Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
28 Mei 2025, 10:40:21

Njiti ya Etonogestrel
Njiti (Implanon) ni kifaa cha uzazi wa mpango cha muda mrefu chenye homoni aina ya etonogestrel. Hupandikizwa chini ya ngozi ya mkono wa juu wa mwanamke na hutoa homoni polepole kwa kipindi cha miaka mitatu. Kifaa hiki kinafahamika pia kwa jina la Nexplanon, ambalo ni toleo jipya zaidi.
Jinsi njiti ya Etonogestrel inavyofanya kazi
Implanon hutoa etonogestrel ambayo:
Huzuia kutolewa kwa yai kutoka ovari (ovulation)
Hubadilisha ute wa mlango wa kizazi kuwa mzito, hivyo kuzuia mbegu kupenya
Hubadilisha ukuta wa mfuko wa mimba (endometrium), kuzuia upandikizaji wa yai lililorutubishwa
Rangi na fomu ya njiti ya Etonogestrel
Implanon ni kijiti kidogo, cheupe, chenye urefu wa takriban sentimita 4 na kipenyo cha milimita 2.Hupandikizwa chini ya ngozi bila kuhitaji upasuaji mkubwa, kwa kutumia kifaa maalum (applicator).
Ufanisi wa Etonogestrel
Ina ufanisi wa zaidi ya 99%
Hutoa kinga dhidi ya mimba kwa kipindi cha miaka mitatu
Uwezo wa kupata mimba hurudi mara tu baada ya kuondolewa
Majina ya kibiashara
ImplanonNexplanon
Matumizi ya njiti Etonogestrel
Njia ya uzazi wa mpango ya muda mrefu kwa wanawake
Hutumika kuzuia mimba bila kuhitaji matumizi ya kila siku
Inatakiwa kupandikizwa na mtaalamu wa afya aliyehitimu na mwenye ujuzi
Dawa/mahitaji yanayoweza kuathiri utendaji wa njiti
Rifampicin
Carbamazepine
Phenytoin
Efavirenz
Griseofulvin
Barbiturates
Dawa za kutibu kifua kikuu na baadhi ya dawa za VVU
Watu wasiopaswa kutumia njiti ys Etonogestrel
Wenye historia ya saratani ya titi (breast cancer)
Wenye magonjwa sugu ya ini au uvimbe wa ini
Wenye kutokwa na damu isiyo ya kawaida ya uke bila sababu inayojulikana
Wenye mzio wa etonogestrel au vifaa vya implant
Tahadhari kwa watumiaji
Kupandikiza kunapaswa kufanyika wakati ambapo hakuna uwezekano wa mimba
Hakikisha haijapotea chini ya ngozi au kuhama mahali ilipopandikizwa
Implanon haiwezi kuzuia magonjwa ya zinaa (kama VVU/UKIMWI)
Wanawake wanaotumia dawa nyingine za muda mrefu wanapaswa kushauriwa kuhusu ufanisi wa Implanon
Matumizi kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha
Haipaswi kutumika wakati wa ujauzito
Salama kwa mama anayenyonyesha, kwani homoni hupita kwa kiwango kidogo kwenye maziwa na haina madhara makubwa kwa mtoto
Madhara ya Etonogestrel
Baadhi ya madhara madogo ni pamoja na
Maumivu ya kichwa
Kuongezeka au kupungua kwa hedhi
Kukosa hedhi
Maumivu ya matiti
Kichefuchefu
Mabadiliko ya hisia au msongo wa mawazo
Uongezekaji wa uzito
Maumivu mahali ilipopandikizwa
Madhara makubwa na adimu ni pamoja na
Maambukizi mahali pa kupandikiza
Kifaa kuhama kutoka sehemu ya awali
Mimba ya nje ya mji wa mimba (ectopic pregnancy), ikiwa mimba imetokea
Ikiwa unataka kuondoa njiti
Ondolewaji hufanywa na mtaalamu wa afya kwa kutumia dawa ya ganzi ya sehemu ndogo
Uwezo wa kushika mimba hurudi mara moja baada ya kuondolewa
Ni muhimu kuripoti ikiwa kifaa hakionekani au kinahisiwa kimehama
Hitimisho
Njiti ya Etonogestrel (Implanon/Nexplanon) ni njia salama, yenye ufanisi mkubwa na inayofaa kwa wanawake wengi wanaotaka udhibiti wa mimba wa muda mrefu bila usumbufu wa kutumia dawa kila siku. Ni muhimu kushauriana na mtaalamu wa afya kabla ya kupandikizwa ili kujua kama njia hii inakufaa kiafya.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara
1. Je, baada ya kutoa njiti mtu anaweza kupata ujauzito hata kama hajaanza kuona siku zake?
Ndiyo. Mara tu baada ya njiti kuondolewa, homoni ya etonogestrel hupungua haraka mwilini, na ovulation inaweza kurudi kabla ya kuona hedhi ya kwanza. Hivyo, ujauzito unaweza kutokea mapema, hata kabla ya kipindi cha kwanza cha hedhi.
2. Njiti inaweza kusababisha kukosa hedhi kabisa?
Ndiyo. Baadhi ya wanawake hupoteza hedhi kwa muda mrefu wakiwa na njiti, jambo ambalo ni la kawaida na si hatari kiafya. Hata hivyo, ikiwa umekosa hedhi ghafla baada ya muda wa kawaida, ni vema kupima ujauzito.
3. Je, njiti inaweza kuathiri uwezo wa kupata mimba baadaye?
Hapana. Njiti haina athari ya kudumu kwenye ovari. Baada ya kuondolewa, uwezo wa kupata mimba hurudi haraka, mara nyingi ndani ya wiki chache.
4. Je, Implanon inalinda dhidi ya magonjwa ya zinaa kama VVU?
Hapana. Implanon haikingi dhidi ya magonjwa ya zinaa. Ili kujikinga, tumia kondomu kila unaposhiriki tendo la ndoa.
5. Ni lini inashauriwa kuondoa njiti kabla ya miaka mitatu?
Inaweza kuondolewa kabla ya muda wake ikiwa:
Unataka kupata ujauzito.
Unapata madhara yasiyovumilika (kama maumivu, damu nyingi au mabadiliko makubwa ya hisia).
Unaanza kutumia dawa zinazoweza kupunguza ufanisi wa njiti.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
6 Novemba 2025, 13:33:18
Rejea za mada hii:-
