Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
8 Aprili 2020 06:27:11
Amoxicillin
Ni antibiotiki inayotibu maambukizi yanayosababishwa na bakteria. Kazi yake kuu kwa bakteria hawa ni kuua ama kuzuia ukuaji wao. Dawa hii huweza kutibu bakteria wa gramu hasina Gram chanya.
Kundi la dawa
Amoxicillin ni antibayotiki mojawapo iliyo kwenye kundi la Penicillin lijulikanalo kama aminopenicillin.
Kundi hili ni la kwanza kujulikana kuwa na uwezo wa kupambana na bakteria wa Gramu hasi ambao hawatoi vomeng’enya vya Beta Lactam.
Sifa za dawa
Hustahimili asidi iliyo tumboni hivyo inaweza kutolewa kama kidonge cha kumeza
Dawa inapatikana kwenye mfumo wa kidonge, kidonge cha kutafuna, tembe na maji maji ya kunywa.
Rangi ya dawa inaweza kuwa nyeupe na kahawia isiyokolea, hata hivyo rangi ya dawa hutegemea kiwanda kinachotengeneza dawa
Hufyonzwa vizuri inapotumika pamoja na chakula
Fomu ya dawa wa Amoxicillin
Dawa hii hupatikana kwenye mfumo wa;
Kidonge milligramu 250-500
Tembe milligramu 250-500
Mfumo wa unga milligramu 250/kwa vayo
Utoaji taka mwilini wa Amoxicillin
Umetaboli wa amoxicillin hufanyika kwenye Ini. Utoaji wa sumu mwilini hufanywa na Figo na matumbo.
Amoxicillin hutibu magonjwa gani?
Dawa ya amoxicillin hutumika kutibu magonjwa yafuatayo yanayosababishwa na bakteria;
Kutibu maambukizi ya bacteria katika njia ya mkojo (UTI)
Kutibu maambukizi ya bacteria katika njia ya upumuaji mfano Neumonia
Kutibu maradhi ya sikio, Jicho na Pia
Kutibu maambukizi katika mfumo wa chakula au tumbo
Kutibu maambukizi ya ngozi na tishu laini
Kutibu maambukizi ya Bacteria H.Pyroli anayesababisha vidonda vya tumbo( hutumika na dawa zinine sio peke yake)
Amoxicillin huua bateria gani?
Baadhi ya Bakteria ambao wanadhuriwa na dawa hii ni:
Escherichia Coli
Haemophilus influenza
Streptococci
Neisseria Gonorrhoea
baadhi ya straini za Staphylococcus
Helicobacter pylori
Angalizo kwa watumiaji wa Amoxicillin
Tumia Dawa hii kwa Umakini kwa wagonjwa hawa
Wenye shida ya aleji au mzio wa Dawa hii na jamii ya Dawa ya penicillin mfano ampicillin, oxacillin
Wenye shida ya Ini
Wenye shida ya Figo
Wenye historia ya Pumu(asthma)
Wenye Aleji au mzio wa kundi la Dawa aina ya cephalosporin
Dawa zisizopaswa kutumika pamoja na Amoxicillin
Dawa hii Hairuhusiwi kutumika pamoja na Dawa zifuatazo kutokana na madhara makubwa yanaoweza kujitokeza
Chanjo hai ya BCG
Chanjo hai ya kipindupindu
Chanjo hai ya taifodi
Demeclocycline
Doxycycline
Eravacycline
Minocycline
Mycophenolate
Omadacycline
Pexidartinib
Pretomanid
Sarecycline
Tetracycline
Usitumie Dawa hii pamoja na Dawa ya probenecid sababu huongeza sumu ya amoxicillin mwilini.
Dawa hii inaongeza ufanyaji kazi wa dawa zinazozuia damu kuganga mfano warfarin, heparin.
Usitumie Dawa hii pamoja na Dawa aina Allopurinol sababu hupelekea Aleji Kali katika ngozi na Kuwashwa kwa ngozi.
Dawa kundi moja na Amoxicillin
Dawa zingine ambazo zipo kwenye kundi moja na Amoxicillin ni zifuatazo :
Ampicillin
Bacampicillin
Amoxicillin haipaswi kutumika kwa wagonjwa gani?
Amoxicillin haipaswi kutumika kwa wagonjwa hawa
Wagonjwa wenye mzio na Penicillin
Wagonjwa wenye mzioa na Cephalosporins
Dawa hii haipaswi kutumika kwa watu ambao hawana Maambukizi ya bakteria ili kuepusha dawa kuishiwa nguvu au bakteria kuwa sugu.
Matumizi ya Amoxicillin kwa wajawazito
Inaweza kutumika kwa mama mjamzito endapo faida ni kubwa kuliko madhara.
Matumizi ya Amoxicillin kwa wanaonyonyesha
Tafiti zinaonyesha kuwa kuna kiwango cha Amoxicillin hupita na kuingia kwenye maziwa ya mama na kumsababishia mtoto maudhi kama kuharisha, lakini hakuna madhara yanayoathiri kiwango cha uzalishaji wa maziwa.
Maudhi ya dawa Amoxicillin
Baadhi ya maudhi madogo ya dawa hi ni pamoja na :
Kuharisha
Kizunguzungu
Kiungulia
Kukosa usingizi
Kichefuchefu
Kuwashwa mwili
Kutapika
Maumivu ya tumbo
Mzio
Maumivu ya kichwa
Kuishiwa damu
Ufanye nini kama umesahau dozi yako?
Endapo umesahau kutumia dozi yako, tumia mara tu unapokumbuka, isipokua endapo muda wa dozi nyingine umefika unatakiwa kuruka hiyo dozi uliyosahau na kuendelea na dozi yako kwa muda kama ulivyopangiwa na daktari wako
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
3 Novemba 2021 11:49:13
Rejea za mada hii:-