Mwandishi:
Imeboreshwa:
Dr.Sospeter Mangwella, MD
17 Juni 2025, 19:15:53
Kisonono cha kujirudia, nini tiba yake?
Swali la Mgonjwa
Mimi na mke wangu tunajitibu kisonono lakini kinajirudia. Tufanyeje?
Kisonono ni nini?
Kisonono, pia hujulikana kama gono, ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aitwaye Neisseria gonorrhoeae. Ugonjwa huu huathiri sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo sehemu za siri, mrija wa mkojo, shingo ya kizazi, sehemu ya nyuma (rektamu), koo, na hata macho.
Wagonjwa wengi huonyesha dalili kama:
Maumivu wakati wa kukojoa
Kutokwa na usaha ukeni au uume
Maumivu ya chini ya tumbo
Kuwashwa au kutokwa na majimaji sehemu za siri
Lakini pia, kuna baadhi ya watu wanaoweza kuwa na maambukizi bila dalili.
Kwa nini gono hujirudia?
Gono linaweza kujirudia kwa sababu kuu mbili:
1. Maambukizi mapya
Kufanya ngono bila kinga na mpenzi ambaye bado ana maambukizi
Kutozingatia ushauri wa daktari kuhusu kujizuia kufanya ngono hadi tiba ikamilike
2. Usugu wa bakteria kwenye dawa
Bakteria wa gono wanazidi kujenga usugu dhidi ya dawa mbalimbali
Tafiti zinaonyesha usugu wa asilimia 100 kwa penicillin na tetracycline, na karibu 80% dhidi ya dawa zingine
Sababu nyingine za kujirudia kwa gono:
Kutotumia dawa ipasavyo (kutomaliza dozi)
Kutumia dawa isiyo sahihi bila vipimo
Matibabu ya upande mmoja (mmoja tu kati ya wapenzi anayetibiwa)
Kuwa na magonjwa mengine ya zinaa ambayo huathiri kinga
Vipimo vya kuthibitisha gono ya kujirudia
Endapo dalili zinajirudia baada ya matibabu:
Daktari atapendekeza kipimo cha “kuotesha bakteria na kufahamu dawa uaji” kutoka kwenye majimaji ya ukeni au uume
Kipimo hiki huonyesha ni dawa gani zina uwezo wa kuua vimelea waliopo kwa sasa
Vipimo vya ziada vinaweza kufanyika kutegemeana na hali ya mgonjwa
Matibabu sahihi ya gono ya kujirudia
Baada ya kupimwa:
Utapewa dozi mpya ya dawa kulingana na majibu ya maabara
Dawa hizi hutolewa kwa pamoja kwa wewe na mpenzi wako
Unaweza kupewa dawa kama ceftriaxone (sindano) na azithromycin au dawa zingine kulingana na usugu uliobainika
Mambo ya kuzingatia ili kuzuia kurudia kwa gono
Tumia dawa zote kama ulivyoelekezwa
Hakikisha mke/mume au mpenzi wako pia anapata matibabu kamili
Epuka ngono hadi matibabu yawe yamekamilika kwa wote
Tumia kondomu kila tendo la ndoa au ngono
Fanya uchunguzi wa mara kwa mara kwa magonjwa ya zinaa
Weka uaminifu katika mahusiano au epuka wapenzi wengi
Tahadhari
Kujitibu mara kwa mara bila ushauri wa daktari kunaweza kusababisha usugu wa dawa na matatizo ya muda mrefu ya afya ya uzazi kwa wanawake na wanaume, ikiwa ni pamoja na:
Ugumba (kutopata mtoto)
Maambukizi sugu kwenye mfumo wa uzazi
Mimba nje ya mfuko wa uzazi
Ushauri wa ziada kwa wagonjwa wanaojitibu mara kwa mara
Kwa wagonjwa wanaorudia kutumia dawa za kutibu gono bila mpangilio au vipimo, hatari ya kuharibu mfumo wa uzazi, kuathiri mayai au mbegu, na hata kupata kansa ya mlango wa kizazi huongezeka.
Endapo unahisi dalili zimejirudia au unajua umetumia dawa bila uchunguzi — tafadhali muone daktari kwa vipimo sahihi.
Rejea za mada
Glozman VN, Borisenko KK. Retsidivy gonorei u muzhchin. Vestn Dermatol Venerol. 1990;(3):51-3.
Bautista CT, et al. Repeat infection with Neisseria gonorrhoeae. Int J STD AIDS. 2017;28(10):962-968.
Fung M, et al. Chlamydial and gonococcal reinfection among men. Sex Transm Infect. 2007;83:304–309.
CDC. Updated STD treatment guidelines. MMWR. 2012;61:590–594.
Ng LK, Martin IE. Laboratory diagnosis of Neisseria gonorrhoeae. Can J Infect Dis Med Microbiol. 2005;16(1):15-25.
Yeshanew AG, Geremew RA. Neisseria Gonorrhoeae in Ethiopia. Antimicrob Resist Infect Control. 2018;7:85.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba