Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dr.Sospeter Mangwella, MD
ULY CLINIC
4 Agosti 2025, 12:59:41
Kinyesi cha kwanza cha mtoto hutoka lini?
Swali la msingi
Je, mtoto asipopata kinyesi ndani ya siku mbili tangu azaliwe ni kawaida?
Ni hali ya kawaida kwa wazazi wapya kuwa na wasiwasi ikiwa mtoto mchanga hajapita choo baada ya kuzaliwa. Moja ya maswali yanayoulizwa sana ni: “Mtoto wangu ni siku ya pili tangu azaliwe hajapata kinyesi, hii ni kawaida?”
Kinyesi cha kwanza cha mtoto: Mekoniam
Kinyesi cha kwanza cha mtoto mchanga huitwa mekoniam. Hii ni aina ya kinyesi kigumu chenye rangi nyeusi au kijani kibichi kilichojikusanya tumboni mwa mtoto wakati wa ujauzito. Meconium hutengenezwa kutokana na seli zilizokufa, kamasi, maji ya tumbo (maji ya chupa ya uzazi) na virutubisho vilivyopitia kwa mtoto akiwa tumboni.
Muda wa kupitisha kinyesi cha kwanza
Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya watoto hutoa meconium ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa.
Baadhi ya watoto wenye afya nzuri hupitisha kinyesi cha kwanza hadi masaa 48 bila matatizo yoyote.
Hata hivyo, kutopitisha kinyesi baada ya masaa 48 kunaweza kuwa dalili ya matatizo ya kiafya yanayohitaji uchunguzi.
Matatizo yanayoweza kusababisha kuchelewa kupitisha kinyesi
Ugonjwa wa Hirschsprung – Hali ambayo sehemu ya utumbo haina mishipa ya neva, hivyo kuathiri kusukuma kinyesi.
Kuvimba kwa njia ya haja kubwa – Hali ya kuzaliwa nayo au ya baada ya kuzaliwa.
Upungufu wa homoni thairoidi wa kuzaliwa – Homoni za tezi shingo zikiwa chini.
Matatizo ya mfumo wa neva au misuli ya utumbo.
Maambukizi au kukosa hewa (mtoto kukosa hewa ya kutosha wakati wa kuzaliwa).
Je, unapaswa kufanya nini?
Kama mtoto wako ni wa kawaida na hana dalili za ugonjwa (kama kutapika, tumbo kuvimba, au kukosa hamu ya kunyonya), bado unaweza kumwangalia kwa karibu hadi kufikia masaa 48. Kama baada ya masaa 48 hajapitisha choo, ni muhimu sana kumpeleka hospitali ili afanyiwe uchunguzi na vipimo vya kitabibu.
Wakati gani umwone daktari haraka?
Dalili zifuatazo zikufanye uonenane na daktari haraka kwa uchaunguzi na tiba;
Mtoto hataki kunyonya
Tumbo kuvimba au kuwa gumu
Kutapika majimaji ya kijani (nyongo)
Kutokuwapo kwa gesi wala kinyesi
Hitimisho
Kuchelewa kupitisha kinyesi ndani ya masaa 24 hadi 48 bado inaweza kuwa kawaida kwa baadhi ya watoto wachanga wenye afya njema. Hata hivyo, kutopitisha kabisa kinyesi ndani ya saa 48 ni kiashiria kinachohitaji tathmini ya haraka ya kiafya.
Rejea za mada hii:
Okoro PE, Enyindah CE. Time of passage of First Stool in Newborns in a Tertiary Health Facility in Southern Nigeria. Niger J Surg. 2013;19(1):20–2. doi:10.4103/1117-6806.111503
Kramer I. The time of passage of the first stool and first urine by the newborn infant. J Pediatr. 1955;46:158–9.
Tunc VT, Camurdan AD, Ilhan MN, Sahin F, Beyazova U. Factors associated with defecation patterns in 0–24-month-old children. Eur J Pediatr. 2008;167:1357–62.
Gulcan H, Gungor S, Tiker F, Kilicdag H. Effect of perinatal factors on time of first stool passage in preterm newborns: An open, prospective study. Curr Ther Res Clin Exp. 2006;67(3):214–25. doi:10.1016/j.curtheres.2006.06.002
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
