Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Daktari wa ULY Clinic
Daktari wa ULY Clinic
28 Januari 2026, 09:40:40

Glucagon
Glucagon (Glukagon)- Homoni Muhimu ya Kudhibiti Kiwango cha Sukari Kwenye Damu
Glukagon hufahamika kwa lugha nyingine pia kama Glucagon ni homoni muhimu ya mwili inayozalishwa na tezi ya kongosho, hususan katika seli maalum zinazoitwa seli alfa (seli alpha). Homoni hii hufanya kazi kwa karibu sana na homoni ya insulin ili kudhibiti kiwango cha sukari (glukosi) kwenye damu.
Kwa ujumla, glukagon hufanya kazi ya kuongeza kiwango cha glukosi na asidi ya mafuta kwenye damu, hasa pale ambapo mwili unakuwa na upungufu wa sukari au unapohitaji nishati ya haraka.
Glukagon huzalishwa wapi?
Glukagon huzalishwa:
Kwenye tezi ya kongosho
Ndani ya seli alfa (seli alpha) za kongosho
Baada ya kuzalishwa, huingia kwenye damu na kuelekea hasa kwenye ini, ambako hufanya kazi zake kuu.
Glukagon hutolewa wakati Gani?
Glukagon hutolewa pale ambapo:
Kiwango cha sukari kwenye damu kimepungua
Mwili unahitaji nishati ya haraka, mfano:
Wakati wa njaa
Wakati wa kazi ngumu au mazoezi makali
Wakati wa msongo wa mwili au tukio la ghafla
Lengo kuu ni kuhakikisha mwili unapata glukosi ya kutosha ili viungo muhimu kama ubongo viendelee kufanya kazi.
Kazi kuu za Homoni ya Glukagon
Glukagon inapokuwa kwenye damu, hufanya kazi zifuatazo:
Kuchochea ini kuvunja glailojen kuwa glukosi (glaikojenolisis)
Kuchochea glukoneojenesisi, yaani:
Kubadilisha amino asidi kuwa glukosi
Kuchochea uvunjwaji wa mafuta (lipolisis):
Mafuta yaliyohifadhiwa hubadilishwa kuwa asidi ya mafuta kwa ajili ya nishati
Kwa kufanya hivyo, glukagon huhakikisha:
Kiwango cha glukosi kwenye damu kinabaki katika hali ya kawaida
Shughuli za mwili zinaendelea bila kukosa nishati
Mabadiliko ya kiwango cha Glukagon Kulingana na Lishe
Kiwango cha glukagon hupungua:
Mtu anapokula vyakula vyenye sukari au wanga kwa wingi
Kiwango cha glukagon huongezeka:
Mtu anapokula vyakula visivyo na sukari
Mtu anapofunga au kuchelewa kula
Kwa wagonjwa wa kisukari:
Udhibiti wa glucagon huwa hauko sawa, jambo linalochangia matatizo ya sukari kupanda au kushuka kupita kiasi.
Uhusiano wa Glukagon na Insulin
Glukagon na insulin ni homoni pinzani lakini hufanya kazi kwa ushirikiano:
Baada ya Kula
Wanga hubadilishwa kuwa glukosi
Kiwango cha glukosi huongezeka kwenye damu
Kongosho hutoa insulin
Insulin:
Hubadilisha glukosi kuwa glaicogen
Huihifadhi kwenye ini na misuli
Wakati wa Njaa au Sukari Kushuka
Kiwango cha glukosi kinaposhuka
Kongosho hutoa glukagon
Glukagon:
Hubadilisha glycogen kuwa glukosi
Huongeza sukari kwenye damu
Kwa pamoja, homoni hizi mbili huhakikisha kiwango cha sukari kwenye damu hakipandi wala kushuka kupita kiasi.
Dalili za Upungufu wa Homoni ya Glukagon
Mtu mwenye kiwango cha chini cha glukagon anaweza kuonyesha dalili zifuatazo:
Njaa kali
Kutetemeka
Woga na wasiwasi
Kuchoka haraka
Kutokwa na jasho jingi
Ngozi kuwa nyeupe
Kulala sana
Kizunguzungu
Dalili hizi hutokana na upungufu wa sukari kwenye damu (haipoglaisemia).
Dalili za Kuzidi kwa Homoni ya Glukagon
Mtu mwenye kiwango kikubwa cha glukagon anaweza kuwa na dalili kama:
Kiu ya maji mara kwa mara
Maumivu ya kichwa
Kutoona vizuri
Kukojoa mara kwa mara
Kuchoka na udhaifu wa mwili
Kupungua uzito
Kiwango cha juu cha glucagon kwa muda mrefu huweza kuhusishwa na matatizo ya kimetaboliki.
Matibabu ya Upungufu wa Glukagon
Kwa wagonjwa wenye upungufu wa glucagon, hasa wanaopata haipoglaisemia kali:
Dawa ya glukagon ya kutengenezwa maabara inaweza kutolewa
Hutumika sana kama:
Huduma ya dharura kwa wagonjwa wa kisukari
Pale ambapo mgonjwa hawezi kumeza sukari kwa mdomo
Umuhimu wa Glukagon katika Afya
Kwa ujumla, glukagon:
Ni muhimu kwa udhibiti wa sukari kwenye damu
Husaidia mwili kujilinda dhidi ya hypoglycemia
Ni homoni muhimu sana kwa:
Ubongo
Misuli
Mfumo wa neva
Bila glukagon, mwili usingeweza kujirekebisha pale sukari inaposhuka.
Hitimisho
Glukcagon ni homoni muhimu inayofanya kazi ya kuongeza kiwango cha sukari kwenye damu pale inapohitajika. Kwa kushirikiana na insulin, homoni hii huhakikisha mwili unapata nishati ya kutosha muda wote. Usawa wa glukagon ni muhimu sana katika afya ya binadamu, hasa kwa wagonjwa wa kisukari na wale wanaopata haipoglaisemia mara kwa mara.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliana na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii
Kwa ushauri zaidi na tiba unaweza kuwasialiana na daktari wa ULY CLINIC kupitia linki ya 'mawasialiano yetu' chini ya tovuti hii
Imeandikwa;
9 Aprili 2020, 10:46:44
Rejea za mada hii;
Healthline. Insulin and glucagon. Available from: https://www.healthline.com/health/diabetes/insulin-and-glucagon [Accessed 8 Apr 2020].
Mayo Clinic. Glucagon injection. Available from: https://www.mayoclinic.org/drugs-supplements/glucagon-injection-route/description/drg-20064089 [Accessed 8 Apr 2020].
Diabetes UK. Glucagon. Available from: https://www.diabetes.co.uk/body/glucagon.html [Accessed 8 Apr 2020].
Hormone Health Network. Glucagon. Available from: https://www.hormone.org/your-health-and-hormones/glands-and-hormones-a-to-z/hormones/glucagon [Accessed 8 Apr 2020].
Medscape. Glucagon. Available from: https://www.medscape.com/answers/2089114-163731/what-is-glucagon [Accessed 8 Apr 2020].
