top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dr.Sospeter Mangwella, MD

ULY CLINIC

23 Februari 2026, 12:10:59

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Dawa ya gono sugu kwa mwanaume

Gono ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria Neisseria gonorrhoeae. Ugonjwa huu huathiri njia ya mkojo, sehemu za siri, puru, na koo. Gono kinapodumu kwa muda mrefu bila matibabu sahihi, hujulikana kama kisonono sugu, na huweza kusababisha madhara makubwa kama ugumba, maambukizi kwenye tezi dume (prostate), na matatizo ya mfumo wa mkojo.


Dalili za gono sugu kwa wanaume

Wanaume wenye gono sugu wanaweza kupata dalili zifuatazo:

  • Maumivu au hisia ya kuwaka moto wakati wa kukojoa

  • Kutokwa na usaha kutoka kwenye uume

  • Kuvimba na maumivu kwenye korodani

  • Maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo

  • Kuhisi haja ndogo mara kwa mara

  • Maambukizi kwenye tezi dume, yanayosababisha maumivu makali


Matibabu ya gono Sugu

Gono sugu huhinahitaji matibabu sahihi ili kuzuia madhara zaidi. Kutokana na ongezeko la usugu wa bakteria kwa baadhi ya dawa, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kitup cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kinapendekeza matibabu kwa kutumia dawa zifuatazo:

  • Sindano ya Ceftriaxone

  • Sindano ya Gentamicin

  • Vidonge vya Azithromycin

  • Doxycycline


NB: Dawa za gono sugu kwa mwanaume hutumika katika utaratibu maalumu ambao utapewa na daktari wako. Matumizi ya dawa katika dozi isiyo sahihi na pasipo kaundikiwa na daktari husababishi usugu wa vimela kwenye dawa.


Usugu wa vimelea kwenye dawa za gono sugu

Bakteria wanaosababisha Gono wamekuwa wakionyesha usugu kwa baadhi ya antibiotiki kama penicillin, tetracycline, na fluoroquinolones. Hivyo ni muhimu kutumia dawa zinazopendekezwa na daktari wako katika dozi sahihi ili kuepuka matumizi ya dawa kiholela.


Mambo muhimu kwenye matibabu ya Gono sugu

Unapokuwa unapata matibabu ya gono unapaswa kuzingatia yafuatayo:

  • Kumaliza dozi zote za dawa kama ilivyoelekezwa na daktari.

  • Kuepuka kujamiiana hadi vipimo vithibitishe kuwa maambukizi yameisha.

  • Kuwataarifu wapenzi wa karibu ili nao wafanyiwe uchunguzi na watibiwe iwapo wataonekana na maambukizi.

  • Kupima magonjwa ya zinaa mara kwa mara kwa wanaume walio katika hatari kubwa ya maambukizi.


Hitimisho

Gono sugu ni tatizo kubwa ambalo linahitaji matibabu sahihi na ya haraka. Ni muhimu kwa wanaume walio na dalili au walio katika hatari ya kupata kisonono kufanya uchunguzi wa kiafya mara kwa mara ili kupata tiba mapema. Matumizi sahihi ya antibiotiki na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ni njia bora ya kupambana na ugonjwa huu.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake


1. Je, “gono sugu” ni nini, na inatofautianaje na gonorrhea ya kawaida?

Gono sugu ni maambukizo ya gonorrhea ambayo hayajatibiwa vyema au yamerudi mara kadhaa licha ya matibabu ya awali. Ni kawaida kutokana na upinzani wa bakteria kwenye dawa za antibayotiki. Tofauti kuu ni kwamba maambukizo ya kawaida yanaponyeka kwa dawa za kawaida, wakati sugu huhitaji matibabu maalum zaidi na mara nyingi kwa uangalizi wa daktari.

2. Ni dawa zipi hutumika kutibu gonorrhea sugu kwa wanaume?

Matibabu ya gono sugu yanategemea mwitikio wa bakteria kwenye dawa. Dawa zinazotumika mara nyingi ni antibayotiki maalum kama:

  • Ceftriaxone (kwa sindano)

  • Cefixime

  • Azithromycin (katika baadhi ya matukio)

  • Doxycycline

Ikiwa bakteria ni sugu sana, daktari anaweza kutumia mchanganyiko wa antibayotiki kulingana na matokeo ya majaribio ya kipimo cha kuotesha bakteria na kuangalia usikivu wa dawa.


Dawa hizi zinapaswa kuandikwa na kutumika chini ya maelekezo ya daktari, kwa sababu gono sugu inaweza kuwa na upinzani mkubwa wa dawa.

3. Kwa nini gono inakuwa sugu kwenye dawa?

Gono inakuwa sugu kwenye dawa kwa sababu bakteria Neisseria gonorrhoeae ametengeneza upinzani dhidi ya antibayotiki mbalimbali, hasa pale endapo dawa hazikatumika vyema (kama kutumia dozi isiyokamilika, matumizi ya antibayotiki bila ushauri wa daktari, au matumizi ya dawa isiyosahihi). Hii ina maana bakteria amejifunza “kuepuka” athari za dawa.

4. Je, ni muhimu kufanya vipimo kabla ya kupata dawa kwa gono sugu?

Ndiyo kabisa. Daktari anaweza kupendekeza:

  • Uchunguzi wa kuotesha bakteria na kuangalia mwitikio wake kwenye dawa

  • Uchunguzi wa jumla wa mkojo

Hii inasaidia kujua dawa ipi itafanya kazi vizuri kwa aina ya bakteria walio mwilini, ambayo ni muhimu sana kwenye gono sugu.

5. Je, matibabu ya gono sugu kwa wanaume ni ya muda gani?

Matibabu ya gono sugu hutofautiana kulingana na:

  • aina ya antibayotiki inayotumika

  • hali ya mtu binafsi

  • matokeo ya vipimo


Kwa kawaida, dawa hutolewa kwa siku kadhaa hadi wiki, na mara nyingi daktari atahitaji kuangalia tena ili kuhakikisha maambukizi yameisha kikamilifu.

6. Je, wanaume wenye gono sugu wanaweza kupona kabisa?

Ndiyo, wanaume wenye gono sugu wanaweza kupona kabisa ikiwa watapata matibabu sahihi na kwa wakati. Mafanikio ya matibabu hutegemea:

  • utumiaji sahihi wa antibayotiki

  • kufuata maagizo ya daktari

  • kufanya vipimo vya kufuatilia

Ikiwa maambukizi yanaendelea kwa muda mrefu bila matibabu, daktari anaweza kupendekeza mchanganyiko wa dawa.

7. Je, ni kuna hatari gani endapo gonoa sugu haitatibiwa?

Kama haitatibiwa kwa wakati, gono sugu inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama:

  • Maambukizi ya tezi dume (prostataitisi)

  • Maambukizi kwenye tezi za uzazi za ndani

  • Kupunguza uwezo wa kutungisha mimba

  • Matatizo ya mrija wa mkojo kama kusinyaa na makovu

  • Maambukizi ya viungo vingine kama uti wa mgongo (kwa nadra)

Kwa hiyo ni muhimu sana kutafuta matibabu mapema.

8. Je, washirika wa ngono wanahitaji pia matibabu?

Ndiyo, washirika wa ngono wa mtu aliye na gono sugu wanapaswa pia kupimwa na kutibiwa, hata kama hawana dalili. Hii inazuia maambukizi ya kujirudia na kuendelea kuenea.

9. Je, gono sugu inaweza kurudi baada ya matibabu?

Inaweza kutokea ikiwa:

  • dawa haikutolewa kulingana na matokeo ya vipimo

  • mtu alikosa kumaliza dozi ya antibayotiki

  • mtu alifanya ngono bila kinga na mpenzi ambaye hajapimwa au kutibiwa

Kwa hivyo kuzingatia ushauri wa daktari na kutumia kinga (kama kondomu) ni muhimu.

10. Je, kuna chanjo au njia za kuzuia gono sugu?

Hadi sasa, hakuna chanjo ya gono kama ilivyo kwa hepataitisi B au HPV. Njia bora za kuzuia ni:

  • Matumizi sahihi ya kinga ya kiume (kondomu)

  • Kupimwa mara kwa mara endapo una tabia ya ngono zisizo salama

  • Kuacha tabia ya ngono isiyo salama au kuwa na mpenzi mmoja tu aliyepima

Kuzuia maambukizi ndio njia ya msingi ya kupunguza hatari ya kupata gono sugu.


Muhtasari wa maneno muhimu katika makala hii
  • Gonorrhea sugu kwa wanaume

  • *Antibayotiki za gono'

  • Matibabu ya gono sugu

  • Upinzani wa dawa za Gono

  • Vipimo vya kuotesha na kuangalia mwitikio wa gono kwenye dawa

  • Dalili na matibabu ya gono kwa wanaume

  • Mchanganyiko wa dawa kwa gono sugu


Rejea za mada hii

  1. Leone PA. Epidemiology, pathogenesis and clinical manifestations of Neisseria gonorrhoeae infection. Inapatikana: www.uptodate.com/contents/epidemiology-pathogenesis-and-clinical-manifestations-of-neisseria-gonorrhoeae-infection?source=see_link#H4 

  2. Centers for Disease Control and Prevention. Sexually transmitted disease surveillance 2010. Inapatikana: www.cdc.gov/std/stats10/gonorrhea.htm

  3. Ontario Agency for Health Protection and Promotion (Public Health Ontario). Guidelines for testing and treatment of gonorrhea in Ontario. Toronto (ON): Queen’s Printer for Ontario; 2013. Inapatikana: www.publichealthontario.ca/en/eRepository/Guidelines_Gonorrhea_Ontario_2013.pdf

  4. Centers for Disease Control and Prevention. Update to CDC’s Sexually Transmitted Diseases Treatment Guidelines, 2010: oral cephalosporins no longer a recommended treatment for gonococcal infections. MMWR Morb Mortal Wkly Rep 2012;61(31):590-4. 

  5. Public Health Agency of Canada. Canadian guidelines on sexually transmitted infections. 2013 Update. Inapatikana: www.phac-aspc.gc.ca/std-mts/sti-its/cgsti-ldcits/section-5-6-eng.php

  6. World Health Organization. Sexually transmitted bacterial pathogen for which there are increasing antimicrobial resistance concerns: Neisseria gonorrhea. Inapatikana: www.who.int/csr/resources/publications/drugresist/IIAMRmanual.pdf 

  7. Public Health Agency of Canada. Canadian guidelines on sexually transmitted infections. July 2013. Inapatikana: www.phac-aspc.gc.ca/std-mts/sti-its/cgsti-ldcits/section-5-6-eng.php#footnote-t1

  8. 6. MacDonald NE, Stanbrook MB, Flegel K, et al. Gonorrhea: what goes around comes around. CMAJ 2011;183:1567.

  9. Kondro W. Untreatable gonorrhea rampant. CMAJ 2012;184:E591.

  10. Ison CA. Antimicrobial resistance in sexually transmitted infections in the developed world: implications for rational treatment. Curr Opin Infect Dis 2012;25:73-8.

  11. Public Health Agency of Canada. Executive summary—report on sexually transmitted infections in Canada: 2009. Inapatikana: www.phac-aspc.gc.ca/sti-its-surv-epi/sum-som-eng.php


Imeandikwa:

8 Juni 2025, 08:25:22

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page