top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dr.Sospeter Mangwella, MD

ULY CLINIC

4 Agosti 2025, 12:50:36

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Kutokwa na ute mweupe kwenye uume asubuhi

Swali la mgonjwa

“Nilifanya mapenzi na mdada, asubuhi yake baada ya kwenda kuoga wakati nakojoa niliona ute mweupe kidogo sana kabla ya kukojoa, rangi kama ya shahawa. Hii ni dalili ya nini? Sina maumivu yoyote.”


Majibu


Kutokwa na ute mweupe kutoka kwenye uume kunaweza kuwa kwa sababu za kawaida au zisizo za kawaida. Uchunguzi wa sababu unategemea muktadha, dalili nyingine zinazoweza kuwepo, na historia ya tendo la ndoa.


Visababishi vya kawaida

Katika hali nyingi, kutokwa na ute mweupe baada ya kufanya tendo la ndoa ni jambo la kawaida, hasa endapo hakuna maumivu, harufu mbaya, au mabadiliko katika kukojoa. Vifuatavyo ni baadhi ya visabbaishi vinavyofahamika sana;


Mabaki ya manii

Baada ya kumaliza tendo la ndoa, sehemu ya shahawa inaweza kubaki kwenye njia ya mkojo na kutolewa taratibu baadaye, hasa wakati wa kukojoa au kuoga. Ute huu huwa na rangi nyeupe au ya krimu na hauna harufu kali. Hii si dalili ya ugonjwa na haitakiwi kukutia wasiwasi kama hakuna dalili nyingine.


Visababishi visivyo vya kawaida

Kama kutokwa na ute huu mweupe kunaendelea, kunakuwa na mabadiliko ya rangi, harufu mbaya, au kuambatana na maumivu au kuwashwa wakati wa kukojoa au ngono, basi inaweza kuwa ishara ya maambukizi. Maambukizi haya mara nyingi husababishwa na magonjwa ya zinaa.


1. Maambukizi ya Trikomoniasis

Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na protozoa aitwaye Trichomonas vaginalis. Kwa wanaume, unaweza kusababisha kutokwa na ute mweupe au kijani mwepesi, hasa asubuhi. Dalili zake zinaweza kuwa:

  • Kutokwa na ute kutoka kwenye uume

  • Kuwashwa kwenye uume au ndani ya njia ya mkojo

  • Kukojoa mara kwa mara au kwa shida


2. Ugonjwa wa gono

Gono husababishwa na bakteria wa Neisseria gonorrhoeae. Mojawapo ya dalili kuu kwa wanaume ni kutokwa na ute mzito mweupe, kijivu au wa njano kutoka kwenye uume. Dalili nyingine ni:

  • Maumivu wakati wa kukojoa

  • Ute wenye harufu mbaya

  • Kuvimba kwa korodani


Mambo ya kuzingatia

Ikiwa unakutana na mojawapo ya dalili hizi zifuatazo, ni muhimu kumuona daktari haraka:

  • Kutokwa na ute mweupe unaorudia au kuongezeka

  • Harufu mbaya ya ute

  • Maumivu wakati wa kukojoa

  • Kuwashwa kwenye uume

  • Kuwa na historia ya kufanya ngono bila kinga


Hitimisho

Kwa kuwa hauna maumivu wala dalili nyingine, kuna uwezekano mkubwa kwamba ute uliotoka ni mabaki ya shahawa. Hata hivyo, endapo hali hii itaendelea au dalili nyingine zitaongezeka, ni muhimu kufanya vipimo vya magonjwa ya zinaa kama gono na trichomoniasis.


Angalizo kwa wanaume

  • Fanya vipimo vya mara kwa mara ikiwa unajihusisha na ngono bila kinga

  • Tumia kondomu kujikinga na magonjwa ya zinaa

  • Usisite kuonana na daktari hata kama dalili ni ndogo


Rejea za mada hii
  1. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.

  2. Centers for Disease Control and Prevention (CDC). Gonorrhea – CDC Fact Sheet (Detailed). [Internet]. Atlanta: CDC; 2021 [cited 2025 Jun 18]. Available from: https://www.cdc.gov/std/gonorrhea/stdfact-gonorrhea-detailed.htm

  3. Hobbs MM, Sena AC. Sexually transmitted infections: Overview and clinical approach. In: Bennett JE, Dolin R, Blaser MJ, editors. Mandell, Douglas, and Bennett’s Principles and Practice of Infectious Diseases. 9th ed. Philadelphia: Elsevier; 2020. p. 1557–1575.

  4. Schwebke JR, Romero J, Feloney M. Trichomoniasis in men: diagnosis and management. Curr Infect Dis Rep. 2020;22(10):35.

  5. World Health Organization. Sexually transmitted infections (STIs). Geneva: WHO; 2022 [cited 2025 Jun 18]. Available from: https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/sexually-transmitted-infections-(stis)

  6. Mayo Clinic. Semen leakage: Should I be worried? [Internet]. Rochester: Mayo Foundation for Medical Education and Research; 2023 [cited 2025 Jun 18]. Available from: https://www.mayoclinic.org

  7. Taylor SN. Diagnosis and management of urethritis in men. Infect Dis Clin North Am. 2013;27(4):709–720.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page