top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dr.Sospeter Mangwella, MD

ULY CLINIC

4 Agosti 2025, 12:44:26

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Kisukari cha mazoezi

Mazoezi ya mwili yana faida nyingi kwa watu wenye na wasio na kisukari. Kwa wagonjwa wa kisukari, mazoezi huchangia kuboresha ubora wa maisha, kuongeza nguvu za mwili, kuongeza uwezo wa chembe hai kutumia insulini ipatayo mwilini, na kuzuia magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na madhara mengine yanayotokana na kisukari.


Faida za mazoezi kwa wagonjwa wa kisukari

  • Kuboresha udhibiti wa sukari kwenye damu

  • Kuongeza uwezo wa mwili kutumia insulini vizuri

  • Kuzuia magonjwa ya moyo na mishipa ya damu

  • Kupunguza madhara na matatizo yanayohusiana na kisukari

  • Kuongeza nguvu na stamina za mwili

  • Kuboresha hisia za ustawi wa akili na kimwili


Mabadiliko ya sukari mwilini baada ya mazoezi

Wagonjwa wa kisukari aina ya kwanza mara nyingine huweza kupata mabadiliko yasiyo ya kawaida ya kiwango cha sukari kwenye damu baada ya kufanya mazoezi.

  • Mazoezi ya nguvu wastani kama kutembea, kuendesha baiskeli, kukimbia taratibu, au michezo ya kawaida, huweza kupunguza kiwango cha glukosi (sukari inayotumiwa kwa nishati) kwenye damu.

  • Mazoezi makali kama mashindano ya riadha, mbio za kasi, kunyanyua vitu vyenye uzito mkubwa, mara nyingine husababisha ongezeko la sukari mwilini wakati au baada ya mazoezi.


Kwa nini kuna ongezeko la sukari mwilini wakati wa mazoezi makali?

Mazoezi huchochea mwili kuzalisha homoni za msongo wa mawazo kama adrenaline na noradrenaline. Homoni hizi husaidia:

  • Kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka kwenye hifadhi ya glukagon kwenye ini ili kutoa nishati zaidi kwa misuli.

  • Ongezeko la homoni hizi huwa kubwa zaidi kadri mazoezi yanavyozidi kuwa makali.

Katika mazoezi ya wastani, kiwango cha glukagon na insulini huongezeka kwa usawa ili kudumisha viwango vya sukari vilivyo sawa. Hata hivyo, mazoezi makali husababisha ongezeko kubwa zaidi la glukagon kuliko insulini, hali inayosababisha kupanda kwa kiwango cha sukari wakati wa mazoezi au baada ya kumaliza.

Kwa watu wenye afya, baada ya mazoezi makali, insulini huongezeka kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari, lakini kwa wagonjwa wa kisukari aina ya kwanza, mchakato huu hushindikana, na sukari huendelea kuwa juu zaidi.


Je, mazoezi husababisha kisukari?

Hali ya ongezeko la sukari baada ya mazoezi kwa watu wasiokuwa na kisukari ni ya kawaida na haimaanishi mtu ana ugonjwa wa kisukari. Kiwango cha sukari hurejea katika hali ya kawaida ndani ya dakika hadi masaa machache baada ya mazoezi.


Visababishi vya ongezeko la sukari mwilini baada ya mazoezi

  • Ukosefu wa uzalishaji wa insulini wa kutosha kukabiliana na homoni za msongo (adrenaline, noradrenaline) baada ya mazoezi makali

  • Kula chakula kikubwa kabla ya mazoezi

  • Kupunguza dozi ya insulini kabla ya mazoezi bila mpango mzuri


Je, kuna hatari ya kushuka kwa sukari baada ya mazoezi?

Ndio, takriban asilimia 30 ya wagonjwa wa kisukari aina ya kwanza wanaweza kupata kushuka kwa kiwango cha sukari chini ya kawaida (hypoglycemia) wakati wa usiku baada ya mazoezi ya aerobiki ya wastani kwa dakika 45 mfululizo jioni.


Namna ya kuzuia kushuka au

kuongezeka kwa sukari baada ya mazoezi

  • Ongeza kiasi cha wanga kabla ya mazoezi kulingana na vipimo vya sukari uliyofanya awali wakati wa mazoezi.

  • Rekebisha kiasi cha insulini unayotumia kabla ya mazoezi kulingana na ushauri wa daktari.

  • Kumbuka kuongeza wanga huongeza nishati, hivyo usizidi kiasi kinachohitajika.

  • Shirikiana na mtaalamu wa afya kwa mpango mzuri wa lishe na dawa kabla na baada ya mazoezi.


Wapi utapata ushauri?

Kwa ushauri wa kitaalamu kuhusu mlo, mazoezi, na usimamizi wa dawa, wasiliana na daktari wako au huduma ya afya ya ULY Clinic kupitia kitufe cha Mawasiliano Yetu kwenye tovuti hii.


Viungo muhimu vya kuendelea kusoma


Rejea za mada hii:
  1. Bracken RM, et al. Exercise-induced hyperglycaemia in the absence of diabetes. Diabetic Medicine. https://onlinelibrary.wiley.com/doi/full/10.1111/j.1464-5491.2010.02960.x. Imechukuliwa 12.07.2021

  2. Zaharieva DP, et al. Prevention of Exercise-Associated Dysglycemia: A Case Study–Based Approach. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4334080/. Imechukuliwa 12.07.2021

  3. Galassetti P, Riddell MC. Exercise and type 1 diabetes (T1DM). Compr Physiol. 2013;3:1309–1336.

  4. Riddell M. The impact of type 1 diabetes on the physiological responses to exercise. In Type 1 Diabetes. Gallen I, Ed. London, Verlag, 2012, p. 29–45.

  5. Sigal RJ, et al. Hyperinsulinemia prevents prolonged hyperglycemia after intense exercise in insulin-dependent diabetic subjects. J Clin Endocrinol Metab. 1994;79:1049–1057.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page