Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dkt. Glory, MD
ULY CLINIC
22 Julai 2025, 12:58:27
Muundo na rangi ya haja kubwa kwa kichanga
Muundo na rangi ya haja kubwa kwa mtoto mchanga inaweza kutofautiana kati kichanga na kichanga kwa kutegemea lishe anayopewa na afya yake kwa ujumla. Makala hii imezungumzia kuhusu rangi na muundo wa kawaida wa haja kubwa kwa mtoto mchanga hadi wiki ya 6 ya maisha yake.

Haja kubwa siku ya 1-3 baada ya kuzaliwa
Haja kubwa huwa nyeusi, yenye mnato na nzito kama lami. Haja hii ni ya kawaida kwa kichanga kwani hutoa vitu vilivyojikusanywa tumboni mwa mtotokabla ya kuzaliwa.
Haja kubwa siku ya 3-5 baada ya kuzaliwa
Haja kubwa huanza kuwa rangi ya kijani au kahawia na kuwa laini zaidi. Inatokea wakati mtoto anaanza kuchakata maziwa ya mama au fomula na hali hii huwa ya mpito.
Siku 7 na kuendelea baada ya kuzaliwa
Haja kubwa baada ya siku 7 za kwanza hutegemea aina ya lishe anayopatiwa mtoto.
Haja kubwa kwa watoto wanaonyonya maziwa ya mama pekee
Haja kubwa huwa ya rangi ya njano, yenye majimaji kidogo, na harufu isiyo kali. Mtoto anaweza kujisaidia mara 3-6 kwa siku au hata kila baada ya kunyonya.
Haja kubwa wa watoto wanaotumia maziwa ya kopo pekee
Haja kubwa huwa yenye rangi ya kahawia au njano iliyokolea, na muundo wake ni mzito zaidi. Mtoto anaweza kujisaidia mara 1-4 kwa siku.
Haja kubwa kwa kichanga wiki ya 4-6
Watoto wanaonyonya maziwa ya mama pekee wanaweza kupata haja kubwa mara chache (mara moja kwa wiki), kwani maziwa ya mama huchakatwa vizuri na kuachwa na mabaki machache yanayotoka kama kinyesi. Watoto wanaotumia maziwa ya kopo wao huweza kupata haja kubwa mara 1-3 kwa siku.
Wakati gani wa kuhofia endapo haja kubwa imebadilika kwa kichanga?
Dalili zifuatazo zikitokea zinapaswa kukutia wasiwasi endapo rangi au muundo wa haja kubwa umebadilika kwa kichanga wako. Wasiliana na daktari wako haraka endapo;
Kichanga hapati haja kubwa kwa zaidi ya siku 3-5
Haja kubwa inaambatana na damu, ute mwingi, au harufu mbaya isiyo ya kawaida.
Kichanga kuharisha kupita kiasi
Kichanga kupata kinyesi kigumu sana kinachosababisha mtoto kukenya wakati wa kujisaidia.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara
1. Habari daktari, mwanangu ana wiki 3 lakini hapat choo mara kwa mara wala kujamba, tumbo linanguruma na anakunjamana. Amepata Belladonna lakini bado hali inaendelea. Nashauriwa vipi?
Jibu:Mtoto wa wiki 3 kutopata choo mara kwa mara ni kawaida ikiwa ananyonya maziwa ya mama pekee, kwani huweza kujisaidia hata mara moja kwa wiki. Hata hivyo, kunguruma kwa tumbo, kukunjamana, na kukosa gesi huashiria gesi au kukwama kwa choo. Belladonna si dawa ya kwanza kupendekezwa kwa kichanga. Mlete kwa daktari afanyiwe uchunguzi, hasa kama tumbo lake linaonekana kujaa sana au linauma.
2. Ni kawaida kwa mtoto mchanga kuwa na haja kubwa ya rangi nyeusi kama lami?
Ndiyo. Hali hii huitwa meconium na ni kawaida kabisa katika siku 1–3 baada ya kuzaliwa. Ni mabaki ya vitu alivyomeza tumboni kabla ya kuzaliwa.
3. Je, ni kawaida kwa mtoto mchanga kupata haja kubwa ya rangi ya njano kama haradali?
Ndiyo. Watoto wanaonyonya maziwa ya mama pekee mara nyingi hupata haja kubwa ya njano, yenye chembechembe, na isiyo na harufu kali. Hii ni dalili nzuri ya umeng’enyaji mzuri.
4. Mtoto wangu wa wiki 4 anapata haja kubwa mara moja tu kwa siku. Je, ni tatizo?
Hapana. Ikiwa mtoto ananyonya vizuri, haonyeshi dalili za maumivu, na haja kubwa yake ni laini — basi kupata haja mara moja kwa siku ni kawaida, hasa kwa wanaotumia maziwa ya kopo.
5. Je, mtoto wa maziwa ya mama anaweza kukaa siku 3 bila choo?
Ndiyo. Watoto wanaonyonya maziwa ya mama pekee wanaweza kukaa hata hadi siku 7 bila haja kubwa bila tatizo, kwani maziwa ya mama huchakatwa kikamilifu. Ila hakikisha haonyeshi dalili za kuvimbiwa kama kukasirika, tumbo kujaa au kukunjamana.
6. Ni nini husababisha haja kubwa ya kijani kwa mtoto mchanga?
Haja ya kijani inaweza kutokana na mpito wa meconium, au kuwa mtoto anapata maziwa tangulizi bila yasiyokidhi mahitaji na maziwa baada ya hapo yasiyotosha. Pia inaweza kuwa alama ya kutopata lishe vizuri au tumbo mchafuko wa tumbo.
7. Je, haja kubwa ya rangi ya udongo au kijivu kwa mtoto ni kawaida?
Hapana. Haja kubwa ya kijivu au kama udongo inaweza kuashiria tatizo kwenye ini au njia ya nyongo. Ni muhimu kumpeleka mtoto hospitalini haraka.
8. Nifanye nini kama mtoto anapata haja kubwa yenye ute mwingi au damu?
Hii si kawaida. Inaweza kuashiria maambukizi, mzio wa chakula au tatizo la tumbo. Mpeleke mtoto hospitali haraka kwa vipimo.
9. Ni lini mtoto mchanga huhitaji dawa ya choo?
Watoto wachanga hawahitaji dawa ya choo kama hali ni ya kawaida. Dawa hutolewa tu baada ya uchunguzi wa kitaalamu, hasa kama kuna kinyesi kigumu sana au dalili za maumivu makali, kufura kwa tumbo, au kutokupata haja kwa siku nyingi zaidi ya kawaida.
10. Je, mtoto anayepata maziwa ya kopo hupata haja kubwa mara ngapi kwa siku?
Kawaida ni mara 1–4 kwa siku, na kinyesi huwa kigumu zaidi kuliko cha maziwa ya mama. Ikiwa ni kigumu kupita kiasi au mtoto analia sana akijisaidia, muone daktari.
Rejea za mada hii:
Arias A, et al, (2001) Educating parents about normal stool pattern changes in infants. J Pediatr Health Care 15:269–274 10.1016/S0891-5245(01)91970-4
Yousaf A, et al (2022) Burden of pediatric functional gastrointestinal disorder in an emergency department-a single-center experience. Pediatr Emerg Care 38:e1512–e1516. 10.1097/PEC.0000000000002807 10.1097/PEC.0000000000002807.
Vandenplas Y, et al (2015) (2015) Prevalence and health outcomes of functional gastrointestinal symptoms in infants from birth to 12 months of age. J Pediatr Gastroenterol Nutr 61:531–537. 10.1097/MPG.0000000000000949 10.1097/MPG.0000000000000949
Velasco-Benítez CA, Collazos-Saa LI, García-Perdomo HA (2022) Functional gastrointestinal disorders in neonates and toddlers according to the Rome IV Criteria: a systematic review and meta-analysis. Pediatr Gastroenterol Hepatol Nutr 25:376–386. 10.5223/pghn.2022.25.5.376 10.5223/pghn.2022.25.5.376
Benninga MA, et al. (2016) Childhood functional gastrointestinal disorders: neonate/toddler. Gastroenterology S0016–5085(16):00182–00187. 10.1053/j.gastro.2016.02.016 10.1053/j.gastro.2016.02.016
Weaver LT (1988) Bowel habit from birth to old age. J Pediatr Gastroenterol Nutr 7:637–640. 10.1097/00005176-198809000-00002 10.1097/00005176-198809000-00002
Tunc VT, ET AL. (2008) Factors associated with defecation patterns in 0–24-month-old children. Eur J Pediatr 167:1357–1362. 10.1007/s00431-008-0669-2 10.1007/s00431-008-0669-2.
den Hertog J, et al. The defecation pattern of healthy term infants up to the age of 3 months. Arch Dis Child Fetal Neonatal Ed. 2012 Nov;97(6):F465-70. doi: 10.1136/archdischild-2011-300539. Epub 2012 Apr 20. PMID: 22522220.
Alvarez M, St J-R (1996) Infant fussing and crying patterns in the first year in an urban community in Denmark. Acta Paediatr 85:463–466. 10.1111/j.1651-2227.1996.tb14062.x 10.1111/j.1651-2227.1996.tb14062.x
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
