top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dkt. Glory, MD

ULY CLINIC

20 Desemba 2025, 16:11:02

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Je, kuna dawa za kutumia ili kufanya kipimo cha HIV kiwe negative?

Maswali ya msingi


  1. Mtu mwenye virus vya ukimwi kuna dawa anaweza meza akienda kupima aonekane negative?

  2. Samahani doctor, ukiwa una vvu kuna dawa unaweza meza ukiebda kupima iwe negative?


Majibu


Hapana, hakuna dawa inayoweza kumfanya mtu mwenye virusi vya UKIMWI (HIV) aonekane (Hasi) negative kwenye vipimo kwa muda mrefu au kudanganya matokeo. Hata hivyo, kuna mambo machache yanayoweza kuathiri matokeo ya vipimo vya HIV ambayo yameorosheshwa hapa chini.


Matumizi ya Dawa za ARVs

Watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV) kwa ufanisi wanaweza kufikia muda kiwango cha virusi kuwa kidogo kuweza kutambulika na kipimo cha kiwango cha virusi kwenye damu. Ikiwa mtu yuko kwenye kiwango hiki kwa muda, hawezi kuambukiza wengine. Lakini hii haimaanishi amepona au yuko negative! Ukifanya kipimo cha kupima kingamwili, bado kitaonyesha kuwa ana HIV.


Kuwa kwenye kipindi cha dirisha la matazamio

Baada ya kuambukizwa VVU, mwili unachukua wiki kadhaa hadi miezi kadhaa kuonyesha kingamwili za HIV. Ikiwa mtu atapima ndani ya siku chache za maambukizi (kabla kingamwili hazijazalishwa), anaweza kupata negative isiyo halisi, yaani, matokeo ya uongo yanayoonyesha hana HIV.


Matumizi ya Dawa za PEP au PrEP

PEP (Dawa za kuzuia UKIMWI baada ya kujihatarisha): Ikiwa mtu ametumia dawa hizi ndani ya saa 72 baada ya kuambukizwa na HIV, zinaweza kusaidia kuzuia maambukizi, wakati PrEP (Dawa za kuzuia kabla ya kuambukizwa) husaidia kuzuia maambukizi. Hata hivyo, hizi dawa hizi hazifanyi mtu aonekane negative ikiwa tayari ameambukizwa.


Hitimisho

Hakuna dawa inayoweza kumfanya mtu mwenye UKIMWI aonekane negative kwenye vipimo kwa muda mrefu. ARVs zinaweza kupunguza virusi hadi visionekane , lakini mtu bado ana UKIMWI.


Njia pekee ya kuwa na uhakika wa kutopata HIV ni kujikinga kwa kutumia kinga kama kondomu, PrEP, au kuzingatia uaminifu wa mpenzi mmoja aliye HIV-negative.



Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, Panado (Acetaminophen/Paracetamol) inaweza kusababisha kipimo cha HIV kisome negative?

Hapana kabisa.Panado (paracetamol/acetaminophen) haiathiri matokeo ya kipimo cha HIV.Ni dawa ya maumivu na homa, na haiingiliani na kingamwili au virusi vya HIV kwenye damu. Hata ukimeza Panado kabla ya kupima, kipimo kitasoma hali yako halisi.

2. Je, Antibayotiki zinaweza kubadilisha majibu ya kipimo cha HIV?

Hapana.Antibiotics hazifanyi kipimo cha HIV kisome negative wala positive ya uongo.HIV si bakteria, ni virusi, hivyo antibiotics hazina athari kwenye vipimo vya HIV.

3. Je, kunywa pombe kali kabla ya kupima kunaweza kuathiri matokeo ya kipimo cha UKIMWI?

Hapana. Pombe haiwezi kuficha HIV kwenye kipimo.Lakini inaweza kuathiri maamuzi ya mtu kuhusu ngono isiyo salama.

4. Je, Vipimo vya Haraka vinadanganyika kirahisi?

Hapana.Vipimo vya haraka vinatumika duniani kote na vina usahihi wa hali ya juu vinapotumika kwa usahihi na baada ya kipindi cha dirisha.

5. Je, Kuna dawa za asili au mitishamba zinazoweza Kufanya kipimo kisome negative?

Hapana.Hakuna dawa ya asili, mzizi, majani, wala mchanganyiko wowote unaoweza kubadilisha ukweli wa maambukizi ya HIV kwenye kipimo.

Tafadhali epuka waganga au watu wanaodai “dawa za kuficha HIV”.

6. Nifanye nini kama nina shaka na majibu ya kipimo cha UKIMWI?

  • Rudia kipimo baada ya wiki 4–12

  • Tumia kituo cha afya kinachotambulika

  • Fanya kipimo cha kuthibitisha

Rejea za mada hii
  1. Fauci, A. S., Lane, H. C., & Redfield, R. R. (2019). HIV/AIDS: The science of the disease and treatment. New England Journal of Medicine, 381(3), 300-310.

  2. Rodger, A. J., Cambiano, V., Bruun, T., et al. (2019). Risk of HIV transmission through condomless sex in serodifferent couples with the HIV-positive partner taking suppressive antiretroviral therapy: Final results of the PARTNER study. The Lancet, 393(10189), 2428-2438.

  3. Cohen, M. S., Chen, Y. Q., McCauley, M., et al. (2016). Antiretroviral therapy for the prevention of HIV-1 transmission. New England Journal of Medicine, 375(9), 830-839.

  4. World Health Organization (WHO). (2021). Consolidated guidelines on HIV prevention, testing, treatment, service delivery, and monitoring: Recommendations for a public health approach. WHO Publications.

  5. Centers for Disease Control and Prevention (CDC). (2023). HIV Treatment as Prevention (TasP). Retrieved from www.cdc.gov

  6. UNAIDS. (2022). Undetectable = Untransmittable (U=U): The Science Is Clear. Retrieved from www.unaids.org


Imeandikwa:

7 Juni 2025, 19:30:13

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page