Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
Jumatano, 14 Mei 2025

Kutokwa damu baada ya kutoa mimba kwa dawa

Tafiti zinaonyesha kuwa wanawake wengi hutokwa damu kwa wastani wa siku 14 tangu kutumia dawa ya kutoa mimba. Hata hivyo idadi ya siku ambazo matone madogo ya damu hutoka huweza kwenda hadi siku 10 zaidi.
Ni kawaida mwanamke kutokwa damu baada ya kutumia dawa kwani damu ni ishara kwamba ujauzito unatoka nje ya mwili. Hata hivyo, muda na kiasi cha damu hutofautiana kulingana na umri wa mimba, aina ya dawa, na mwitikio wa mwili wa kila mtu.
Mabonge ya damu
Katika Makala hii, neno damu nyingi, damu kidogo na mabonge ya damu yametumika kuelezea wingi wa damu kwa kufananisha na matunda:
Bonge dogo ukubwa wa zabibu ni sawa na damu kidogo
Bonge dogo ukubwa wa ndimu ni sawa na damu kiasi
Bonge la ukubwa wa chungwa ni sawa na damu nyingi sana
Aina ya dawa zinazotumika
Dawa | Kazi Kuu | Maelezo ya Matumizi |
Mifepristone | Huzuia homoni ya projesterone, hivyo mfuko wa mimba unashindwa kuendeleza ujauzito. | Humezwa kwanza chini ya uangalizi wa mtaalamu. |
Misoprostol | Husababisha misuli ya mfuko wa mimba kusinyaa na kutoa kondo la mimba nje. | Hutumika masaa 24–48 baada ya mifepristone (kwa kawaida kwa njia ya mdomo, chini ya ulimi, au kwenye uke). |
Wakati mwingine, misoprostol pekee hutumika pale ambapo mifepristone haipatikani, lakini njia hii inaweza kusababisha kutokwa damu kwa muda mrefu zaidi na ufanisi mdogo kidogo.
Uhusiano kati ya umri wa mimba, muda, kiasi na sifa za damu
Umri wa Mimba | Muda wa kutokwa Damu | Kiasi cha Damu Kinachotarajiwa | Sifa za Damu | Maelezo Muhimu |
Wiki 1–6 | Siku 2–5 | Kiasi cha wastani, sawa na hedhi nzito | Damu nyekundu au kahawia nyepesi, vipande vidogo vya damu vinaweza kuonekana | Kwa umri huu wa mimba, damu hupungua haraka; mara nyingi maumivu ni madogo. |
Wiki 7–8 | Siku 5–10 | Kiasi kikubwa siku 1–3, hupungua baadaye | Damu nyekundu, wakati mwingine na chembe za tishu laini za ujauzito | Maumivu ya tumbo hujitokeza zaidi; ni kawaida kuona vipande vya damu. |
Wiki 9–10 | Siku 7–14 | Kiasi kikubwa mwanzoni, hupungua taratibu | Damu nyekundu au inayoelekea nyeusi, na mabonge madogo ya damu | Kiasi cha damu kinaweza kuwa kingi kuliko hedhi ya kawaida; ufuatiliaji unashauriwa. |
Wiki 11–12 | Siku 10–21 | Damu nyingi na ya muda mrefu zaidi | Damu inayoelekea nyeusi au nyekundu sana, yenye mabonge makubwa | Hatari ya kutokwa damu kupita kiasi au mabaki ya mimba ni kubwa zaidi; ni lazima uchunguzwe na daktari. |
Zaidi ya Wiki 12 | Hadi siku 21–28 | Damu nyingi na inaweza kuhitaji ufuatiliaji wa karibu | Damu nzito yenye tishu nyingi na mabonge makubwa | Mara nyingi huhitaji uchunguzi wa hospitali au usaidizi wa kitabibu ili kuhakikisha mimba imetoka yote. |
Muda na mabadiliko ya kutokwa damu
Masaa 4–6 baada ya kutumia misoprostol, damu huanza kutoka kwa wingi pamoja na vipande vya damu au tishu.
Damu nyingi hutoka kwa siku 1–3, kisha hupungua taratibu.
Kwa wagonjwa wengi, doa dogo au damu kidogo huendelea hadi wiki 2.
Ikiwa damu inaendelea zaidi ya wiki 3–4, au inaongezeka badala ya kupungua, ni ishara ya tatizo.
Mwongozo wa kutathmini kiasi cha damu kwa kutumia idadi ya pedi
Kiasi cha damu | Idadi ya pedi kubwa zinazoloweshwa | Muda wa kutokea (kwa saa) | Maelezo ya mwonekano wa damu | Tafsiri ya kitabibu | Hatua ya kuchukua |
Kidogo | Pedi 1–2 kwa siku | Kila baada ya masaa 6–8 | Damu nyekundu au kahawia nyepesi, doa dogo linaweza kuendelea | Kawaida siku za mwanzo au mwisho wa kutoa mimba | Endelea kufuatilia; ni hali ya kawaida |
Wastani | Pedi 3–4 kwa siku | Kila baada ya masaa 3–4 | Damu nyekundu, wakati mwingine na vipande vidogo vya damu | Kawaida katika siku 1–3 za kwanza baada ya kutumia dawa | Hali ya kawaida, lakini endelea kufuatilia |
Nyingi | Pedi 1–2 kila saa kwa zaidi ya saa 2 mfululizo | Ndani ya saa 1–2 | Damu nyekundu ang’avu au giza, ina mabonge makubwa | Inaonyesha damu nyingi kupita kiasi (heavy bleeding / hemorrhage) | Mwone daktari haraka au nenda hospitali |
Hatari sana | Pedi 1 kamili kila dakika 30–60 kwa zaidi ya saa 2 | Mara kwa mara bila kupungua | Damu nyekundu ang’avu, mabonge makubwa, kizunguzungu au udhaifu | Hatari ya upotevu mkubwa wa damu (anaemia au shock) | Nenda hospitali mara moja! |
Jinsi ya Kutumia Jedwali Hili
Hesabu pedi unazotumia kila siku na uangalie kwa muda wa saa ngapi zinajaa.
Tazama rangi na mwonekano wa damu: nyekundu ang’avu = damu mpya; kahawia = damu ya zamani.
Ikiwa unalowesha pedi 1 kubwa kila saa kwa zaidi ya saa 2, au una kizunguzungu, udhaifu, au mapigo ya moyo ya haraka, hiyo ni ishara ya hatari — tafuta huduma ya dharura mara moja.
Ikiwa damu kidogo inaendelea zaidi ya wiki 3, wasiliana na daktari kwa uchunguzi wa ultrasound au kipimo cha β-hCG.
Dalili za kawaida
Maumivu ya tumbo ya kuvuta (cramps) yanayofanana na hedhi nzito.
Kutokwa damu kwa wingi siku za mwanzo kisha kupungua taratibu.
Utoaji wa vipande vya damu au tishu laini za ujauzito.
Kichefuchefu, kuharisha, au homa ya muda mfupi (chini ya 38°C).
Dalili hizi ni za kawaida na zinaonyesha mwili wako unajibu dawa ipasavyo.
Wakati gani uonane na daktari haraka?
Mwone daktari mara moja ikiwa una mojawapo ya dalili zifuatazo:
Kutokwa damu nyingi sana — mfano, unalowesha pedi moja kubwa kila dakika 30–60 kwa zaidi ya saa 2 mfululizo.
Damu inaendelea zaidi ya wiki 3 bila kupungua.
Homa zaidi ya 38°C inayodumu zaidi ya siku moja.
Maumivu makali ya tumbo yasiyopungua hata baada ya kutumia dawa za maumivu.
Harufu mbaya kutoka ukeni au ute unaofanana na usaha.
Kizunguzungu kikubwa, udhaifu mwingi, au mapigo ya moyo kwenda kasi.
Hakuna damu kabisa baada ya kutumia dawa – inaweza kumaanisha dawa hazijafanya kazi na mimba bado ipo.
Matunzo ya nyumbani
Baada ya Kutoa Mimba kwa Dawa
Tumia pedi badala ya tamponi ili kufuatilia kiasi cha damu.
Kunywa maji ya kutosha na kula vyakula vyenye chuma kama maini, nyama nyekundu, mboga za majani, na maharage.
Pumzika vya kutosha, lakini unaweza kufanya shughuli nyepesi nyumbani.
Epuka kufanya ngono hadi damu itakapokoma kabisa (kwa kawaida wiki 2).
Panga uchunguzi wa ufuatiliaji ndani ya siku 7–14 kuthibitisha kuwa mimba imetoka kabisa (kwa ultrasound au kipimo cha β-hCG).
Makala hii imejibu maswali yafuatayo
Je inachukua muda gani damu kukatika baada ya kutoa mimba kwa dawa?
Je ni kiasi gani cha damu hutoka baada ya kutoa mimba kwa dawa?
Je , damu inakatika lini baada ya kutoa mimba kwa dawa?
Je, damu inaanza kutoka lini baada ya kutumia dawa za kutoa mimba?
Je ni dalili gani ya hatari baada ya kutoa mimba kwa dawa?
Je kutokwa na mabonge ya damu ni kawaida baada ya kutoa mimba kwa dawa?
Hitimisho
Kutokwa damu baada ya kutoa mimba kwa dawa ni jambo la kawaida na ni sehemu ya mchakato wa kutoa ujauzito nje ya mwili. Hata hivyo, ni muhimu kutambua tofauti kati ya dalili za kawaida na zile za hatari. Ufuatiliaji wa kitabibu unahakikisha kuwa mimba imetoka yote, hakuna mabaki ya tishu, na hakuna maambukizi.Kama unaona damu nyingi kupita kawaida, harufu mbaya, au maumivu makali, mwone daktari mara moja au tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe.
Mambo mengine unayopaswa kufahamu baada ya kutoa mimba
Baada ya kutoa mimba unaweza kupata mimba nyingine mara moja, hivyo utapaswa kutumia kinga ili kuzuia mimba nyingine. Linki ifuatayo ina video zinazoainisha siku za hatari kulingana na mzunguko wako wa hedhi. Bofya kiungo cha makala husika hapa chini ili kufahamu ni lini unaweza kushika ujauzito hivyo uchukue hatadhari.
Maswali yaliyouliziwa mara kwa mara
1: Mwanamke alikunywa dawa ya kutoa mimba, damu ikatoka nyingi sana kwa siku kadhaa, lakini baada ya wiki mbili alipima tena mimba ikawa bado inaonekana. Inawezekana kweli mimba bado ipo?
Jibu: Ndiyo, inawezekana mimba bado ipo.
Kutokwa na damu nyingi baada ya kutumia dawa za kutoa mimba siyo ushahidi wa moja kwa moja kwamba mimba imetoka yote. Damu inaweza kutoka kwa sababu ya athari za dawa au kutokana na utolewaji wa sehemu ya ujauzito (incomplete abortion). Ikiwa mimba haijatoka yote, mabaki ya ujauzito huweza kubaki ndani ya mfuko wa uzazi, hali inayoweza kuendelea kusababisha damu kuvuja au kipimo cha mimba kuendelea kuonyesha majibu chanya kwa muda.
Kwa kawaida, homoni ya mimba (hCG) huendelea kuwepo mwilini hata baada ya kutoa mimba kwa siku 7 hadi 28. Ndiyo maana kipimo cha mimba kinaweza kuonyesha mimba hata kama mimba imetoka. Lakini kama kipimo kinaendelea kuonyesha mimba wiki mbili hadi tatu baada ya kutoa mimba, ni lazima kufanyiwa uchunguzi wa ultrasound ili kuthibitisha kama mimba bado ipo au kama kuna mabaki ndani ya mfuko wa uzazi yanayohitaji kusafishwa kitaalamu.
2. Je, antibiotics zinaweza kuathiri kipimo cha mimba?
3. Nilitoa mimba na damu zilivuja kwa siku 6 kisha zikaacha. Baada ya siku 11, damu zilianza kutoka tena. Nilipima kipimo cha ujauzito cha mkojo na kikawa positive. Baada ya hapo nilikaa bila damu hadi tarehe 5 mwezi huu ambapo nilipata hedhi yenye damu nyingi na mabonge. Damu imeisha jana, lakini leo asubuhi nimepima tena mkojo na bado kipimo kinaonyesha positive. Je, kwa nini kipimo bado kinaonyesha ujauzito ilhali sina dalili zozote za mimba inayoendelea?
4. Je, vipimo vyote vya mimba vina uwezo sawa wa kugundua hCG baada ya kutoa mimba?
5. Kwa nini kipimo cha damu kinaweza kuonyesha matokeo tofauti na cha mkojo baada ya kutoa mimba?
6. Je, homoni ya hCG hupungua kwa kiwango kipi kila wiki baada ya kutoa mimba?
7. Ni dalili gani za hatari baada ya kutoa mimba zinazoashiria kuhitaji matibabu ya haraka?
8. Je, kutokwa na mabonge ya damu baada ya kutoa mimba ni kawaida?
9. Je, ninaweza kuendelea kuwa na hedhi ya kawaida baada ya kutoa mimba?
10. Kwa nini daktari anaweza kupendekeza ultrasound hata kama kipimo cha mimba kinasoma positive?
11. Je, mimba ya nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancy) inaweza kusababisha kipimo kubaki positive baada ya kutoa mimba?
12. Je, ninaweza kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango mara moja baada ya kutoa mimba?
13. Je, mazoezi au kazi nzito baada ya kutoa mimba yanaweza kuchelewesha kushuka kwa hCG au kusababisha damu kurudi?
14. Daktari, nilikuwa na ujauzito wa wiki 6 na nimetumia vidonge 4 vya Misoprostol kwa njia ya uke masaa 12 yaliyopita. Nimeona damu kidogo pamoja na mabonge, pia nina maumivu ya wastani ya tumbo na homa. Nimebadili pedi mara tatu tu ndani ya saa 12, na nina historia ya pumu. Je, hali hii ni ya kawaida na baada ya kutoa mimba damu inatakiwa kudumu kwa muda gani?
15. Nilitoa mimba ya mwezi 1 damu imetoka siku2 tu je nikawaida?
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
7 Novemba 2025, 02:59:06
Rejea za mada hii:
Davis A, Westhoff C, De Nonno L. Bleeding patterns after early abortion with mifepristone and misoprostol or manual vacuum aspiration. J Am Med Womens Assoc (1972). 2000;55(3 Suppl):141-4. PMID: 10846324.
https://womenshealthclinic.org/what-we-do/abortion/after-an-abortion/. Imechukuliwa 25.01.2023
National Abortion Federation (2008) Early Medical Abortion; in Clinical Policy Guidelines Washington, DC; pp 7-11.
Breitbart V, Repass DC. The counseling component of medical abortion. J Am Med Womens Assoc 2000; 55(suppl 3):164-166.
Creinin MD. Randomized comparison of efficacy, acceptability and cost of medical versus surgical abortion. Contraception 2000; 62:117-24.
Henderson JT, Hwang AC, Harper CC et.al. (2005) Safety of mifepristone abortion in clinical use. Contraception 72:175-8.
Chen AY, Mottl-Santiago J, Vragovic O et.al. (2006) Bleeding after medication-induced termination of pregnancy with two dosing schedules of mifepristone and misoprostol. Contraception 73: 415-19.
Allen RH, Westhoff C, DeNonno L, Fielding SL, Schaff EA. Curettage after mifepristone-induced abortion: Frequency, timing, and indications. Obstet Gyncecol 2001;98:101-6.
Schaff EA, Fielding SL, Westhoff C, Ellertson C, Eisinger SH, Stadalius LS, Fuller L. Vaginal misoprostol administered 1, 2, or 3 days after mifepristone for early abortion. JAMA 2000;284:1948-1953.
American College of Obstetricians and Gynecologists. Early Pregnancy Loss. ACOG Practice Bulletin No. 200. Obstet Gynecol. 2018;132(5):e197–e207.
Barnhart KT, Sammel MD, Rinaudo PF, Zhou L, Hummel AC, Guo W. Symptomatic patients with an early viable intrauterine pregnancy: HCG curves redefined. Obstet Gynecol. 2004;104(1):50–5.
Cole LA. hCG, the wonder of today's science. Reprod Biol Endocrinol. 2012;10:24.
National Health Service (NHS). Pregnancy test. London: NHS; 2023 [cited 2025 Aug 10]. Available from: https://www.nhs.uk/pregnancy/trying-for-a-baby/doing-a-pregnancy-test/
Morse CB, Sammel MD, Shaunik A, Barnhart KT. Performance of human chorionic gonadotropin curves in women with symptomatic early pregnancy: a pooled analysis. Fertil Steril. 2012;98(5):1228–33.
World Health Organization. Safe abortion: technical and policy guidance for health systems. 2nd ed. Geneva: WHO; 2012.
Papp C, Toth-Pal E, Papp Z. Retained products of conception: diagnosis and management. Best Pract Res Clin Obstet Gynaecol. 2009;23(4):529–38.
Horne AW, van den Driesche S, King AE, Burgess S, Myers M, Ludlow H, et al. Endometrial natural killer cells and angiogenesis in recurrent miscarriage. Hum Reprod. 2008;23(4):805–12.
