top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dr.Sospeter Mangwella, MD

ULY CLINIC

4 Agosti 2025, 12:32:32

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Kuna umuhimu wa kutumia bia na waini nyekundu??

Kunywa waini nyekundu kwa kiasi imekuwa ikizungumziwa sana kama njia inayoweza kusaidia afya ya moyo. Pombe pamoja na baadhi ya kemikali maalum zinazopatikana kwenye waini nyekundu, zinazojulikana kama antioksidanti, zinaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya mishipa ya moyo, hasa ile aina ya koronari.


Jinsi Waini Nyekundu Husaidia Afya ya Moyo

Magonjwa ya mishipa ya moyo ya koronari husababishwa na kujaa kwa mafuta kwenye ukuta wa mishipa ya damu (atherosclerosis). Hali hii inaweza kusababisha kuziba kwa mishipa ya damu na kusababisha mshituko wa moyo au kiharusi, hasa pale ambapo mishipa hiyo midogo ya moyo au ubongo imeziba.

Waini nyekundu ina antioksidanti kama vile resveratrol, ambayo ni polyphenol inayopatikana pia kwenye vyakula vingine kama zabibu, blueberries, mulberries na karanga. Kemikali hii huonyesha uwezo wa:

  • Kusaidia kuondoa kolestro mbaya (LDL) mwilini, ambayo huchangia kuziba kwa mishipa ya damu.

  • Kuongeza kiwango cha kolestro nzuri (HDL) inayosaidia kuosha damu na kuondoa LDL kutoka kwenye mishipa ya damu.

  • Kulinda kuta za ndani za mishipa ya damu dhidi ya uharibifu wa kemikali na viumbe vinavyoweza kuleta kuvimba na kuzeeka kwa mishipa.


Je, Waini Nyekundu Inazuia Mshituko wa Moyo?

Uhusiano kati ya waini nyekundu na kupunguza hatari ya mshituko wa moyo bado haujaeleweka kikamilifu. Hata hivyo, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa ulaji wa kiasi kidogo cha waini nyekundu unaweza kuwa na faida kwa afya ya moyo kutokana na uwezo wake wa antioksidanti.


Resveratrol: Mlinzi wa Mishipa ya Damu

Resveratrol ni kemikali inayozalishwa na mimea kama njia ya kujilinda dhidi ya vimelea kama fangasi na bakteria. Inapatikana kwa wingi kwenye:

  • Zabibu nyekundu na ngozi yake (ambapo hutengenezwa waini nyekundu)

  • Matunda ya madogo kama blueberries, mulberries na forosadi

  • Karanga na vyakula vingine vya mimea

Resveratrol hufanya kazi kwa kupunguza mkazo wa oksidi (oxidative stress) unaosababisha kuharibika kwa seli za mishipa ya damu na kuongeza utendaji wa kolestro nzuri (HDL).


Kiasi Sahihi cha Kunywa Waini Nyekundu

Kiwango cha pombe kinachopendekezwa kwa afya ya moyo kinatofautiana kulingana na jinsia na hali ya mtu binafsi. Kwa ujumla:

  • Wanawake wanashauriwa kunywa kiasi kidogo kuliko wanaume, kwa wastani glasi moja (125 ml) kwa siku.

  • Wanaume wanashauriwa kunywa glasi moja hadi mbili kwa siku.

Kunywa zaidi ya haya kunaweza kuleta madhara makubwa kwa afya na kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa ini, saratani na matatizo ya moyo.

Kwa maelezo zaidi kuhusu pombe na afya, unaweza kusoma makala maalumu kwenye tovuti hii kuhusu Pombe na Afya ya Mwili.


Rejea za mada hii
  1. Siasos G, Tousoulis D, Oikonomou E, et al. The role of red wine polyphenols on endothelial function and atherosclerosis. Eur J Pharmacol. 2018;834:49-62. doi:10.1016/j.ejphar.2018.07.039.

  2. Renaud S, de Lorgeril M. Wine, alcohol, platelets, and the French paradox for coronary heart disease. Lancet. 1992 Jun 20;339(8808):1523-6. doi:10.1016/0140-6736(92)91277-f.

  3. Das DK, Mukherjee S, Ray D. Resveratrol and red wine, healthy heart and longevity. Heart Fail Rev. 2010 Mar;15(3):273-80. doi:10.1007/s10741-009-9164-z.

  4. Chiva-Blanch G, Arranz S, Lamuela-Raventós RM, Estruch R. Effects of Wine, Alcohol and Polyphenols on Cardiovascular Disease Risk Factors: Evidence from Human Studies. Alcohol Alcohol. 2013 Mar-Apr;48(3):270-7. doi:10.1093/alcalc/agt170.

  5. Estruch R, Sacanella E. Clinical evidence for a cardioprotective effect of red wine. J Cardiovasc Pharmacol. 2011 Apr;57(4):363-7. doi:10.1097/FJC.0b013e3182085f5a.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page