top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt . Benjamin L, MD

12 Novemba 2025, 12:24:53

Sindano ya uzazi wa mpango

Sindano ya uzazi wa mpango ni mojawapo ya njia maarufu na ya uzazi wa mpango yenye kemikali aina ya medroxyprogesterone acetate ambayo hufanya kazi kama homoni progesterone kuzuia ujauzito. Huchomwa kila baada ya miezi mitatu na hujulikana pia kwa jina la Medroxyprogesterone acetate au kwa majina ya kibiashara kama Depo provera.


Je sindano ya uzazi wa mpango huzuiaje ujauzito?

Sindano ya depo huzuia ujauzito kwa kudumaza uzalishaji wa mayai katika ovari pamoja na kufanya ute unaozalishwa kuwa mzito kutoruhusu manii kupenya na kuingia katika kizazi.


Je sindano ya uzazi wa mpango huzuia magonjwa ya zinaa?

Ingawa sindano ya uzazi wa mpango huzuia kupata ujauzito, kemikali hii haizuii kupata magonjwa ya zinaa hivyo utapaswa kutumia njia zingine za kujikinga na magonjwa ya zinaa.


Je, sindano ya uzazi wa mpango hutumikaje?

Sindano ya kwanza ya uzazi wa mpango hutolewa mara nyingi ndani ya siku 7 za kwanza mara unapoona damu ya hedhi. Hata hivyo inaweza kutolewa wakati mwingine pale ambapo wewe na mtoa huduma mnauhakika kwamba hauna ujauzito. Utapimwa kipimo cha ujauzito kwanza kabla ya kuchomwa sindano hii.

Baada ya kuchomwa sindano ya uzazi wa mpango, hakuna hatua za ziada utakazopaswa kuchukua kuzuia ujauzito.


Utahitaji kuchoma sindano inayofuata kila baada ya miezi mitatu na unashauriwa usichelewe zaidi ya wiki mbili tangu kukamilika kwa miezi mitatu la sivyo unaweza kushika ujauzito.


Je sindano ya uzazi wa mpango huanza kufanya kazi baada ya muda gani?

Sindano ya depo huanza kufanya kazi mara moja baada ya kuchoma endapo itachomwa wakati upo kwenye kipindi cha hedhi. Kama ikitolewa muda mwingine tofauti na huu katika mzunguko wako wa hedhi, utahitajika kusubiria kwa angalau siku 10 kabla ya kushiriki ngono bila kutumia kizuia ujauzito kingine.


Je, mwanamke yeyote anaweza kutumia sindano ya uzazi wa mpango?

Hapana! Licha ya sindano hii kuweza kutumika kwa wanawake wengi, baadhi ya wanawake wenye hali na magonjwa yafuatayo hawashauriwi kutumia njia hii ya uzazi wa mpango kuepuka madhara. Wanawake hao ni wale wenye:

  • Kutokwa damu ukeni bila sababu

  • Ugonjwa wa ini

  • Saratani ya matiti

  • Lupasi

  • Kiharusi

  • Magonjwa ya moyo


Maudhi ya sindano ya uzazi wa mpango

Mwanamke anayetumia sindano ya uzazi wa mpango anaweza kupata miongoni mwa maudhi yafuatayo ambayo hutokea sana.

  • Kubadilika kwa mzunguko wa hedhi, unaweza kuwa mfupi au mrefu

  • Maumivu ya kichwa

  • Hofu

  • Huzuniko

  • Chunusi

  • Kubadilika kwa hamu ya kula

  • Kuongezeka uzito

  • Kuongezeka kwa vinyweleo vya mwili haswa uoni na kiwiliwili

  • Kukatika kwa nywele za kichwani

  • Ugonjwa wa udhoofu wa mifupa( osteoporosis)


Tafiti zinaonyesha kuwa, baada ya kutumia kwa mwaka mzima, asilimia 50 ya wanawake (yaani wanawake 50 kati ya 100) huacha kuona damu ya mwezi. Mwanamke anapaswa kupata period kila mwezi ili kuwa na afya njema na hurejea baada ya kuacha kutumia sindano.


Utachukua muda gani kupata mimba baada ya kuacha kutumia sindano ya uzazi wa mpango?


Kupata ujauzito ni suala linalotegemeana na mwitikio wa mwili wako kwenye kemikali ya sindano ya uzazi wa mpango (depo-provera). Tafiti zinaonyesha utaweza kupata ujauzito katika kipindi cha wiki 12 (mezi 3) hadi 14 baada ya kuacha kutumia sindano ya uzazi wa mpango. Hata hivyo wanawake wengine wanaweza kupata mimba baada ya mwaka 1 hadi 2 kupita tangu kuacha kutumia sindano ya uzazi wa mpango.


Majina mengine ya sindano ya uzazi wa mpango


Sindano ya uzazi wa mpango hufahamika pia kwa majine mengine kama

  • Sindano ya depo

  • Sindano ya depo-provera

  • Sindano ya Medroxyprogesterone acetate

  • Uzazi wa mpango kwa sindano

  • Dawa ya kuchoma ya uzazi wa mpango


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara


1 Je, ni kawaida kutopata hedhi kwa miezi miwili baada ya kuchoma sindano ya uzazi wa mpango (Depo-Provera)?

Ndiyo, ni kawaida kabisa kutopata hedhi kwa muda baada ya kuchoma sindano ya uzazi wa mpango aina ya Depo-Provera. Sindano hii hufanya kazi kwa kuzuia yai kupevuka na pia hubadilisha mazingira ya mji wa mimba ili yasifae kwa ujauzito. Moja ya athari za kawaida ni mabadiliko ya hedhi, ambayo yanaweza kujumuisha:

  • Kukosa hedhi kwa muda (amenorea)

  • Hedhi nyepesi au isiyo ya kawaida

  • Kutokwa na damu kidogo kidogo kwa vipindi visivyotabirika


Kwa wanawake wengi, baada ya sindano ya pili au ya tatu, hedhi hukoma kabisa kwa muda wa matumizi ya Depo-Provera — jambo ambalo si hatari kiafya. Hii ni athari ya kawaida na haimaanishi kuna tatizo, lakini ikiwa unahofia au una dalili nyingine kama maumivu ya tumbo, ni vyema kumwona mtaalamu wa afya kwa uchunguzi zaidi.

2 Je, sindano ya Depo-Provera inaleta matatizo ya uzazi baadaye?

Kwa kawaida, haina madhara ya kudumu kwa uzazi. Baada ya kuacha kutumia, uzazi unaweza kuchelewa kurudi kwa miezi 6 hadi 12, lakini baadaye uwezo wa kushika mimba hurudi kawaida.

3 Depo-Provera hulinda dhidi ya magonjwa ya zinaa?

Hapana. Sindano hii hailindi dhidi ya VVU/UKIMWI wala magonjwa mengine ya zinaa. Ni kwa ajili ya kuzuia mimba tu. Tumia kondomu kwa ulinzi kamili.

4 Naweza kushika mimba muda gani baada ya kuacha sindano?

Mimba inaweza kuchelewa. Kwa wastani, wanawake hushika mimba ndani ya miezi 9 hadi 12 baada ya dozi ya mwisho.

5 Je, Depo-Provera husababisha kuongezeka uzito?

Ndiyo, baadhi ya wanawake hupata ongezeko la uzito kutokana na mabadiliko ya homoni na hamu ya kula. Lishe bora na mazoezi vinaweza kusaidia kudhibiti hali hii.

6 Je, ninaweza kupata hedhi nzito au damu isiyoisha baada ya kuchoma sindano?

Ndiyo, katika miezi ya mwanzo baadhi ya wanawake hupata damu isiyotabirika, nzito au inayoendelea kwa muda. Hali hii huimarika baada ya muda.

7 Ninaweza kuchoma sindano wakati wa kunyonyesha?

Ndiyo. Depo-Provera ni salama kwa mama anayenyonyesha na haiathiri ubora wa maziwa ya mama.

8 Sindano ya Depo-Provera huchomwa kila baada ya muda gani?

Kila baada ya wiki 12 (yaani kila baada ya miezi mitatu). Ni muhimu kuchoma kwa wakati ili kuendelea kuwa salama dhidi ya mimba.

9 Je, ninahitaji vipimo kabla ya kuanza kutumia Depo-Provera?

Mara nyingi hapana, lakini ni vizuri kumwona mtaalamu wa afya ili kuhakikisha huna hali yoyote ya kiafya inayozuia matumizi ya sindano hii.

10 Nifanye nini kama nimechelewa kuchoma sindano inayofuata?

Ikiwa imepita zaidi ya wiki 13 tangu sindano ya mwisho, unaweza kuwa katika hatari ya kupata mimba. Wasiliana na mtaalamu wa afya haraka na tumia njia ya dharura au kinga nyingine.

11. Nimekuwa nikitoka damu muda murefu 19/10/2025mpaka Leo hii zinatoka taratibu,na hii baada ya kutumia depo, nifanyaje?

Kama damu ni nyingi na inatoka kwa muda mrefu baada ya kutumia Depo, hiyo si hali ya kawaida. Inaweza kuashiria mwitikio usio mzuri wa mwili au upungufu mkubwa wa homoni za estrojeni. Nenda hospitalini haraka ili upimwe kiwango cha damu (hemoglobini), mfuko wa uzazi ukaguliwe, na upewe dawa za kusimamisha damu au kubadilishiwa njia ya uzazi wa mpango. Usichelewe, kwani kutokwa damu nyingi kunaweza kusababisha upungufu wa damu hatari.


Imeandikwa:

16 Oktoba 2024, 10:17:38

ULY clinic inakushauri siku zote ufuate ushauri wa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia mawasiliano yetu.

Rejea za mada hii:

  1. Depo provera. https://my.clevelandclinic.org/health/drugs/4086-depo-provera-birth-control-shot. Imechukuliwa 16.10.2024

  2. Hatcher RA, et al., eds. Injectable contraceptives In: Contraceptive Technology. 21st ed. Ayer Company Publishers; 2018.

  3. Kaunitz AM. Depot medroxyprogesterone acetate (DMPA) for contraception: Formulations, patient selection and drug administration. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 16.10.2024

  4. Kennedy CE, et al. Self-administration of injectable contraception: A systematic review and meta-analysis. BMJ Global Health. 2019; doi:10.1136/bmjgh-2018-001350.

  5. Hatcher RA, et al. Progestin-only contraceptives. In: Managing Contraception 2019-2020: For your pocket. 15th ed. Bridging the Gap Foundation; 2020.

  6. Hapgood JP, et al. Hormonal contraception and HIV-1 acquisition: Biological mechanisms. Endocrine Reviews. 2018; doi:10.1210/er.2017-00103.

  7. Kaunitz AM. Depot medroxyprogesterone acetate for contraception: Efficacy, side effects, metabolic impact, and benefits. https://www.uptodate.com/contents/search. Accessed Oct. 13, 2019.

  8. Long VE, et al., eds. Injectable contraceptives overview. In: Telephone Triage for Obstetrics & Gynecology. 3rd ed. Wolters Kluwer Health; 2019. http://ovidsp.ovid.com. Accessed Oct. 14, 2019.

  9. Lopez LM, et al. Progestin-only contraceptives: Effects on weight. The Cochrane Database of Systematic Reviews. 2016; doi:10.1002/14651858.CD008815.

  10. Lerma K, et al. Injectable contraception: Emerging evidence on subcutaneous self-administration. Current Opinion in Obstetrics & Gynecology. 2019; doi:10.1097/GCO.0000000000000574.

  11. Medroxyprogesterone acetate: Uses, Interactions DrugBank.https://go.drugbank.com/drugs/DB00603. Imechukuliwa 16.10.2024

bottom of page