top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Dkt. Benjamin S, MD

Dkt. Lugonda, MD

6 Februari 2026, 04:28:59

Kizuizi/diaphragm

Uzazi wa mpango wa kizuizi/kiwambo aina ikifahamika kwa majina mengine ya dayaframu au diaphragm ni mojawapo ya njia zisizo za homoni zinazotumika kuzuia mimba. Njia hii hufanya kazi kwa kuzuia mbegu za kiume kuingia kwenye mfuko wa uzazi wakati wa tendo la ndoa. Ni chaguo linalowafaa wanawake wanaopendelea njia ya muda mfupi, inayotumika pale inapohitajika, na isiyo na homoni.


Kiwambo cha uzazi wa mpango ni nini?

Kiwambo ni kifaa cha raba laini (au silikoni) chenye umbo la duara lililopinda kama pia. Huwa na kingo laini zinazosaidia kukaa vizuri kwenye mlango wa shingo ya kizazi (seviksi).

  • Huwekwa ndani ya uke kabla ya tendo la ndoa

  • Hufunika kabisa mlango wa kizazi

  • Mara nyingi hutumika pamoja na dawa ya kuua mbegu za kiume (Viua manii) ili kuongeza ufanisi


Kiwambo hufanya kazi vipi?

Kiwambo cha uzazi wa mpango huzuia mimba kwa njia zifuatazo:

  1. Huzuia mbegu za kiume kupenya kuingia kwenye mfuko wa uzazi

  2. Dawa ya kuua mbegu (ikitumika) huua au kudhoofisha mbegu za kiume

Kwa pamoja, mbinu hizi huzuia urutubishaji wa yai kabla mimba haijatokea.


Diaphragm huwekwa na nani?

  • Kiwambo cha uzazi wa moango huchaguliwa na kupimwa ukubwa wake na mtoa huduma wa afya aliyepata mafunzo

  • Daktari au muuguzi humsaidia mwanamke kuchagua ukubwa sahihi na kumfundisha namna ya kuiweka na kuitoa

  • Baada ya mafunzo, mwanamke anaweza kujiwekea mwenyewe nyumbani


Hutumika lini na kwa muda gani?

  • Huwa inawekwa kabla ya tendo la ndoa (dakika chache hadi saa kadhaa kabla)

  • Lazima ibaki ndani ya uke kwa angalau masaa 6 baada ya tendo la ndoa

  • Haipaswi kubaki zaidi ya masaa 24 mfululizo


Ufanisi wa kiwambo cha uzazi wa moango ni kiasi gani?

Ufanisi hutegemea matumizi sahihi:

  • Matumizi ya kawaida: takribani 83%

  • Matumizi sahihi kila wakati: hadi 94%

Kutumia viua manii kila mara huongeza ufanisi.


Faida za kutumia diaphragm

  • Hakina homoni

  • Hutumika pale inapohitajika

  • Haiathiri uzalishaji wa maziwa ya mama

  • Mwanamke ana udhibiti kamili wa matumizi

  • Uwezo wa kushika mimba hurudi mara moja baada ya kuacha kutumia


Madhara yanayoweza kutokea

Baadhi ya watumiaji wanaweza kupata:

  • Kuwashwa au muwasho ukeni

  • Maumivu au usumbufu wakati wa kujamiiana

  • Mzio wa mpira (latex) au viua manii


Hatari zinazojulikana


1. Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

Matumizi ya diaphragm yanaweza kuongeza hatari ya kupata UTI, hasa kwa wanawake wanaopata UTI mara kwa mara.


2. Sindromu ya mshituko wa sumu (TSS)

  • Ni nadra sana, lakini imewahi kuripotiwa

  • Wanawake wenye historia ya sindromu ya mshituko wa sumu hawashauriwa kutumia kiwambo


Je, mabadiliko ya uzito yanaathiri matumizi ya diaphragm?

Ndiyo.

  • Kupungua au kuongezeka sana kwa uzito, kujifungua, au kufanyiwa upasuaji wa nyonga

  • Kunaweza kusababisha diaphragm isikale vizuri kwenye mlango wa kizazi

Hali hii huhitaji kupimwa upya au kubadilishiwa diaphragm.


Nani anafaa kutumia diaphragm?

Inafaa kwa wanawake:

  • Wanaotaka njia isiyo ya homoni

  • Wenye mpango wa muda mfupi wa uzazi

  • Wanaonyonyesha

  • Wanaotaka kudhibiti wenyewe matumizi ya uzazi wa mpango


Nani hapaswi kutumia kiwambo?

Haipendekezwi kwa wanawake:

  • Wenye historia ya sindromu ya mshituko wa sumu

  • Wanaopata UTI mara kwa mara

  • Wenye mzio wa mpira au viua manii

  • Wasioweza kutumia kwa usahihi kila mara


Je, kiwambo hulinda dhidi ya magonjwa ya zinaa?

Hapana, kondomu inapaswa kutumika pamoja na diaphragm kwa kinga dhidi ya VVU na magonjwa ya zinaa.


Hitimisho

Diaphragm ni njia salama ya uzazi wa mpango wa kizuizi kwa wanawake wanaotaka njia isiyo na homoni na inayotumika inapohitajika. Hata hivyo, ufanisi wake unategemea matumizi sahihi na nidhamu. Ushauri wa mtoa huduma ya afya ni muhimu kabla ya kuanza kuitumia.



Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara kuhusu kiwambo cha uzazi wa mpango(Dayaframu) na majibu yake

1. Kiwambo cha uzazi wa mpango ni nini?

Kiwambo cha uzazi wa mpango ni kifaa cha raba laini au silikoni chenye umbo la duara lililopinda kama pia, kinachowekwa ndani ya uke wa mwanamke ili kufunika mlango wa kizazi (shingo ya kizazi). Lengo lake kuu ni kuzuia mbegu za kiume kuingia kwenye mfuko wa uzazi, hivyo kuzuia mimba isitunge. Ni njia ya uzazi wa mpango wa kizuizi na haina homoni.

2. Kiwambo hufanya kazi vipi kuzuia mimba?

Kiwambo hufanya kazi kwa kuweka kizuizi cha kimwili kati ya mbegu za kiume na yai. Kinapowekwa vizuri juu ya mlango wa kizazi, mbegu hushindwa kupenya kuingia kwenye mfuko wa uzazi. Mara nyingi hutumika pamoja na dawa ya kuua mbegu za kiume (viua manii), ambayo huua au kudhoofisha mbegu ili kuongeza ufanisi wa kuzuia mimba.

3. Kiwambo huanza kufanya kazi baada ya muda gani?

Kiwambo huanza kufanya kazi mara moja endapo kitawekwa kwa usahihi kabla ya tendo la ndoa na kutumika pamoja na viua manii. Hakihitaji kusubiri saa au siku ili kuanza kufanya kazi, lakini ni muhimu kuhakikisha kimekaa vizuri kabla ya kujamiiana.

4. Ufanisi wa kiwambo cha uzazi wa mpango ni kiasi gani?

Ufanisi wa kiwambo hutegemea namna kinavyotumika:

  • Kwa matumizi ya kawaida, ufanisi wake ni takribani 83%

  • Kwa matumizi sahihi na ya nidhamu, pamoja na spermicide kila mara, ufanisi unaweza kufikia hadi 94%

Hii inaonyesha kuwa matumizi sahihi ni muhimu ili kupata kinga bora dhidi ya mimba.

5. Madhara ya kutumia kiwambo cha uzazi wa mpango ni yapi?

Baadhi ya wanawake wanaweza kupata madhara madogo kama:

  • Muwasho au kuwaka ukeni

  • Usumbufu wakati wa kujamiiana

  • Mzio wa mpira (latex) au spermicide Madhara haya mara nyingi huwa ya muda mfupi na hupungua kadri mwili unavyozoea.

Madhara makubwa ni nadra sana.

6. Je, kiwambo kinaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)?

Ndiyo. Matumizi ya kiwambo yanaweza kuongeza hatari ya UTI, hasa kwa wanawake wanaopata maambukizi ya njia ya mkojo mara kwa mara. Hii hutokana na shinikizo la kiwambo kwenye urethra, ambalo linaweza kuzuia mtiririko mzuri wa mkojo.

7. Ni nani hapaswi kutumia kiwambo cha uzazi wa mpango?

Kiwambo hakipendekezwi kwa wanawake:

  • Wenye historia ya sindromu ya mshituko wa sumu (TSS)

  • Wanaopata UTI mara kwa mara

  • Wenye mzio wa mpira (latex) au dawa za kuua mbegu

  • Wasioweza kukitumia kwa usahihi kila mara Katika hali hizi, ushauri wa mtaalamu wa afya unahitajika ili kuchagua njia mbadala.

8. Je, mabadiliko ya uzito yanaathiri matumizi ya kiwambo?

Ndiyo. Kuongezeka au kupungua sana kwa uzito, kujifungua, au kufanyiwa upasuaji wa nyonga kunaweza kusababisha kiwambo kisikale vizuri kwenye mlango wa kizazi. Hali hii huhitaji mwanamke kupimwa upya au kubadilishiwa kiwambo ili kuendelea kupata ufanisi mzuri.

9. Je, kiwambo hulinda dhidi ya magonjwa ya zinaa?

Hapana. Kiwambo hailindi dhidi ya VVU wala magonjwa mengine ya zinaa. Kwa kinga dhidi ya maambukizi, inashauriwa kutumia kondomu pamoja na kiwambo.

10. Je, ninaweza kushika mimba mara tu baada ya kuacha kutumia kiwambo?

Ndiyo. Kiwambo hakibadilishi uwezo wa mwanamke kushika mimba kwa muda mrefu. Uwezo wa kushika mimba hurudi mara moja baada ya kuacha kutumia kiwambo, endapo hakuna tatizo jingine la kiafya.


Imeandikwa:

3 Novemba 2021, 12:31:24

ULY clinic inakushauri siku zote ufuate ushauri wa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia mawasiliano yetu.

Rejea za mada;

  1. World Health Organization. Family planning: A global handbook for providers. 3rd ed. Geneva: World Health Organization; 2018.

  2. World Health Organization. Medical eligibility criteria for contraceptive use. 5th ed. Geneva: World Health Organization; 2015.

  3. World Health Organization. Selected practice recommendations for contraceptive use. 3rd ed. Geneva: World Health Organization; 2016.

  4. Centers for Disease Control and Prevention. Barrier methods of contraception. Atlanta: CDC; 2020.

  5. Faculty of Sexual and Reproductive Healthcare (FSRH). Barrier methods for contraception. London: FSRH; 2019.

  6. Trussell J. Contraceptive failure in the United States. Contraception. 2011;83(5):397–404.

  7. Hatcher RA, Nelson AL, Trussell J, et al. Contraceptive technology. 21st ed. New York: Ayer Company Publishers; 2018.

bottom of page