Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dr.Sospeter Mangwella, MD
ULY CLINIC
21 Februari 2026, 03:16:48
.jpeg)
Mashilingi kwenye ngozi
Shilingi kwenye ngozi, pia huitwa vishilingi kwenye ngozi au mashilingi kwenye ngozi, ni majina ya Kiswahili yanayotumika kumaanisha ugonjwa wa fangasi wa ngozi wenye mwonekano wa duara kama shilingi kwa jina jingine ikiitwa ringworm auTinea corporis. Huonekana kama doa au kidonda cha mviringo chenye kingo zilizoinuka na sehemu yake ya kati huwa imeathiriwa kidogo au kutoathirika kabisa na fangasi.
Kumbuka: Ingawa neno la Kiingereza “ringworm” lina “worm”, huwa haimaanishi kuwa ni minyoo bali maambukizi ya fangasi.
Muonekano wa kawaida
Duara au ovali kama shilingi
Kingo nyekundu kwa watu weupe au zambarau kwa watu weusi, zilizoinuka au zenye magamba
Sehemu ya kati ya duara huwa haijaathiriwa kwa kiasi kikubwa
Huambatana na muwasho
Huongezeka ukubwa polepole
Sehemu zinazoweza kuathirika
Mikono na miguu
Kifuani au mgongoni
Shingoni
Mapajani (lakini eneo la kinena lina aina maalum iitwayo tinea cruris)
Chanzo na namna ya kuambukizwa
Shilingi kwenye ngozi husababishwa na fangasi wa kundi la dermatophytes. Maambukizi huenea kwa:
Kugusana ngozi kwa ngozi na mtu aliyeambukizwa
Kushirikiana taulo, nguo, mashuka
Kugusa wanyama walio na fangasi (hasa paka na mbwa)
Kutembea peku sehemu zenye unyevunyevu
Fangasi hupendelea mazingira ya:
Jasho
Unyevunyevu
Ngozi iliyochubuka
Magonjwa yanayofanana na shilingi
Ingawa vishilingi mara nyingi ni ugonjwa wa Tinea corporis, kuna hali nyingine zinazoweza kutoa dalili za kufanana kama vile:
Izima ya numula – pumu ya ngozi yenye madoa ya mviringo, lakini mara nyingi eneo ndani ya mduara huwa limeathirika sana.
Soriasisi – mabaka mekundu au zambarau kwa watu weusi yenye magamba meupe, huwa sugu na hujirudia.
Utambuzi sahihi ni muhimu kabla ya kuanza tiba.
Utambuzi wa mashilingi
Daktari huchanganya historia ya mgonjwa na vipimo rahisi kuthibitisha kuwa ni fangasi, ili kuepuka kuchanganya na magonjwa mengine ya ngozi.
Daktari huthibitisha kwa:
Uchunguzi wa macho
Kipimo cha KOH (kuangalia fangasi chini ya darubini)
Wakati mwingine kuotesha fangasi
Jedwali 1: Njia za utambuzi wa mashilingi
Njia ya uchunguzi | Inafanywaje | Nini huonekana | Umuhimu wake |
Uchunguzi wa macho | Daktari huangalia ngozi moja kwa moja | Duara lenye kingo nyekundu/zambarau na katikati halijaathiriwa sana | Mara nyingi hutambua haraka bila vipimo |
Kipimo cha KOH | Hukwangua ngozi kidogo na kuiweka kwenye kemikali (KOH) chini ya darubini | Nyuzi za fangasi (hyphae) huonekana | Ndiyo kipimo rahisi na cha uhakika zaidi |
Kuotesha fangasi | Sampuli huwekwa maabara ili fangasi ukue | Hutambua aina halisi ya fangasi | Hutumika kama tiba imeshindikana au maambukizi ni sugu |
Maelezo Muhimu
Kipimo cha KOH hutoa majibu haraka (dakika chache)
Kuotesha fangasi huchukua wiki kadhaa lakini hutoa uthibitisho kamili
Utambuzi sahihi huzuia kutumia dawa zisizofaa kama steroidi
Tiba ya shilingi/Vishilingi kwenye Ngozi
Matibabu hutegemea ukubwa na eneo la maambukizi. Wagonjwa wengi hupona kwa krimu pekee, lakini baadhi huhitaji dawa za kunywa. Daktari anaweza kukuandikia dawa zifuatzo kulingana na ugonjwa aliouona
i. Dawa za kupaka za fangasi
Daktari anaweza kukuandikiwa kati ya dawa zifuatazo kama tiba ya kwanza kwa maambukizi madogo au ya eneo moja kama shida yako imefahamika kuwa ni fangasi baada ya uchunguzi.
Mfano wa dawa:
Clotrimazole
Ketoconazole
Terbinafine
Jinsi ya kutumia kwa usahihi
Hupakwa mara 1–2 kwa siku
Matumizi huwa kwa wiki 2–4 (hata dalili zikiondoka mapema)
Hupakwa hadi nje kidogo ya mipaka ya kidonda (takriban sentimita 2)
Mikono inashauriwa kusafishwa na kukaushwa kabla ya kupaka
Wagonjwa wengi huanza kuona nafuu ndani ya siku 5–10, lakini tiba lazima iendelee hadi kukamilika ili kuzuia kurudia.
ii. Dawa za kunywa
Hutolewa na daktari ikiwa krimu pekee haitoshi.
Huhitajika wakati:
Maambukizi ni makubwa au mengi mwilini
Hayaponi baada ya wiki 2–3 za krimu
Yapo usoni, kichwani au sehemu nyeti
Mgonjwa ana kisukari au kinga dhaifu
Fangasi hurudia mara kwa mara
Dawa hizi humezwa kwa wiki kadhaa kulingana na ushauri wa daktari.
Mambo ya kuzingatia wakati wa tiba
Ili dawa ifanye kazi kikamilifu na kuzuia kurudi kwa fangasi, zingatia yafuatayo:
Maliza kozi ya dawa hata dalili zikitoweka mapema; Fangasi huweza kubaki chini ya ngozi; kusimamisha dawa mapema husababisha kurudia na kuwa sugu.
Safisha na kausha ngozi vizuri kabla ya kupaka dawa; Dawa hufanya kazi vizuri kwenye ngozi kavu; paka pia kidogo nje ya mipaka ya kidonda.
Epuka kushirikiana taulo, nguo au mashuka; Huzuia kujirudia na kuwaambukiza wengine nyumbani.
Badilisha nguo za ndani na soksi kila sikuIkiwezekana mara mbili kwa siku kama unatoka jasho sana.
Usipake krimu zenye steroidi bila ushauri wa daktari; Steroidi huficha dalili na kufanya fangasi kuenea.
Nawa mikono baada ya kugusa kidonda; Huzuia kusambaza fangasi sehemu nyingine za mwili.
Usifunge kidonda kwa plasta muda mrefu; Unyevu uliotegwa huchelewesha kupona.
Ufuatiliaji sahihi wa hatua hizi hupunguza sana kurudia kwa maambukizi na kuharakisha kupona.
Wakati gani wa kumwona Daktari haraka?
Muone mtaalamu wa afya mapema ukiona mojawapo ya dalili hizi:
Vidonda vinaenea haraka au vinaongezeka ukubwa licha ya kutumia dawa
Vinatoa usaha, damu au vinakuwa na maumivu makali (huashiria maambukizi ya bakteria juu ya fangasi)
Homa au kuvimba kwa tezi — ishara ya maambukizi makubwa
Mtoto mchanga au mtoto mdogo ameathirika (wanahitaji uchunguzi wa karibu zaidi)
Hakuna nafuu baada ya wiki 2–3 za dawa sahihi
Vipo usoni, kichwani au sehemu za siri
Una kisukari, UKIMWI au kinga dhaifu
Vidonda vimekuwa vyeusi sana, vinawaka au vinatoa harufu
Dalili hizi zinaweza kuashiria maambukizi sugu, aina nyingine ya ugonjwa wa ngozi, au hitaji la dawa za kunywa badala ya krimu pekee.
Kinga ya Shilingi / Vishilingi kwenye Ngozi
(Fangasi ya ngozi — Tinea corporis)
Kuzuia fangasi kunategemea kudhibiti unyevu, jasho, na maambukizi kwa kugusana. Chini kuna jedwali 2 ni muhtasari rahisi.
Jedwali 2: Hatua muhimu za kinga ya mashilingi kwenye ngozi
Hatua ya kinga | Kwa nini ni muhimu | Jinsi ya kufanya sahihi |
Oga na ukaushe mwili vizuri | Fangasi hukua kwenye unyevunyevu | Kaushia mwili hasa kwapa, mapaja, chini ya matiti, kati ya vidole kwa taulo safi na kavu |
Vaa nguo za pamba zisizobana | Hupunguza jasho na joto la ngozi | Badilisha mara moja nguo zinapopata jasho |
Epuka kushirikiana vitu/nguo binafsi | Fangasi huambukiza kwa kugusana | Tumia taulo, soksi na mashuka yako pekee |
Safisha vifaa vya michezo | Fangasi hukaa kwenye vitu muda mrefu | Safisha glavu, helimeti, mikeka ya mazoezi mara kwa mara |
Linda miguu maeneo ya umma | Maambukizi hutokea sakafuni penye unyevunyevu | Vaa ndala bafuni au bwawani |
Epuka kupaka dawa jamii ya steroidi bila ushauri | Hufanya fangasi kufichika na kusambaa | Tumia dawa baada ya utambuzi |
Dhibiti jasho | Jasho ni mazingira rafiki kwa fangasi | Oga baada ya mazoezi na kausha mwili |
Angalia wanyama wa kufugwa | Wanyama huambukiza sana | Tibu paka/mbwa wenye mabaka ya duara kama unaishi nao |
Imarisha kinga ya mwili | Kinga dhaifu hurudia maambukizi | Lala vizuri na kula lishe bora |
Dhibiti magonjwa sugu | Kisukari huongeza fangasi | Fuata matibabu kikamilifu |
Kanuni 5 Rahisi za Kukumbuka
Kavu kuliko dawa — kausha ngozi vizuri kila siku
Usishirikiane taulo au nguo
Badilisha nguo za jasho haraka
Tibu wanyama wenye mabaka ya duara
Usitumie krimu kiholela
Majina mbadala yanayotumika na watu
Kishilingi — Doa dogo la duara na moja
Vishilingi — madoa madogo ya duara zaidi ya moja
Mashilingi — madoa mengi ya duara
Shilingi — doa la duara
Vibarango — shilingi kichwani
Hutokana na umbo la duara kama coin
Rejea ya mada hii
James WD, Berger TG, Elston DM. Andrews' Diseases of the Skin: Clinical Dermatology. 13th ed. Philadelphia: Elsevier; 2019.
Habif TP. Clinical Dermatology: A Color Guide to Diagnosis and Therapy. 6th ed. Elsevier; 2015.
Bolognia JL, Schaffer JV, Cerroni L. Dermatology. 4th ed. Elsevier; 2017.
Mayo Clinic. Eczema (atopic dermatitis). [Internet]. 2023 [cited 2025 Jun 17]. Available from: https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/eczema/
World Health Organization. Skin diseases. [Internet]. 2023 [cited 2025 Jun 17]. Available from: https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/skin-diseases
Imeandikwa:
17 Juni 2025, 08:09:23
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
