Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD & Dkt. Salome A, MD
2 Aprili 2026, 16:17:51

Kucheua kwa watoto
Kucheua ni hali ya kurudisha chakula au maziwa kutoka tumboni kupitia koo la chakula hadi mdomoni (wakati mwingine puani) baada ya kula au kunyonya.
Hali hii ni kawaida kwa watoto, na huonekana zaidi kuanzia miezi 4 hadi 6 , hupungua taratibu baada ya muda na ni nadra sana kuendelea baada ya umri wa miezi 18.
Wakati mwingine pia huweza kuashiria tatizo kubwa zaidi kwa mtoto kama vile ugonjwa wa kucheua, kasoro katika mfumo wa umeng’enyaji wa chakula au aleji na maziwa (hasa ya ng’ombe). Kama mzazi hupaswi kuwa na wasiwasi endapo mtoto anayecheua sana ana afya njema na anaongezeka uzito.
Kwanini watoto hucheua?
Zifuatazo ni sababu zinazopelekea watoto kucheua baada ya kunyonya au kula;
Kutokomaa kwa maumbile ya mfumo wa umeng’enyaji wa chakula. Koki inayoruhusu chakula kuingia na kutotoka tumboni kutofunga ili kutoruhusu chakula kurudi kooni baada ya kula au kunyonya.
Maziwa pia huchangia kutokea kwa hali hii kwani maziwa yapo kwenye majimaji hivyo ni rahisi kurudi juu na kutolewa tena mdomoni.
Kunyonya au kushiba sana kupitilliza.
Kuwa na hewa tumboni kutokana na mama kutokufahamu namna ya kunyonyesha kwa usahihi, au mtoto kulia na kukohoa wakati wa kunyonya.
Mambo yanayoongeza hatari ya kucheua sana kwa watoto
Mambo yafuatayo huongeza hatari ya kucheua sana kwa watoto wadogo;
Kuzaliwa njiti
Kupewa maziwa ya ng’ombe
Kupewa maziwa ya fomula
Uzito mkubwa uliopitiliza
Je, ni magojwa gani husababisha mtoto kucheua isivyo kawaida?
Ingawa kucheua ni hali ya kawaida kwa mtoto, kucheua kulikokithiri na kuambatana na dalili nyingine kunaweza kuashiria mambo yafutayo;
Mzio kwenye protini ya maziwa ya ng’ombe
Ugojwa wa kucheua tindikali
Kuziba kwa umio
Kupungua kipenyo cha umio
Ni muda gani wa kuhofia endapo mtoto anacheua?
Endapo mtoto anacheua na anadalili zifuatazo fika kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi;
Anakataa kunyonya
Anapumua kwa shida
Kikohozi kisichoisha
Anajikamua kabla ya kucheua au anatapika
Anacheua manjano au kijani
Anapata tabu kumeza chakula
Kutotulia kwa kulialia baada ya kula au kunyonya
Anapata choo chenye damu
Ameanza kucheua sana baada ya miezi 6 ya kuzaliwa
Mambo ya kufanya nyumbani ili kupunguza hali ya kucheua
Fanya mambo yafutayo ikiwa mtoto wako anacheua sana;
Muweke begani mara baada ya kumyonyesha au kula kwa muda wa dakika 10 hadi 30 ili kutoa hewa katika tumbo
Mlaze chali badala ya kifudifudi au ubavu
Usimnyonyeshe au kumlisha sana ikiwa hana njaa
Mpe milo midogo midogo mara nyingi
Mzuie kuvuta moshi wa sigara katika mazingira
Ongeza unga maalumu wa nafaka kwenye maziwa ya mama yaliyokamuliwa
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 16:17:51
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
​
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
