top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dr.Sospeter Mangwella, MD

ULY CLINIC

20 Julai 2025, 20:05:07

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Dawa ya gono kwa mwanaume

Swali la msingi


Kijana wa miaka 27 anayeishi mkoani anasema, wiki moja baada ya kushiriki tendo la ndoa bila kinga na mpenzi mpya, alianza kuhisi maumivu makali wakati wa kukojoa na kugundua ute mzito wenye usaha ukitoka kwenye uume wake kila asubuhi. Kwa hofu na aibu, alianza kutumia antibiotiki alizobakiza nyumbani bila kwenda hospitali. Baada ya siku tano, hali haikubadilika—maumivu yalizidi na usaha ukaongezeka na akaanza kujiuliza:

  • Je, ni kweli nina gono au ni ugonjwa mwingine?

  • Ni dawa gani sahihi za kutumia?

  • Kwanini dawa nilizotumia hazijasaidia?

  • Je, nikichelewa kwenda hospitali kuna madhara?


Katika makala hii ya ULY clinic, tutajibu maswali kama ya kijana huyyu kwa ufasaha wa kitabibu sambamba na kuelezea mambo yafuatayo;

  • Dawa ya kutibu gono kwa mwanaume ni ipi?

  • Orodha ya dawa za gono kwa mwanaume.

  • Dawa ya kutibu usaha uumeni.

  • Dawa ya kuondoa usaha kwenye uume.


Maelezo muhimu ya kufahamu kabla ya kufahamu dawa

Gono ni moja ya ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na maambukizi ya bakteria mwenye jina la Nisseria gonorrhoear, ambaye huenezwa kwa njia ya kujamiana na mtu mwenye maambukizi. Dalili kuu ya ugonjwa zimeelezewa katika makala nyingine ya dalili za gono kwa wanaume.


Dawa za kutibu gono zipo za aina nyingi kutegemea eneo na eneo pia nchi na nchi. Utofauti huu huletwa na mambo mbalimbali ikiwa pamoja na hali ya mwitikio wa kimelea kwenye dawa husika. Baadhi ya vimelea vimebadili tabia na hivyo havisikii dawa ambazo hapo awali zimekuwa zikitibu ugonjwa huo.


Kwa kawaida watu wengi huchanganya ugonjwa wa gono na magonjwa mengine ya zinaa, kwa kuzania kuwa kutoka usaha kwenye uume kunasababishwa na gono tu. Hii si kweli, kuna magonjwa mengine yanaweza kupelekea uume kutoa usaha ambayo mara nyingi huwa magonjwa mengine ya zinaa pia. Hii ndio maana endapo una dalili hii ya gono ni muhimu kutibiwa magonjwa mengine ya zinaa yanayosababisha dalili hii ili kuhakikisha unapona haswa pale ambapo vipimo huwa havifanyiki au kutohitajika kufanyika.


Dawa za gono kwa wanaume

Inashauriwa ili kupata matibabu sahihi, wasiliana na daktari wako kwa ushauri na tiba. Baadhi ya dawa za kutibu gono kwa wanaume ni;

Kuona orodha kamili ya dawa za kutibu gono bofya soma makala ya dawa za gono.


Kumbuka

Endapo mgonjwa atatumia dawa sahihi na dozi sahihi atapona kwa wakati. Inashauriwa kutotumia dawa pasipo kushauriwa na daktari ili kuepuka madhara ya dawa na usugu wa vimelea kwenye dawa.


Majina mengine ya gono

Gono hufahamika kwa majina mengine kama kisonono.


Kwanini gono haiponi?

Matibabu ya ugonjwa wa gono mara nyingi hulenga kutibu magonjwa yote ya zinaa yanayosababisha kutokwa na usaa kwenye uume, hii ni kwa kuwa hufanana sana. Hivyo kuna wakati daktari atakuandikia dawa zaidi ya moja ili kuua vimelea kadhaa wanaosababisha dalili kama za gono.


Kutokana na maelezo haya, unaweza uzipone gono kwa kutumia dawa moja tu kwa kuwa kisababishi kinaweza kisiwe gono. Hata hivyo pia matumizi holela ya dawa hizi yamepelekea usugu wa vimelea kwenye dawa, hii ndio maana kumekuwa na wimbi la watu kutopona kwa dawa hizi zilizokuwa zinatumika awali na kuleta matokeo mazuri.


Kwenye matumizi holela, mtu anaweza kutumia dozi isiyo sahihi, mchanganyiko wa dawa zisizo sahihi, dawa zilizopita muda wa matumizi n.k


Unashauriwa kuwasiliana na daktari wako muda wote kabla ya kutumia dawa yoyote.


Hitimisho

Usaha kutoka uume ni dalili ya hatari ya magonjwa ya zinaa. Ni vyema kufanyiwa vipimo na kupata matibabu kamili na sahihi kutoka kwa daktari. Epuka kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu kwani kunaweza kusababisha usugu wa vimelea na kushindwa kupona.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara

1 Dawa ya gono kwa mwanaume ni ipi?

Dawa ya gono hutegemea majibu ya vipimo. Kwa kawaida, madaktari hutumia dawa kama Ceftriaxone (sindano) pamoja na Azithromycin (tembe) kama tiba ya awali kwa wanaume waliothibitika kwa kipimo kuwa na gono.

2 Nitumie dawa gani kutibu gono nyumbani?

Haitakiwi kujitibu nyumbani bila vipimo na ushauri wa daktari. Dawa hutolewa kulingana na majibu ya maabara na hali ya mgonjwa binafsi.

3 Je, Azithromycin inatibu gono?

Ndiyo, Azithromycin hutumika kama sehemu ya mchanganyiko wa dawa kwa matibabu ya gono, hasa kwa wagonjwa waliothibitika kupitia vipimo. Haifai kutumika peke yake.

4 Cefixime inatumika kutibu gono kwa namna gani?

Cefixime ni dawa ya mdomo inayotumika pale ambapo sindano ya Ceftriaxone haipatikani, lakini si chaguo la kwanza. Lazima iandikwe baada ya vipimo kuonyesha maambukizi ya gono.

5 Je, kuna dawa ya sindano kwa ajili ya gono?

Ndio. Ceftriaxone ni sindano inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kutibu gono. Dozi na matumizi yake hutegemea ushauri wa daktari baada ya vipimo.

6 Naweza kupata dawa ya gono bila vipimo?

Haishauriwi hata kidogo. Kutumia dawa bila vipimo kunaweza kusababisha kutopona au kuua vimelea wasiohusika, na pia kuongeza usugu wa dawa.

7 Je, gono linaweza kupona kwa kutumia dawa moja tu?

Wakati mwingine linaweza, lakini mara nyingi hutibiwa kwa dawa mbili kwa pamoja ili kushambulia vimelea kwa ufanisi zaidi, hasa pale ambapo kipimo hakijafanywa kwa magonjwa mengine yanayofanana na gono.

8 Kwa nini nimeshatumia dawa lakini gono haiponi?

Inawezekana dawa uliyotumia haikufaa, au ulitumia dozi isiyo sahihi. Pia huenda maambukizi si ya gono pekee, au vimelea wamepata usugu wa dawa. Hali hii inahitaji vipimo vya uchunguzi zaidi.

9 Je, kutumia dawa ya mtu mwingine kunaweza kunisaidia?

Hapana. Matibabu ni ya mtu binafsi baada ya vipimo. Dawa ya mtu mwingine inaweza isiwe sahihi kwa hali yako na inaweza kukuletea madhara au usugu wa dawa.

10 Nifanyeje kama uume wangu unaendelea kutoa usaha baada ya kutumia dawa?

Muone daktari mara moja kwa uchunguzi zaidi. Hii inaweza kuashiria kuwa kuna maambukizi mengine, au gono haikutibiwa ipasavyo.

11 Ni muda gani inachukua kwa dawa ya gono kuonyesha matokeo?

Dalili nyingi hupungua ndani ya siku 3 hadi 7 baada ya kuanza dawa sahihi, lakini unashauriwa kukamilisha dozi na kuacha ngono hadi utakapopona kabisa.

12 Je, nifanye mapenzi baada ya kutumia dawa ya gono?

Subiri hadi utakapomaliza dozi yote, na kuhakikisha kuwa dalili zimekwisha kabisa. Pia hakikisha mwenza wako ametibiwa ili kuepuka maambukizi ya kurudia.

13 Naweza kutumia dawa za asili kutibu gono?

Dawa za asili hazijathibitishwa kisayansi kutibu gono. Matibabu ya uhakika yanatolewa kwa kutumia dawa za hospitali baada ya vipimo rasmi.

14 Je, gono linaweza kujirudia baada ya matibabu?

Ndiyo. Ikiwa mwenza wako hajapona au ukijihusisha tena na ngono isiyo salama, unaweza kuambukizwa tena.

15 Kuna tofauti gani kati ya gono na magonjwa mengine ya zinaa yanayosababisha usaha?

Magonjwa kama chlamydia, mycoplasma, au trichomoniasis pia huweza kuleta usaha. Vipimo ni muhimu kutofautisha visababishi kabla ya kuanza dawa.

16 Kwa nini ninatakiwa kupewa dawa zaidi ya moja?

Hii husaidia kutibu magonjwa mchanganyiko ya zinaa yanayosababisha dalili zinazofanana. Pia hupunguza uwezekano wa usugu wa dawa.

17 Je, mwanamke wangu pia anatakiwa kutumia dawa za gono?

Ndio, hata kama hana dalili. Wenzi wote wanapaswa kutibiwa kwa pamoja ili kuepuka kuambukizana tena.

18 Kuna madhara gani ya kutumia dawa za gono bila ushauri wa daktari?

Unaweza kupata madhara ya dawa, kutopona, au kukuza usugu wa vimelea dhidi ya dawa. Hali hii huongeza ugumu wa tiba.

19 Je, gono linaweza kusababisha ugumba kwa mwanaume?

Ndiyo. Kama halitatibiwa mapema, linaweza kuathiri mirija ya uzazi na kuleta matatizo ya uzazi au maumivu ya kudumu.

Nawezaje kuzuia kuambukizwa tena gono baada ya kupona?

Tumia kondomu kila unapofanya ngono, fanya vipimo mara kwa mara, epuka wapenzi wengi, na hakikisha mwenza wako ametibiwa pia.


Rejea za mada hii;
  1. World Health Organization. Gonorrhoea [Internet]. Geneva: WHO; 2023 [cited 2025 Jul 20]. Available from: https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/gonorrhoea

  2. Centers for Disease Control and Prevention. Sexually Transmitted Infections Treatment Guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.

  3. Unemo M, Lahra MM, Escher M, Eremin S, Cole MJ, Galarza P, et al. World Health Organization Global Gonococcal Antimicrobial Surveillance Program (WHO GASP): review of new data and evidence to inform international collaborative actions and research efforts. Sex Health. 2019;16(5):412–25.

  4. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually Transmitted Infections Treatment Guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(No. RR-4):1–187.

  5. Hook EW III, Handsfield HH. Gonococcal infections in the adult. In: Holmes KK, Sparling PF, Stamm WE, et al., editors. Sexually Transmitted Diseases. 4th ed. New York: McGraw-Hill; 2008. p. 627–45.

  6. Wi T, Lahra MM, Ndowa F, Bala M, Dillon JAR, Ramon-Pardo P, et al. Antimicrobial resistance in Neisseria gonorrhoeae: Global surveillance and a call for international collaborative action. PLoS Med. 2017;14(7):e1002344.

  7. Tanzanian Ministry of Health. Standard Treatment Guidelines and Essential Medicines List 6th Edition. Dodoma: MoHCDGEC; 2021.

  8. Unemo M, Seifert HS, Hook EW III, Hawkes S, Ndowa F, Dillon JAR. Gonorrhoea. Nat Rev Dis Primers. 2019;5(1):79.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page