pedis.


Ugonjwa huu huchanganywa mara nyingi na magonjwa mengine ya soriasis ya mikono na keratolisis eksfolietiva. Katika makala hii utajifunza dalili zake.

 

TInea manuum ni ugonjwa wa ngozi unaosababishwa na maambukizi ya fangasi aina ya dematofaiti, huathiri sana mikono na miguu na kwa mara chache hutokea kwenye mikono tu pekee. Hata hivyo maeneo ya mikono yanayoweza kuathiriwa ni viganja vya mikono, katikati ya vidole au sehemu za nyuma ya kiganja cha mikono.

Dalili za tinea manuum

Dalili za tinea manuum hutegemea fangasi anayesababisha ugonjwa huo, dalili zilizo hapa chini zinaweza kutokea, si lazima uwe na dalili zote, lakini unaweza kuwa na dalili kuanzia 3 na kuendelea

 • Mwonekano wa harara yenye umbo la shiringi,huanza kidogo na kukua jinsi mdaunavyokwenda

 • Maambukizi huanzia kwenye kiganja cha mkono na baadae kusambaa kweney vidole au nyuma ya kiganja

 • Kubanduka kwa ngozi

 • Kupata miwasho kwenye ngozi yenye fangasi

 • Kukauka kwa ngozi

 • Kuongezeka kwa alama kwenye ngozi

 • Kubanduka kwa ngozi

 • Kufanyika kwa malenge kwenye miishio ya vidole vya mikono- huwa na majimaji safi yanayonata 

Dalili za kipekee kabisa za ugonjwa huu zinazotofautisha ugonjwa huu na demataitizi ya mikononi ni;

 

 • Mara nyingi hutokea kwenye mkono mmoja

 • Endapo mikono miwili imeathiriwa, maranyingi ugonjwa wa mkono mmoja na mwingine huwa haufanani

 • Alama kwenye mikono huongezeka sana kwenye demataitis, wakati tinea manuum huwa haina alama kwa sababu ya kufanyika kwa magamba na kutoka

 • Huathiri kiganja cha mkono na nyuma ya kiganja kama mwendelezo wa ugonjwa

 • Harara huweza kuwa na mwinuko kwenye ukingo

 • Kucha zilizo karibu na ugonjwa huweza kuathiriwa pia

Visababishi

Visababishi vya fangasi kwenye ngozi ya mikono ni maambukizi ya fangasi, aina hizi za fangasi zinaweza kuwa kutoka kwa fangasi wanaodhuru wanyama, au wale wanaodhuru binadamu

Fangasi wanaodhuru binadamu ni

 • Tinea rubrum

 • Tinea interdigitale

 • Epidermophyton floccosum

Fangasi wanaodhuru wanyama

 • Trichophyton erinacei — Kutoka kwa nungunungu

 • Tinea verrucosum — Kutoka kwa ngombe

 • Microsporum canis — Kutoka kwa paka au mbwa

 • Nannizzia gypsea — Wanaopatikana kwenye udongo

Vihatarishi

Unaweza kupata fangasi mikononi kwa;

 • Kushika maeneo ambayo yameathirika na fangasi kwa mfano ukiwa na fangasi miguuni, au kwenye kinena

 • Kushika mgonjwa mwenye fangasi hasa maeneo yenye ugonjwa inaweza kuwa wakati wa kupeana mikono, kugusana wakati wa michezo kama mpira wa miguu n.k

 • Kumshika mnyama mwenye fangasi, inaweza kuwa wakati wa kuwahudumia n.k

 • Kushika udongo wenye fangasi

 • Kushika vifaa vyenye fangasi mfano matumizi ya taulo au vifaa vya kufanyia usafi na kilimo

 • Matumizi ya vyoo na bafu za kwenye jamii(Matumizi ya bafu na vyoo vya watu wengi)

 • Kuugua ugonjwa wa demataitizi ya mikono

 • Kufanya kazi zinazosababisha kutokwa na jasho mikononi

 • Kutokwa na jasho sana mikononi

 

Vipimo na matibabu


Ugonjwa unatambuliwaje?

Kipimo cha kutumia hadubini na culture ya magamba na ngozi ilokwanguliwa kutoka kwenye kidonda hufanyika ili kutofautisha ugonjwa huu na mengine yanayofanana nayo.

Matibabu

Matibabu huhusisha matumizi ya dawa za antifangasi. Dawa za kupaka hutumika kwa ugonjwa ambao si mkali, na dawa za kumeza hutumika kwa ugonjwa sugu au ulio mkali


Wasiliana na daktari wako kukwambia ni aina gani ya dawa inakufaa wewe. Hata hivyo ugonjwa huwa hauondoki kirahisi inaweza kuchukua zaidi ya mwezi mmoja

Kujikinga

Ugonjwa wa tinea manuum hutibika endapo utapata matibabu sahihi. Baadhi ya watu ugonjwa unaweza kuwa sugu na kuhitaji dawa za kunywa. Watu wengi ugonjwa unaweza kupotea baada ya wiki chache hadi mwezi

Ili kujikinga na ugonjwa huu fanya mambo yafuatayo

 • Hakikisha mikono yako inakuwa misafi, nawa na  kausha kwa kitambaa endapo una tatizo la kutokwa na jasho au unatumia glovu sana

 • Acha kushikana mikono na mgonjwa mwenye fangasi wa mikononi au kugusa sehemu yoyote ile ya mwili yenye ugonjwa

 • Usitumie vitu vya mgonjwa mwenye fangasi kama taule, nguo n.k

 • Endapo una fangasi sehemu nyingine ya mwili, zuia kukwangua kwa mikono mitupu kuepuka kuwasambaza mikononi, unaweza kutumia glavu ili kuzuia kujiambukiza sehemu nyingine ya mwili

 • Hakikisha unaonana na ikiwa umetumia dawa bila kupata mafanikio yoyote yale

 

Nenda kwenye makala nyingine zaidi za magonjwa ya ngozi kwa kubonyeza hapa


Imeboreshwa mara ya mwisho, 1.11.2020

ULY CLINIC inakushauri siku zote ufuate ushauri wa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kaifya

 

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri zaidi na tiba kupitia namba za simu au kubonyeza pata tiba chini ya tovuti hii.


Rejea za mada hii;

 1. Dermanet. NZ. Tinea manuum. https://dermnetnz.org/topics/tinea-manuum/. Imechukuliwa 31.10.2020

 2. Health line. Tinea manuum. https://www.healthline.com/health/tinea-manuum. Imechukuliwa 31.10.2020

 3. NCBI. Tinea manuum. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK559048/. Imechukuliwa 31.10.2020

 4. American Family Physician. Dermatophyte Infection. https://www.aafp.org/afp/2003/0101/p101.html. Imechukuliwa 31.10.2020

 5. Uptodate. Dematophyte(tinea( infections. https://www.uptodate.com/contents/dermatophyte-tinea-infections. Imechukuliwa 31.10.2020

bottom of page